Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipewa maelezo ya zana mojawapo ya 
Kivita katika Zoezi la Onesha Uwezo Medani Mkoani Arusha. Picha na IKULU
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 
Dkt. John Pombe Magufuli amefunga “Zoezi la Onesha Uwezo Medani” 
lililoandaliwa na kutekelezwa na Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu ambalo ni
 sehemu ya Jeshi la wananchi Tanzania katika eneo la Lang’arurusu nje 
kidogo ya Chuo Cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli Mkoani Arusha.
Akizungumza na Askari na Maafisa wa Jeshi
 la wananchi Tanzania kabla ya kufunga zoezi hilo, Rais Magufuli amesema
 katika awamu yake ya tano ya uongozi amedhamiria kulitumia Jeshi la 
wananchi Tanzania katika kujenga uchumi, ikiwemo kuanzisha viwanda na 
kampuni za ujenzi ili kuharakisha maendeleo.
Ametoa mfano wa kiwanda cha Nyumbu 
ambacho kipo chini ya jeshi la wananchi Tanzania na kueleza kuwa wakati 
umefika wa kukiimarisha na kukiendeleza kiwanda hicho, ili kiweze 
kufanya uzalishaji mkubwa kwa manufaa ya nchi ikilinganishwa na hali 
ilivyo hivi sasa.
“Zipo nchi nyingi ambazo majeshi yao 
yanatumika katika uchumi na yanafanya kazi nzuri ya kupigiwa mfano, 
wakati umefika na sisi kufanya hivyo. Hata hizi sare za jeshi na viatu, 
hatuna sababu ya kuvinunua kutoka nje ya nchi, tunaweza kutengeneza sisi
 wenyewe” Alisisitiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la 
wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kuandaa “Zoezi Onesha Uwezo Medani” 
ambalo limethibitisha uwezo, weledi na utayari lilionao katika jukumu 
lake la kiulinzi.
Ameahidi kuwa ataendeleza juhudi 
zilizofanywa na viongozi wenzake waliotangulia za kuliimarisha kwa 
vitendea kazi na maslai ya wanajeshi ili liweze kutekeleza wajibu wake 
bila vikwazo.
Pamoja na kuwapongeza Askari na maafisa 
wa Jeshi la wananchi Tanzania walioshiriki katika zoezi hilo, Rais 
Magufuli ameagiza Askari Mgambo na Askari wa Jeshi la kujenga Taifa 
(JKT) walioshiriki zoezi hilo kuajiriwa na jeshi la wananchi Tanzania.
Akitoa maelezo ya awali kabla ya hotuba 
ya Rais Magufuli, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. 
Hussein Ali Mwinyi, amesema Wizara yake itaongeza na kusimamia juhudi za
 kuliboresha jeshi hilo kwa zana, vifaa na maslai kwa wanajeshi ili 
kuwajengea uwezo na morali ya kutekeleza majukumu yao ya kuilinda nchi, 
pamoja na kutoa msaada stahiki kwa nchi zenye kuhitaji ulinzi wa amani 
popote duniani.
Kwa upande wake Mkuu wa majeshi ya Ulinzi
 nchini, Jenerali Davis Adolf Mwamunyange amemhakikishia Rais Magufuli 
kuwa Jeshi la wananchi Tanzania lipo imara na litaendelea kutekeleza 
majukumu yake kwa weledi, nidhamu ya hali ya juu na uzalendo mkubwa.
Kabla ya kuwahutubia maafisa wa jeshi la 
wananchi, Askari na wananchi waliohudhuria ufungaji wa “Zoezi Onesha 
Uwezo Medani”, Rais Magufuli ameoneshwa zana mbalimbali za kivita ikiwa 
ni pamoja na kushuhudia upigaji wa mizinga ya masafa mafupi, masafa ya 
kati na masafa marefu.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha
22 Januari, 2016

0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena