Mshambuliaji wa Simba, Jamal Mnyate, ameomba barua kwa uongozi wa timu hiyo itakayomruhusu kuondoka na kwenda kwenye klabu nyingine kucheza soka.
Awali, kulikuwepo na taarifa za mshambuliaji huyo kuwepo kwenye orodha ya wachezaji watakaoachwa kwenye usajili huu wa dirisha dogo lililofunguliwa Novemba 15, mwaka huu.
Mchezaji mwingine anayetajwa kuachwa ni mshambuliaji Juma Liuzio ambaye yeye uongozi wa Simba umepanga kumtoa kwa mkopo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Gazeti la Championi limedai kuwa, mshambuliaji huyo anaomba barua hiyo ya kuachwa ili aende zake akaichezee Lipuli FC inayonolewa na Selemani Matola.
Aliongeza kuwa, mshambuliaji huyo tayari amekutana na mabosi wake huku akiahidiwa kupatiwa barua hiyo ya kuondoka Simba baada ya kukosa nafasi ya kucheza.
“Mnyate hatutakuwa naye katika mzunguko wa pili wa ligi kuu, kwani yeye mwenyewe ameomba barua ya kuachwa baada ya kuwepo taarifa za kutolewa kwa mkopo. “Hivyo, yeye mwenyewe ameomba aachwe moja kwa moja na siyo kwa mkopo kama wanavyotaka wenyewe Simba na maamuzi hayo ameyatoa baada ya kuona anakosa nafasi ya kucheza,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Kocha Mkuu wa Lipuli FC, Selemani Matola kuzungumzia hilo juu ya mshambuliaji huyo kuomba aende huko, alisema: “Ni kweli kabisa hizo taarifa, kama mambo yakienda vizuri basi Mnyate tutakuwa naye katika mzunguko wa pili wa ligi kuu.
“Kwani yeye mwenyewe ameonyesha nia ya kuja kuichezea Lipuli, hivyo ninamkaribisha na kama unavyojua timu yangu ina tatizo katika safu ya ushambuliaji, ninaamini kama akija yeye basi timu itaimarika zaidi.
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena