Header Ads Widget

Responsive Advertisement

AFYA YAKO : Zijue hatua za mabadiliko yanayojitokeza katika ukuaji wa mtoto kimwili


Wazazi wenye watoto wadogo wanategemea wakue na baadae kuwa watu wazima wanaojitegemea na wanaweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Pamoja na kuwa na matarajio hayo wazazi wengi hawajui hatua ambazo watoto wao wanapaswa kuzipitia ili kufikia malengo hayo. Katika Makala hii, FikraPevu inakuletea ufafanuzi wa hatua husika.
Aina za mabadiliko katika ukuaji wa mtoto
Utafiti unaonyesha kwamba, watoto hupitia hatua kadhaa za mabadiliko yanayohusisha ukuaji wa kimwili na kiakili mpaka kufikia hatua ya kujitegemea.
Ukuaji wa kimwili unahusisha ongezeko la kimaumbile ambalo linaambatana na mabadiliko katika urefu, uzito, upana na kukua kwa ubongo kulingana na umri wa mtoto.
Mbali na mabadiliko ya kimwili, pia kuna mabailiko ya kiakili yanayojidhihirisha kupitia utendaji wa mtoto unaohusisha matumizi ya viungo mbalimbali vya mwili wake.
Lakini, ili mtoto akue vizuri kimwili na kiakili, anahitaji huduma muhimu kama vile  chakula kilicho na mchanganyiko wa virutubisho vyote na vyenye kutosheleza mahitaji ya mwili wa mtoto kulingana na umri wake. Pia anahitaji huduma za afya, uchangamshi, upendo, mafunzo ya awali, ulinzi, usalama na mazingira safi na salama.
Kwa ujumla, kadri mtoto anavyokua viungo vyake huongezeka ukubwa na ubongo huongezeka uzito. Pia, hupata uwezo wa kiakili unaomwezesha kujua kutumia viungo vyake katika kutenda mambo mbalimbali kama vile kuelewa mazingira yake, kutambua vitu mbalimbali, kuinua vitu, kutupa, kutembea, kukimbia, kucheza na kudaka.
Vigezo vinavyotumika kupima ukuaji wa mtoto kimwili
Mabadiliko yanayoambatana na ukuaji wa mtoto kimwili kulingana na umri yanaweza kupimwa kwa kutumia vigezo kadhaa. Kuna uzito; kimo; matumizi ya viungo mbalimbali vya mwili na jinsi anavyoweza kumudu viungo vyake kwa kufanya mazoezi ya viungo; na kupima mzingo wa mkono, kichwa na kifua.
Mwanzo wa ukuaji na maendeleo ya mtoto kimwili
Uhai wa mtoto huanza mara mimba inapotunga. Na ukuaji na maendeleo ya mtoto kimwili huanza siku hiyo. Mimba huchukua muda wa miezi 9 hadi mtoto kuzaliwa.
Lakini, ili mtoto aweze kuzaliwa akiwa mwenye afya nzuri mama mjamzito anapaswa kuhudhuria kliniki ya mama na mtoto mapema ili kupata huduma kadhaa.
Huduma hizi ni pamoja na elimu ya afya ya msingi, mfano umuhimu wa kumpunguzia mjamzito kazi, kupima ukuaji wa mimba, kuchunguzwa magonjwa yanayoweza kumuathiri mtoto kama vile kaswende, na kupata chakula chenye mchanganyiko wa virutubisho vyote vinavyotosheleza mahitaji ya mwili wa mama na mtoto aliyeko tumboni.
Huduma zingine ni pamoja na kupata chanjo ya pepopunda, kupata kinga ya magonjwa mbalimbali kama vile malaria, minyoo, na dawa za kuongeza damu.
Pia wanapaswa kuchunguzwa dalili za hatari kama vile kupanda kwa shinikizo la damu, kuvimba miguu, mtoto kulala vibaya tumboni, upungufu wa damu, maandalizi ya kujifungua salama, kupata ushauri nasaha kuhusu maambukizi ya virusi vya UKIMWI toka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) pamoja na kupima afya yake.
Mabadiliko yanayotokea mara baada ya mtoto kuzaliwa
Kwa kawaida mtoto anapozaliwa anapaswa kuwa na uzito usiopungua kilo 2.5. Anatarajiwa kuongezeka na kufikia kilo tano baada ya miezi 6 na kilo 7.5 baada ya miezi 12.
Lakini, mara baada ya mtoto kuzaliwa wazazi, walezi na jamii hawana budi kuendelea na kazi ya kumpatia mtoto malezi yanayohusisha matendo ya uchangamshi hadi anapofikia umri wa miaka minane.
Kwa ajili ya kuelewa maana na umuhimu wa pendekezo hili, hebu sasa tuangalie hatua mbalimbali anazopitia motto katikaukuaji wake.
Mabadiliko kati ya miezi sifuri mpaka miezi mitatu
Kati ya miezi sifuri mpaka mitatu, mtoto hutabasamu anapoonyeshwa tabasamu na mtu mwingine na huweza kufuatilia vitu vyenye rangi mbalimbali.
Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake muonyeshe mtoto tabasamu, mtazame machoni, jaribu kuongea naye au kumsemesha semesha, mwelekeze au mpe njia na mbinu za kuweza kuona, kusikia, kuhisi kujisogeza na kuchezesha viungo vyake vya mwili.
Mabadiliko kati ya miezi mitatu mpaka miezi sita
Kati ya miezi mitatu mpaka sita, mtoto anaweza kunyoosha na kuinua kichwa, anaweza kugeuka akisikia sauti, anaonja kila kitu, anaweza kukaa mwenyewe na anafuatilia vitu kwa macho.
Ili kumchangamsha mtoto na  kuchochea maendeleo yake jaribu kumpa vifaa vyenye rangi na vinavyotoa mlio, kumwimbia mtoto, kuongea naye, kumsaidia kujifunza kukaa na kumpa uangalizi wa kutosha.
Mabadiliko kati ya miezi sita mpaka miezi tisa
Kati ya miezi sita mpaka tisa, mtoto anaweza kuinuka na kukaa, anaweza kuokota punje ndogo ndogo kwa kutumia dole gumba na kidole kidogo, anaweza kutambaa na kujifunza kusimama.
Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake mpatie vitu visafi na salama kwa ajili ya kushika na kumpa uangalizi wa kutosha.
Mabadiliko kati ya miezi tisa mpaka miezi 12
Kati ya miezi tisa mpaka12, mtoto anaweza kusimama vizuri bila kuegemea kitu chochote na anaweza kutembea kwa kushikilia vitu, anaweza kupunga mkono na kupiga makofi.
Ili kumchangamsha mtoto na kuchochea maendeleo yake mpe mazoezi ya kusimama bila msaada na kumsaidia kutembea, mwonyeshe vitu vinavyoviringika na kumhimiza na kumpongeza anapofanikiwa kufanya kitu chochote.
Mabadiliko kati ya mwaka mmoja mpaka miwili
Kati ya mwaka mmoja mpaka miwili, mtoto anaweza kutembea vizuri, anaweza kusimama kwa mguu mmoja kwa msaada, anakimbia mbele na kinyume nyume bila kuanguka, anapiga mpira kwa miguuu, anaweza kuweka vitu kwenye chombo, anaweza kuiga kazi ndogo ndogo za nyumbani kama kufua, kupiga deki, kufagia na kupika pika.
Ili kumchangamsha mtoto na kuchochea maendeleo mpe vifaa vya michezo, mhimize kwenda mbele na nyuma bila kuanguka kwa njia ya michezo, mtume shughuli ndogo ndogo kama kuleta kikombe, mpe vitu anavyoweza kukusanya na kuviweka kwenye chombo na kuvitoa.
Mabadiliko kati ya miaka miwii mpaka mitatu
black-baby1
Kati ya miaka miwili mpaka mitatu, mtoto anaweza kuonyesha sehemu mbalimbali za mwili na anajifunza mwenyewe.
Ili kuweza kumchangamsha mtoto huyu na kuchochea maendeleo yake mfundishe michezo mbalimbali, mtengenezee vifaa vya michezo, mhimize kula mwenyewe na mwelekeze jinsi ya kula vizuri.
Mabadiliko kati ya miaka mitatu mpaka minne
Kati ya miaka mitatu mpaka minne, mtoto anaweza kuosha mikono mwenyewe, anaweza kucheza michezo ya kukimbizana, anaweza kuruka kwa mguu mmoja bila ya kuanguka na anajifunza kuvaa nguo mwenyewe. Ili kumchangangamsha na kuchochea maendeleo yake mwelekeze na kumhimiza kufanya mambo kwa usahihi.
Mabadiliko kati ya miaka minne mpaka mitano
Kati ya miaka minne mpaka mitano, mtoto anaweza kusimama kwa mguu mmoja bila kuanguka, anaweza kukimbia kufuata mstari ulionyooka na anaweza kuruka ruka mbele hatua kadhaa kwa mpangilio.
Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake mwepushe na michezo isiyo salama.
Mabadiliko kati ya miaka mitano mpaka saba
baby1
Na kati ya miaka mitano mpaka saba, mtoto anaweza kutupa na kudaka vitu bila kusaidiwa, anaweza kutupa kitu huku akilenga na anaweza kubeba vitu kutoka mahali hadi mahali pengine.
Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake mpe shughuli ndogo ndogo zitakazomjengea uwezo wa kujitegemea na mpe vifaa vya michezo ya kutupa na kulenga.
Hivyo, basi, wazazi wanashauriwa kuzisoma na kuzielewa hatua hizi za mabadiliko katika ukuaji wa watoto ili waweze kutimiza majukumu yao vema kama walezi

Post a Comment

0 Comments