Header Ads Widget

Responsive Advertisement

SIMULIZI | Namna Operation ya Vita ya Kagera Ilivyofanyika - Inasimuliwa na Gen. Kiwelu | Episode 1.

Wengi wetu tumeisoma hii vita tukiwa shule kwa kufundishwa sababu za hii vita na madhara yake tuliyopata katika hii vita, Leo tupate fursa ya kufahamu operesheni ya hii vita ilikuwaje kutoka kwa moja wa makanda wakubwa sana waliopambana katika hii vita kufa na kupona na mpaka Leo hii anakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika hii vita.

Anaanza kwa kusema hivi; "kazi ya kwanza ilikuwa kuwajenga kisaikolojia. Kazi ya pili ilikuwa ni kupata reinforcement (kuongeza nguvu) kazi ambayo niliyomwachia Ernest Mwita Kiaro, hata CDF naye alikuja akakaa mahala fulani pale Bukoba (jirani), kwa hiyo Dar es Salaam tulimpa kazi Mwakalindile ndiye aliyekuwa anakaimu kama Chief of Staff, halafu Kiaro, chifu wa mgambo kazi yake ilikuwa kukusanya mgambo wote nchini, akina Mwakalindile ni kukusanya JKT, Polisi na Magareza, wote walikuja kule.

Ninaposema kulikuwa na changamoto kubwa sana ni kwamba hawa askari hata siku moja hawakuwahi kuwa eneo la vita ama eneo la mafunzo ya kivita kwa pamoja. Kwa hiyo, ilikuwa kazi kubwa, ndiyo maana ikatuchukua muda pale kabla hatujaruka daraja, ilikuwa ni lazima nifanye mafunzo ya pamoja ili kuwaweka watu (askari kutoka Magereza, Polisi, Mgambo na JKT) waweze kufanya kazi pamoja.

Lengo ilikuwa kuondoa fikra za kitabaka vitani, kuachana na mambo ya huyu mgambo au JKT. Kwa hiyo nilianzisha range ya kupiga silaha, mtu unampa risasi kumi anapiga zote wash out (anakosa kulenga shabaha), maana sisi (jeshini) tuna kitu kinaitwa bull, inner, outer n.k, sasa huyu unampa risasi zote anapiga wash out, tunampa nyingine, akipiga ile target namwambia umepiga bega (target hasa ni kifuani kwenye moyo au kichwani) sasa wakati mwingine ukimpa risasi tano… mbili anapiga ndani, nikasema sasa wameiva.

Kwa hiyo ilikuwa ni mafunzo ya msingi. Kwa mfano, ukiwa porini na ndege ya adui inakuja ufanye nini?. Unaulizwa ukiona ndege ya adui inatoka kule wewe unakwenda wapi? Namna gani mnaweza kusonga mbele, mnajihami vipi na namna gani mnaweza kupumzika kwa sababu askari hawezi kupumzika chini ya kivuli cha mti. 

Sasa baada ya mafunzo hayo ya pamoja, tukaridhika askari wetu wameiva, tukaanza kusonga mbele kutoka Katoro hadi tukafika karibu na mpakani, tukasema kambi ambayo mpaka leo ipo pale, nyuma ya Mtukula". KUSHAMBULIWA KWA DARAJA LA KAGERA. "Daraja hili wakati nimefika tu, kutoka kupewa ile amri (ya kwenda vitani), nimefika Kaboya, siku hiyo hiyo jioni nikatoka kwenda kutazama daraja. 
Nikafika darajani upande wa kulia kama unakwenda Mtukula umbali wa kilomita moja, nikaliona daraja ambalo baada ya dakika 15 nikiwa pale likalipuka, kwa hiyo sikuweza kuwahi kuweka askari pale darajani.

Wakati nafika pale na mtu mmoja anaitwa Kanali Kitete tunatazama, nataka sasa kufanya mbinu namna gani nitavuka daraja ili majeshi yangu yakae upande mwingine.

Basi nikarudi zangu Kaboya kwa ajili ya kuanza kufanya mkakati mwingine maana pale daraja limekwishavunjwa, nikaripoti daraja limevunjwa, hakuna daraja kuanzia sasa. 
Ndipo tukaanza mipango mingine kuhusu daraja, tukaleta madaraja ya muda na mtu mmoja anaitwa Brigedia Rajabu ndiye aliyekuja na vifaa hivyo kutoka kikosi chetu cha uhandishi na tukamweka sehemu ya umbali wa kama kilomita tano kutoka kwenye daraja, ndipo alipofanya mafunzo yake ili baadaye kufunga daraja la muda". MUDA ULIOTUMIKA KUJENGA DARAJA. "Unajua kuna wanazungumza kwa ushabiki mambo ya vita tu wakati hawajui chochote kuhusu vita, watu hawa mimi nawaita majitu, hawajui maana ya vita. Wapo wengine wanafikiri jeshi hii la Tanzania lilikuwa tayari kwamba unakwenda tu kwenye vita, sasa ukiwaambia kwamba jeshi hili tulipokwenda kwenye vita tulikuwa na mchanganyiko wa watu wote hawa, halafu pia kuleta vifaa vya kuvuka daraja, kuwafundisha namna ya kuweka daraja, kuleta vifaru, ndipo wataona ugumu wa kazi uliokuwapo.

Pale ni lazima uwe na nguvu ya kutosha kuhakikisha kwamba mkivuka (daraja) hakuna kurudishwa nyuma. Wale askari wetu waliokuwa kule awali, walikuwa wachache na walivurumishwa na adui kiasi cha morali yao kuwa chini kivita, kwa hiyo ilikuwa ni lazima nihakikishe sasa watu wangu ni imara, vifaa viko sawa. 
Tulikuwa tunafanya mipango na ukaguzi pamoja na makamanda wangu, akina Jenerali Marwa, Jenerali Luhanga, Mayunga, Walden, tunakwenda hadi tunafika pale kwenye daraja kwa sababu Idi Amin alirudisha majeshi yake (Uganda) akiamini kazi imekwisha. Sasa tulikuwa na makamanda wangu hao tunakwenda pale kupanga mikakati, lakini, swali kwamba wapi tupite (kuvuka daraja) na lini sikuwaambia.

Hakuna mtu aliyejua hata Edward Sokoine (aliyekuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Mwalimu Nyerere) alikuja akaniuliza, sasa General nafikiri tumechelewa sana kuvuka (daraja), sasa unavuka lini na unapitia wapi?

Nikamwambia hiyo ni siri ya kijeshi, akasema hata mimi? Nikamwambia ndiyo mzee. Kwa hiyo mimi nilikuwa napita kando ya ule mto kwa gari hadi Murongo, halafu watu wanapiga mabomu kila sehemu lakini hawajui tunaruka wapi kupitia wapi. 
Tuliweka watu (askari) hadi eneo la Kakunyu huku Bukoba Vijijini, kwa hiyo kuna ambao walijua tunaruka kupitia huko. Hatimae nikaona sehemu ya kuvuka ni pale pale walipovunja (daraja), lakini sikuwaambia wapiganaji wetu.

Sasa imefika siku ya kuvuka, ndani ya saa 24. Nikawaita makamanda wangu nikawaambia sasa inabidi tuvuke kwenda kumshambulia adui, vifaa na kila kitu tayari, na askari kama tulivyofanya mafunzo wako tayari.

Makamanda wakasema tunangoja tu amri yako, nikasema amri itatoka, wakauliza na kutaka niwaambie tunavuka kupitia eneo lipi, nikasema nitawaambia.

Ilipofika saa tano usiku nikawaambia makamanda, Marwa utakuwa katikati, Mayunga ukivuka tu unakwenda kushoto kuelekea eneo la Mbarara, Walden ukivuka tu unaelekea eneo la Minziro, Luhanga ukivuka tu unafuata njia ya Marwa halafu makamanda wengine watakuwa tayari kusubiri lolote (reserve). Baada ya maelekezo hayo nikawataka waende kuwaambia askari wao kwamba tunaruka leo (usiku huo), nikamwita Mhandisi Mkuu Rajabu na kumwambia kutatandaza daraja lako (juu ya mto) saa nane usiku, akafanya kazi hiyo.

Saa nane usiku mpaka kufika saa tisa kuelekea saa 10 (takriban saa mbili hivi mfululizo) vikosi vikaanza kuvuka kwa mujibu wa amri ya operesheni (operation order) ilivyotamkwa. Ilikuwa bahati mbaya nilipoteza askari mmoja tu pale wakati wa kuvuka daraja

Tukutane Tena sehemu inayofuata.......

Post a Comment

0 Comments