Maisha ya Kibiti sasa ni shwari hamna shari na tayari bei za vitu kama viwanja na huduma kama za nyumba za kulala wageni (gesti) zimeanza kupanda bei upya kama ilivyokuwa awali.
Taarifa hiyo yenye kuashiria dalili njema za kurejea kwa amani na utulivu kwa wakazi wa wilaya hiyo iliyopo mkoani Pwani, ilithibitishwa na jeshi la Polisi kupitia kwa msemaji wake, Barnabas Mwakalukwa.
Hivi karibuni, wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji mkoani Pwani, zilielekea kuwa tishio jipya la ulinzi na usalama nchini baada ya kuwapo kwa taarifa za mauaji ya kila mara ya watu wasio na hatia, wakiwamo viongozi wa vijiji, vitongoji, polisi na hata raia wa kawaida. Jumla ya watu zaidi ya 30 waliripotiwa kuuawa katika matukio tofauti ya kipindi cha takribani mwaka mmoja tu uliopita.
Tishio hilo la usalama Kibiti lilisababisha baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo kukimbia na kwenda kuishi maeneo mengine nchini na pia, taarifa zilisambaa hata kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kuhusiana na athari za kiuchumi zilizosababisha bei za viwanja, mashamba, nyumba na hata huduma kama za gesti kushuka kwa kiasi kikubwa.
Mwakalukwa amesema hali ya Kibiti sasa ingali ikitengemaa kila uchao kutokana na jitihada kubwa zilizofanyika katika kudhibiti uhalifu na kwamba sasa, hakuna tena tishio na hata bidhaa zimeanza kupanda tena bei kuashiria kurejea kwa hali ya amani na utulivu.
Hata hivyo, Mwakalukwa amesema kuwa kuwepo kwa ushirikiano kati ya Wananchi na Jeshi la polisi na kuanzishwa kwa kanda maalumu inayohusisha wilaya hizo tatu na Mafia kumeimarisha doria kwa kiasi kikubwa na matunda yake ni kurejea kwa hali ya usalama.
“Kwa mfano, sasa Kibiti iliyokuwa na sifa mbaya inaondoka. Eneo lolote ambalo lilikuwa na uhalifu na serikali ikaimarisha usalama, mfano Tarime, ikiwa na kanda maalumu, hali huimarika. Sasa kumetulia, si huko tu, hata Amboni mkoani Tanga kwenye mapango, Arusha…kote tumeimarisha ulinzi baada ya kujua chanzo cha uhalifu huo ni nini”, amesema Mwakalukwa kwenye mahojiano yake na Gazeti la Nipashe.
Imeelezwa kuwa katika baadhi ya maeneo ambako bei ya nyumba za kulala Wageni (Gesti) ilishuka kwa kukosa wateja wa uhakika, kwa sasa iko katika kiwango cha kuanzia Sh. 15,000 hadi 40,000 kulingana na eneo na ubora wa gesti husika.
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena