Kuna baadhi ya masuala ambayo kwa hakika kabisa kama hatutajiandaa nayo sawia basi pamoja na juhudi zetu zote za kutaka kujikwamua tunaweza kujikuta miaka hamsini ijayo bado tukawa tunapambana na masuala haya haya ambayo tunapambana nayo leo hii.
Mzee Kikwete aliwahi kusema kwamba "hatuna mjomba duniani", akimaanisha kwamba ni lazima tujijengee dhamira ya kutaka kujitegemea na kuondokana na dhana ya kutaka kusaidiwa ili kufika kule tunakotaka kwenda. Lakini ni ajabu kwamba bado nchi zetu zimekuwa tegemezi na wepesi wa kupokea kila aina ya "project" kutoka ughaibuni ambayo inakuja na rangi ya kutaka 'kutusaidia'.
Ni jambo lililo dhahiri kwamba… hakuna nchi yoyote duniani ambayo ati wanaumiza vichwa kutaka kukwamua nchi nyingine kwenye umasikini. Kila tonge la msaada ambalo tunalishwa ndani yake lina donge chungu la 'interest' za wenye kutoa tonge hilo.
Swali ambalo binafsi najiuliza ni kwa kiasi gani vyombo vyetu vya usalama… hasa hasa Idara ya Usalama wa Taifa na viongozi wetu wakuu wamejipanga kung'amua hila zinazokuja zikiwa zimefichwa ndani ya matonge haya ya misaada yenye mchuzi mtamu juu yake.
Hapa chini najaribu kutoa mifano michache ya namna ambavyo nchi kama Marekani wanavyotumia makampuni makubwa ya kibiashara ya nchini kwao pamoja na mashirika yao ya misaada kulinda maslahi yao duniani na kueneza propaganda zenye kulinda kile wanachokitaka.
ZunZuneo
Katika miaka ya hivi karibuni mitandao ya kijamii imekuwa sehemu muhimu sana ya maisha yetu. Nguvu ambayo mitandao ya kijamii imekuwa nayo imekuwa ni ngumu na haiwezekani kabisa kuiepuka isikuguse kwa ubinafsi kwenye maisha yako. Nguvu hii ya mitandao ya kijamii ilidhihirika zaidi kwenye miaka ya 2011 na 2012 katika vugu vugu la 'Arab Spring' ambako mtandao wa Facebook ulitumika kwa kaisi kikubwa na vijana kujiratibu katika nchi za kiarabu na kuweza kuwaondoa madarakani viongozi wenye nguvu kubwa kwenye nchi za Tunisia, Misri, Yemen na Libya. Kisanga hiki cha Arab Spring natamani siku tupate nafasi tukidadavue ka mapana na Marefu yake.
Sasa basi, nguvu ya mitandao ya kijamii hata kabla ya ulimwengu mzima kuanza kuishudia mwaka 2011 wamarekani wenyewe walishaing'amua tangu mwaka 2010. Wote tunafahamu kwamba moja ya maadui wakubwa zaidi wa miaka mingi wa nchi ya Marekani ni Cuba.
Wamarekani kupitia shirika lao la misaada ya USAID walianzisha programu za kusaidia vijana nchini Cuba. Kama moja ya sehemu ya Programu ukazinduliwa mtandao mahususi kwa ajili ya vijana ambao uliitwa ZunZuneo (ZunZuneo.com). Mtandao huu ulikuwa messaging na microbloging platform ukifanya kazi kama ulivyo mtandao wa twitter. Watu mpaka wakaibatiza jina la 'twitter ya Cuba' (Cuban Twitter)
Kwenye mtandao huu mwanzoni mijadala ilikuwa inahusu michezo, maisha, ujasiriamali, urembo na vitu vya kufanana na hivyo. Lakini mwishoni mwa mwaka 2010 baada ya umaarufu wa mtandao huu kuwa mkubwa… mijadala ikahamishwa na kuanza kuwa ni mijadala ya kisiasa ambayo ilikuwa inachochea na kuhamasisha vijana kuiwajibisha serikali yao ya kijamaa.
Serikali ya Cuba ikaanza kushitukia janja hii na kuanza kuja juu dhidi ya mtandao huu. Uchunguzi ukaanza kufanyika na taasisi mbali mbali ikiwepo shirika la habari la AP.
AP walikusanya ushahidi wa kutosha kwamba mtandao wa ZunZuneo ulikuwa unafadhiliwa mahususi kabisa na serikali ya Marekani kwa lengo la kueneza propaganda za kupinga ujamaa na kuhamasisha kukumbatia umagharibi. Na lengo kuu lilikuwa ni kuhamasisha vijana wa Cuba wafanye mapinduzi kama yale ambayo wenzao wa nchi za Kiarabu wamefanya.
Serikali ya Marekani mwanzoni walikataa huhusika wowote lakini baadae walikubali kufadhili mtandao wa ZunZuneo lakini wakakataa kwamba walilenga kuhamasisha vijana kupindua serikali.
Licha ya kukataa kote huku lakini ushahidi wa wazi kabisa unaonyesha ZunZuneo ilikuwa ni programu maalumu ya kutumia vijana kuondoa serikali madarakani. Moja wapo wa ushahidi huu ni kitendo cha akaunti za benki za mtandao huu kuingiziwa fedha kutoka kwenye akaunti za siri zilizopo Benki za Cayman Islands na ukifiatilia fedha hizo zinaonyesha kabisa zimetoka serikali ya Marekani na shirika la USAID.
Kwa aibu kubwa USAID iliwabidi kuufunga mtandao huu mwaka 2012 kwa madai kwamba 'bajeti yake ya kuundesha imekwisha'.
Sasa hivi kuna mtandao mpya huko Cuba unaitwa 'Piramideo' ambao nao unafanya kazi kama Twitter na zimeanza tetesi kwamba mtandao huu unaweza kuwa ni mbadala ya ZunZuneo iliyofungwa na kuna kila dalili ya mkono wa Wamarekani ndani ya Piramedeo.
Project Pedro
Wote tunafahamu namna ambavyo vita baridi ya Marekani na Urusi ilivyowatesa pande zote mbili wakihaha kujaribu kila mmoja kuvutia nchi zingine duniani kuwa upande wake.
Katika miaka ya 1950s na 1960s katika tafiti ambayo ilifanyika nchini Mexico ilibaini kwamba robo tatu ya raia wa Mexico walikuwa na mtazamo 'neutral' juu ya itikadi ya ujamaa. Kwamba hawakuona kama ni kitu kibaya lakini pia hawakuunga mkono moja kwa moja. Hii ilikuwa ni dalili mbaya kwa Marekani kwa kuwa nchi ya Mexico iko 'kibarazani' kwao kabisa. Walikuwa wanataka raia wa Mexico wachukie ujamaa.
Serikali ya Marekani ikaingia kazini kuandaa kampeni ya propaganda. Kipindi hicho Marekani walikuwa na idara inayoitwa United States Information Agency (USIA) ambayo siku hizi iko ndani ya 'Broadcasting Board of Governors. Hawa ndio walipewa jukumu la kuandaa kampeni maalumu ya propaganda ya kubadili mitazamo ya raia wa Mexico kuchukia ujamaa.
USIA wakaja na programu waliyoipa jina la Project Pedro.
Kwenye miaka hii ya 1950s bado hakukuwa na vituo vya televisheni vinazorusha matangazo kwa cable, au satelite. Kipindi hicho kulikuwa na kitu kinaitwa "newsreels". Newsreels ni kama filamu fupi kuhusu matukio yanayoendelea. Yaani ni kama taarifa ya habari ambayo imerekodiwa alafu inaonyeshwa kwenye majumba ya sinema. Kila newsreel inakuwa inalenga suala fulani mahususi. Mfano kuna newsreel za siasa, michezo, biashara na kadhalika.
Idara ya USIA ikashirikiana na wamiliki na waongozaji wakubwa na watengenezaji wa filamu (mfano mzuri ni Richard K. Tompkins) na kuanza kuzalisha newsreels zenye maudhui ya kuponda ujamaa na kuisifu marekani na umagharibi na kisha kuzisambaza kwenye majumba ya sinema nchini Mexico. Ili kuondoa chembe za kutiliwa shaka… makampuni makubwa ya Kimarekani kama vile Coca Cola na Pepsi yalitumika kudhamini newsreels hizi. Kila wiki kulikuwa na zaidi ya Majumba ya sinema 400 nchi nzima ya Mexico ambayo yalikuwa yanaonyesha Newsreels zilizotengenezwa kwa maslahi ya nchi ya Marekani pasipo nchi ya Mexico yenyewe kujua.
Nirejee tena kwenye swali langu…
Nchi zetu za kiafrika na hii Tanzania yetu… tumejidhatiti vipi kujilinda dhidi ya vita za propaganda kutoka nje ya nchi yetu? Tuna mfumo thabiti wa kupima na kudadavua kila tonge la msaada na programu tunazosaidiwa?
Wanasema kwamba kwenye maisha, vitu vyenye nguvu vinakula vitu dhaifu… hiyo ni kanuni namba moja ya maisha. The law of natural selection. Survival of the fittest.
Tusipo elewa tunachokifanya juu ya uso wa dunia na tukiishi kana kwamba tuna mjomba wetu mahala fulani duniani… miaka hamsini ijayo tunaweza kuwa bado ni vibaraka wa mabwana wakubwa badala ya kuwa nchi yenye heshima na maendeleo ya kutukuka. Written and Compiled by Habib Anga - The Bold.
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena