Pendo Ojijo (Kushoto) ambae ni Mwenyekiti wa Muda ACT Wazalendo Mkoani Mwanza akizungumza na GB Pazzo (Kulia).
Na:George GB PazzoChama cha Alliance For Changes And Transparency (ATC WAZALENDO) kinatarajia kuwasha moto wa Kisiasa Mkoani Mwanza, ikiwa ni mwendelezo wa Chama hicho kuendelea na Mikutano yake ya hadhara katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Jana Mwenyekiti wa Muda wa Chama hicho Mkoa wa Mwanza Pendo Ojijo aliiambia Binagi Media Group kwamba, ACT Wazalendo kinatarajia kufanya Mkutano wake wa hadhara siku ya Jumapili ya April 19 katika Uwanja wa Furahisha Wilayani Ilemela kuanzia majira ya Saa nane Mchana.
Alisema katika Mkutano huo, viongozi mbalimbali wa Chama hicho ambao ni pamoja na Kiongozi wake Mkuu Zitto Zubery Kabwe, watakuwa na ulingo mpana wa kuzungumza na Wananchi kwa ajili ya kuwaeleza masuala mazito na mapana yenye maslahi ya Kitaifa hivyo ni vyema wananchi wote wakajitokeza kwa wingi katika Mkutano huo bila kujali itikadi za kisiasa za vyama vyao.
ACT Wazalendo ilifanya uzinduzi wake rasmi March 29 mwaka huu ikiwa ni siku moja baada ya kufanya Uchaguzi wake mkuu ambapo Anna Mghwira alichaguliwa kuwa Mwenyekiti, Makamu mwenyekiti bara Shaban Mambo, Makamu mwenyekiti Zanzibar Ramadhan Suleiman Ramadhan, Katibu Mkuu Samsoni Mwigamba na Kiongozi Mkuu akiwa ni Zitto Zubery Kabwe.
Hatimae chama hicho kilianza mikutano yake katika Mikoa mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kuwatambulisha viongozi wake kwa wananchi huku pia kikiwa kimelenga kuelezea mwelekeo wake wa kisera katika kuijenga Tanzania mpya yenye kufuata misingi ya Usawa, Uzalendo, Uwazi, Uwajibikaji, Demokrasia pamoja na Uadilifu ambapo katika mikoa ambayo chama hicho tayari kimeifanya kimeweza kupokelewa vyema na Watanzania walio wengi.
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena