Header Ads Widget

Responsive Advertisement

MAKALA | KAMATA FURSA UFANYE MABADILIKO KIJANA MWENZANGU

Kuwa kwenye biashara pekee bado haitoshi wewe kufanikiwa. Kila mtu anaweza kufungua biashara na kuiendesha, lakini ni wachache ambao wanaweza kuona zaidi ya ile biashara waliyoko nayo sasa.
Kama unataka kufikia mafanikio makubwa kupitia biashara unayofanya, unahitaji kuona mbali zaidi ya hapo ulipo sasa. Unahitaji kuziona fursa zaidi zitakazoiwezesha biashara yako kukua na kuleta faida zaidi.
Wewe kama MPENDA BAISHARA mwenzetu, tunahakikisha unajua mbinu zote muhimu kwako kuweza kufanikiwa kwenye biashara. Na hapa tunakuletea njia tano unazoweza kutumia kuziona fursa nzuri zaidi za kibiashara.
  1. Malalamiko ya wateja.
Wafanyabiashara wengi huona malalamiko ya wateja kama tatizo kubwa, lakini hii ni fursa nzuri sana ya kuikuza biashara yako. Kama kuna kitu chochote ambacho hakiwapendezi wateja, maana yake una nafasi nzuri ya kukirekebisha ili wateja wakifurahie. Kumbuka lengo lako kubwa kwenye biashara ni kutengeneza wateja wanaoiamini biashara yako. Shughulikia malalamiko yao, ni sehemu nzuri ya kukuza biashara yako.
  1. Teknolojia mpya.
Kila siku kuna teknolojia mpya zinavumbuliwa ambazo kama ukiweza kuzitumia utarahisisha sana biashara yako na kuweza kuikuza zaidi. Pendelea kujifunza mambo ya biashara, kufuatilia habari za biashara na utakuwa wa kwanza kujua teknolojia mpya zinazoweza kuirahisisha biashara yako. Teknolojia hizi zinaweza kuwa kwenye kutangaza biashara, kutunza kumbukumbu za biashara na mengine mengi.
  1. Kitu ambacho kinafanywa sivyo.
Angalia kwenye ile biashara ambayo unafanya na angalia wafanyabiashara wengine wanafanya biashara zao kwa njia gani. Utagundua kuna njia za kibiashara ambazo wengine wanafanya sivyo. Huenda kuna huduma wanazotoa kwa hali ya chini sana, huenda wanauza bidhaa ambazo hazina viwango. Sasa wewe unaweza kutumia nafasi hii kutoa huduma bora sana au bidhaa zenye viwango vya hali ya juu. Kwa watu kujua wewe ni wa kuaminika ukilinganisha na wengine, watapenda kufanya biashara na wewe.
  1. Kama isingekuwepo...
Kuna maswali ambayo ukijiuliza unaweza kuona fursa nyingi sana ambazo wengine hawazioni. Jiulize kama suluhisho lililopo sasa lisingekuwepo, watu wangefikiriaje? Kama bidhaa inayopatikana sasa isingekuwepo, watu wangefikiriaje? Kisha fikiria kwa misingi hiyo na utaona njia nyingi za kuboresha huduma au bidhaa unazouza.
  1. Mabadiliko yanayokuja.
Mabadiliko yanatokea kila siku kwenye maisha yetu, japo watu wengi hawapendi mabadiliko. Kama unataka kuziona fursa nyingi zaidi, anza kutegemea mabadiliko. Unapoona mabadiliko yanaanza kidogo sana, anza kuchukua hatua. Mabadiliko yanapokolea wewe unakuwa tayari kuweza kuwasaidia wengine kwa mabadiliko hayo kupitia biashara yako.
Usiendeshe biashara kwa vile tu una biashara, mara zote unapokuwa kwenye biashara yako, fikiria ni fursa gani zipo kwenye biashara hiyo ila bado hujaziona. Ukijizoesha kujiuliza na kujibu swali hili utaona fursa nyingi mpaka mwenyewe utashangaa ulichelewa wapi kujua mbinu hii muhimu.

Post a Comment

0 Comments