SURA YA TANO MWANZO WA MAPAMBANO Yule kijana alipoangalia usoni mwa Willy mara moja alijua huyu mtu hakuwa na mzaha. Hivi akiwa mikono yake ikiwa imeshika kwenye usukani wa gari na mwili wake mzima akiwa amekauka kama mti uliopigwa radi alimjibu Willy, "Tafadhali niache, mimi ni Robert Sikawa." "Nitajuaje kama wewe ni Robert Sikawa?" Aliuliza Willy hali uso wake ukiwa bado mzito. "Maana wewe ni Willy Gamba, kiongozi wa 'Kikosi cha Kisasi' kwa kifupi KK, ambacho makao yake makuu yako Lusaka..." "Oke, siku nyingine ujiangalie unaweza kupatwa na matatizo bure. Vile vile unapofuata mtu, inabidi ufunye vizuri kuliko ulivyofanya hasa unapofuata mtu mwenye ujuzi katika mchezo wetu huu," Willy alimweleza Robert huku akiwa ameisharudisha bastola yake na tayari uso wake ukiwa unaonyesha urafiki, na vile vile akiwa amempa nafasi Robert kutoka ndani ya gari na kusimama wote nje ya gari la Robert. "Ama kweli ndiyo sababu umechaguliwa kuongoza 'KK'", alieleza Sikawa. "Mimi nilishangaa nilipoambiwa inabidi nichukue amri toka kwako tangu wakati utakapofika, maana mimi mwenyewe najiamini sana. Hivi sikuona kwanini tena aje mtu nichukue amri kutoka kwake badala yake yeye kuchukua amri kwangu. Hivi nilikuwa uwanja wa ndege kukupokea na vile vile kukujaribu una ujuzi kiasi gani. Jaribio langu dogo hili linanidhihirishia kuwa kweli wewe ni mjuzi katika mchezo wetu huu, maana mimi ninapomfuata mtu huwa ni vigumu sana kunigundua. Kule kwetu Lusaka katika idara yetu huwa wananiita 'Nyoka wa kijani' sababu hii hii. Hivyo bosi wangu ninakukaribisha mjini Kinshasa," alieleza Robert. "Ulijuaje kama ninakuja?". "Chifu wako alinitumia habari jana pamoja na picha yako ambayo ingeweza kunifanya nikutambue". "Picha, bado unayo?" "Ndiyo". "Tafadhali itatue sasa hivi. Si vizuri kiusalama mpelelezi kutembea na picha ya mpelelezi mwenziwe, kitu anachobidi kufanya ni kuhakikisha kuwa anaangalia picha mara moja na kuiweka sura yake ndani ya kichwa chake kisha anaitatua hiyo picha hapo hapo", Willy alimshauri. "Vizuri", alijibu Robert huku akitoa picha ya Willy ndani ya mfuko wa koti lake na kuwasha kibiriti na kuichoma hiyo picha pale pale. "Utafikia hoteli gani?", aliuliza Robert. "Nafikiri Memling Hoteli itanifaa". "Yaa, hoteli hiyo ni tulivu itakufaa. Sijui tuonane muda gani ili niweze kukupa habari nilizonazo kikamilifu?" "Tuonane jioni saa mbili hivi na kuendelea, maana sasa hivi itabidi nipumzike kidogo". "Sawa basi tuonane Vatcan Klabu huko Matonge saa hizo. "Sijui unaifahamu?". "Hamna taabu, naifahamu." Alijibu Willy. "Oke basi tuonane huko saa hizi". "Oke Robert, asante sana, tutaonana", alijibu Willy huku akiondoka na kuelekea kwenye gari lake. Robert alibaki amesimama pale penye gari lake akimwangalia Willy kwa shauku. Willy alipanda gari lake akalitia moto na kuondoka kuelekea Memling Hoteli. Alipofika Memling Hoteli alikuta kuna nafasi. "Karibu," alikaribishwa na mfanyakazi mmoja msichana aliyemkuta hapo kwenye mapokezi ya hoteli hii. "Naweza kupata chumba?", aliuliza Willy. "Bila shaka, unakaribishwa kwa dhati. Una mzigo?". "Nina mkoba mmoja uko ndani ya gari". Yule msichana alimwita mchukuzi ili akachukue ule mzigo. "Acha tu nitakwenda kuuchukua mwenyewe", Willy alieleza huku akienda kwenye gari. "Tunavyo vyumba wazi kwenye ghorofa ya pili, tatu na tano, sijui ungependelea ghorofa ipi?", yule msichana alimuuliza Willy, aliporudi na mkoba wake. "Wewe unafikiri ghorofa ipi ni nzuri?". "Hii inategemea na uchaguzi wa kila mtu binafsi". "Uchaguzi wako ndiyo utakuwa wangu", Willy alimwambia yule msichana huku akimtolea bonge la tabasamu. "Chumba nambari 240 kwenye ghorofa ya pili kitakufaa," yule msichana alimjibu Willy naye akitoa tabasamu. "Asante sana, hicho hicho chumba kitanifaa." Willy alijaza fomu kama ilivyo desturi, kisha akapelekwa na askari wa hoteli mpaka chumbani kwake. Chumba alichokuwa amepewa kilikuwa kwenye sehemu nzuri sana na chumba chenyewe kilikuwa kimepangwa na kuwekwa vyombo vizuri saana. Askari alipokuwa amekwishaondoka, Willy alianza kukipekua kile chumba, na kukikuta salama. Alipokwisha kufanya hivyo alifungua mkoba wake na kuanza kupanga vitu vyake. Alipomaliza alienda akaoga kisha akatelemka chini kwenda kupata chakula cha mchana. Alipomaliza kula alipita pale kwa yule msichana wa mapokezi. "Haya kisura bado unaendelea na kazi!" "Ndiyo, heri nyinyi wenye bahati ya kutembea nchi mbali mbali na kustarehe. Sijui lini mimi nitapata nafasi kama hii!", alijibu yule msichana kwa masikitiko. "Siku ipo itafika usiwe na shaka, ya Mungu mengi sana. Fanya kazi yako kwa bidii, tumia mapato yako kwa mpango, huku ukiweka akiba kwa ajili ya safari kama hii, ukifanya hivi nina imani siku moja ndoto zako za kutembea nchi mbali mbali zitakuja kweli," alimshauri Willy. "Ndivyo wewe ulivyofanya?" Yule msichana alimuuliza. "Lazima, hamna dawa nyingine," alijibu Willy huku akitoa pesa ili kubadilisha kutoka kwenye dola ili apate Zaire. Msichana yule alipombadilishia pesa zake, Willy alitoa Zaire kumi akampatia yule msichana. "Za nini?" Yule msichana alimuuliza. "Asante yako kwa kunipokea vizuri. Wewe unaitwa nani?" "Naitwa Mwadi," yule msichana alisema huku akionekana kuwa na mshangao. "Jina zuri 'Mwadi', haya asnate Mwadi tutaonana jioni". "Jioni nitakuwa nimeishamaliza kazi, namaliza saa tisa mchana, hivi nitakuwa nyumbani." "Basi tutaonana kesho," "Haya asante," alijibu Mwadi, huku akimwangalia Willy kwa macho malegevu. Willy alipoondoka alimwacha yule msichana moyo wake unapiga haraka haraka. Maishani mwake alikuwa ameishaona wavulana wengi sana, hasa ukitilia maanani kazi yake hii, lakini alikuwa hajaonana na mvulana mwenye kusisimua kama huyu. Pale pale alijawa na moyo wa kimapenzi juu ya Willy. Willy naye alienda chumbani kwake na kupumzika. Baada ya kuondoka nyumbani kwa Pierre, Jean aliendesha gari lake moja kwa moja mpaka kwake 'G.A.D'. Alikuta kazi ya kutengeneza magari inaendelea kama kawaida. Alikaguakagua kazi kisha akawaita faraghani wafanyakazi wake wawili ambao walikuwa wakisimamia kazi. Mmoja aliitwa Kabeya Mwabila na mwingine Charles Besaleti, mwenye asili ya Kibeligiji. "Jamani kuna kazi muhimu", aliwaeleza. "Tunatakiwa tuchunge kiwanja cha ndege na mahoteli yote kuhakikisha kuwa hakuna mgeni ambaye anaingia mjini hapa bila sisi kuwa na maelekezo yake. Mnaweza kuweka watu wengi mnavyoweza na kutumia kiasi chochote ili mradi jambo hili lishughulikiwe kikamilifu. Kufanyika lifanyike kwa siri kama kawaida kiasi cha kwamba Polisi au CND* haiwezi kututuhumu. Tumeelewana?". alimaliza Jean. "Tumeelewa, hilo hamna taabu, litafanyika kwa makini kabisa maana kila hoteli tunaye mtu kwenye orodha yetu ya mshahara ambaye kazi yake ni hiyo kila tuhitajipo maelezo," alijibu Charles. "Sitaki kusikia makosa, Kazi hii ifanyike kikamilifu kabisa, watu mnao, pesa zipo, ninachohitaji ni utekelezaji." Jean aliwatilia mkazo. "Usitie shaka, kazi itakwenda kama siku zote," Kabeya alimhakikishia na wote wawili wakatoka ndani ya ofisi ya Pierre tayati kufanya kazi. *CND* Idara ya Upelelezi ya Zaire. "Wewe shughulikia mahoteli na mimi nitashughulikia njia zote za kuingia Kinshasa, hasa uwanja wa ndege na kwenye kivuko cha kwenda Braville." Charles alimshauri mwenziwe. "Vizuri, mahoteli yote nitayashughulikia mimi na pale patakapokuwa lazima nitapashughulikia mwenyewe". "Oke, basi tulishughulikie mara moja". Kila mmoja aliondoka na kupita kwa vijana waliokuwa wanashughulikia magari, wakiitwa mmoja mmoja hapa na pale tayari kwenda kwenye shughuli hii maalumu ambayo kimsingi ndiyo ilikuwa kazi waliyoajiriwa. Haya mambo ya kutengeneza magari ilikuwa geresha tu, ili kuivuruga serikali isijue maovu yao. Ilikuwa yapata saa tisa kasoro robo wakati Kabeya ambaye alikuwa ofisini mwake huku akipiga simu mahotelini kwa wadukuzi wake alipofika Memling Hoteli kwenye orodha yake. "Hapo ni Memling Hoteli?" aliuliza. "Ndiyo". "Mwadi yupo?" Mwandi ndiye alikuwa kwenye orodha ya mshahara ya 'WP' hapa Memling Hoteli kutokana na habari alizokuwa akizitoa kuhusu wageni. Kwa vile alikuwa akilipwa vizuri kwa kutoa habari ambazo alifikiria hazina madhara, alikuwa anaona kama ni bahati kwa upande wake alipoambiwa na Kabeya kufanya hivyo kwa malipo hayo. "Ndiyo, yupo subiri", alijibiwa. Baada ya muda kidogo aliweza kuunganishwa na Mwadi. "Halo Mwadi hapa". "Ohoo Mwadi, Kabeya hapa habari yako?" Moyo wa Mwadi ulistuka kidogo kumsikia ni Kabeya, ingawaje alikuwa anajua habari alizokuwa anazitoa kwa Kabeya hazikuwa mbaya, lakini wakati mwingine alikuwa akiingiwa na wasiwasi hasa kwa vile sura ya Kabeya ilikuwa ikionyesha uovu mwingi sana. Kwa hivi alipopata simu mchana huu kutoka kwa Kabeya moyo wake ulishtuka sana, bila kuwa na sababu kamili. "Mzuri, habari yako na wewe?". "Mzuri tu". "Unasemaje, maana mimi namaliza kazi nataka kwenda kupumzika". "Nina kazi kidogo tu Mwadi, ile ya kila siku. Naomba unipe majina na maelezo ya wageni walioingia hotelini kwako toka jana hadi leo na vile vile endelea kunipa kwa siku hizi zitakazofuata. Malipo yako yatakuwa mara tatu ya kawaida. Tafadhali maelezo hayo yanahitaji kabla ya saa kumi leo. Yatakuja kuchukuliwa mahali pa kawaida. Sawa Mwadi?" Mwadi ambaye mara moja mawazo yake yalikwenda kwa kijana yule ambaye alikuwa amewasili mchana ule alisita kidogo kisha akasema. "Sawa Kabeya nitashughulikia". "Asante", alijibu Kabeya na kukata simu. Mwadi alibaki huku akiwa na wasiwasi, na alikuwa hajui kwa nini roho yake ilikuwa haipendi kufikiria juu ya kutoa maelezo ya huyu kijana Willy Chitalu kwa Kabeya. "Sijui ni kwa sababu nimempenda?" alijiuliza. Mawazo mengine yalimjia yakiwa yanamshauri kuwa maelezo haya yalikuwa yakitakiwa kwa ubaya ndiyo sababu walikuwa wako tayari kumlipa mara tatu ya kawaida. Hata hivyo moyo wake nao ulikuwa na wasiwasi na Willy maana kijana huyu alimsisimua sana. Mwishoni aliamua kuwa afadhali atengeneze orodha na kumpelekea Kabeya bila ya kina la Willy, kusudi kama maelezo haya yatakuwa kwa ubaya, ubaya huu usije ukamdhuru kijana huyu ambaye moyo wake ulikuwa umempenda bila kijana mwenyewe kujua. "Afadhali mimi nipate matatizo kuliko yule kijana," alijisemea. Ilikuwa saa tatu wakati Willy alipofika Vatcan Klabu. Alikuta magari yamejaa kiasi cha yeye kukosa maegesho. Hivi aliondoka na kwenda kuegesha gari lake kwenye mtaa wa Kasavubu. Vatcan Klabu ni Klabu nzuri sana. Watu wenye heshima zao hufika hapa ili kustarehe. Hamna fujo na kila mtu ambaye anafika hapa inabidi kujiheshimu. Hivi watu wa madaraka Serikalini, makampuni, watu tajiri na mabalozi mara nyingi ndiyo hufika hapa ili kustarehe. Kwa sababu Robert alikuwa akipewa heshima za Kibalozi, mara kwa mara alikuwa akifika kustarehe katika klabu hii ambayo ndiyo ya hali yake. Ingawaje Kinshasa ni mji unaojulikana Ulimwengu mzima kwa kuwa na bendi nyingi zenye ujuzi wa hali ya juu katika mambo ya muziki, lakini Vatcan Klabu ni Klabu kubwa ambayo haina bendi bali kuna 'disco'. Baada ya kuegesha gari lake, Willy alienda moja kwa moja mpaka kwenye lango la ua wa Klabu hii ambapo alifunguliwa na kukaribishwa na askari aliyekuwa pale. Alipita na kwenda mpaka kwenye mlango wa klabu ambao ulifunguliwa na mtu mwingine na kukaribishwa ndani. Ndani ya Vatcan Klabu mna nafasi kubwa sana. Wakati unapoingia ndani ya klabu karibu na mlango kuna vyumba vitatu vitatu kila upande. Mbele ya vyumba hivi kuna uwanja wa kuchezea dansi huku ukiwa umezungukwa na sehemu nyingi za kukaa na mbele yake ndipo kuna kaunta ya klabu hii. Hivi Willy alipoingia alikuta watu wameisha jaa alipita akaangalia chumba hadi chumba bila kumuona robert, alipotokea kwenye uwanja wa muziki ambao kwa wakati huo ulikuwa hauna mtu ndipo alipomuona Robert kushooto kwake akiwa amekaa na kijana mwingine. Kwa vile alikuwa hana haja ya kuonana na mtu mwingine ila Robert alikata shauri kwenda kulia kwake ambapo alipata meza iliyokuwa haina kitu na kukaa. Robert alikuwa amemuona alijitafadhalisha kwa kijana aliyekuwa amekaa naye na kuhamia mezani kwa Willy. "Habari za saa hizi?" Robert alimpa Willy hali. "Safi tu, naona umeisha wahi kabisa kabisa," alimtania Willy. "Ee bwana, chelewa chelewa mbaya," alijibu Robert kimatani vile vile. "Robert alimwita mfanyakazi na kumwagiza vinywaji. Yeye alikuwa amehama na kinywaji chake. "Utakunywa nini Willy?". "Anipe Dimple kubwa na tonic soda." "Umesikia, kalete haraka, mimi niongezee Martel", Robert alimsisitiza mfanyakazi. "Kabla sijaanza mambo mengi, nimepata habari kutoka Lusaka kwa Chifu, ameniambia nikueleze kuwa Petit Ozu na Mike Kofi watawasili hapa kesho mchana na ndege ya shirika la ndege la Nigeria, ambayo itatua mjini hapa saa nane kamili. Hivi ndizo habari nilizopata." "Asante sana, nitawashughulikia watakapofika." alijibu Willy huku akipokea kinywaji, "Sasa tuendelee unipe hata kama ni kwa muhtasari tu mambo yalivyo hapa." Robert alisafisha koo kwa kohozi ili apate kueleza vizuri. "Mimi nimefika hapa mjini Kinshasa toka mwisho wa mwaka jana. Nilijaribu sana kuchunguza kifo cha Meja Komba lakini bila mafanikio. Nimeweza kuwa na uhusiano na afisa mmoja wa C.N.D ambayo ndiyo idara ya upelelezi ya hapa, ili niweze kupata habari zingine kutokana na upelelezi waliokuwa wameufanya, lakini na wao vile vile hawakuweza kufika popote. Jambo hili liliweza kunifanya nihisi mambo mawili, aidha Komba alikuwa ameuawa kwa mpango ambao Serikali iliujuwa kikamilifu au alikuwa ameuawa na kikundi cha kijasusi ambacho ni chenye ujuzi wa hali ya juu. Hili jambo la kwanza nililitilia wasiwasi maana baada ya kufanya upelelezi sana ilionekana uliokuwa umefanywa na Serikali ya Zaire ulikuwa umefanywa kwa dhati na kiukweli. Hivi nilibaki na jambo la pili ambalo nimekuwa nalifanyia upelelezi bila kufika popote hadi hapa majuzi ndugu Mongo alipouawa. Suala hili la kuwepo kwa kikundi cha ujasusi kinachoendesha uovu limeweza kuthibitika kwangu kutokana na mauaji haya ya juzi. Tatizo lililopo hapa Kinshasa ndugu Willy ni kwamba, nchi hii ina watu wa nje wengi na inafanya biashara na nchi nyingi sana hata Afrika ya Kusini na Rhodesia. Hivi ni rahisi sana kwa majasusi wa kutoka nchi hizo kuweza kuingia nchini hapa na kufanya uovu kama huo. Kwa mfano katika upelelezi wangu nimekuta kuwa kila mwaka Zaire inapata bidhaa toka Afrika Kusini zenye zaidi ya thamani ya R40m. Vitu hivi hutumwa kupitia Rhodesia na Zambia kwa Reli na kwa bahari mpaka Matadi. Lakini vile vile bidhaa nyingine inaingia Zaire kwa njia ya barabara kwa kupitia Rhodesia na Zambia. Kwa mfano hivi karibuni kumekuwa na mkataba kati ya Zaire na Rhodesia ambapo malori makubwa kiasi cha mia mbili yanaingia Zaire kutoka Rhodesia kila mwezi. Mia moja na ishirini ya malori hayo hubeba makaa ya mawe na yaliyobaki hubeba mahindi. Kutokana na mipango kama hii ni rahisi sana kwa majasusi ya Afrika Kusini na Rhodesia kuingia mjini hapa wakiwa aidha kama madereva wa magari haya au makarani. Vile vile utakuta kuwa kampuni za Afrika Kusini za biashara ziko na wakala wao hapa mjini Kinshasa. Kwa mfano Zaire ina mpango wa kupeleka bidhaa yake Japan kwa kupitia Afrika Kusini, na mkataba wa tani 125,000 za shaba ziendazo huko Japan kwa mwaka ulitiwa saini ya kusafirisha tani hizo kupitia kampuni moja iitwayo Grindrod Cots Stevedoring iliyoko mjini East London, Afrika Kusini. Kampuni hii ina wakala wake mjini hapa. Kutokana na ukweli wa mambo haya ulivyo ni wazi kuwa, ni rahisi sana kuwa na ukanda wa kijasusi wa Afrika Kusini ukifanyakazi yake hapa unapoona ya kuwa watu wanaouawa ni wale wenye uhusiano na wapigania uhuru wa Kusini mwa Afrika. Kutokana na hali hii mimi ningeshauri tuanze upelelezi mkali kwa watu wa makapuni haya yenye asili ya Afrika Kusini", alimalizia Robert. Willy ambaye alikuwa amesikiliza maneno yote haya kwa makini alimuuliza, "Marehemu Mongo alikuwa amefikia hoteli gani?" "Intercontinental hoteli", Robert alijibu. "Uliwahi kukagua vyombo vyake uliposikia ameuawa?". "Ndiyo, nilifika pale nikiwa pamoja na ofsa huyu wa C.N.D. Kusema kweli tulikuta chumba kile kimepekuliwa sana ingawaje kwa ustadi ambao mtu wa kawaida hawezi kugundua. Hatujui mtu aliyekuwa amekipekua alitaka nini au alichukua nini sababu hatukuona kitu cha maana kilichochukuliwa. Vitu vyake vingi hata zile karatasi za maelezo ya mkutano wa Libreville tulizikuta. C.N.D wamejaribu kupata alama za vidole bila mafanikio. Hii ina maana kuwa walitumia mifuko ya mikono 'gloves', Baadaye siku ile nilifanya upelelezi wangu kwa watu kadhaa na pale Intercontinental ambao walikuwepo tokea Ndugu Mongo anawasili pale kama waliwahi kuona kitu chochote cha kutilia mashaka lakini hawakunipa jambo lolote la maana. "Alikuwa akilala chumba namba ngapi?", Willy aliuliza. "Nambari 501". "Hili gari marehemu alikuwa amepewa na nani?". "Lilikuwa la Wizara ya Mambo ya Nchi za nje". "Alikuwa akiendesha mwenyewe?". "Wakati alipopatwa na ajali alikuwa mwenyewe". "Jaribu kupeleleza ni wakati gani alipewa hilo gari. Na kabla ya kupewa hilo gari lilikuwa wapi. Ni mahala gani alipokuwa ameliegesha, na kama kuna mtu maalumu aliyelishughulikia gari hilo kabla marehemu hajapewa. Kwani alikuwa na muda gani Kinshasa tangu kufika kwake hadi kuuawa?". "Yeye aliwasili hapa saa nne za usiku, kesho yake saa tano ndipo alipopatwa na ajali hii," Willy alifikiri sana kisha akasema. "Vizuri Robert, nitaenda kuyafikiria maelezo yote uliyonipa usiku huu na uamzi wangu nitakueleza kesho nini tufanye. Umekuwa ukifanyakazi na maelezo yako ni ya kufaa sana. Mazishi yatakuwa kesho saa ngapi?". "Saa nne asubuhi, na atazikwa kitaifa", Robert alijibu. "Mimi nitahudhuria mazishi". "Na mimi nitakuwepo", alijibu Robert. "Kwa hiyo tuta...", Willy alikatwa kauli na jamaa mmoja aliyefika kwenye meza yao akiwa ameandamana na msichana mmoja. "Hallo Robert, habari za leo?" "Oho Kalenga, habari zenu, karibu bibie", Robert aliwakaribisha hawa watu. "Asante asante," alijibu Kalenga huku akikaa. "Willy onana na Bwana na Bibi Kalenga Mbizi. Bwana Kalenga ni Meneja Maslahi katika kampuni ya Fiat, yeye ndiye aliyenifanyia mpango wa kununua gari yangu ya Fiat 132 GLS. Na huyu ni ndugu willy Chitalu kutoka Lusaka, yeye ni mfanyabiashara. Ni wakala wa makampuni ya nchi za nje katika Zambia", Robert aliwafahamisha. "Vizuri kuonana". "Vizuri kuonana", walijibishana. Pombe ziliagizwa na muziki ulianza kuwa moto moto, hivi kundi hili likageuka kutoka mazungumzo waliyokuwa nayo na kuwa kundi la starehe, maana saa hizi watu wa kila aina wliojuana na Robert walipoingia walienda kukaa kwenye meza hiyo hiyo. Asubuhi yake Willy alipoamka alikuwa mchovu sana, maana usiku ule alikunywa pombe za kutosha, kwani walikaa Vatcan mpaka saa saba za usiku huku wakinywa na kucheza dansi. Alipoangalia saa yake alikuta ni saa moja unusu, basi aliamka na kuelekea maliwatoni. Baada ya kukoga, alinyoa ndevu, kisha akavaa vizuri kabisa na kuonekana mtu wa amani, tayari kamili kwa shughuli za siku hiyo. Kisha alitelemka chini ili kuwahi chemsha kinywa. Alipokuwa anapita pale mapokezi alimwona Mwadi tayari yuko kazini, hivi aliamua kumsabahi. "Hallo Mwadi, Sango nini?", alimsabahi kwa kilingala kiutani. Mwadi ambaye alikuwa akishughulika na kujaza rejesta ya wageni aliinua kichwa na kumwona Willy, alipomuona tu mwili wake ukasisimka. "Ohoo Willy malamu", alimjibu huku akiwa amemjengea tabasamu kubwa. Willy alirudisha tabasamu hilo na kuendelea zake kwenda kwenye chumba cha chakua. Baada ya kustafutahi, Willy alirudi chumbani mwake, akajitayarisha tayari kwa kwenda kwenye mazishi. Ilikuwa saa tatu kamili alipotoka hotelini kwake kuelekea mazishini. Alipopita pale mapokezi alimkuta Mwadi akiwa na shughuli nyingi hivi alienda akapanda gari lake na kuondoka. Robert alikuwa amemwambia kuwa mazishi yatafanyika kwenye makaburi yaliyoko mtaa wa 30 Juin. Alipofika kwenye makaburi haya alikuta watu wamejazana kibao. Alirudi nyuma na kuegesha gari lake kwenye maegesho ya jengo liitwalo INSS. Alipomaliza kufunga milango alirudi na kuja kungojea maiti pamoja na wananchi wengine. Kusema kweli mazishi haya yalikuwa yametayarishwa kitaifa. Kulikuwa na gwaride la askari wa jeshi la Zaire, wakiwa tayari kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu huyu ambaye alikuwa mwanamapinduzi imara wa Afrika. Ilipokaribia saa nne, watu wenye vyeo vikubwa wakiwa mawaziri, mabalozi na viongozi wengine wa serikali waliwasili. Saa nne kamili ndipo maiti ya marehemu ilipofika. na pale pale bendi ya jeshi ikaanza kupiga wimbo wa kimapinduzi ambao uliwafanya maelfu ya wananchi waliofika kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu wakitokwa na machozi. Mkuu wa majeshi ndiye aliongoza mazishi haya ambayo hayatasahaurika katika historia ya mjini Kinshasa. Uchungu huu uliwapata hawa wananchi wa kawaida mpaka wale watu wa vyeo vya juu waliohudhuria mazishi haya, ndiyo uchungu ule ule uliompata Willy. Kwani mtoto mmoja aliyekuwa amesimama karibu na Willy alimuuliza, "Mzee kama mtu huyu alikuwa anapendwa na watu wote hivi kwanini wamemuua", Willy alimwangalia mtoto huyu asiyezidi umri wa miaka nane akajibu, "Mtu hakosi adui, unaweza kupendwa na watu maelfu lakini ukachukiwa na mtu mmoja tu". "Kama ndio hivyo kwanini watu wengi hawa wasimpate mtu huyo na kumuua? Maana mama ameniambia asubuhi eti mtu aliyemuua hawamjui!" "Tutamtafuta tukimpata tutamuua vile vile", alijibu Willy huku akizidi kupandwa na uchungu." "Kweli, ukimpata ukamuua nitafurahi." Yule kijana alijibu. Mtoto huyu alimzidishia mawazo Willy hivi akaamua kutoka pale na wazo moja. Ampate huyu muuaji wa Mongo, amuue ili watoto wa Afrika waweze kufurahi na kuzidisha mapambano dhidi ya wapinga maendeleo. Kwa sababu watu walikuwa wengi sana aliona kuwa asingeweza kuona jambo lolote la maana hivi akaamua kurudi hotelini kwake ili akajitayarishe kwenda kuwapokea akina Ozu. Alipofika hotelini alimkuta Mwadi akiwa peke yake. "Hallo Willy, ulitoka saa ngapi? Maana sikukuona wakati ukitoka". "Wakati ninatoka ulikuwa na shughuli nyingi usingeweza kuniona", alijibu Willy huku kwa mara ya kwanza tangu amuone Mwadi alianza kutambua kuwa msichana huyu alikuwa na kitu fulani ambacho kilikuwa kinagusa moyo wake. Si kwamba Mwadi alikuwa msichana mzuri sana la hasha, alikuwa msichana mzuri kiasi cha kawaida tu, lakini kitu hiki alichokuwa nacho kilichokuwa kikigusa moyo wa Willy, kilimfanya Willy aamue kuwa karibu na msichana huyu ili aweze kukijua ni kitu gani hiki. "Ulishawahi kufika Kinshasa au hii ni mara yako ya kwanza?", Mwadi aliuliza. "Nilishawahi kufika ingawaje sikukaa sana". Alijibu Willy. "Ahaa..." Mwadi alionekana anataka kusema kitu, halafu akasita. "Leo unatoka saa ngapi?". Aliuliza Willy. Huku macho yake yakitoa mwanga wa kuonyesha furaha ya kuulizwa swali hili Mwadi alijibu, "Kama jana tu, nitaondoka saa tisa na kuingia tena kesho asubuhi saa moja". "Una muda mwingi sana wa kupumzika", alisema Willy halafu akatania, "Sijui nani anakusaidia kuusukuma muda wote huo?". "Aka, sina mtu maalumu anayenisaidia kuusukuma muda wangu. Hata wewe unaweza kusaidia kuusukuma ukitaka!" Alijibu Mwadi kwa sauti ya utani. Willy aliona hapa hapa ndiyo ulikuwa muda wa kuanzisha urafiki na huyu msichana. "Na kweli kabisa, maana sina msichana wa kusaidia kuusukuma muda wangu hasa ukitilia maanani kuwa mimi niko mapumzikoni ingawaje na kazi". "Karibu basi nyumbani jioni, nitakupikia 'Maboke'. Umeisha kula maboke ya hapa Kinshasa?". Aliuliza Mwadi. "Kwanza sijui maboke ni nini", alijibu Willy. Mwadi aliangua kicheko kisha akasema, "Hii inaonyesha kuwa kweli bado hujaifahamu Kinshasa. Maboke ni chakula kinachopendwa na watu wote hapa mjini, ni samaki na nyama ambayo hupikwa ndani ya majani ya ndizi. Vipi utakuja?". "Nitakuja", alijibu Willy, "Sijui unakaa wapi?" "Ninakaa huko Bandalugwa mtaa wa Kimbondo nyumba nambari 79, utapajua?". "Usiwe na shaka nitakuja, nisubiri saa moja hivi jioni". "Haya asante, tutaonana saa hizo", alijibu Mwadi kwa moyo wa kuridhika sana, maana alikuwa ameweza kirahisi sana kumpata kijana huyu ambaye alikuwa akimsisimua sana.
Ilikuwa saa saba kamili, Willy alipoingia ndani ya baa ya uwanja wa ndege wa Ndjili wa mjini Kinshasa, tayari kuwapokea akina Ozu. Ndani ya baa mlijaa watu wengi waliokuwa wakisubiri wageni wao. Willy aliamua kwenda kwenye kaunta ambapo aliagiza kinywaji. Ilipotimia saa saba unusu Robert naye aliingia ndani ya baa hii na alipomuona Willy alimfuata moja kwa moja. "Vipi umeshafika huku?" Rbert alimuuliza Willy. "Bila shaka nimefika ndiyo sababu niko huku". Alijibu Willy kimatani. "Salama lakini?". "Salama tu". "Vipi ulifika kwenye mazishi?". "Ndiyo nilifika, lakini watu walikuwa wengi mno sikukaa sana". "Lo, kweli marehemu kazikwa kishujaa kweli kweli. maelfu ya wananchi wamehudhuria mazishi. Watu wamesema yalikuwa mazishi ya kihistoria." "Hata mimi sijawahi kuona mazishi kama haya", alijibu Willy. "Juu ya mambo yale uliyoniagiza jana. Marehemu alipewa gari lile asubuhi ya siku ile aliyouawa saa mbili hivi. Hili gari lilikuwa limetoka matengenezo siku hiyo hiyo." "Gereji gani?". Aliuliza Willy kwa sauti nzito. "Gereji moja iitwayo Papadimitriou, ambayo ni kati ya nyingi maarufu zinazotengeneza magari aina ya Peugeout hapa mjini Kinshasa". "Una maana gari alilokuwa anatumia marehemu ilikuwa aina ya Peugeout?". "Ndiyo ilikuwa Peugeout 504. Na inasemekana kuwa marehemu hakuwa ameliweka mahali popote kwa muda mrefu kiasi cha mtu kuweza kulifanyia mbinu za namna hiyo. Lakini ukifikiria teknolojia ilivyo kwa sasa hivi inaweza kumchukua mtu muda mfupi sana kutega bomu kwenye injini ya gari." "Hii gereji ni ya nani?". "Gereji hii ni ya Mpakistani mmoja tajiri sana aitwaye Papadimitrian. Ni mtu anayeheshimika sana hapa mjini, na ana mahusiano mazuri na Serikali, sababu magari mengi ya serikali yanatengenezwa kwake." "Ni mzaliwa wa wapi?". "Ni mzaliwa wa Pakistani, lakini ameingia hapa kwa kutokea Zambia ambako alikuwa akifanya biashara", Hata mimi nakumbuka kuwa alikuwa na duka kubwa sana la nguo mtaa wa Cairo mjini Lusaka. Yeye aliingia hapa mwaka 1968 na kabla ya kuwa na gereji hii alikuwa na duka kubwa la madawa huko Gombe mtaa wa Posta. Kwa ujumla ni mtu mwenye sifa nzuri na hana rekodi yoyote mbaya". "Sikuwa na maana kuwa anaweza kuwa na ubaya, ila tu nilitaka kuwa na uhakika na gereji hii ni ya namna gani." "Ni sawa kabisa kumtilia mashaka maana jambo hili lilipotokea hata mimi ilinibidi niwe na uhakika na gereji hii kabla sijaendelea popote." Mara walikatwa kauli na tangazo. "Tafadhali sikilizeni, tunawatangazia kuwasili kwa ndege ZC 883 ya Shirika la Ndege la Nigeria itokayo Logos na kupitia na kisha kuelekea Librevile na kisha kuelekea Brazaville. Abiria wote wanaoondoka na ndege hiyo wanaombwa kuelekea kwenye chumba cha kuondokea. Asanteni. "Hao wanaingia, je wewe unawafahamu?" aliuliza Robert. "Ndiyo, kwa picha. Wewe je?". "Mimi siwafahamu ila nilifikiri kuwa utakuwa unawafahamu ndiyo sababu nimekuwahi." Waliondoka na kuelekea sehemu ya kuagiza 'waving bay', watu walikuwa wamejazana sehemu hii. Willy na Robert walijipenyeza na kuiangalia ndege hii ya aina ya DC 8 ikishuka taratibu. Wakati ndege hii ya Shirika la Ndege la Nigeria ikitelemka, huko Limete kwenye gereji iitwayo 'Garage du Peuple' aliingia kijana mmoja wa kizungu ambaye alionekana kuwa na wasiwasi sana. "Bwana Pierre yupo?", aliuliza. "Ndiyo yupo. Nenda moja kwa moja ndani". Alimjibu kijana mmoja aliyekuwa mlangoni. Alipofika ndani ya maofisi ya gereji hii, alimwendea msichana mmoja aliyekuwa anapiga mashine na kumweleza. "Nataka kumwona Bwana Pierre." "Nenda chumba cha tatu toka hiki upande huu huu." Alijibiwa. Alipoingia hiki chumba alikuta kuna wasichana wawili ambao alihisi ni waandishi mahsusi wa Pierre. "Bwana Pierre yupo." Aliuliza bila hata kuwasabahi. "Yupo. Unamhitaji kwa jambo gani?". Aliulizwa na msichana mmojawapo. "Mwambie nimetumwa na wakala." "Yule msichana aliinua simu na alipokwisha kuzungumza na Pierre alimwambia apite ndani. "Karibu, lete habari," Pierre aliuliza upesi upesi kijana yule alipoingia. Bila kujibu kitu kijana yule alitoa karatasi ya teleksi na kumpa Pierre. Pierre alipoisoma sura yake ilibadilika akasema, "Haya asante kwa heri", Kwa maneno haya ya mkato yule kijana aliondoka. Pierre aliinua simu na kuanza kupiga yeye mwenyewe moja kwa moja. "Jean". "Ndiyo". "Pierre hapa". "Ehe". "Nimepata habari, kutoka Wakala. Wamesema habari kutoka kwa wateja wetu wanasema kuna spea zinawasili hapa toka Nigeria kwa ndege ya shirika la ndege la Nigeria ambayo inaingia sasa hivi tunavyozungumza. Ni spea za aina mbili. Moja ni ndefu kama futi 5inchi 10, nyeusi, imefunikwa kwa suti nyeusi. Nyingine nayo ni ndefu futi 5 inchi 6, maji ya kunde, imefunikwa kwa suti nyeusi vile vile. Spea hizi ni za hatari sana lazima zikaangaliwe zinapelekwa duka gani ili iwe rahisi kuzinunua. Kwa sababu ni za hatari, lazima watu wenye ujuzi wa juu ndio wapelekwe kuzitambua. Umenielewa?" 'Hakuna taabu, tayari nina watu wenye ujuzi wa hali ya juu katika spea huko uwanja wa ndege nitawapasha habari mara moja". "Wapashe habari mara moja, maana saa zenyewe ni hizi". "Oke, nitapiga baada ya kuwapasha habari," alijibu Jean na kukata simu. Wakati mlango wa ndege unafunguliwa ili abiria wapate kutoka ndani ya ndege, Mtu mmoja ambaye ni mfanyakazi wa Idara ya Uhamiaji ya Zaire alikuwa akipokea simu. Mtu huyu alikuwa kwenye orodha ya mishahara ya 'WP' kwa ajili ya kutoa habari na vile vile kuwa kiungo kati ya ofisi ya 'WP' na wafanyakazi wa 'WP' ambao wanaweza kuwa kiwanjani. Mtu huyu alikuwa akipata maagizo moja kwa moja kutoka kwa Charles wa G.A.D. gereji. Hivi simu hii aliyokuwa ameipokea ilikuwa imetoka kwa Charles ikiwa na maagizo kwa wafanyakazi wawili wa 'WP'ambao walikuwa wamepelekwa hapo uwanja wa ndege ili kuchunguza watu wote waliokuwa wakiingia Zaire kwa njia ya ndege. Baada ya kupata simu hii aliinuka na kupanda ngazi haraka haraka kwenda kwenye sehemu ya kuagia ambapo alijua ndipo Mulumba mmoja wa wafanyakazi wa 'WP' waliokuwa hapo uwanjania alikuwa. Watu walikuwa wengi sana, lakini kwa bahati Mulumba alikuwa amesimama kando kwenye sehemu ambayo mtu alimwona moja kwa moja.
"Mulumba, nina maagizo yako", huyu mtu alimwambia alipofika.
"Nitakuja ofisini kwako," Mulumba alijibu.
"Ni ya haraka sana inatoka kwa Charles." Alimweleza huku akimvuta kando.
"Ehe anasemaje?".Mulumba aliuliza kwa makini.
"Kati ya watu wanaotelemka ndani ya ndege hii, mna wapelelezi wawili mashuhuri wa Afrika. Mmoja ni mweusi kiasi cha futi 5 inchi kumi kwa urefu amevaa suti nyeusi na mwenzie ni maji ya kunde kiasi cha furi 5 inchi 6 nae amevaa suti nyeusi. Wanatoka Lagos Nigeria. Anasema ni watu ambao hamuwezi kuwakosa, lazima mtawatambua. Vile vile ameonya kuwa ni watu hatari sana hivi msiwafanyie jambo lolote ila tu muwafuatie mjuwe wamefikia wapi na mripoti moja kwa moja kwake. Vile vile lazima mlinde mahali watakapofikia mpaka hapo watu wengine watakapokuja kuchukua nafasi zenu. Amesema kuwa msiwaache wakawapotea hata kidogo hiyo ni amri."
"Oke, hao abiria wanaanza kutoka, nenda kwenye chumba cha kufikia ukamweleze Kasongo yuko huko", Mulumba alieleza.
"Oke, bahati njema", Mulumba alijiweka sawa kwenye nafasi ambayo angeweza kuona vizuri kila abiria anayetelemka bila kujua kwamba hatua tu kwenye jukwa hilo hilo walikuwa wamesimama wapelelezi mashuhuri wa Afrika waliokuwa wamefika kungojea watu wale wale ambao yeye naye alikuwa akiwangojea.
Willy na Robert walikuwa wakiwaangalia abiria waliokuwa wanatelemka kwa makini sana vile vile bila kujua kuwa hatua chache tu kutoka sehemu waliyosimama kulikuwa na mtu wa 'WP' kikundi ambacho ndicho alikuwa hasa ametumwa kuja kukitafuta.
"Huyo ni Kofi", Willy alimweleza Robert wakati kijana mmoja aliyevalia suti nyeusi na huku akitembea kifahari alipokuwa akitelemka kutoka katika ndege.
"Ahaa," aliitikia Robert huku akimwangalia Kofi kwa makini ambaye alikuwa akielekea chumba cha kufikia pamoja na abiria wenzake. Ozu ndiye alikuwa mtu wa mwisho kutelemka ndani ya ndege, na mara alipojitokeza tu Willy alimtambua na hata Robert ambaye alikuwa bado hajawahi kumwona alihisi ya kuwa huyo ndiye alikuwa Ozu kutokana na miondoko yake ilivyokuwa.
Mulumba naye alipomwona Ozu naye alihisi mara moja kuwa ni mmojawapo wa watu aliokuwa ameelezwa, ingawaje Kofi alitelemka bila yeye kumtambua. Hivi baada ya kumhisi huyu mtu Mulumba alitelemka upesi upesi ili akambonyeze Kasongo kuwa amemtambua mtu huyu.
"Huyo ndiye Ozu", Willy alimweleza Robert.
"Hata mimi nilihisi ndiye yeye, miondoke na umbo lake la kimwanariadha limemfanya aonekane waziwazi".
"Telemka chini tukawasubiri," alishauri Willy wakaanza kutelemka.
"Mpango utakuwa ka ule uliofanya. Sisi tutabana mahali ambapo mtu yeyote hatatuona na kuwaacha watangulie kuondoka, halafu sisi tutawafuata. Mimi nitatangulia wewe utanifuata nyuma. Kama kutatokea kitu chochote cha kutaka cha kutaka wewe usihusike nitatoa mkono wangu nje na kuuonyesha juu. Nikifanya hivyo nipite moja kwa moja ukanisubiri hotelini. Na kama kuna kitu nataka tusaidiane nitatoa mkono wangu nje na kuuegesha kwenye dirisha, nikifanya hivyo jiweke katika hali ya tahadhari," alishauri tena Willy.
"Kwani unadhani kitu chochote kinaweza kutokea?". Aliuliza Robert.
"Huwezi kujua maana inabidi ujuwe kuwa Ozu na mwenzake ni wapelelezi mashuhuri".
Ozu ambaye alitelemka mwisho alifanya hivyo kwa sababu maalumu. Alikuwa amevaa miwani, na miwani hii haikuwa ya kawaida ingawaje ilionekana kama miwani ya jua ya kawaida. Miwani hii ilikuwa na kioo maalumu kinachovuta vitu vilivyo mbali na kuvileta karibu. Hivi Ozu alipotokea kwenye mlango wa kutokea wa ndege aliiweka miwani hii na kuangalia moja kwa moja kwenye jukwa ambapo watu wanasubiri wageni hukaa. Na mara moja aliweza kutambua kitu ambacho alikuwa akihisi. Baada ya kutambua kitu hiki alitoa hiyo miwani na kuendelea kutelemka ngazi za ndeeg.
Mulumba ambaye aliingia ndani ya chumba cha kufikia wasafiri, alionekana mtu mwenye wasiwasi sana na mara Kasongo alipomwona katika hali hii alijua lazima kuna kitu hivi alimsogelea.
"Vipi?", Kasongo aliuliza.
"Nimemtambua mmoja wao lakini mwingine bado, kwa sababu wako safari moja itakuwa rahisi kuwatambua. Maana itabidi wawe pamoja", alijibu Mulumba.
"Kwa hiyo tuwe macho na huyu mtu uliyemtambua, tusimuachie hata kwa dakika moja".
"Huyo anaingia", Mulumba alimtambulisha Kasongo.
Kasongo alimwangalia kwa chati kijana huyu ambaye alipita sehemu za uhamiaji bila wasiwasi wowote. Walijaribu kuchunguza katika abiria wote kama wangeweza kumtambua huyu wa pili ambaye alikuwa ameelezwa, lakini bila mafanikio, kwani kulikuwa na abiria wengi waliokuwa na maelezo sawa na yale yaliyotolewa juu ya mtu huyu wa pili, hivi ilikuwa vigumu sana kumtambua.
"Itabidi tumg'ang'anie huyu ndiye atatuonyesha huyu wa pili", alishauri Kasongo.
"Sawa, twende nje tukamsubiri kule", Mulumba alikubaliana/
"Hapana siye tukae hapa hapa kwenye makochi kwa vile tutaona kila kitu nje itakuwa rahisi kumwona na atakapochukua gari ndipo sisi tutamfuata bila mtu kushuku", alishauri Kasongo.
Mulumba alikubaliana na jambo hili wakaketi kwenye makochi kama watu wengine waliokuwa wakisubiri wageni.
Willy na Robert walipotelemka chini walienda moja kwa moja mpaka kwenye chumba cha kupokelea wageni ambao husafiri ndani ya Zaire tu. Walichagua sehemu hii maana ilikuwa sehemu nzuri ambayo mtu anaweza kuangalia mambo yote yanayoendelea kwenye sehemu ya nje ya uwanja wa ndege, na vile vile kuangalia kitu kinachofanyika ndani ya chumba cha kupokelea wageni watokao nchi za nje. Maana sehemu zote hizi ni vioo vitupu. Hivi Willy na Robert walipoingia walichanganyikana na kundi la watu ambao walikuwa wamefika kuwapokea ndugu zao lakini macho yao yakiwa katika tahadhari ya kuangalia mambo yote ambayo yangeweza kutokea hapo nje.
Bila kujua nini kinatendeka. Kofi alikuwa katika kundi la kwanza lililomaliza kukaguliwa. Akiwa katikati ya kundi hili la wenzake aliweza kuingia kwenye chumba cha kupokelewa na kisha kutoka nje bila ya Mulumba na mwenzake kumtambua ingawaje alipita mbele yao. Kofi na Ozu walikuwa wamepanga kuwa wafikapo Kinshasa kila mtu achukue njia yake ila tu waonane baadae wakishafika mjini. Kwa sababu hawakuwa wageni sana mjini Kinshasa jambo hili lilionekana safi kabisa kiusalama.
Wakati Kofi anatoka nje, Willy na Robert alimwona, "Huyo Kofi anatoka", Robert alimweleza Willy ambaye alikuwa akiangalia mambo mengine. Walimwangalia Kofi ambaye alikuwa pamoja na abiria wengine, akienda na kuingia ndani ya teksi iliyokuwa karibu na kuondoka huku wakipita mbele ya Willy na Robert kuelekea mjini. Willy alichukua namba ya teksi na kuiweka kichwani.
"Ngoja mimi nimfuate Kofi, halafu wewe utamfuata Ozu akitoka maana naona wamekata shauri kila mmoja wao kuchukua njia," Robert alishauri.
"Hapana tusiwe na haraka tumsubiri Ozu mpaka naye atoke", Willy alieleza.
Ozu ambaye kama nilivyokwisha eleza hapo nyuma alikuwa amevuta sura za watu waliokuwa jukwaani wakati anateremka katika ndege kwa miwani yake, na katika sura zilizokuwa hapo sura tatu kati ya hizo alizitilia mashaka kwani macho ya sura hizi yalionekana yakimwangalia yeye moja kwa moja. Naye mara moja sura hizi akaziweka kichwani mwake, hivi alipomaliza kukaguliwa na kuingia kwenye chumba cha kupokea wageni, alizungusha macho yake kwa chati kwa watu wote waliokuwa humo. Macho yake yalipomwangalia Mulumba yalimtambua moja kwa moja lakini wale wengine hakuweza kuwatambua. Hivi akijifanya kama hakuna kitu aliendelea na abiria wenzake na kutoka nje. Baada ya Ozu kutoka nje. Mulumba na Kasogo walisimama na kwenda hadi karibu na mlango na kumwangalia Ozu ambaye alikuwa akizungumza na dereva wa teksi. Kisha alipanda ndani ya teksi na kuondoka kuelekea mjini.
Willy na Robert nao walikuwa wakimwangalia OZu kwa uangalifu kabisa. Baada ya gari la Ozu kuzunguka na kupita mbele yao tayari kwa kuelekea mjini walikata shauri kutoka nje ili wapate kumfuata. Walipokuwa wakifungua mlango ili watoke, waliona watu wawili nao wanafungua mlango wa chumba cha kupokelea wageni watokao nchi za nje na kutembea haraka haraka nusu wakikimbia kuelekea kwenye maegesho ya magari.
"Hebu ngoja," Willy alimsukuma kidogo Robert na kurudi ndani, "Unawaona wale watu?"
"Ndiyo,"
"Hebu tuone wanataka kufanya nini".
Watu hawa walikuwa ni Mulumba na Kasongo ambao waliingia ndani ya gari lao na kuondoka kwa kasi sana kumfuata Ozu.
"Sasa Robert itabidi tuondoke ndani ya gari moja, maana inaonekana watu wawili wanamfuata Ozu kutokana na jinsi walivyoondoka. Unasemaje?".
Willy na Robert waliingia ndani ya gari la Willy alilokodi na kuondoka zao kuwafuata hawa watu waliotangulia.
Mulumba na Kasongo walikwenda kasi kwenye hii barabara ya P.E. Lumumba ili wapate kuisogelea teksi iliyokuwa imembeba Ozu. Ingawaje magari yalikuwa mengi wakati kama huu wa mchana lakini walifanya kila ujuzi kuyapita magari mengine na kulisogelea gari la Ozu. Walipokuwa wameacha gari moja kati ya gari lao na gari la Ozu, walituliza mwendo wao na kufuata wakiwa nyuma ya gari hili jingine.
Ozu ambaye wakati wanaondoka uwanja wa ndege alipata fursa kumwona tena huyu kijana aliyekuwa amemwona kwenye jukwa akiwa amesimama kwenye mlango wa kutokea ndani ya chumba cha kupokelea wageni watokao nchi za nje, alihisi kuwa lazima alikuwa anafuatwa hivi mara kwa mara aliangalia nyuma kuona kama kulikuwa na mtu aliyekuwa anafuata.
Willy na Robert nao walitumia kila ujuzi wao mwenye msululu huu wa magari mpaka wakawa wameacha magari mawili kati yao na gari la akina Mulumba na kutuliza mwendo wao.
"Hawa watu ni watu gani?" Aliuliza Robert.
"Tutajua tu, usiwe na haraka", alijibu Willy bila wasiwasi.
Walipokaribia njia panda ya barabara ya P.E. Lumumba na barabara ya 'Poids Lourds', Ozu ili kusudi aweze kuhakikisha kama kweli anafuatwa alimwambia dereva teksi.
"Tuingie barabara ya 'Poids Lourds'.
"Likambo te!" Alijibu teksi dereva katika Kilingala, maana yake 'hamna taabu', na kuonyesha taa za gari kuwa anachepuka kuingia barabara nyingine. Mulumba na Kasongo kuona hivi nao wakaonyesha taa kuwa na wao walikuwa wanachepuka kuingia barabara hiyo.
"Kaa macho, huyu mtu ujue ni mpelelezi maarufu kama tulivyoelezwa kwa hivi ni mtu hatari anaweza kuwa ametuhisi, hivi anatafuta njia ya kujihami. Hivyo weka bastola yako tayari, maana hii barabara haina watu wengi ni ya upweke sana, anaweza kuanzisha kitu chochote", alieleza Mulumba huku akiwa na wasiwasi kidogo.
Willy na Robert walipoona gari la Ozu na la hawa watu wengine yakichepuka na kuingia Poids Lourds hawakuwa na budi ila nao kuingia barabara hii.
"Kwanini Ozu anaingia barabara ya upweke namna hii na huku anafuatwa?". Aliuliza Robert.
"Inawezekana amehisi kitu na anataka kuhakikisha," alijibu Willy huku akiwa tayari ameingia ndani ya barabara hii ya Poids Lourds.
"Lakini barabara hii ni ndefu sana na ya upweke sana kiasi kwamba jambo lolote likikutokea kupata msaada ni vigumu."
"Ngoja tuone nia yake ya kufanya hivi ni nini".
Ozu alipoona magari mawili yanamfuata nyuma huku yakiwa yameweka umbali ambao hayakuwa yanauzidi kati yao, aliridhika kuwa alikuwa anafuatwa na vile vile alihakikisha kuwa wale watu wawili aliokuwa amewaona kwenye jukwaa lakini hakuwa amewaona ndani ya chumba cha kupogkelea wageni, nao walikuwa wanamfuata ndicho kisa cha kuwepo magari mawili yakifuatana. Alifikiri afanye nini, lakini moyo wake ulimkataza asifanye chochote maana upinzani ungekuwa mkali sana kwake. Hivi akaamua kuendelea hivi hivi mpaka mjini ambako huenda angeweza kupata nafasi ya kuwakwepa watu hawa. Kwa hiyo alimwambia dereva, "Hebu ongeza mwendo kwa kadri ya uwezo wako".
"Barabara hii ina mashimo mengi sana lakini nitajitahidi", alijibu dereva huku akiongeza mwendo.
Mulumba na Kasongo walipoona gari iliyombeba Ozu inaongeza mwendo, nao wakaongeza mwendo. Akili yao ilikuwa imejawa na kumfuata Ozu kiasi cha kwamba hawakutilia maanani gari lililokuwa linawafuata nyuma.
"Inaonekana Ozu ametambua kuwa anafuatwa angalia jinsi gari lake ambavyo limeongeza mwendo", Robert alisema.
"Naona hata mimi. Ili kusudi tuhakikishe kuwa watu hawa wanamfuata Ozu ni lazima sisi tuwasimamishe. Maana inaonekana haja yao ni kumfuata tu wala si kumsimamisha na kumfanyia chochote. Kwa vile pia tumetambua kweli kuwa wanamfuata litakuwa jambo la maana kuwakamata watu hawa tujuwe ni akina nani na kwanini wanafanya hivi. Hasa ninapofikiria ya kwamba Ozu na Kofi wameingia hapa mjini kisiri, hili jambo la watu kuwafuata linatia wasiwasi," Willy alieleza wasiwasi wake.
"Sawa, mimi niko tayari kwa kitendo chochote utakachoamua".
"Vizuri, una silaha?".
"Sina", alijibu Robert.
"Kwanini unatembea bila silaha nawe unajua uko kazini?"
"Mimi ninatumia silaha inapokuwa lazima sana. Kawaida yangu katika kashikashi ya kawaida judo, karate na kung fu ambayo nina ujuzi wa hali ya juu sana, wewe mwenyewe utachoka ukiniona niko kazini," Robert alieleza kwa sauti ya kujiamini sana.
Willy ambaye alimwamini moja kwa moja alimweleza, "Kwa sababu hujui watu hawa ni watu wa namna gani lazima uwe tayari kwa yote. Mimi nitalitia gari mwendo wa kasi kiasi cha kuwapita hawa jamaa. Nikishawapita tu nitapiga breki mbele yao kiasi cha kwamba watatugonga nyuma. Hapo ruka mara moja na kumteka jamaa wa upande wako, nami nitamteka wa upande wangu. Kwa sababu tutawashtua nafikiri kazi itakuwa rahisi sana", Willy alitoa bastola ndani ya koti na kumpa Robert, "Chukua hii".
"Asante, kwa upande wangu hamna taabu, sijui wewe dereva".
"Kwangu ndiyo hamna kabisa," alijibu Willy huku akiongeza mwendo.
Walipopita gereji ya Fiat tu. Willy aliweka mwendo wa kasi sana kwa gari hili la aina ya Mercedes Benz na gari likapaa. Sehemu hii waliyokuwa wamefikia ilikuwa sehemu ya upweke sana, na Willy aliiona ndiyo sehemu safi ya kufungia kazi.
Mulumba ambaye ndiye alikuwa akiendesha gari lao aina ya Fiat 124 aliona kwenye kioo chake cha kuendeshea, gari lililokuwa nyuma yao linakuja kasi sana. Mara moja akaingiwa na wasiwasi na kumwambia Kasongo aweke silaha tayari.
Gari hilo sidhani lina usalama," alimalizia na huku gari la akina Willy linaanza kuwapita. Willy aliwapita kwa mwendo huo huo, alipopita mbele yao tu, akaliingiza gari sawasawa na gari la akina Mulumba, huku akiwa kana kwamba ameona shimo. Alifunga breki ghafla na kuliacha gari lijililie. Mulumba alishindwa kulikwepa gari hili na akaligonga kwa nyuma kama vile Willy alivyotaka. Willy na Robert waliruka toka ndani ya gari lao, na huku wakati ule ule, Mulumba na Kasongo nao waliruka toka ndani ya gari lao, Kasongo ndiye alikuwa wa kwanza kufyatua, lakini risasi yake ikamkosa Robert ambaye alikuwa amekwisha jirusha toka alipoangukia na kuangukia karibu na Kasongo, na kufumba na kufumbua akaipiga teke bastola ya Kasongo na kuangukia upande. Robert kuona hivi alirudisha bastola yake ndani ya koti ili amkabiri Kasongo mikono mitupu.
Naye Willy aliporuka alijiviringisha na alipoinuka tu akakuta Mulumba naye anajiweka tayari kufyatua risasi, lakini Willy alikuwa mwepesi zaidi akawahi kufyatua risasi ya kichwa na kumuua pale pale. Alipoona hivi aliruka mara moja kwenye upande ule ambako Robert na Kasongo walikuwa wanazipiga na kumkuta Kasongo amepigwa ile mbaya mpaka hajiwezi kabisa.
"Basi, basi, inatosha, mwingize ndani ya gari yetu, twende naye, huyu ndiye atatupa habari".
Wakati Robert anamwingiza Kasongo ndanu ya gari. Willy aliangalia lile gari kwenye karatasi za bima akakuta ni gari la kukodi la S.T.K. Kisha akajaribu kunyoosha gari lake kwa nyuma ambako lilikuwa limebonyea kiasi cha kugusa kwenye tairi. Alipolinyoosha kiasi cha gari kuweza kwenda, alipanda ndani ya gari akalipiga moto na kuondoka. Tayari Robert na mtu wake walikwisha starehe nyuma ya gari. Mambo yote haya hayakuchukua zaidi ya dakika mbili. Willy alifikiria wapi wampeleke mtu huyu kumhoji, mara akapata wazo. Aliendelea moja kwa moja mpaka akaingia barabara ya 30 Juin kisha akaingia barabara ya Kasavubu halafu akaingia barabara ya Sendwe halafu barabara ya Universete. Alipoingia ndani ya barabara hii akaenda moja kwa moja mpaka Chuo Kikuu. Alipofika hapa Robert ambaye alikuwa anashangaa wanakwenda wapi aliuliza, "Wapi tunakwenda?".
"Sehemu ambayo huyu ndugu yetu anaweza kutueleza vizuri mambo tunayotaka kuyajua", Willy alijibu Robert naye alihisi sehemu gani Willy alikuwa amefikiria.
Walipofika kwenye msitu ulio karibu na Chuo Kikuu na shule ya sekondari ya wasichana ya Kimwenza, Willy alienda taratibu na kuyaacha magari yampite. Yalipokuwa yamempita magari yote alisimama na kutoka. "Bado amezirai?", Willy aliuliza.
"Anaanza kupata fahamu".
"Tumbebe, hapa ndipo mahali petu ambapo tunaweza kuzungumza na huyu mtu", walimbeba na kuingia naye ndani ya msitu huu. Kwa vile Kasongo alikuwa bado hajapata fahamu vizuri, Willy alichukua galonoya maji iliyokuwa ndani ya gari na walipopata mahali pazuri ndani ya msitu huu walimweka chini Kasongo na kuanza kumwagia maji. Kasongo alipopata fahamu vizuri Willy alitoa bastola yake na kuilenga kichwani mwa Kasongo na kuanza kumhoji.
"Wewe ni nani?", Willy aliuliza.
"Kwani nyie ni nani?", Naye Kasongo aliuliza.
"Tafadhali kijana kama unataka usishi tafadhali sana jibu maswali yetu tutakuacha uende nyumbani, la hutaki leo ndiyo mwisho wako.
"MSipoteze muda wenu. Mimi sintawaeleza lolote, kama ni kuniua basi niueni mwende zenu."
"Lakini tuna njia nyingi za kuweza kukushawishi ujibu maswali yetu, lakini sisi tusingependa kuzitumia njia hizi kama utatujibu moja kwa moja".
"Nimesema nimesema, kama kuniua mniue neno hata moja hamtapata kutoka kwangu", alijibu Kasongo kwa ujasiri mwingi sana.
"Wewe unamkawiza", Robert alimwambia Willy, "Majitu kama haya hayafai kubembelezwa maana yamezoea taabu", Robert alimfungua Kasongo suruali, halafu akamtelemsha suruali pamoja na chupi, kisha akawasha kiberiti chake cha gesi na kuanza kumchoma kwenye sehemu zake za siri. Kasongo alianza kupiga kelele maana alipata uchungu mwingi sana.
"Niache, niache, aaa mnaniua", alilia Kasongo.
"Jibu wewe ni nani na nani amekutuma?".
"Sijui... aaa... sijui", aliendelea kupiga makelele, Robert alisogeza moto, Kasongo aliachama na kuzungusha zungusha ulimi wake halafu kitu kama peremende ndogo sana kikatokea mdomoni mwake na kukazana kukimeza. Willy alipokiona tu alimrukia kusudi asikimeze lakini kwa bahati mbaya hakuwahi. Kwani Willy alikitambua kitu hiki kuwa ni kidonge cha sumu ambacho hutumiwa hasa na majasusi ya hali ya juu sana wanaposhikwa ili wajiue wasiweze kutoa siri.
"Ni kazi bure tumefanya Robert, atakufa sasa hivi, amemeza kidonge cha sumu. Inaonekana hawa ni majambazi ambao wanalifanyia kazi kundi la hali ya juu sana, maana kundi la kawaida haliwezi kutumia njia hizi", alisema Willy kwa huzuni sana.
"Mimi kwanza nilikuwa na wasiwasi nikijua tumepambana na vijana wa CND, lakini hii imehakikisha kuwa kuna kundi la kijasusi mjini hapa na leo tumelitonesha kidogo, sasa tusubiri tuone nini kitafanyika", Robert alieleza. Willy alikagua mifuko yote ya Kasongo, kitu cha kutatanisha alichokipata kilikuwa kikaratasi kidogo kigumu kilichoandikwa, "Muone Kabeya Charles", Willy alikiangalia sana kikaratasi hiki kisha akampa Robert ambaye naye alikiangalia sana.
"Kitatue, lakini majina hayo yaweke kichwani, huenda yakawa na maana sana", alishauri Willy.
"Lazima ni ya maana sana, lakini tukiweke kwanza," alijibu Robert.
Waliondoka sehemu hii na kurudi mjini huku wakiwa na mawazo mengi sana juu ya tukio hili la kushangaza. Kwani huenda walikuwa kwa bahati mbaya wameligusa kundi linalohusika na mauaji ya wapigania uhuru, hivi ndivyo waifikiri wakati wakirudi .
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena