Napenda kuungana na mamilioni ya Watanzania kumpongeza Rais wa Jamhuri Muungano Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kutokana na uzalendo, uthubutu na ujasiri aliouonyesha katika katika kulinda rasilimali zetu zimnufaishe Mtanzania.
Watanzania tulio wengi tunashindwa mambo kuyafanya kutokana na kukosa ushupavu wa uthubutu katika kuamua kuyafanya mambo. Hakuna jambo lililowahi kufanikiwa bila ya kuwepo kitu uthubutu. Uthubutu ndio mwanzo wa mafanikio ya jambo lolote lile.
Mwalimu Nyerere alijizatiti akiwa na malengo ya kupigania Uhuru wa Tanganyika wakati akijua fika kuna mkoloni Mwingereza aliyekuwa akitawala lakini alitanguliza mbele uthubutu wa kuweza jambo na hatimaye mnamo Disemba 9, 1961 malengo yake yalitimia.
Miaka ya 1980's kuliibuka genge kubwa la wahujumu uchumi nchini ambao walificha bidhaa ili waje wazilangue. Kuliibuka mafisadi wa kiuchumi ambao walikuwa na nguvu iliyopitiliza ya kuogopwa lakini akaibuka Ndugu Edward Moringe Sokoine kupambana nao vikali kwa kutanguliza uthubutu kwanza na hatimaye wahujumu uchumi wenyewe wakaanza kutoa mafichoni Mali na bidhaa walizozificha kutokana na kuibuka kiongozi shupavu na jasiri aliyekuwa na uthubutu wa kukabiliana nao. Hatimaye Sokoine alifanikiwa kushinda vita dhidi yake na wahujumu uchumi.
Hayo yote ni matokeo ya uthubutu. Leo hii ameibuka kiongozi mwingine Rais Dk. John Pombe Magufuli ambaye ni mfano bora wa kuigwa kutokana na kutanguliza mbele uzalendo na uthubutu wa kupambana na wahujumu rasilimali zetu na yupo tayari kuzilinda.
Uzalendo wa Rais Magufuli ulianza kwa kuzuia makontena 277 yenye mchanga wa madini yasisafirishwe kwenda nje na kuunda tume mbili ambazo zimetufunua macho juu ya matrilioni ya pesa tuliyokuwa tunaibiwa.
Watanzania hatukupaswa kabisa kuwa maskini, kukosa madawa hospitalini, kukosa miundombinu bora, kuwa na Kilimo duni huku tukikosa pembejeo, kula mmoja. Watanzania hatukustahili maisha ama maumivu haya.
Waliotufikisha hapa Rais Magufuli amewafuta kazi, ameagiza walio nje ya madaraka waanze kuhojiwa Mara moja. Na kauli ya Rais inakwenda mbali zaidi ya hapo kwamba hawataishia kuhojiwa tu bali watapandishwa mahakamani.
Kwa muda mrefu tumekuwa tukilalamika tukiibiwa madini, tumekuwa tukilalamika rasilimali zetu hazitunufaishi Watanzania. Tulikosa kabisa jasiri Mzalendo wa kuanzisha vita hii ya ukombozi wa kiuchumi.
Naupongeza uzalendo na uthubutu aliouonyesha Rais Magufuli. Sasa ni wajibu wetu kama Taifa kuungana kwa pamoja ili kuziokoa rasilimali zetu zitunufaishe sote na vizazi vyetu.
Emmanuel John Shilatu
12/06/2017
0767488622
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena