MAMLAKA
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kiama kwa watumiaji vibaya na
wahalifu wote wa mitandao nchini, kuwa siku zao zinahesabika kwani
ifikapo Septemba mosi, mwaka huu, Sheria ya Uhalifu wa Mitandao itaanza
kutumika na wengi huenda wakaishia gerezani.Mamlaka
hiyo imebainisha kuwa kwa sasa Tanzania inaongoza kwa kuwa na watumiaji
vibaya wengi wa mitandao ya kijamii, jambo linalosababisha taarifa za
mitandao mingi kutoaminika hadi nchi za nje kutokana na kujaa uzushi,
uongo, uchochezi na lugha na picha za matusi.Akizungumza
na mtandao huu Dar es Salaam jana, Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent
Mungy alikiri kuwa pamoja na kwamba mamlaka hiyo imefanya kazi kubwa ya
kuelimisha jamii juu ya utumiaji sahihi wa mitandao hiyo, bado matumizi
yake si mazuri hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi na kwa watu
maarufu.
“Napenda
kuwatahadharisha Watanzania na watumiaji wa mitandao hii kwa ujumla
kuwa sheria hii si ya kupuuzwa, kwani kwa hali ilivyo wengi watatozwa
faini na watashindwa kulipa na kuishia gerezani,” alisisitiza.
Alisema
kutokana na kukithiri kwa matumizi mabaya ya mitandao nchini, kwa sasa
nchi nyingi haziamini tena taarifa za mitandao ya kijamii na wala
hawazitumii hali inayopaswa kubadilishwa.
“TCRA
tumebaini kuwa watu wengi wanatumia mitandao hii lakini hawajui hasa
matumizi yake sahihi, tunashauri kabla mtu hajafungua mtandao wake kama
vile blogu, ukurasa wa facebook au hata whatsApp lazima wajielimishe
kwanza kuwa wanafungua kwa malengo gani, na wataitumia kwa manufaa yao
na si vinginevyo,” alisisitiza Mungy.
Alisema
mamlaka hiyo kazi yake kubwa ni kusimamia matumizi ya mitandao hivyo
kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, itahakikisha inadhibiti kwa
kuelimisha na kuwabaini wale wote wanaotumia vibaya mitandao hiyo.
“Kazi
yetu sisi si kuwakamata hawa wahalifu, sisi tunasimamia na tuna uwezo
wa kuwatambua wale wote wanaotumia vibaya mitandao hii hata kama
watabadilisha kadi zao za simu mara 300 na kubadili majina, tuna uwezo
wa kuwatambua na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria pale tunapotakiwa
kwa mujibu wa taratibu,” alisisitiza.
Alisema
tayari wameshaanza kampeni ya kuelimisha matumizi sahihi ya mitandao
kupitia vipindi na semina zinazojumuisha kada mbalimbali muhimu kama
vile wasanii na vyombo vya habari juu ya kujihadhari na matumizi mabaya
ya mitandao.
“Hivi
karibuni tulifanya semina ya wasanii ambao ndio waathirika wakubwa wa
matumizi haya ya mitandao na kuwaelimisha namna ya kuitumia mitandao
hii, pia vyombo vya habari tumevielimisha na kuvisisitiza kutotegemea
taarifa za mitandao hasa kipindi hiki cha uchaguzi kwa kuwa nyingi si
sahihi,” alisema bosi huyo wa TCRA.
Tayari
Rais Jakaya Kikwete ameshasaini Sheria hiyo ya Makosa ya Mtandao ya
Mwaka 2015 na inatarajiwa kuanza kufanya kazi rasmi Septemba mosi, mwaka
huu.
Sheria
hiyo katika eneo la adhabu kwa wahalifu wa mtandao pamoja na
wasambazaji wa picha za utupu na ngono, wasambazaji wa taarifa za uongo,
za kibaguzi na matusi na watu wengine wanaofanya udanganyifu unaohusu
kompyuta, adhabu ni kwenda jela hadi miaka 10 au kulipa faini
isiyopungua Sh milioni 50.
Kwa
upande wa kusambaza picha za ngono, matusi, uasherati atalipa faini
isiyopungua Sh milioni 30 au kwenda jela miaka 10 au vyote. Lakini mtu
atakayesambaza picha za utupu atalipa faini isiyopungua Sh milioni 20 au
kwenda jela miaka saba au kutumikia adhabu zote kwa pamoja.
Pia
kwenye muswada huo mtu ambaye atatoa taarifa, takwimu au maelezo kwa
njia ya picha, maandishi, alama au aina nyingine yoyote zikiwa ni za
uongo akipatikana na hatia atalipa faini isiyopungua Sh milioni tatu au
kutumikia kifungo jela kisichopungua miezi sita au vyote.
Kwa
upande wao, Jeshi la Polisi Tanzania, limesema tayari limeanza kuchukua
hatua dhidi ya watumiaji vibaya wa mitandao ya kijamii na hadi sasa
imekamata watumiaji hao wengi na wako katika hatua ya kuhojiwa na
wengine kufikishwa mahakamani.
“Natumia
fursa hii kuwaonya watu waache tabia ya kutengeneza ujumbe wa
uchochezi, matusi, uongo na uzushi kwa visingizio vya itikadi, dini na
siasa kwani Jeshi la Polisi halitovumilia tabia hizo na watakaobainika
watafikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema msemaji wa jeshi hilo, Advera Bulimba.
Alikiri
kuwapo na tabia ya watu kuandika kwenye mitandao ya kijamii taarifa za
uchochezi na uzushi dhidi ya watu maarufu wakiwemo viongozi au taasisi
na baadhi yao wanachunguzwa na wakibainika watachukuliwa hatua za
kisheria.
Alitolea
mfano wa mmoja wa watumiaji mtandao ambao jeshi hilo lilibaini
aliandika taarifa za uchochezi kuhusu tukio la ujambazi na mauaji la
Kituo cha Stakishari Ukonga jijini Dar es Salaam na sasa anakabiliwa na
kesi ya uchochezi mahakamani.
Mpekuzi blog
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena