Header Ads Widget

Responsive Advertisement

MAKALA | UJASUSI NDANI YA ULIMWENGU WA SOKA ( Kisa cha Ronaldo Kuugua Ghafla Siku ya Fainali 1998) | Sehem ya 1.

Related image
Ulimwengu wetu wote ni kama vile limashine limoja likubwa linaloendeshwa kwa mifumo kama kiwanda. Wazo hili la kuuona ulimwengu kama mashine inaleta wazo lingine mtambuka la kukufanya ufikiri kama ulimwengu ni limashine limoja likubwa basi pasina shaka kuna wenye kuiendesha mashine hii. Nasema kwamba wako wenye kuiendesha “mashine” hii kutokana na namna ambavyo kwa karne na karne tumeshuhudia matukio makubwa ambavyo awali tuliyaona yanatokea kwa sababu za asili lakini baadae tukafumbuka macho na kufahamu kuwa matukio hayo nyuma yake yalikuwa na uratibu wa binadamu wenzetu kwa makusudi kabisa.

Katika miaka ya hivi karibuni kuna masuala ambayo binafsi yangu nimekuwa nikiyatazama kwa namna ya tofauti kabisa nikijaribu kuyaelewa undani wake.

Yawezekana siku ya mapumziko kama leo hii uko umepumzika kwenye veranda ya nyumba yako labda ukiwa na kinywaji baridi cha kukonga nyoyo yako na pengine ukitazama mpira wa miguu au mchezo mwingine maarufu. 
Kwa milenia kadhaa sasa tangu binadamu kuwepo juu ya uso huu wa dunia michezo na mshindano ya kiathletiki imekuwa moja ya njia kuu ya binadamu kujiliwaza, kuonyeshaumahiri, uhodari na hata kujijengea utukufu wa nafsi.
Ni ajabu mno kwa namna ambavyo kwa karibia miongo mitatu ya hivi karibuni ulimwengu huu wa michezo na burudani umebadilika mno kutokana nao kuingia kwenye mtego wa kuratibiwa kwa urubuni na kuondoa dhana halisi ile ya asili iliyofanya suala hili kushamiri kwa milenia kadhaa.

Mpaka leo hii naikumbuka mechi ya mpira wa miguu ya kukata na shoka, fainali ya kombe la dunia ya mwaka 1998 kati ya mabingwa watetezi timu ya taifa ya Brazil na wenyeji wa kombe hilo mwaka huo, timu ya taifa ya Ufaransa. Nakumbuka nilikuwa bwana mdogo kabisa wa shule ya msingi… sikumbuki haswa mechi nyingine zote za mashindano yale ya lakini mpaka leo hii naikumbuka sawia kabisa mechi ya fainali kati ya Brazil na Ufaransa, naikumbuka kwa ufasaha kabisa kama niikumbukavyo hadithi ya Pamela na kipini niliyoisoma nikiwa darasa la pili.


Naikumbuka kwa usahihi kabisa siku ile ya tarehe 12 July 1998 usiku wa kama saa nne au tano usiku ambapo kutokana na uadhimu wa mechi ile ya fainali mzee wangu alinipa ‘ofa’ ya kwenda na mimi kutazama mechi hiyo pamoja na marafiki zake kwenye bar iliyoitwa ‘The New Weekend Bar’ ambayo ilikuwa maeneo ya Magomeni Mwembechai na ilikuwa kijiwe maarufu sana cha kutazama mpira enzi hizo.

Shauku yangu kubwa haikuwa fainali tu bali shauku yangu kuu zaidi ilikuwa ni kwenda kumtazama “Ronaldo de Lima”, mwanasoka ambaye mtaani watoto kwa wakubwa tulikuwa tunamuhusudu kama ‘masihi wa mpira’. Mwanasoka ambaye aikuwa kwenye kiwango cha juu kabisa cha utukufu wake wa umaarufu na uchezaji uwanjani. Nakumbuka katika miaka ile mtaani ndipo zilikuwa zimeingia bazoka ambazo ndani yake zimevingirishwa karatasi yenye picha za wachezaji mpira. Mitaa mingi hapa Dar es salaa wenye maduka walikuwa wanatoa ofa kama ukifanikiwa kununua bazoka na ndani yake ukapata picha ya Ronaldo basi unapata bazoka nyingine kumi kama zawadi. Watoto tulikuwa ukipewa hela ya kwenda kula chakula shule inaishia yote kwenye kununua bazoka ambazo hasa hatukuwa tunanunua ili tupate kumung’unya utamu wake, bali tulinunua bazoka ili tupate picha za wachezaji mpira, na haswa tulinunua tukisaka picha ya Ronaldo.


Ronaldo alipendwa, Ronaldo alihusudiwa, Ronaldo aliabudiwa… kwa hakika hakukuwa na wakufananisha na Ronaldo. Kwa kipindi kile kutokana na utoto sikujua hasa umaarufu ule wa Ronaldo ulitokana na nini haswa, nilichokijua tu ni kwamba kwa wakati ule hakukuwa na mtu ambaye alikuwa na uwezo wa kuugusa mpira kama Ronaldo. Miaka michache baadae ndipo nilifahamu kuwa licha ya uwezo mkubwa wa uchezaji uwanjani lakini pia umaarufu wa Ronaldo ulitokana na mafanikio makubwa ambayo alikuwa nayo kwa miaka ile. Ronaldo alikuwa ameenda kwenye kombe lile la dunia akiwa ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa FIFA kwa miaka miwili mfululizo, 1996 na 1997. Alikuwa ameshinda tuzo ya Balloon d’or mwaka uliopita 1997. Mwaka huo 1998 alikuwa pia ametamkwa kama mchezaji bora wa msimu kwa ligi ya Serie A ya Italia. Ronaldo alikuwa kwenye kiwango cha juu kabisa cha umashuhuri wake. Kwa hiyo katika kombe hili la dunia 1998 sio mtaani kwetu tu bali ulimwengu mzima macho yalikuwa kwa Ronaldo de Lima.

Licha ya msisimko ule ambao nilikuwa nao siku ile nilipokwenda kutazama mtanange ule na mzee wangu, nilijikuta narejea nyumbani machozi yakinitoka kutokana na kile ambacho kilitokea, kitu ambacho sikuamini macho yangu… kitu ambacho hakuna ambaye alikitegemea. Timu ta taifa ya Brazil ililala kwa kipigo cha goli tatu kwa sufuri huku Ronaldo akionyesha kiwango kibovu kabisa ambacho hakikuwahi kuonekana.


Kwa mara ya kwanza kabisa Nike walizindua viatu vya ufanisi wa hali ya juu katika mchezo wa soka na viatu hivi vilibuniwa na Ronaldo na timu yake ya ufundi na vilipewa jina la “Nike Mercurial” boots na kwa heshima ya Ronaldo vilipachikwa jina “R9” ambayo ni herufi ya kwanza ya jina la Ronaldo pamoja na namba ya yake ya jezi uwanjani. Viatu hivi ambavyo kwa sasa vinatumiwa na kupigiwa chapuo na wachezaji wakubwa kama Cristiano Ronaldo, Frank Ribery, Edzen Hazard, Raheem Sterling na wengineo wengi vikiwa kwenye toleo lake la kumi na moja na vikibeba majina tofauti tofauti dukani kama cr7 na kadhalika kwa mara ya kwanza ndio vilizinduliwa na Ronaldo de Lima mwaka huu 1998 na ni yeye na timu yake (na kushirikiana na timu ya ufundi ya Nike) walivibuni.

Kwa hakika lilikuwa ni dili nono, dili la kihistoria. Kwa hiyo Ronaldo alipoingia katika mashindano ya kombe la dunia alikuwa anaiwakilisha nchi yake lakini pia alikuwa na mzigo mkubwa zaidi wa kuiwakilisha kampuni ya Nike. Alikuwa na mzigo mkubwa sana kuhakikisha kwamba ulimwengu mzima uliokuwa unatazama ulikuwa unajua kuhusu toleo jipya la viatu mahususi kwa ajili ya mpira wa miguu, viatu vya “Nike Mercurial Boots”. Na si viatu peke yake bali pia alikuwa ameibeba bendera yote ya kampuni ya Nike. Kwa ulimwengu ambao ulikuwa unatazama ilionekana kwamba huli lilikuwa ni jambao jema sana la kupongezwa na kuhusudiwa pasina kujua kwamba dili hili lilikuwa ni mwiba ambao ulikuwa unaelekea kuigharimu timu ya taifa ya Brazil na ilikuwa kana ‘kitorondo alikuwa ameingia kwenye kokwa la embe’. Kwamba…
Wakati ulimwengu ukisheherekea dili hiyo ya Ronaldo na Nike, mpinzani wake mkuu kwenye kombe la dunia, Zinedine Zidane alikuwa pia amepewa dili nono la ubalozi wa kampuni ya Adidas mpinzani mkuu wa Kampuni ya Nike.

Kwa hiyo mechi ile ya fainali haikuwa tu ni kumenyana kati ya Brazil dhidi ya Ufaransa, bali pia ilikuwa ni mchuno kati ya Ronaldo na Zidane na pia mpambano kati ya Nike dhidi ya Adidas.
Sasa basi…

Siku ya fainali, yaani 12 July 1998 katika hoteli ambayo timu ya taifa ya Brazil ilikuwa imefikia kulikuwa na hali ya tofuti sana. Tofauti na siku zote ambapo walikuwa wanaondoka hotelini kwa shamra shamra kubwa wakicheza michezo ya samba, siku ya leo ilikuwa ya tofauti mno. Timu ya Brazil ilikuwa inaondoka kimya kimya wakiwa wameinamisha vichwa chini bila mbwembwe wala mikogo yoyote. Mashabiki ambao walikuwa wamejaa nje ya hoteli kuwashangilia kama ilivyo siku zote walishikwa na bumbuwazi kwani hii haikuwa Brazil ambao walikuwa wanaijua. Wachezaji walikuwa wanatoka hotelini wakiwa wamejiinamia na kuingia kwenye basi la kuwapeleka uwanjani kimya kimya bila hata kupungia mashabiki mkono. Huzuni ilikuwa haijifichi kwenye nyusio zao. Kwa wale ambao walibahatika kuwaona wakiwa wanatoka pale hotelini walijua dhahiri kabisa kwamba kuna suala kubwa haliko sawa sawa.

Mbaya zaidi ni kwamba kuna moja ya wahudumu wa hoteli alidai kwamba alimshuhudia kocha mkuu wa timu ya taifa ya Brazil Mario Zagolla akitoka kwenye chumba cha kulala cha Ronaldo akiwa analia.

Watu wakaanza kuhoji… kuna nini kinaendelea?? Wachezaji wa Brazil wakiongozwa na Dunga nao wakaanza kumshinikiza kocha kutaka kujua ni nini hasa ambacho kilikuwa kinaendelea?? Ndipo ambapo kocha hakuwa na namna nyingine zaidi ya kuwapasulia jipu kwamba Ronaldo hatocheza mechi hiyo ya fainali… hii ilikuwa pengine ni habari mbaya zaidi kwa wale wachezaji wa Brazil kuwahi kuisikia katika maisha yao yote ya soka. Ronaldo alikuwa ndiye tegemeo la timu, Ronaldo ndiye alikuwa kama ‘masihi’, kwa nini asicheze?? Mbaya zaidi hakuwa na majeruhi.

Taarifa hii ilianza kuvuja ndani kwa ndani… simu zikaanza kumiminika. Inasemekana mpaka rais wa nchi ya Brazil kipindi kile Fernando Cordoso alipiga simu kutaka ufafanuzi kwa nini Ronaldo hatocheza mchezo huo wa fainali. Ndipo hapo ambapo Mario Zagolla akiwa anabubujikwa na machozi akawatobolea siri kwamba, kwa mud wa masaa sabini na mbili yaliyopita Ronaldo de Lima amekuwa anadondoka kifafa na kupoteza fahamu hivyo hawezi kumchezesha kwa kuwa anahofia kuhatarisha maisha ya mchezaji wake.

Tukutane Tena Hapa Kumalizia Makala Hii Ya Kusisimu 


Source | Habib Anga (The Bold Instagram Page)

Post a Comment

0 Comments