SHEIKH Mohamed Ameenullah Kashmiri si jina maarufu miongoni mwa Watanzania. Lakini, bila shaka, Kanali Mstaafu, Ameen Kashmiri (79), ni miongoni mwa Watanzania waliolifanyia Taifa letu makubwa.
Wakati Taifa letu lilipoamua kuanzisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) baada ya maasi ya Jeshi ya Januari 1964, ni Kashmiri pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Majeshi, Mirisho Sarakikya, ndiyo waliosimama imara kuhakikisha Jeshi linakuwa imara.
Akiwa Mkuu wa Lojistiki na Uhandisi Jeshini, Kashmiri ndiye aliyeanzisha na kusimamia ajira kwa wanajeshi wapya hadi kufikia idadi iliyotakiwa wakati huo.
Watu wengi hawafahamu lakini baada ya maasi yale, Jeshi la Tanzania halikuwa hata na wanajeshi 1,000. Ni Kashmiri ndiye aliyepewa kazi ya kuhakikisha anaajiri askari 2,000 kila baada ya miezi sita ili kufikisha idadi ya askari waliotakiwa.
Ni bwana huyuhuyu ndiye aliyesimamia ujenzi wa kambi zote muhimu za kijeshi zilizopo hapa nchini. Ni askari huyuhuyu aliyekuwa mbele katika kutaka Tanzania iwe na Chuo Kikuu cha Kijeshi chenye hadhi ya Kimataifa ambacho leo ndiyo kile Chuo cha Jeshi cha Monduli (TMA).
Kama JWTZ baadaye iliamua kufunza wananchi wa nchi za Kusini mwa Afrika waliotaka kukomboa nchi zao, Kashmiri naye alikuwa nguzo katika hilo.
Yeye ndiye aliyetakiwa, kwa mujibu wa nafasi yake hiyo ya jeshini, kujua wapigania uhuru hao wangeishi wapi, wangepata silaha wapi, kiasi gani na wangepata mahali pa kula na mavazi.
Kazi yote hii akifanya mtu ambaye alistaafu jeshini akiwa na cheo cha Kanali pekee!
Kanali Mstaafu, Ameen Kashmiri, ndiye Mtanzania wa Kwanza kupata daraja la Uafisa katika JWTZ. Kwa mujibu wa rekodi zilizopo, yeye ndiye raia wa kwanza wa Afrika Mashariki kupata cheo hicho.
Leo hii, Sarakikya ni Luteni Jenerali. David Musuguri naye ni Jenerali kamili. Akina Robert Mbona, George Waitara, Davis Mwamunyange na wengine waliokuja nyuma yake wote ni majenerali.
Lakini Ameen Kashmiri bado ana cheo cha Kanali ! Hii haikubaliki.
Katika nchi yetu ambayo tunajaribu kujenga mifano inayotakiwa kwa watu kupenda kuwajibika, ni aibu kwetu kuamua kuwadharau watu wa aina ya Kashmiri.
Ni kweli kwamba Kashmiri aliamua mwenyewe kuacha jeshi kwa hiari yake katika miaka ya 1970. Ni Mwalimu Nyerere ndiye aliyeamua kumwondoa jeshini na kwenda kumpa kazi ya kuanzisha Shirika la Taifa la Maendeleo ya Sukari.
Hata hivyo, ni Mwalimu huyohuyo ndiye pia aliyemwondoa Sarakikya jeshini wakati huo na kwenda kumpa Uwaziri katika Wizara ya Vijana.
Kama ilivyokuwa kwa Kashmiri, Sarakikya hakuagwa rasmi na Jeshi kama ilivyo taratibu. Ni Rais Benjamin Mkapa ndiye aliyekuja kurekebisha kasoro hii kwa kumpa Sarakikya hadhi yake na leo amestaafishwa jeshini kwa heshima.
Sijui ni kwanini serikali iliona ni muhimu kurejesha heshima kwa Sarakikya na kumwacha Kashmiri. Moyo wangu unaniambia kwamba inawezekana ilikuwa ni kupitiwa tu. Lakini, hata hivyo, ukweli unabaki palepale kwamba Kashmiri hajastaafishwa rasmi na kupewa heshima na wadhifa aliostahili.
Kwa sababu ya nidhamu ya kijeshi aliokua kwayo, Kashmiri anaweza kuamua kukaa kimya na asiseme au kulalamika kuhusu chochote lakini ukweli bado utabaki palepale; kwamba hajatendewa haki.
Kibinadamu tu, Kashmiri alikuwa na tabia ya kipekee kuhusu ufisadi. Sidhani kama kuna kiongozi wa Jeshi atakuja kupata fursa ya kuiba au kufanya ufisadi kama alioipata askari huyu.
Kumbuka, huyu ndiye mtu aliyepewa jukumu la kutengeneza jeshi kutoka mwanzo kabisa. Kununua sare na silaha, kujenga kambi na kuajiri askari aliotaka.
Kama angekuwa na roho ya baadhi ya askari wetu wanaonunua helikopta na mavazi yenye utata, sidhani kama leo tungekuwa na jeshi tulilonalo. Au kama angeamua kuajiri watu wenye asili kama yak wake pekee sijui pia ingekuwaje.
Jambo la msingi kuliko yote hapa ni ukweli kwamba kutowajali na kuwaheshimu watu kama akina Kashmiri kunajenga kada ya watumishi wa umma wasioona umuhimu wa uadilifu.
Kuna faida gani ya kuwa mwadilifu wakati mwisho wa utumishi wako hutopata lolote? Unaweza ukakosa fedha lakini kwa watu kama akina Kashmiri, fedha si lolote kwao zaidi ya heshima.
Kama Mkapa alifanya kama alivyofanya kwa Sarakikya, ni wazi kwamba Rais Jakaya Kikwete anaweza kufuata nyayo kwa kumtendea haki Kashmiri.
Askari huyu sasa ana umri wa miaka 79. Mungu anajua mwisho wa uhai wa mtu lakini hatuna uhakika sana kama Amiri Jeshi Mkuu ajaye naye atakuwa na fursa ya kuishi muda mrefu na Kashmiri kama aliyonayo Kikwete.
Kama tumeweza, hatimaye, kuwatuza akina Muhidin Mwalimu Gurumo, Bi Kidude na wengineo baada ya miaka 50 ya Uhuru, ni wazi kwamba fursa ipo kwa Afande Kashmiri kama tukitaka.
Mpira huu sasa uko kwa Rais Kikwete. Anaweza kuamua anavyotaka.
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena