Alicheza Ligi Kuu kwa muda wa miezi miwili bila kufunga goli lolote. Alionekana kukosa magoli rahisi zaidi kufunga kuliko kukosa.
Inaonekana alikuwa akiathirishwa na mzigo mkubwa kichwani, kwani inadaiwa hadi usajili wake kukamilika, zimetumia dola 100,000 za kimarekani ambazo ni zaidi ya Sh. Milioni 200 za Kitanzania.
Hata hivyo, msaada wake kwenye timu ulionekana hauendani na kiasi cha pesa aliyotumika kusajiliwa. Huyo ni Obrey Chirwa, straika raia wa Zambia.
Mmoja wa watu walioonekana kutokubaliana na usajili huo ni mwanachama mkongwe wa klabu hiyo, Ibrahim Akilimali.
Hatimaye, alifunga bao lake la kwanza Oktoba 12 mwaka jana, kwenye dakika tatu za nyongeza za kipindi cha kwanza, Yanga ikicheza dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Uhuru na kuiwezesha timu yake kuondoka na ushindi wa mabao 3-1. Huo ndiyo ulikuwa mwanzo mzuri wa mchezaji huyo.
Ingawa amekuwa hana namba ya kudumu kwenye klabu hiyo, Jumapili iliyopita alifanya jambo moja la kukumbukwa na wanachama na mashabiki wa Yanga. Nalo ni kuitoa timu hiyo kwenye nafasi ya pili na kuipeleka moja kwa moja kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mabao mawili aliyoyafunga kwenye Uwanja wa Taifa dhidi ya Mwadui, yaliifanya timu yake kupata ushindi wa mabao 2-0 na kupanda kileleni kwa pointi 46, dhidi ya 45 za Simba.
Ilikuwa ni mechi ngumu ambayo ilionekana kama Yanga ingetoka sare ya bila kufungana na timu hiyo. Chirwa ambaye aliingia kipindi cha pili, aliweka mambo sawa na kufanya kile ambacho wanachama na mashabiki wa Yanga walikuwa wakikitarajia kwa muda mrefu.
Mchezaji huyo aliyejiunga msimu huu akitokea FC Platinum ya Zimbabwe, amefikisha jumla ya magoli saba kwenye kibindo chake mpaka sasa.
Ilibaki kidogo tu mchezaji huyo atemwe kwenye kipindi cha dirisha dogo. Ilikuwa apelekwe kwa mkopo kwenye timu yake ye zamani FC Platinum ili nafasi yake ichukuliwe na Mzambia mwingine Wiston Kalengo.
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena