Header Ads Widget

Responsive Advertisement

NEWS | MASHINE ZA BVR ZAWASILI NCHINI

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Julius Mallaba.


Hatimaye mashine 248 za kisasa za kuandikisha wapigakura katika daftari la kudumu la wapigakura kwa kutumia mfumo wa elektroniki wa Biometric Voters Registration (BVR) zimewasili nchini, ili kuongeza kasi ya mwenendo wa mchakato huo, ambao umekuwa wa kusuasua.

Kusuasua kwa mchakato huo ulioanza mkoani Njombe, Februari 23, mwaka huu kabla ya kusimama, kunatokana na mashine 250 za awali za kuandikisha wapigakura zilizokuwa zikitumika, kushindwa kufanikisha kazi ya kuandikisha wapigakura.

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Julius Mallaba (pichani), alithibitisha jana kuwasili kwa mashine hizo nchini.

“Mashine hizo zimeshawasili. Ziko Dar,” alisema Mallaba, ambaye hata hivyo alikataa kueleza lini zimewasili alipotakiwa na NIPASHE jana kujibu swali hilo. 

Wiki iliyopita, akijibu maswali ya waandishi baada ya kutangaza kuahirishwa kwa kura ya maoni hadi itakapotangazwa tena, kuhusu idadi ya mashine, ambazo zimewasili, Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva, alisema walitarajia kupata 248 siku yoyote kuanzia siku hiyo, ambazo zitatumika kwenye mikoa minne.

Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Iringa, Ruvuma, Mtwara na Lindi na kuwa ratiba yake ingetolewa hivi karibuni.

Jaji Lubuva alisema mashine nyingine 1,600 zitawasili wakati wowote na kwamba serikali imetoa Dola za Marekani milioni 72 (Sh. bilioni 133).

Kuwasili kwa mashine hizo, kunaifanya Nec kupokea mashine 2,098, huku ikisubiri mashine 5,902, ili kukamilisha 8,000 zinazotakiwa. Alisema vifaa hivyo vinanunuliwa na serikali kupitia kampuni ya Lithotech Export ya Afrika Kusini, ambayo imeingia mkataba na Nec na inaviagiza China.

Jaji Lubuva alisema uandikishaji unaendelea mkoani Njombe na utakamilika Aprili 18, mwaka huu na vifaa (BVR Kits 250) zilizokuwa zinatumika zitatumika katika mikoa itakayofuata. Alisema vifaa hivyo vinanunuliwa na serikali kupitia kampuni ya Lithotech Export ya Afrika Kusini, ambayo imeingia mkataba na Nec na inaviagiza China.

Taarifa zilizopatikana ndani ya Nec zinaeleza kuwa kampuni hiyo ndiyo inayotoa muundo wa ndani (Soft Ware) ya mashine hizo na kwamba utengenezaji wa mashine moja na kuweka vifaa vyote muhimu inachukua wiki sita. Uandikishaji wapiga kura mkoani Njombe ulianza Februari 23, mwaka huu, na hadi kukamilika Aprili 18, mwaka huu, utakuwa umetumia siku 45, ukitoa siku za sikukuu na Jumapili.

Aidha, Nec ilisema ina uhakika wa kuandikisha wapigakura katika daftari hilo hadi Julai, mwaka huu, na kwamba jiji la Dar es Salaam na Zanzibar, itakuwa ya mwisho ili kuwezesha vifaa vyote 8,000 kutumika kwa pamoja.

Jaji Lubuva alisema Nec iliomba vifaa Kenya na Nigeria, lakini ilishindikana kwa maelezo kuwa vinatumika katika ngazi za serikali za mitaa, na kwamba kuomba vifaa nje ni utaratibu wa kawaida kwa nchi za Kusini mwa Jagwa la Sahara.

“Nchi za Malawi na kwingine zinakuja kujifunza kwetu, hapa kwetu tatizo kubwa ni viongozi na siku zote Nabii hakubaliki kwao,” alisema Jaji Lubuva

Post a Comment

0 Comments