Header Ads Widget

Responsive Advertisement

UTAFITI: kampuni zilizowekeza katika mafuta na gesi Tanzania



JACKA Resources Limited ni kampuni ya Australia ambayo imeandikishwa pia kwenye Soko la Hisa la Australia (ASX: JKA) ikijihusisha na utafiti wa mafuta na gesi ikiwa imewekeza kwenye nchi za Australia, Tunisia, Nigeria, Tanzania na Somalia.
Kwa ujumla, kampuni hii imelenga uwekezaji katika Bara la Afrika na katika uwekezaji huo mpaka sasa inajivunia kusimamia rasilimali za mafuta zenye akiba ya mapipa takriban milioni 133 ambayo yamethibitishwa katika maeneo husika.
Nchini Tanzania, Jacka Resources inamiliki asilimia 100 katika kitalu cha Ruhuhu mkoani Ruvuma ambako inatafiti mafuta, lakini huko Tunisia inamilikia asilimia 15 katika Kitalu cha Bargou na nchini Nigeria inamiliki asilimia 5 katika Kitalu cha Aje Fields (OML113).

Uwekezaji Tanzania
Leseni ya Bonde la Mto Ruhuhu kusini-magharibi mwa Tanzania inahusisha eneo la kilometa za mraba 10,343 ambapo Jacka Resources ndiye mwendeshaji mkuu ikifanya utafiti wa mafuta kwenye eneo hilo ambalo ni mfumo wa Bonde la Ufa la Afrika Mashariki.
Eneo hilo la Bonde la Ruhuhu linahusisha pia sehemu ya Ziwa Nyasa na kwa namna mfumo wa bonde hilo unavyoshabihiana, kuna uwezekano wa kugundulika kwa mafuta kama ilivyotokea katika nchi za Uganda na Kenya.
Kwa ujumla, eneo la Bonde la Ruhuhu pamoja na sehemu ya Ziwa Nyasa ambayo ni sehemu ya Bonde la Ufa la Afrika Mashariki, linafahamika kuwa na hazina kubwa ya makaa ya mawe aina ya Permian pamoja na masalia mengi ya viumbehai. Makaa hayo ya mawe na masalia ya viumbehai yanaonyesha Dhahiri kwamba kunaweza kuwepo na kiwango kikubwa cha gesi pamoja na mafuta.
Upitiaji wa kina wa leseni ya eneo hilo ulikamilika katikati ya mwaka 2014 na sasa ndio unaotumika kama mwongozo wa program ya utafiti ambapo maandalizi rasmi ya utafiti wake yalianza Desemba 2014.
Taratibu za awali zitakapokamilika, uchimbaji utaanza mara moja ili kuanza rasmi utafiti huo kwa kutumia taarifa zilizopatikana.
Kampuni hiyo kwa kutumia kampuni ya ushauri kutoka Marekani, ilianza kushawishi wengine waingie nayo ubia kwenye eneo hilo, ikiwa inalenga kampuni za kimataifa, kabla yenyewe haijaanza kutoa fedha zake kuanza utafiti.
Nigeria
Katika eneo la Aje Field ambalo liko kitalu cha OML113, takriban kilometa 24 baharini magharibi mwa Nigeria, Jacka ina asilimia 2.667 za ushiriki kwenye leseni, asilimia 6.675 za uchangiaji na asilimia 5.0006 za faida ya mapato. Leseni hiyo ipo katika eneo maarufu ambalo gunduzi nyingi za mafuta zimefanyika kati ya Nigeria na Ghana katika miaka ya karibuni.
Mwendeshaji mkuu ni kampuni ya Yinka Folawiyo Petroleum na mshauri wa ufundi ni kampuni ya Folawiyo Aje Services Limited, ambayo ni kampuni ya ubia. Washirika wengine kwenye ubia huo ni New Age (32.077% za uchangiaji), FHN (22.5% za uchangiaji), EER (22.5% za uchangiaji) na Panoro (16.255% za uchangiaji).
Eneo la OML113 lina kilometa za mraba 835 na kina cha maji kutoka meta 100 hadi 1,500. Visima vingi vimekwishachimbwa katika eneo hilo tangu mwaka 1996 na kuthibitika kuwepo kwa ya akiba ya mafuta.
Kitalu cha Bargou
Nchini Tunisia, Jacka inamiliki asiimia 15 katika Kitalu maarufu cha Bargou kwenye ghuba ya Hammamet. Ubia huo unahusisha kampuni za Dragon Oil (55%), Cooper Energy (30%) na Jacka yenyewe.
Sekta ya mafuta na gesi nchini Tunisia ni maarufu Zaidi ambapo kuna visima zaidi ya 45, mitambo ya kusafisha na miundombinu mingine ya kusafirishia katika masoko ya Ulaya.
Kitalu cha Odewayne
Jacka imefanya utafiti wa mafuta katika eneo la Kitalu cha Odewayne ambapo mkataba huo (PSA) unahusisha eneo lenye ukubwa wa kilometa 22,000 nchini Somalia likihusisha vitalu vya SL6, SL7 na SL10 ambao ulisainiwa mwaka 2005.

Post a Comment

0 Comments