Header Ads Widget

Responsive Advertisement

INJILI | MASALIO NA UTUME WAKE

Utangulizi


Kanisa la ulimwenguni linajumuisha wale wote ambao kwa kweli wanaoamini katika Kristo lakini katika siku za mwisho wakati wa kuenea kwa uasi, watu wa masalio wameitwa watoke wazitunze amri za Mungu na imani ya Yesu. Hawa masalio wanatangaza saa ya kuja kwa hukumu, wakihubiri wokovu katika Kristo, na kupiga mbiu ya kukaribia kuja kwake mara ya pili. Tangazo hilo linawakilishwa na mfano wa malaika watatu wa Ufunuo 14; linaambatana na kazi ya toba na matengenezo duniani. Kila muumini anatakiwa binafsi kuwa na sehemu katika ushuhuda huu wa ulimwenguni mwote.” (Uf. 12:17; 14:6-12; 18:1-4; 2Kor.5:10; Yuda 3, 14; 1Pet. 1:16-19; 2Pet.3:10-14; Uf. 21:1-14)
Jukumu la kuchukua utume ni la kila muumini ulimwenguni mwote, lisifikiriwe kuwa ni kazi ya kikundi Fulani tu au ya viongozi wa kanisa, bali ya watu wote. Katika hali yoyote ile sharti tuwe na nia ya kuutangaza ujumbe wa Kristo kiusahihi. Kmbuka, Joka limeangusha theluthi ya malaika na linavizia mtoto azaliwe na mwanamke ili amle. Likiweza, litakuwa limeshinda vita. (Uf.12:4, 7-9). Joka linarukia lakini mtoto ananyakuliwa na Mungu. Mwanamke anajificha nyikani kwa muda wa siku 1260. (Uf. 12:6, 13, 14).
Kushindwa kwa shetani pale msalabani Yoha 12:31 lilikuwa ni tendo la ushindi mkuu si duniani tu bali hata mbinguni; Uf. 12:10, 11) Ili kutuliza hasira zake, Joka amekuwa akimsumbua mwanamke (Uf. 12:13) na mwanamke alijificha nyikani. Baada ya miaka 1260, Joka anakasirikia masalio, na kufanya vita na wazao wake waliosalia (Uf. 12:17).
Mwanzo wa Masalio
Kanisa la awali lilipouacha upendo wake wa kwanza kama ilivyotabiliwa katika Ufunuo 2:4, liliacha usafi wa mafundisho ya kweli, viwango vya juu vya maisha ya ukristo vilishushwa chini na kufutilia mbali mivuto ya Roho Mtakatifu kwa madai ya kuvuviwa nuru mpya. Umaarufu na uwezo binafsi wa watu vikaanza kutumika kuchagua viongozi. Usimamizi wa Kanisa chini ya Roho Mtakatifu uliachia urasimu wa kikasisi chini ya Askofu.
Hivyo uongozi wa Kanisa ukafikiriwa kuwa ndiyo utawala wenye mamlaka ya juu ya Kanisa; kuanzia hapo viongozi wakakoma kuwa watumishi wa wote badala yake wakafanywa wapatanishi wa mwanadamu na Bwana. (SDA Bible Commentary 4 uk. 385).
Chini ya mfumo huo wa uasi, kanisa la kikristo lilianza kuzama kwenye uasi zaidi. Mnamo mwaka 533 Baada ya Kristo, kwenye Amri za Justianian, iliwekwa ibara ya kumtambua Askofu wa kanisa la kikristo lililoko Rumi alitawazwa kuwa kiongozi wa makanisa yote ulimwenguni pote; pamoja na uwezo wake wa kuwatenga walioitwa wazushi. Askofu huyu wa Rumi alipata uhuru zaidi Mwaka 538, baada ya utawala wa Ostrogoth kuondoshwa. Hata hivyo kuondoshwa kwa utawala wa waostrogoth ulikuwa ni utimilizo wa unabii wa Danieli uliotabiliwa kuwa pembe ndogo ingeliziondoa pembe tatu. Hivyo akapata madaraka zaidi kutumia waraka wa Justinian wa mwaka 533.
Na huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa miaka 1260 ya mateso ya watu wa Mungu iliyotabiriwa (Dan. 7:25, Uf. 12:6, 14; 13: 5- 7). Wakristo wengi waliacha imani yao kwa kuhofia mateso makali sana yalioyakabili waliokuwa wakipinga utawala huu wa Askofu wa Rumi, na baadhi yao waliuawa sana hata waliosalia kuitetea imani ya watakatifu wakawa wachache sana.
Kabla ya matengenezo, sauti zilisikika ndani ya kanisa zikipinga kuua waprotestanti pasipo huruma, madai ya uwongo ya mamlaka ya kanisa na ufisadi. Hatimaye mwaka 1798, Kanisa hili la kikristo lilipata jeraha la mauti kama ilivyotabiliwa katika Ufunuo 13: 3. Berthier, Jemedari wa Napoleon, alifika Rumi na kumteka askofu mkuu wa Rumi yaani Papa Pius VI, ambaye alifia uhamishoni. Tendo hilo lilikuwa utimilizo wa unabii mkuu wa siku za mwisho.
Kushuka chini kwa viwango vya juu vya maisha ya ukristo ndani ya kanisa la kikristo na kufutilia mbali mivuto ya Roho Mtakatifu kwa madai ya kuvuviwa nuru mpya yaliyotokea zama za giza ni matokeo ya kuyakataa Mafundisho ya kweli na kuyageukia mafundisho yasiyofuata Biblia. Hali hii ni dhahiri kuwa hata leo yaweza kujitokeza tena; kwa mtu mmoja mmoja ndani ya kanisa anapoyakataa mafundisho ya kweli ya kanisa na kuyaambata yale ya uwongo anajifungamanisha mwenyewe na ibilisi sawasawa na uasi ulivyojiingiza kanisani zama za kanisa la awali.
Waprotestant wamekuwa wakiyataja mafundisho yaliyoshusha hali ya kiroho ya kanisa la awali kuwa ni pamoja na: -
1. Kiongozi wa kanisa kuwa Mungu duniani na mwakilishi wa Mwana wa Mungu duniani; cf. Mt. 23:9)
2. Utakatifu wa Kanisa na kiongozi wake – Kanisa linadai halijapata kukosea na halitakaa likosee wala kiongozi wake hawezi kukosea. Uf. 14: 8, Uf. 18:1-3)
3. Kanisa peke yake ndilo lenye uwezo wa kutoa Wokovu kwa wanadamu; Hoja hii hujaribu kuzima huduma ya Yesu ya Upatanisho (c/f Ebr. 4:16)
4. Wokovu kwa njia ya matendo; husaidia kufuta dhambi zilizofanywa baada ya ubatizo (c/f Rum. 3: 20)
5. Usawa wa mamlaka kati ya mapokeo (human experience) na maandiko matakatifu (Biblia)
6. Kanisa lina mamlaka ya kufanya mabadiliko yoyote ya kimaandiko chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu na uzoefu wa watawala.
Kuanzia karne ya 14 wanamatengenezo waliinuka wakiwamo John Wycliffe, Martin Luther wakipinga ibada za watakatifu kama Maria, fundisho la pagatori, namna ya kuadhimisha Meza ya Bwana na mafundisho mengine ya uongo kama yaliyoorodheshwa hapo juu.
Kushindwa kuendelea kwa matengenezo
Kama ilivyokuwa ujio wa Yesu Kristo mara ya kwanza, ulivyotanguliwa na ujio wa Yohana mbatizaji kutengeneza njia ya Bwana, ndivyo ilivyokuwa kuinua kwa Matengenezo ya kanisa la Kikrsto zama hizi za uasi. Karne ya 16 matengenezo yalikuwa yamefanya kazi kubwa ila hayakukamilisha kuileta nuru ya Biblia yote ndani ya kanisa. Mafundisho ya ubatizo wa kuzamisha majini, kutokufa kwa roho, Sabato ya kweli ya siku ya saba, kuadhimisha meza ya Bwana kwa kutawadhana miguu bado yaliachwa gizani.


KUTIMIA KWA UNABII WA MASALIO


Pamoja na uasi na mateso makali toka kanisa la rumi ya miaka 1260, baadhi ya waumini wakristo waliendelea kuakisi usafi wa kanisa la mitume. Wakati mateso yalipokoma mnamo mwaka 1798, (mwaka wa kutimia kwa unabii wa miezi 42) Joka alikuwa ameshindwa kufutilia mbali watu waaminifu wa Mungu. Yohana anasema, Joka akamkasirikia mwanamke, akaenda zake kufanya vita na wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu na kuwa na ushuhuda wa Yesu (Uf. 12:17).
Usemi huo wa Yohana Uzao uliosalia (Remnant) ulimaanisha mabaki. Masalio ni akina nani? Biblia inawaonyesha kuwa ni kundi la watu wa Mungu ambao pamoja na majanga, vita na uasi, bado wamebaki kuwa watiifu kwa Mungu kiukamilifu kwa kanuni zile zile za uchaji Mungu kama ilivyokuwa kwa watakatifu waliowatangulia wa zama za kale. Na hivyo watu hao waliosalia wanao sifa sawasawa na zile za manabii wa kale; yaani ni mabaki ya watu wa imani ya kale.
Hawa ndio wanaotumika kupandikiza kanisa la Mungu linaloonekana hadi leo ulimwenguni. Hawa ndio wasiotiwa unajisi pamoja na wanawake, kwa maana ni bikira. Hawa ndio wamfuatao Mwana-Kondoo kila aendako. Hawa wamenunuliwa katika wanadamu, malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo. Na katika vinywa vyao haukuonekana uongo. Maana hawana mawaa UFu 14:4-5. yaani hao ndio wazishikao Amri za Mungu na kuwa na ushuhuda wa Yesu. (2Nyak. 30:6; Ezr. 9:14, 15; Isa. 10: 20-22; Yer. 42:2; Eze. 6:8; 14:22).
Maandiko yakiwachambua watu wanaopaswa kuwa masalio inaoneshwa kuwa
1. Wana imani ya Yesu (Uf. 14:12) yaani wanatangaza habari njema kama ushuhuda kwa wanadamu (Uf.14: 6, 7; 10:11 Mt. 24:14)
2. Wanatii amri za Mungu; Kwa neema waliyopewa na Kristo, wanatii amri za Mungu zisizobadilika (Kut. 20: 1- 17; Mt. 5: 17-18; 19: 17; Wafil. 4:13)
3. Wana ushuhuda wa Yesu ambao ni Roho ya Unabii (Uf. 19:10). Ni kazi ya Roho kwa njia ya karama kuukamilisha mwili wa Kristo hadi utimilike (Efe. 4:12, 13).
4. Kuinuka kwake, kunakuja baada ya miaka 1260 yaani baada ya mwaka 1798 na kushambuliwa na Shetani (Uf. 12:6, 17).
5. Wanamfuata mwanakondoo kila aendako; wanaenenda kama Yesu alivyoenenda (1Yoh.2:6), Wanatii amri za Mungu kama Yesu alivyozitii (Yoh. 15:10). Kwa kuwa ni masalio, matendo yao lazima yafanane na imani ya watakatifu waliotangual yaani mitume na Manabii, la sivyo si kila mtu amwitaye Yesu atauona uzima (Mt. 7:21).
Utume wa Masalio
Kutimia kwa unabii huu wa kufunuliwa kwa kundi hili maalumu la masalio ulikuwa ni mwanzo wa utume wao. Mungu aliagiza masalio watangaze haki yake ulimwenguni na katika mlima Sayuni (Isa. 37:31, 32; 66: 20 c/f Uf. 14:1). Pamoja na utume huu wa kipekee, wengi wa masalio wametanga mbali na kuziendea njia zao mbaya kwa kuuacha utume wao pekee waliopewa na Mungu kuutangaza kwa mataifa na kujiinua nafsi (Rejea somo la masalio)
Unabii huu wa Ufunuo ndiyo unaodhihirisha utume wa Masalio. Kutangaza ujumbe wa malaika watatu wa Ufunuo 14: 6 - 12 kurejesha ukweli wa injili kabla Yesu hajarejea. Kutangaza haki ya Mungu, hukumu na ijili ya milele Matha 28:19-20
Ujumbe wa Malaika wa Kwanza (Uf. 14:6, 7), Ujumbe unotagaza toba ya kweli kwa ulimwengu kumwendea muumbaji (Mith. 8:13. Injili ya milele ni habari ile njema iliyohubiriwa na mitume (Ebr. 4:2 na kuzaa matunda (Yoh. 15:8). Pia tumeitwa kumtukuza Mungu katika miili yetu (1Kor. 6:19, 20) na kwa tendo lolote tunalotenda; naam hayo ndiyo mapito ya mitume na manabii (1Kor. 10:31). Hukumu inamaanisha mchakato wote wa uchunguzi hadi kufikia kuachiliwa au kupewa kifo (mt.16:27, Rum. 6:23 na Uf. 22:12). Saa ya hukumu pia yatangaza hukumu ya Mungu kwa uasi (Dan. 7:9-11, 26 na Uf. 17, 18). Ujumbe wa malaika wa kwanza pia unatuita kumwabudu Muumbaji aliyeumba mbingu na nchi na chemichemi za maji (Uf.14:7 c/f Kut. 20:11). Hivyo ujumbe huu unauita ulimwengu kuikumbuka sabato ya siku ya saba ya juma. Hatimaye, ujumbe huu hurejeza sheria ya Mungu iliyovunjwa na mtu wa kuasi (2Thes. 2:3).
Kwa ufupi, Mungu anaita wanadamu wamwabudu katika roho na kweli. Ndiye aliyewaumba na ndiye atakayewakomboa.
Ujumbe wa Malaika wa Pili (Uf.14:8) Tangu awali, jiji la Babeli lilijidhihirisha kuwa kinyume na Mungu. Mnara wake ulikuwa kituo cha uasi (Mwa. 11:1-9), Lusifa (Shetani) alikuwa kiongozi wake asiyeonekana (Isa. 14;4, 12 -14)na alitaka kuifanya Babeli kuwa kiongozi wa kutawala dunia yote. Wakristo wa awali waliita Rumi Babeli (1Pet. 5:13). Babeli ni mama wa makahaba (Uf. 17:5). Huwakilisha utawala utakaompinga Mungu (Uf. 13:15-17). Ujumbe wa malaika wa pili unasema Babeli ndiyo iliyonywesha dunia mvinyo wa uasherati. Uasherati ni mahusiano ya Babeli na Mataifa, hapo kanisa linapoacha mume wake ambaye ni Yesu (Eze.16:15, Yak. 4:4). Babeli inaanguka kwa kuwa inakataa Ujumbe wa Malaika wa Kwanza. Mwisho wa wakati, Mungu atawaita waumini wake watoke humo. (Uf. 18:1-4) yaani, mpango wowote wa wokovu usiomhusisha Mungu lazima utashindwa.
Ujumbe wa Malaika wa Tatu (Uf. 14:9-12), ni onyo kali la Mungu kwa wanadamu ambao waliukataa ukweli Mungu na kuziendea ibada ya uwongo. Ibada hii ya uwongo itakayoshinikizwa baada ya muungano wa serikali za kidunia na mamlaka ya kanisa la kikristo duniani itatengeneza sabato bandia kuwa kiini cha ibada ya Mungu wa Kweli. ((1Thes. 2:2-4; Dan. 7:8, 20-25; 8:9-12). Hatimaye, suala la ibada ya kweli na ya uongo ndiyo yatakuwa masuala yanayohusu pambano kuu la mwishoo la historia ya dunia. Wakati serikali kuu za dunia zikifanya makubaliano ya kuisimika sabato bandia chini ya mwamvuli wa imani za kikristo zilizofungamanishwa pamoja kuunda umoja wa kidini, ndilo tendo pekee litakalozalisha Sanamu ya mnyama. Kama ilivyokuwa nyakati za mfalme Nebukadneza wa babeli alivyosimamisha sanamu katika uwanja wa dura, hivyo hivyo muunganiko huo wa makanisa ya kikristo na serikali yatakavyosimamisha sanamu ya mnyama yaani sabato bandia kuwa siku pekee ya kuabudu kwa wakristo wote badala ya sabato ya kweli ya Biblia kama ilivyo sasa.
Ni katika zama hizi zilizotabiliwa ambao maisha ya uchaguzi wa mwanadamu yatakuwa chini ya utawala wa mwovu. Watu wote watalazimishwa kufuata alama ya mnyama kama ilivyokuwa wakati wa sanamu ya Nebukadneza. Wanaheri wale nanaofanya uchaguzi wa kumtumikia Mungu wa kweli tangu sasa, maana uchaguzi wa wakati huo hautakuwa rahisi kama ilivyo sasa. Kwa kuwa atakayechagua alama ya mnyama, atakutana na ghadhabu ya Mungu na atakayemchagua Mungu atakutana na hasira za Joka (Uf.12:17). Hata hivyo, tunalotumaini katika Kristo Yesu; maana ni katika Wakati huo Mikaeli atasimama, jemadari mkuu, asimamaye upande wa wana wa watu wa Mungu kama alivyosimama kwa Anania, Azaria na Mishaeli katika tanuru la Moto, naye tatsimama ili kuwaokoa watakatifu wake dhidi ya hasira za joka. Pamoja na mateso na taabu kali ambazo mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo Masalio wa Mungu wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile cha uzima. Daniel 12:1. Baada ya mateso na kipindi hiki kigumu cha taabu hatimaye Bwana Yesu Kristo atashuka na kuwalipa kila mmoja sawa sawa na Kazi yake. Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya Yesu anasema “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo” Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele. Na walio na hekima watang'aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang'aa kama nyota milele na milele.
Ni wazi kuwa maamuzi ya njia yunayoichagua leo au tutakayoichangua siku zijazo ndiyo yatakayobainisha mwelekeo wa maisha yetu katika pambano hili la mwisho wa wakati. Wapo wanadamu wengi wanaoshindwa kutambua umuhimu wa kujiunga na kundi hili la kiunabii la masalio kwa kushindwa kuona utofauti wa unyeti wa kundi hili katika maisha ya kiroho. Lakini hatari nyingine ni ile ya watu waliokwisha kutambua unyeti wa utume masalio na huenda wakaamua kujiunga na kundi hili la kiunabii la masalio la siku za mwisho (yaani baada ya miaka 1260 kutimia) lakini bado wangali wakitumia fursa hii muhimu maishani mwako kipuuzi. Wakitenda matendo mbali mbali yanayoudharirisha umasalio wao, wakiishi kwa tabia na matendo ya kibabeli, wakila na kuvaa kibabeli na hata wakiabudu kwa nyimbo, sala na mafundisho ya kibabeli, hao nao wataipokea alama ya mnyama sawasawa na uasi wao waliokuwa wakienenda kwao kabla ya pambano la mwisho.
Hatupaswi kusubiri kwa hamu wala kwa hofu kulikabili pambano la mwisho wa wakati hali tukiishi na kuenenda katika dimbwi la kuipenda dunia na anasa zake. Ibada bandia ndani ya maisha ya mkristo huzaa imani bandia. Imani bandia inayoyakataa mafundisho ya kweli ya Mungu ndani ya kanisa huzaa ukristo bandia, na ukristo bandia huzaa mkristo bandia; mkristo bandia huishia kuwa mwana masalio bandia; mwana masalio bandia ndiye asiyetambua utume halisi wa masalio, wakati wa pambano kuu la mwisho wa historia masalio bandia wataipoke sabato bandia na kuiabudu sanamu ya mnyama.


Sote hatuko salama, lakini tunayo heri ndugu msomaji kwa kuwa nawe umebahatika kusoma somo hili nyeti ili kupitia hili somo tufanye matengenezo sahihi ya maisha yetu kama wana masalio. Tunapaswa kusahihisha mapito yeetu, jinsi tunavyoenenda na kutenda kama wana masalio wa siku za mwisho, maana tumeitwa tutoke babeli (Ufu 18:4) tumeitwa kuzikimbia ibada zenye mafundisho ya uwongo na tumeitwa tumwabudu Muungu muumbaji katika roho na kweli.
Tukiijua kweli itatuweka huru, nayo itatufunulia kuikataa dhambi na mafundisho ya uongo. Naam, blog hii ipo kwa ajili ya kukufunulia ukweli huo. Endelea kubarikiwa na masomo mengine katika blog hii. Bwana akubaliki na kukuzidishia nguvu ya kulitafuta Neno la kweli maishani mwako. Pale mwanadamu anapokubali Yesu Kristo amuongoze, Baraka za Bwana hazipungui tena maishani mwake daima. Kumbuka: UIMARA WA AKILI NI KUISHI MAISHA MATAKATIFU.
Amina

Post a Comment

0 Comments