ALIYEKUWA mgombea wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Ngoyayi Lowassa; Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana; Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wanatarajiwa kukutana katika kongamano litakalohusu Demokrasia na Siasa za Ushindani Nchini.
Kongamano hilo litafanyika katika ukumbi wa Anartouglou ulioko Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam kuanzia saa mbili.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Mwenyikiti wa Chadema Wilaya ya Ilala, Makongoro Mahanga, amesema kuwa nia ya kongamano hilo ni kuwafahamisha wananchi na wadau wengine kuwa ushindani wa kisiasa ni jambo linalokubalika duniani kote na pia kujenga ufahamu kuhusu dhana ya ushindani wa kidemokrasia.
Mmoja wa waratibu wa kongamano hilo, Baraka Mwago, naye akifafanua jambo.
“Wapo wananchi wengi ambao bado hawajaelewa vyema kwamba ushindani wa kisiasa siyo uadui na wala siyo kosa kisheria kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi,” alisema.
Aliongeza kuwa kongamano hilo linatarajiwa kuwakutanisha viongozi wote wa vyama vya siasa ili kuzungumza juu ya umuhimu wa demokrasia katika vyama vya siasa.
“Kesho katika kongamano hili hatutazungumzia masuala ya vyama vyetu wala mitazamo yetu bali tutazungumzia demokrasia tu na hatutazungumza kitu chochote kuhusu vyama vyetu kwenye kongamano hilo,” alisema Makongoro.
Kutoka kushoto ni mmoja wa waratibu wa kongamano hilo, Allen Mazoko, Makongoro Mahanga na Baraka Mwago.
Alisisitiza kwamba waandaji wa kongamano hilo ni Chadema kupitia Wilaya ya Ilala ambao ndiyo wamewapelekea barua za mialiko viongozi wote wa vyama vya siasa nchini na wadau wengine zikiwemo taasisi za haki za binadamu.
Miongoni mwa wazungumzaji wakuu wa kongamano hilo ni Deus Kibamba, Jenerali Ulimwengu, Zitto Kabwe, Harold Sungusia na wengine.
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena