Wakati Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaanza vikao vyake
mjini Dodoma tangu 26 Januari 2016, bado Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
haijamalizia uteuzi wa viporo vitatu vya ubunge wa viti maalum kutokana
na kutokamilika kwa kiporo cha uchaguzi wa ubunge katika jimbo la
Kijitoupele, kwenye mkoa wa Mjini Magharibi huko Zanzibar.
Kwa mujibu wa maamuzi ya NEC kupitia vikao vyake vilivyofanyika kati ya
tarehe 14 na 15 Januari mwaka huu, uteuzi wa wabunge hao watatu sasa
utafanyika baada ya kukamilika kwa kiporo hicho cha uchaguzi wa ubunge
katika jimbo la Kijitoupele. NEC haikutaja tarehe kamili ya uchaguzi
katika jimbo hili.
Hata hivyo, baadhi ya wadadisi wa mambo ya kisiasa hapa nchini,
wamekosoa uamuzi huo wa NEC kwa kuwa kiporo cha uchaguzi katika jimbo la
Kijitoupele hakiwezi kubadilisha takwimu za matokeo ya uchaguzi viporo
kama zinavyosimama leo.
Jimbo la Kijitoupele ni miongoni mwa majimbo nane ya uchaguzi ambayo
hayakufanya uchaguzi tarehe 25 Oktoba 2015 kwa sababu mbalimbali. Kwa
mujibu wa takwimu rasmi za NEC, jimbo hili linao wapiga kura 18,016
pekee.
Majimbo mengine saba, yakiwa katika mtiririko wake wa kialfabeti ni:
Arusha Mjini (Arusha), Handeni Mjini(Tanga), Ludewa (Njombe), Lulindi
(Mtwara), Lushoto (Tanga), Masasi Mjini (Mtwara), na Ulanga Mashariki
(Morogoro). Tayari majimbo haya saba yamemalizia viporo vya uchaguzi.
Mwanasiasa mmoja, ambaye hakupenda jina lake litajwe, ameiambia
FikraPevu
kwamba kulingana na matokeo ya chaguzi ndogo ambazo zimekamilika mpaka
sasa, CCM wana viti viwili, CHADEMA kiti kimoja, na vyama vingine havina
kitu.
Kwa mujibu wa matangazo ya NEC kupitia wasimamizi wa uchaguzi wa
majimbo, matokeo ya ubunge katika majimbo haya saba yanaonyesha kuwa
kura zimegawanyika kivyama kama ifuatavyo:
Kati ya jumla ya kura halali 262,465 zilizopigwa, CCM wamepata kura
150,072 sawa na asilimia 57.18, CHADEMA kura 92,958 sawa na asilimia
35.42, na vyama vingine kura 21,143 sawa na asilimia 8.06.
Kwakuwa kuna viti vitatu ambavyo ni viporo, hii maana yake ni kwamba CCM
wanastahili viti 1.72, Chadema viti 1.06, na vyama vingine viti 0.24.
Tukikaribisha takwimu hizi kwa namba nzima iliyokaribu, tunaona kwamba
hatimaye CCM watapata viti viwili, CHADEMA kiti kimoja, na vyama vingine
viti sifuri.
Hivyo, ni kweli kwamba mgawanyo huu wa nafasi tatu za viti maalum
ambavyo ni viporo hauwezi kubadilishwa na uchaguzi kiporo wa Kijitoupele
Zanzibar kwa sababu iliyo wazi.
Kwa mujibu wa takwimu zililizo katika tovuti ya NEC, katika mwaka 2015, Jimbo la Kijitoupele, lilikuwa na wapiga kura 18,016 tu.
Hata kama wapiga kura hawa wakijitokeza wote katika uchaguzi
unaosubiriwa, halafu idadi hii ikaongezwa kwenye kura za sasa za CCM, au
kura za sasa za CHADEMA, au au kura za sasa za chama kingine chochote
cha siasa, hakutakuwa na mabadiliko yoyote katika mgawanyo wa nafasi
hizi.
Kwa sababu hii, wadau wa siasa wanasema kuwa, NEC ingekuwa imetenda haki
zaidi kwa taifa kama ingewatangaza sasa hivi wabunge viporo kupitia
utaratibu wa viti maalum, ili waungane na wenzao Dodoma kuanzia tarehe
26 Januari 2016.
Kama kura zilizotokana na chaguzi viporo mpaka sasa zitafanyiwa
mchanganuo kimajimbo kwa kuzingatia vyama na wagombea wake walioshiriki
uchaguzi, mgawanyo ni kama ifuatavyo:
Kutokana na kiporo cha uchaguzi katika jimbo la Arusha Mjini matokeo
yalikuwa kama ifuatavyo: Godbless Lema (CHADEMA) kura 68, 848, Philemon
Mollel (CCM) kura 35,907, Voi Mollel (ACT-Wazalendo) kura 342, Zuberi
Mwinyi (CUF) kura 106, na Mkama Jralya (NRA) kura 43.
Kutokana na kiporo cha uchaguzi katika jimbo la Handeni Mjini matokeo
yalikuwa kama ifuatavyo: Omari Kigoda (CCM) kura 10,315, Shundi Aidan
(CUF) kura 2,419, Daud Lusewa (CHADEMA) kura 648, Doyo Hassani (ADC)
kura 184, Bakari Makame (TLP) kura 19, na Bakari Mhina (AFP) kura 06.
Kutokana na kiporo cha uchaguzi katika jimbo la Lulindi matokeo yalikuwa
kama ifuatavyo: Jerome Bwanausi CCM kura 17,715, Modesta Makaidi (NLD)
kura 1,638, Amina Mshamu (CUF) kura 714, na Francis Ngaweje (ACT) kura
213.
Kutokana na kiporo cha uchaguzi katika jimbo la Lushoto matokeo yalikuwa
kama ifuatavyo: Shaaban Shekilindi (CCM) kura 19,775, Dickson Shekivuli
(Chadema) kura 4,402, Majabu Kusaga (ACT-Wazalendo) kura 350, Salimu
Kaoneka (CUF) kura 350.
Kutokana na kiporo cha uchaguzi katika jimbo la Masasi Mjini matokeo
yalikuwa kama ifuatavyo: Rashid Chuachua (CCM) kura 16,597, Ismail
Makombe (CUF) kura 14,019, Swaleh Ahmad (Chadema) kura 512, Omary
Timothy (ACT-Wazalendo) kura 347, na Angelus Thomas (NLD) kura 70.
Kutokana na kiporo cha uchaguzi katika jimbo la Ulanga Mashariki matokeo
yalikuwa kama ifuatavyo: Goodluck Mlinga (CCM) kura 25,902, Pankras
Ligongoli (Chadema) kura 10592, na Issaya Maputa (ACT-Wazalendo) kura
626.
Na kutokana na kiporo cha uchaguzi katika jimbo la Ludewa matokeo
yalikuwa kama ifuatavyo: Ngalawa Deogratias (CCM) kura 23,861 na
Msambichaka Mkinga (Chadema) kura 7,956.
Kwa mujibu wa NEC, kanuni inayotumika kukokotoa idadi wa wabunge wa viti
maalum inaonyesha kwamba, mwaka huu kuna jumla ya viti maalum 113. Viti
hivi ni sawa na asilimia 40 ya wabunge wote 281wanaopaswa kuwemo
katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka huu.
Mpaka sasa, wabunge wa Viti Maalum 110 wamekwishatangazwa na NEC. Kati ya hawa wabunge 110, CCM walipata viti 64
CHADEMA viti 36, na CUF viti 10. Vyama vingine havikupata chochote kwa
kuwa havikutimiza asilimia tano ya kura zote za ubunge wa kuchaguliwa
kama inavyotakiwa na ibara ya 78 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, 1977.
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena