Header Ads Widget

Responsive Advertisement

FAHAMU | Ushuhuda wa jinsi Mwimbaji Wa Nyimbo za Injili Prince Amos alivyookolewa na Yesu.

Image may contain: 1 person, standing and outdoor
Nilipokuwa mitaani kabla sijaingia Dogodogo Center. Malaika wa Mungu waliniokoa kutoka kwenye hatari nyingi sana ambazo kama sio Mungu leo nisingalikuwa hai. Nakumbuka kuna siku nilienda kuomba chakula kwenye nyumba flani, kumbe jana yake walikuwa wameibiwa, waliponiona walidhani mimi ni wale wale. Walinikamata wakaniingiza ndani, nikakuta kuna mwenzangu wamemkamata wamemfunga kwa kamba na wamempiga sana. Na mimi walinifunga na kuanza kunipiga na walikusudia kutuua. Mara kati yao akatokea mtu mmoja na kuanza kututetea ndipo baada ya muda wakatuachia. Kuna siku niligongwa na gari aina ya toyota maeneo ya Mnazi mmoja Dar es salam, nilirushwa mbali, watu walinikusanyikia wakidhani kwamba nitakuwa nimeumia vibaya sana, lakini sikuwa nasikia maumivu yoyote na nilipoenda kuchunguzwa sikukutwa na jeraha lolote. Kwenye majalala makubwa ndipo palipokuwa makao yetu haswa. Tulikuwa tukiokota vyakula vinavyotupwa na kuvila kama vilivyo na hatukua tunaugua. Nyakati nyingine tulikuwa tunavizia vyakula vinavyobakizwa na watu kwenye mahoteli au kwenda kuomba mikate kwenye nyumba za Wahindi, wakati mwingine tulikuwa tunapata, lakini kuna wakati tulikuwa tunakosa. Nilikuwa nikiomba omba pesa barabarani kwenye mataa au kwenye maduka ya Wahindi. Baadae nilianza kufanya kazi ya kuosha magari kwenye maegesho ya magari na ilinipa ahueni kubwa sana ya maisha. Niliwahi kukutana na watu hatari sana lakini kila walipokuwa wakitaka kunidhuru, miongoni mwao alitokea mtu aliyenitetea. Nakumbuka nilikutana na mtu mmoja aliyetaka kunifundisha ujambazi, roho yangu ilikataa kabisa na ikanilazimu kuhama maeneo hayo. Mara kwa mara nilikamatwa na Polisi na kulala rumande kwa kosa la uzururaji lakini kila nilipokuwa nafikishwa mahakamani hakimu alikuwa akiniachia. Nakumbuka kuna siku nilikuwa navuka barabara maeneo ya mbezi ya kimara, gari aina ya Costa ilikuwa inakuja kwa kasi sana, nilikuwa nimeshafika katikati ya barabara. Ghafla nilisikia mtu amenivuta na kunitoa barabarani haraka sana, gari likapita. Nilipogeuka nyuma nione ni nani alienivuta, sikuona mtu yeyote hapo karibu ila watu walikuwa kwa mbali wakipiga kelele. Malaika wa Mungu waliniokoa

Post a Comment

0 Comments