AFYA za wakazi wa Jiji la Dar es Salaam
ziko hatarini kutokana na kudaiwa kula mayai ya kuku mabovu ambayo
yameingizwa nchini kinyemela na baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa ni
wawekezaji. Akizungumza na Tanzania Daima
jijini jana kwa masharti ya kutotajwa jina, mmoja wa madaktari wa
mifugo, alisema mayai hayo yamekuwa yakisambazwa mitaani kwa wingi kila
siku.
Alisema kama Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi
itashindwa kuwadhibiti wakezaji hao wasio waminifu wakaingiza mayai hayo
kinyume na sheria, basi serikali ijiandae kwa fedha nyingi kwa ajili ya
kuja kutibu magojwa yatakayotokana na ulaji wa mayai hayo.
“Nimejaribu
kupita katika maeneo yanakouzwa kwa kweli hali ni mbaya, kwani ni uozo
mtupu kiasi kwamba hata wakazi wanaoishi karibu na maduka hayo kiafya
wako mashakani na wanashangaa kuona mayai hayo yakiachwa bila
kudhibitiwa,” alisema daktari huyo.
Alizitaja majina baadhi ya
kampuni (zinahifadhiwa kwa sasa), zinazohusika na uingizaji wa mayai
hayo, huku zikidaiwa pia kuwa na mashine za kutengenezea mayai bandia
katika mashamba yao yaliyoko wilayani Mkuranga mkoani Pwani.
Wakati
hali ikiwa hivyo, Tanzania Daima imepata waraka kutoka kwa Ofisa
Mfawidhi (ZVC), Kanda ya Mashariki Temeke, ukiomba kupatiwa askari kwa
ajili ya zoezi la ukamataji wa mayai na nyama za kuku zinazoingizwa
nchini kinyume na sheria, kanuni na taratibu.
Waraka huo umesainiwa na mtu aliyetambulika kwa jina la Dk. Mapouusa A.R.M, kwa niaba ya Ofisa Mfawidhi ZVC wa kanda hiyo.
Waraka
huo kumb. Na. VEZ/D6/01/51 ulioandikwa Oktoba 28 mwaka huu, ulikuwa
ukiomba kupatiwa askari wanne kwa ajili ya zoezi la kukamata mayai na
nyama za kuku zinazoingizwa kutoka nje ya nchi kinyume cha sheria na
taratibu za nchi.
Sehemu ya waraka huo, unaonesha kuwa kazi hiyo
ya kukamata chakula hicho itakuwa ya mwezi mmoja, ikianzia Oktoba 28
hadi Novemba 28 mwaka huu.
Dk. Mapoussa, alibainisha kufanya
hivyo kunatokana na ukweli kwamba, uingizaji huo wa mayai na nyama ni
kinyume cha sheria ya magonjwa ya mifugo ya 2003 na kanuni ya mwaka
2007.
“Tunapaswa kuyakamata na kuwapeleka mahakamani wahusika ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema Mapoussa.
Hata
hivyo, Tanzania Daima, limebaini mayai hayo bado yanaendelea kuingizwa
na kusambazwa katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kwa wingi. Tanzania Daima.
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena