MALAYSIA FLIGHT 370: UTATA, USIRI & COVER UPS SEHEMU YA PILI Genesis Katika sehemu niliyopita mwishoni mwa makala nilirudi mwanzoni kabisa… mwanzo wa safari ya ya Malaysia Flight 370 siku ya March 8, 2014. Tuendelee… Kama ambavyo nilieleza ndege hii ilikuwa inaruka kutoka mji wa Kuala Lumpur nchini Malaysia na kuelekea mjini Beijing nchini China. Safari hii ilikadiriwa kwamba itatumia muda wa masa 5 na dakika 34. Kwa hiyo, ilipaswa kuruka kutoka hapa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kuala Lumpur mida ya 00:35 MYT na ilitazamiwa kutua uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Beijing muda wa 06:30. Pamoja na wale abiria 227 na wahudumu 10 na marubani 2 pia ndege hii siku hii ya safari ilibeba mizigo yenye jumla ya uzito wa kilo 14,296. Kwa urefu wa safari hii ya masaa 5 na dakika 34 ilitegemewa kwamba ndege hii itatumia jumla ya kilo 37,200 (lb 82,000) za mafuta ya ndege. Lakini ndege hii kabla ya kuruka uwanjani kumbukumbu za uwanja wa ndege zinaonyesha kwamba ilijaza jumla ya kilo 49,100 za mafuta ya ndege kwa ajili ya safari hii pamoja na 'reserve'. Hii ilimaanisha kwamba kwa ujazo huu wa mafuta ilikuwa inaipa ndege hii uwezo wa kuruka masaa 7 na dakika 31 zaidi kuzidi urefu wa safari yake rasmi endapo kama itahitaji kufanya hivyo (naomba ushike vizuri detail hii ya ujazo wa mafuta na masaa ya ziada, nitaiongelea tena hapo mbele kidogo). Ilipofika saa 00:42 MYT ndege hii ikiwa katika njia (runway) namba 32R hapo uwanja wa ndege iliruhusiwa na Air Traffic Control kuanza kuruka kufikia katika 'flight level' 180. Hapa ieleweke kwamba 'flight level' haimaanishi moja kwa moja urefu wa kutoka ardhini. Katika masuala ya usafiri wa anga 'flight level' inakokotolewa kwa kuhusianisha urefu wa ndege kutoka ardhini pamoja na pressure. Kwa mfano nikisema 'flight level' 180 tukikokotoa kwenda kwenye urefu wa kawaida tunapata takribani futi 18,000 (mita 5,500) kutoka usawa wa bahari. Kwa hiyo ndege iliruhusiwa na ATC (Air Traffic Control) kuruka kutoka runway 32R kwenda flight level 180 moja kwa moja katika njia (waypoint) ya ngani inayojulikana kama IGARI (njia hii ya anga iko kwenye 6° 56' 12"N 103°35' 5"E). Uchambuzi wa kumbukumbu za sauti kutoka kwenye chumba cha rubani kwenda ATC unaonyesha kwamba kabla ndege haijaruka ni msaidizi wa rubani alikuwa akisimamia mawasiliano na ATC na baada ya kuruka ni rubani mkuu alisimamia mawasiliano na ATC. Baada ya ndege kuruka kutoka uwanja wa ndege mawasiliano ya kuongoza ndege yalihamishwa kutoka ATC kwenda Kuala Lumpur Air Control Centre (ACC) kwa kutumia frequency 132.6 MHz. Nieleze pia hapa kidogo, katika masuala ya usafiri wa anga Air Traffic Control (ATC) wanaongoza ndege kutoka uwanja wa ndege. Baada ya ndege kuruka au ikiwa inatoka mahala kwingine inakuja uwanja wa ndege kabla haijafika uwanja wa ndege kwanza kabisa inawasiliana na ACC (hiki ni kituo mara nyingi kinakuwa chini ya serikali kwa ajili ya kuratibu vyombo vinavyopita kwenye anga lake) kisha mawasiliano yanapelekwa ATC. Vivyo hivyo ndege ikiwa inaondoka mawasiliano yanahamishwa kutoka ATC kwenda ACC. Na hiki ndicho hicho nilichoeleza hapo juu kwamba mawasilia ya uongozahi MH 370 yalihamishwa kutoka Air Traffic Control kwenda Malaysia Air Control Centre Frequecy inayotumiwa kwa mawasiliano na ndege zilizo 'en route' kupita kwenye peninsula na maji ya Malaysia imebatizwa jina la "Lumpur Radar". Kwa maana hiyo basi, Mawasiliano na ndege hii mara tu baada ya kuruka yalihamishwa kutoka ATC kwenda "Lumpur Radar". --------------------- Sauti za mwisho za Marubani kutoka kwenye flight 370 (Nashindwa kuweka audio hapa kama milivyoweka kwenye grouo whatsapp... sijui inakuwaje) Sekunde 1 - 2:30, ndege ikipata ruhusa ya kuruka kutoka runway 32R (utasikia humo anasema 32 Right) 2:31 - 2:50, ndege ikipata ruhusa kuruka kwenye flight level 350 - 370 2:51 - 3:19, Rubani Mkuu, Captain Shah akiconfirm kwamba ndege inaruka kwenye flight level 350 (haya ndiyo yalikuwa mawasiliano ya mwisho ya kuongea kwa maneno kutoka kwenye ndege hii) ------------------
Majira ya saa 00:46, Lumpur Radar waliruhusu ndege hii kuruka hadi flight level 350 mpaka 370 (kama mita 10,700 kutoka usawa wa bahari). Majira ya saa 01:01 MH 370 iliripoti kwa Lumpur Radar kwamba imefika flight level 350. Saa 01:08 waliripoti tena kwamba wako kwenye flight level hiyo hiyo ya 350. Ilipofika majira ya saa 01:19 MH 370 ilikuwa inakaribia kutoka kwenye anga la Malaysia na kuingia anga la Vietnam. Kwa hiyo saa 01:19 sekunde ya 30 rubani mkuu wa ndege hii, Bw. Shah aliwasiliana na Lumpur Radar 'kuconfirm' kwamba mawasiliano yahamishwe kutoka Lumpur Radar kwenda Ho Chi Minh ACC (Radar ya nchi ya Vietnam na kituo cha kuongoza ndege zilizo 'en route', kupita kwenye anga lake). Baada ya mawasiliano haya na Lumpur Radar kuconfirn kubadilishwa mawasiliano, marubani wa ndege hii walikuwa wanatarajiwa sasa kuwasiliana na Ho Chi Minh ACC iliyo chini huko ardhini nchini Vietnam. Lakini mawasiliano haya hayakufanyika. Baada ya watu wa Radar ya Ho Chi Minh ACC kufanya majaribio kadhaa ya kuwasiliana na ndege hii bila mafanikio iliwabidi wawasiliane na ndege nyingine ambayo ilikuwa njia moja na Flight 370 wajaribu kama wanaweza kufanikisha mawasiliano hayo. Saa 01:30 rubani wa ndege hii nyingine alituma 'distress signal' kwenda Flight 370 kuwajulisha kwamba Ho Chi Minh ACC huko ardhini wanajaribu kuwasiliana nao bila mafanikio. Simu ilifika kwenye Flight 370 lakini rubani wa ndege hii nyingine anasema alikuwa anasikia minong'ono tu na hakuna mtu ambaye alikiwa anaongea. Iliwabidi Ho Chi Minh Aare Control Centre kuwasiliana na Kuala Lumpur Area Control Centre majira ya saa 01:38 kuwaeleza kwamba wanashindwa kupata mawasiliano na Flight 370 ambayo waliiona kwenye radar mwanzoni. Kwa muda wa takribani dakika ishirini vituo hivi viwili viliendelea kuwasiliana mara kwa mara lakini hakukuwa na taarifa yoyote mpya kuhusu kufanikiwa kuwasiliana na Flight 370. Hii ilipelekea majira ya saa 02:03 Kuala Lumpur ACC kuwasiliana na kituo cha huduma cha shirika la ndege la Malaysia (Malaysia Airlines Operations Centre) kuwataarifu kuwa wanashindwa kuwasiliana na ndege yao ya Flight 370 na hawana uhakika na mahala ilipo uko angani. Shirika la Malaysia Airlines kupitia kituo chao hiki cha huduma wakawajibu kwamba wao hawaoni hilo tatizo kwani wanapokea 'signal' kutoka kwenye ndege yao na inaonekana kwamba iko kwenye anga la Cambodia. Saa 02:15 Kuala Lumpur ACC waliwasiliana na Ho Chi Minh ACC kuwataarifu kuwa wamepata taarifa kwamba Flight 370 iko kwenye anga la Cambodia. Lakini baadae 'supervisor' wa kituo cha Kuala Lumpur ACC akaanza kupatwa na mashaka zaidi kuwa kuna jambo haliko sawa. Akafanya mawasiliano na Ho Chi Minh ACC kuwauliza kama ilikiwa sahihi kwa Flight 370 kupita kwenye anga la Cambodia kwa kulingana na njia yao wanayopaswa kupita angani. Ho Chi Minh ACC walijibu moja kwa moja kwamba kwa kuzingatia njia ambayo flight 370 inapaswa kupita, si sahihi kwa ndege hiyo kupita kwenye anga la Cambodia. Iliwabidi Ho Chi Minh ACC kuwasiliana na Phnom Penh ACC (kituo cha uongozaji na usimamizi wa nga la Cambodia) kuwauliza kama wana taarifa yoyote ile ya Flight 370. Phnom Penh ACC wakajibu kwamba hawana taarifa yoyote ile ya flight 370 na hata wakiitafuta wafanye nayo mawasiliano wanashindwa kuipata. Taarifa hii ikarejeshwa tena Malaysia. Baada ya kupokea taarifa hii Iliwapasa Kuala Lumpur ACC kuwasiliana tena na kituo cha huduma cha shirika la ndege la Malaysia kutaka kujua 'status' ya ndege yao ya Flighy 370. Hii ilikuwa tayari inapata majira ya saa 02:34.
Ajabu ni kwamba kituo cha uendeshaji/huduma cha shirika la ndege la Malaysia walijibu kwamba ndege yao iko salama salimini kabisa na bado wanapata signal na iko kwenye anga la Cambodia kwenye coordinates 14° 54' 00" N 109° 15' 00" E. Hii iliwachanganya akili zaidi vituo vyote vya ACC kuanzia Kuala Lumpur, Ho Chi Minh na zaidi Phnom Penh kule nchini Cambodia. Ilibidi zifanyike juhudi nyingine za ziada ili wajaribu kupata mawasiliano. Kule angani nchini Cambodia kulikuwa na ndege nyingine ya shirika hilo hilo la Malaysia ambayo ndege hii yenyewe ilikuwa inaelekea Shangai. Ndege hii iliombwa kujaribu kuwasiliana na flight 370 ambayo inaaminika kwamba iko juu ya anga hilo la Cambodia. Ndege hii nyingine walitumia frequency ile ile ya Lumpur Radar ambayo kwa mara ya mwisho Flight 370 waliitumia kabla ya kukata mawasiliano ghafla, waliitumia frequency hii kujaribu kupata mawasiliano lakini wakagonga mwamba, hakukuwa na majibu yoyote yale. Ilibidi Kuala Lumpar ACC kuwasiliana tena na Ho Chi Minh ACC kuwaomba wafanye mawasiliano na Chinese Air Traffic Control kujua kama wana taarifa zozote za flight 370 (flight 370 kama tunavyojua ilikuwa inaelekea China). Wachina wakatoa jawabu kwamba hawajaona flight 370 kwenye radar. Sasa masaa kadhaa yalikuwa yamepita na kila kituo cha anga na kila radar walikuwa wanatoa jibu lile lile, hawajaona flight 370. Saa 05:09 Kuala Lumpur ACC waliwasiliana na Singapore ACC kujua kama wana taarifa yoyote lakini jibu lilikuwa ni lile lile, hawajaiona flight 370. Kwa hiyo hakukuwa na njia nyingine yoyote zaidi ya kurudi tena kufanya mawasiliano na watu pekee ambao wao ndio bado wanasema wanaiona flight 370, kituo cha huduma cha shirika la ndege la Malaysia Airlines. Lakini hapa ndipo kitu cha ajabu na utata ulikoanzia… Saa 05:20 Kuala Lumpur ACC waliwasiliana na Malaysia Airlies Operations Centre ili kujua kwa sasa wanaiona ndege yao iko wapi, ajabu ni kwamba ghafla tu shirika la ndege la Malaysia Airlines wakageuka na kusema hawajui ndege yao ilipo. Na hawakuishia hapo tu bali walienda mbali zaidi na kusema kwamba hata taarifa waliyoitoa mwanzo kwamba ndege yao iko salama, kwenye anga la Cambodia na zile coordinates walizotoa zote walidai kwamba sio sahihi? Walipoulizwa kwa nini wanadai sio sahihi wakati wao ndio wamezitoa na walidai kuwa wanapata signal kutoka kwenye ndege?? Malaysia Airlines walijibu kwamba walitoa taarifa ile kwa kuzingatia tu makisio ya "flight projection" na sio vinginevyo na ndio maana wanasahihisha kuwa taarifa yao ya awali haikuwa sahihi. Hili lilikuwa ni jambo la kushangaza haswa na la kutia mashaka makubwa. Kwa sababu hata kama walitoa maelezo yale kwa kuzingatia "flight pjojection" isingeliwezekana wao waseme ndege iko kwenye anga la Cambodia kwa sababu ruti ya ndege haipiti huko. Kwa hiyo kama umetoa jawabu kuwa unapata signal ndege iko kwenye anga la Cambodia maana yake kuwa ni kweli unapata signal na sio fligjt projection. Utata huo haukuishia hapo tu… Saa 05:29 kuna afisa wa ngazi za juu kabisa wa serikali ambaye mpaka leo hii hajawahi kutajwa alipiga simu Kuala Lumpur ACC akitaka kujua kinachoendelea kuhusu Flight 370. Mkuu wa kituo cha Kuala Lumpur ACC alimjibu kuwa hawafahamu hiyo ndege iko wapi na kumekuwa na taarifa nyingi zenye mikanganyiko. Afisa huyo wa serikali aliamuru kwamba juhudi za kuitafuta ndege hiyo zifanyike kwenye anga na eneo la Malaysia tu kwa kuwa kuna taarifa za uhakika za ndani zinaonyesha kwamba *Flight 370 haikutoka nje ya anga la Malaysia.!!* Pengine hii ndio ilikuwa taarifa yenye utata zaidi. Kwa sababu mara ya mwisho rubani wa flight 370 alipofanya mawasiliano mida ya saa 01:19 sekunde ya 30 alikuwa anaconfirm mawasiliano yahamishwe kutoka Kuala Lumpar ACC kwenda Ho Chi Minh ACC (Vietnam) ikimaanisha kwamba walikuwa wanatoka kwenye anga la Malaysia na kuingia anga la nchi ya Vietnam. Lakini taarifa hii ilikuwa inatoka kwa mtu mzito serikalini, ilikuwa ni lazima ifanyiwe kazi.
Satellite ya Inmarsat-3 Saa 05:33 Supervisor wa Kuala Lumpur ACC aliwasiliana na ARCC (Kuala Lumpur "Aeronautical Rescue Coordination Centre). Zoezi la kuisaka Malaysia Airlines Flighg 370 likaanza rasmi. Saa 07:24 MYT takribani saa moja mbele ya muda ambao ndege ilipaswa kutua Beijing, Shirika la ndege la Malaysia walitoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari kwamba Malaysia Flight 370 imepotea na haijulikani ilipo na uwezekano mkubwa ni kwamba itakuwa imezama baharini na zoezi la kuisaka limeanza rasmi.! Kama moto wa petroli, habari hii ikasambaa kwa haraka sana kwenye vyombo vya habari vya kimataifa. Ndugu wa abiria wakabaki kwenye sintofahamu kubwa. Lakini wakati hayo yote yakiendelea, waliohusika kufuatilia ndege hii kuanzia mwanzo hadi mwisho ikipotea walibakia na maswali mengi zaidi kichwani. Kwa nini shirika la ndege la Malaysia ghafla tu walibadili taarifa yao na kusema kwamba "hawajui ndege ilipo?" Kwa nini yule afisa wa serikali aseme haikutoka nje ya anga la Malaysia?? Maswali haya yalikuwa mazito lakini majibu yake yalikuwa mazito zaidi kwani yalikuwa yanaleta hisia kwamba "kuna la zaidi nyuma ya pazia." Lakini zaidi ya hayo yote kuna jambo kubwa zaidi, kwa wakati ule hawakulijua. Kuna msemo wanasema "ukweli una tabia ya kukataa kupuuzwa" na huwezi kupumbaza watu wote wakati wote… Kwa nini? Wakati shirika la ndege la Malaysia na serikali wakitoa taarifa hii kwa ulimwengu saa 07:24 MYT kwamba ndege imepotea, hawakujua kitu kimoja… au kama walijua basi hawakudhani kwamba kingetokea… lakini tuamini kwamba hawakujua kwa muda ule kwani kama lisaa limoja mbele baada ya wao kutoa taarifa hiyo kwa ulimwengu, kwamba ndege imepotea na uwezekano mkubwa imezama baharini, lisaa limoja baadae, labda niwe mahususi zaidi… saa 08:19 sekunde ya 29 ndege hiyo hiyo inayosemwa kwamba imezama baharini "satellite data unit" ya ndege hiyo ilituma "log-on request" kwenda kwenye satellite ya INMARSAT juu angani.!! Nitarudi kueleza zaidi, ni dhahiri… kuna la zaidi nyuma ya pazia!! Itaendelea…
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena