TIMU ya Zanzibar imeanza vyema michuano ya CECAFA Challenge baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Rwanda mchana wa leo Uwanja wa Kenyatta, Machakos nchini Kenya. Zanzibar Heroes waliuanza mchezo huo vizuri na kufanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya 34 kupitia kwa kiungo Mudathir Yahya Abbas. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko na dakika mbili tu mara baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, Rwanda walifanikiwa kusawazisha kupitia kwa Muhadjiri Hakizimana dakika ya 47. Hata hivyo, Zanzibar Heroes wakazinduka tena na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 52 kupitia kwa Mohamed Juma. Rwanda wakaingia kwenye jitihada za kusaka bao la kusawazisha kwa kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Zanzibar, lakini bahati haikuwa yao. Na bahati mbaya zaidi kwao wakapachikwa bao la tatu dakika ya 86, mfungaji Kassim Khamis na kujikuta wakipoyeza mchezo wa pili mfululizo, baada ya kufungwa 2-0 na wenyeji Kenya kwenye mchezo wa kwanza Jumapili. Zanzibar itarejea uwanjani keshokutwa kumenyana na ndugu zao Tanzania Bara, kabla ya kumenyana na Kenya Desemba 9 na kukamilisha mechi zake za Kundi A kwa kucheza na Libya Desemba 11 huko huko Machakos. Kikosi cha Zanzibar leo kilikuwa; Mohammed Abdulrahman, Ibrahim Mohammed Said, Mwinyi Hajji Mngwali, Abdallah Salum Kheri, Issa Haidari Dau, Abdulaziz Makame, Mohammed Issa Juma, Mudathir Yahya Abbas, Ibrahim Hamad Ahmada, Feisal Salum Abdallah na Suleiman Kassim ‘Selembe’/Seif Abdallah Karihe.
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena