Dar es Salaam. Baadhi ya wabunge wa Chadema wamezungumzia taarifa zinazosambaa zikieleza kuwapo mkakati wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhamia katika chama hicho, wengi wao wakimkaribisha.
Wakati wabunge hao wakikubali kumpokea,
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa amesema wananchi wasubiri
mambo yatakapokuwa tayari badala ya kutegemea mitandao ya kijamii.
“Nitazungumza
pale mambo yatakapokuwa sawa, siwezi kuzungumza sasa, subirini… sasa
hivi mambo mengi yanazungumzwa kwenye mitandao,” alisema Dk Slaa ambaye
pia anatajwa kuwa mgombea wa chama hicho ndani ya Ukawa.
Msemaji
wa Lowassa, Aboubakary Liongo alipoulizwa kuhusu kuwapo kwa mpango huo
alisema hawezi kulizungumzia hilo kwa kuwa ni suala la mtu binafsi. Hata
hivyo, jitihada za kumpata Lowassa jana hazikufanikiwa kwani simu yake
iliita pasi na kupokewa.
Hivi karibuni, idadi kubwa ya
madiwani wa CCM walirudisha kadi zao na kujiunga na Chadema wakisema
sababu ni kutoridhishwa na kukatwa kwa jina Lowassa kati ya wagombea
urais wa CCM.
Kadhalika, mtandao wa kijamii uliokuwa
ukimuunga mkono mbunge huyo wa Monduli unajulikana kwa jina la 4U
Movement ulitangaza kuhamia Chadema hali inayoashiria kuwa kuna dalili
ya Lowassa pia kujiunga nao.
Wakiandika katika akaunti
ya Twitter ya 4U Movement, wafuasi hao walisema: “Ukimya ni hekima na
ukimya ni busara. Ukimya wa Edward Lowassa ni kutafakari Safari ya
Matumaini... Tuungane kuyapata mabadiliko nje CCM.”
Chadema ni kanisa la wokovu
Akizungumzia
taarifa hizo, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa
alikifananisha chama hicho na kanisa ambalo kwa kawaida halikatai mtu,
bali linawapokea wenye dhambi na kuwaongoza kufanya toba.
“Chadema
ni kama kanisa, hakataliwi mtu, tunahubiri habari njema ya wokovu,
ukija hapa unatubu unaendelea kufanya kazi,” alisema.
Kuhusu
viongozi wa CCM kuhamia Chadema, Msigwa alisema inawezekana kasi hiyo
inachagizwa na Lowassa kukosa nafasi aliyoitaka ndani ya chama hicho.
“Unapokuwa
mwanasiasa unakuwa na wafuasi, inawezekana wengine wanaohamia Chadema
ni watu wake ambao wameona mtu wao amekosa nafasi aliyoitaka ndiyo maana
wanakihama chama,” alisema.
Msigwa alisema Chadema
ilikuwa inakusanya wanachama wapya kwa muda mrefu hata kabla ya vuguvugu
la Lowassa na chama chake kuibuka na ushindi na wanaohamia wanafanya
hivyo kwa sababu wanakipenda chama na wameichoka CCM.
Huenda akatimiza safari ya matumaini
Akizungumzia
ujio wa Lowassa kwenye chama hicho, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless
Lema alisema iwapo Lowassa atahamia Chadema anakaribishwa na huenda
akaitimiza safari yake ya matumaini.
“Namkaribisha Lowassa Chadema, huenda safari yake ya matumaini ikaishia huku, akawa mwanachama au hata kiongozi,” alisema.
Alisema
hakuna shaka kuwa mbunge huyo wa Monduli ana nguvu ndani ya CCM ndiyo
maana viongozi wengi wa chama hicho wanakihama wakati huu.
“Hiyo
ilijionyesha kuanzia kwenye Kamati Kuu ya CCM, Halmashauri Kuu, Lowasa
amekamata wajumbe kwa asilimia 80 na hiyo ni ishara kuwa ameishika CCM,”
alisema.
Lema aliongeza kuwa wanaoihama CCM hawaihami kwa bahati mbaya, bali wameona mtu wao waliyemtarajia ameondoka.
“Ni
wengi wanaohamia Chadema, kwa sasa kadi zimetuishia na hiyo ni ishara
kuwa CCM inakufa, ripoti za mikoa yote tunazo,” alisema.
Mbunge
wa Viti Maalumu, Lucy Owenya alisema wanaoihama CCM kwa sasa
wamegundua kuwa chama pekee kinachoweza kutetea wananchi ni Chadema.
“Sisi
tunawakaribisha kwa mikono miwili, waje tuchape kazi, ilimradi
wanafuata kanuni na taratibu za chama, basi. Wamejionea wenyewe kuwa
CCM hakuna chochote,” alisema.
Alisema CCM waliamua
kupitisha katiba bila kuwapo kwa Ukawa, lakini sasa wameona kuwa
walichokifanya ni makosa na wameanza kurudi Chadema ambako wanaamini
kuna demokrasia ya kweli.
Mbunge wa Viti Maalumu,
Cecilia Paresso alisema: “Tunamkaribisha kwa mikono miwili.
Tumekinyooshea CCM vidole kwa muda mrefu kuwa kuna rushwa na makundi na
hilo linajidhihirisha sasa. Lakini wale wote wanaokuja Chadema,
tunawakaribisha ili mradi wafuate kanuni na taratibu zetu.”
Paresso
alisema hana tathmini ya kina kuhusu wafuasi wa Lowassa wanaoihama CCM,
bali wanaokihama chama hicho wameona kina matatizo.
Atakiwa akidhi vigezo na masharti
Licha
ya kuonyesha kumkaribisha, katika chama hicho, baadhi ya wabunge
walimtaka Lowassa afuate kanuni ili awe mwanachama mwenye sifa.
Mbunge
wa Mbozi Magharibi, David Silinde alisema anakaribishwa lakini hana
budi kufuata sheria na kanuni za chama... “Anatakiwa afuate taratibu za
chama, milango ipo huru, lakini afuate kanuni… asije akafikiri ataleta
taratibu zake hapa, sitakubali.”
Silinde alisema
wanaohamia Chadema hawajapendezwa na mwenendo mzima wa uteuzi wa mgombea
wa urais na hivyo wameifuata demokrasia ya kweli ndani ya chama hicho.
Mbunge
wa Kawe, Halima Mdee hakutaka kuzungumzia kwa undani suala hilo lakini
alisema endapo atajiunga, chama hicho kitampokea kulingana na vigezo na
taratibu.
“Akihamia Chadema nitatoa maoni yangu lakini
ninachoweza kusema ni kuwa kila mtu ana haki ya kwenda chama chochote
ili mradi ana tija,” alisema.
Mdee alisema wanaCCM wanaohamia Chadema wamesoma alama za nyakati na kuona kuwa CCM haiendani na ahadi zake.
Mbunge
wa Viti Maalumu, Susan Lyimo alisema, Lowassa ni binadamu wa kawaida
kwa hiyo kuhamia kwake Chadema si kitu cha ajabu ilimradi afuate
kanuni... “Cha muhimu afuate masharti ya chama, kanuni na taratibu,
kama watu wanahama vyama vingine yeye ni nani asihame CCM?”
Lyimo alisema wanaCCM wengine wanakaribishwa kujiunga kwa sababu kwenye siasa hakuna rafiki wa kudumu wala adui wa kudumu.
Mbunge
wa Viti Maalumu, Pauline Gekul, aliwataka wana CCM na Lowasa kuhamia
zaidi Chadema ili kuunganisha nguvu na kuichukua nchi.
“Mfikishie salamu Lowassa mwambie karibu kwenye jeshi la ukombozi,” alisema.
Katibu wa CCM amuonya
Akizungumza
na waandishi wa habari jana katika Ofisi za CCM Mkoa wa Dodoma, Katibu
wa CCM mkoa huo, Albert Mgumba alisema ingawa kuhama chama ni hiari ya
mtu, Lowassa hapaswi kuchukua uamuzi wa hasira kiasi hicho badala yake
awe mstari wa mbele kuhamasisha umoja ndani ya chama.
Alimtaka
kutothubutu kuihama CCM na endapo afanya uamuzi huo atambue kuwa hawezi
kukisababishia pengo lolote zaidi ya kujipunguzia hadhi yake ya
kisiasa.
“Mgombea tuliyempata sasa ni makini kuliko, anapendwa, utendaji wake unajulikana kila mahali,” alisema Mgumba.
Endelea hapa====>>>>>
Endelea hapa====>>>>>
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena