Banza alizaliwa Oktoba 20, 1972 katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar na kupata elimu ya msingi katika Shule ya Mnazi Mmoja ambapo alihitimu mwaka 1987.
Banza alianza kufanya muziki wa Hip Hop
mwaka 1989 ambapo yeye na wenzake walikuwa wakiimba katika redio
mbalimbali na wakati mwingine walikuwa wakienda maeneo ya Coco Beach
kuonesha vipaji vyao vya muziki, jambo ambalo liliwafanya waonekane
wahuni.
Mwaka 1990 ndipo alipoamua kuingia rasmi kwenye muziki wa dansi.
Alifanikiwa kupata fedha katika kucheza dansi ambapo aliamua kwenda
kujiendeleza na masomo ya muziki katika Kituo cha Utamaduni cha Korea
jijini Dar kati ya mwaka 1990 hadi 1991.
BENDI ALIZOZITUMIKIA
Baada ya kuhitimu elimu ya cheti alianza kuimba katika bendi
mbalimbali za muziki ikiwemo Twiga, The Heart String na Achigo Band.
Mbali
na bendi hizo, Banza amewahi kupitia katika bendi kadhaa ambapo akiwa
kwenye Bendi ya Twanga Chipolopolo alitunga Wimbo wa Hujafa Hujasifiwa
ambao umebeba ujumbe unaosema ‘ningependa kujua baada ya kifo changu
mimi Banza Stone watu watasema nini hapa duniani’. Baadaye alipitia TOT
Band, Extra Bongo, Twanga Pepeta na nyinginezo.
Enzi za uhai wake aliwahi kusema kwamba
hakuwa akidumu kwenye bendi moja kwani alizoea kuhamahama ambapo mwaka
1995 alitua rasmi kwenye Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’
ndipo safari yake ya muziki ilipoanza kukua kwa kasi.Baada ya hapo,
Banza anatajwa kama mmoja wa waasisi wa Mtindo wa Twanga Pepeta
unaotumiwa mpaka leo.
ALIOTESHWA KIFO
Nakumbuka mwaka 2012, Banza alikiri na kuripotiwa katika magazeti ya
Global akisema kwamba ameota kwamba amekufa hivyo anaona siku zake za
kuishi ni chache na kwa wakati huo akaahidi kwamba anatunga nyimbo za
wosia ambazo zitapigwa katika siku ya kifo chake.
Lakini kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa na afya yake kudhoofu, Banza hakuweza kutimiza lengo hilo hadi alipofariki dunia.
SIKU 167
Banza alianza kuugua ‘serious’ Februari, mwaka huu ambapo alipitia
mateso makubwa kwa takriban siku 167 hadi alipopatwa na umauti.
Katika kipindi hicho ndipo iligundulika
kwamba alikuwa akisumbuliwa na fangasi za kichwani, akawa anatibiwa
katika Hospitali ya Sinza-Palestina lakini wiki mbili kabla ya kifo
chake alilazwa katika Hospitali ya Mwananyamala.
Mwanamuziki Banza alifariki dunia Ijumaa iliyopita nyumbani kwao,
Sinza jijini Dar na kuzikwa katika Makaburi ya Sinza, Jumamosi ambapo
ameacha mtoto mmoja anayejulikana kwa jina la Haji Ramadhan.
Banza amewahi kuzushiwa kifo zaidi ya
mara 20 ambapo mwenyewe alikuwa akisema kwamba atakufa kwa ahadi ya
Mungu na siyo kwa maneno ya binadamu ambao siku zote hawakosi la
kuongea.
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena