Mbunge
wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono akisisitiza jambo alipokuwa
akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisini
kwake jijini Dar es Salaam jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dar es Salaam.
Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono ambaye hivi karibuni
alinusurika kifo akidaiwa kulishwa sumu akiwa London, Uingereza
amesimulia jinsi tukio hilo lilivyomkuta.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Mkono alisema endapo uchunguzi wa suala
hilo utakamilika na kuthibitisha kwamba alilishwa sumu, atapambana na
wahusika kwa kuwa wamehatarisha maisha yake.
Mkono ambaye
pia ni wakili maarufu nchini, alitoa kauli hizo jijini hapa jana,
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuelezea mwenendo wa afya
yake.
Alidai kwamba, lengo la kumlisha sumu ni kuharibu figo zake ndani ya saa 72 wakati alipokuwa katika ziara ya nchini humo.
“Niko
vizuri na afya njema… kama kuna mtu anawinda jimbo langu mwambieni
ameshindwa na wananchi wangu nawaeleza kuwa niko salama wasiwe na hofu.
Ninataka kujua nani kanilisha sumu na kwa nini?” alisema Mkono.
Akisimulia
tukio hilo alisema, Novemba 11 akiwa miongoni mwa wajumbe 11 wa Kamati
ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, walisafiri kutoka Dar es Salaam
kwenda Uingereza akiwa salama salimini.
Aliwataja baadhi ya
wabunge walioambatana nao kuwa ni William Ngeleja (Mwenyekiti wa kamati
hiyo), Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika.
“Tukiwa
uwanja wa ndege nilipokea ujumbe mfupi wa maandishi (hakutaka kuuweka
wazi kwa sababu upelelezi haujakamilika), ukinitahadharisha kuwa makini,
ujumbe ule ulinishtua kwa kweli.”
“Niliwaonyesha wenzangu
niliokuwa nao na pale tulikunywa chai kabla ya kuondoka na tulipofika
kule mimi nilikaa hoteli yangu na wenzangu wakakaa ya kwao,” alisema.
Huku
akisimama na kunyoosha mikono kuonyesha yuko vizuri, Mkono alisema siku
iliyofuata ratiba iliwataka kuhudhuria Bunge la Uingereza.
“Niliamka
na kwenda Ubalozi wetu na kwa kuwa tulitakiwa kufika bungeni saa 5.00
asubuhi, niliwahi na wenzangu na walipokuja tuliungana… tulipokuwa ndani
katika Bunge la Uingereza, ghafla nilianza kujisikia vibaya hali
iliyonisababisha nipoteze fahamu kwa saa sita. “Lakini kabla ya kupoteza
fahamu niliwaeleza wanipeleke nyumbani (Tanzania), wenzangu wanasema
nilikuwa napiga kelele, nirudisheni hawa wanataka kuniua,” alisema Mkono
kwa sauti ya chini na kuongeza:
“Hapa nasimuliwa sasa kuwa
walinipeleka hospitalini na waliponifikisha madaktari wa pale waliamua
kuwasiliana kwanza na Daktari wangu, (Lusangulila Kapitain) ili kujua
kama wakati natoka Tanzania nilikuwa na tatizo.”
Alisema,
“Kapitain baada ya kuelezwa hali niliyonayo naye aliwaeleza kuwa huyo
(Mkono) atakuwa amelishwa sumu kwani wakati anatoka huku alikuwa salama
kabisa na akawaomba wanipatie dawa ambazo zilinirejesha katika hali
yangu ya kawaida kuanzia saa 12 hadi saa moja jioni.”
Mkono
alisema kitu ambacho hadi sasa hajakielewa na anapenda kukifahamu ni kwa
nini na malengo yapi akisema kama ni sakata la escrow lilikuwa wazi
bila kificho.
“Serikali ilikuwa ni mteja wangu katika kesi
kati ya Tanesco na IPTL… nikiwa bungeni siwezi kuongea hadi nipate
kibali cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutokana na maadili ya kazi
zetu, lakini uchunguzi ukibainika kwamba nililishwa sumu kwa sababu hiyo
nitaweka kando maadili ya kazi.”MWANANCHI
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena