“Kama unataka kuiba, iba kwa akili, na kwa namna iliyo nzuri.
Iwapo utaiba sana ili uwe tajiri wa kutupa usiku mmoja tu, utakamatwa”
Haya si maneno yangu ni maneno aliyosema Mobutu Sese Seko, mwezi Mei Mwaka
1976, akikemea rushwa nchini Zaire au Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo kama
inavyojulikana sasa.
Iwapo mtafaruku wa kisiasa nchini Zaire uliweza kumng’oa mtawala wa muda mrefu Mobutu Sese Seko na kumlazimu kulikimbia Kasri lake la Gbadolite—Mobutu hakukosa sehemu ya kumuhifadhi: Alikuwa nNyumba ya kifahari katikati ya jiji la Paris, hekalu la vyumba 32 Uswisi, na Kasri la karne ya 16 Hispania.
Mtawala huyo wa kiimla asingalikuwa na shida yoyote kulipia usafiri binafsi kutoka Zaire. Katika baadhi ya ziara zake nje ya nchi, ikiwemo ziara ya kitaifa jijini Washington DC na mapumziko kwenye eneo la anasa huko marekani lijulikanalo kama Disney World, mara nyingi alilipia bata alilokula kwa pesa taslimu. Kama huniamini endelea kusoma…
Mwaka 1987 mathalani, Mobutu alisimama njiani kwa muda Mji wa Maine, nchini Marekani na wahudumu wa Hoteli ya Bayview Inn walishuhudia mmoja wa watu waliokuwa kwenye msafara wake akifungua sanduku la kuburuza lililosheheni pesa taslimu na akahesabu zaidi ya dola $50,000( takribani zaidi ya Shilingi 100,000,000) kulipia bili ya malazi kwenye hotelini hapo, kwa mujibu wa msemaji wa hoteli hiyo. Jamani mmeona bata hilo?
Katika kipindi cha miaka 26 ya utawala wake, huku nchi yake ikizama kwenye lindi la umaskini na hali ya kukata tamaa miongoni mwa wananchi, Mobutu aliibuka kuwa miongoni mwa viongozi tajiri mno, huku akiwa mmiliki wa majumba kwenye maeneo nyeti, akiwa na pesa lukuki zilizofichwa kwenye akaunti za mabenki nchini Uswisi. Zaidi ya hayo inasemekana alikuwa na hisa nyingi za biashara barani Ulaya. Jarida maarufu la Forbes liliwahi kumtaja miongoni mwa madikteta tajiri kabisa duniani.
Wadadisi wa mambo, ikiwemo mabalozi na wakufunzi vyuo vikuu kutoka Zaire wanaoishi uhamishoni—hawana shaka Mobutu alisheheni utajiri mkubwa kwa kufuata ushauri wake yeye mwenyewe “ Iba kwa akili”
Hata hivyo, wakosoaji wake, walimfananisha na mdhalimu(dictator) Ferdinand Marcos wa ufilipino na Jean-Claude Duvalier wa Haiti aliyekomba hazina ya nchi yake kujilimbikizia mabilioni ya fedha za kigeni nje ya nchi.
Na kufuatia wiki ya sintofahamu na vuguvugu la kisiasa nchini Zaire Mobutu alilazimika kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na wapinzani kwa mara ya kwanza. Wakosoaji hao walibaini na kutumai Mobutu—kama ilivyokuwa kwa watawala wenzake dhalimu Duvalier na Marcos waliomtangulia—angali achia ngazi ya madaraka na kudondoka chini puu!!!.
Ilikuwa siku ya Jumapili, Mobutu alilazimika kumtaja kiongozi wa muda mrefu wa upinzania Etienne Tshisekedi kuwa waziri mkuu hatua ilioashiria anguko kuu la utawala dharimu wa zaidi ya miongo miwili chini ya Mobutu. Hata hivyo wawili hao wakaonekana kusigana kimadaraka, huku Tshiseketi akimwita Mobutu “Zimwi”(Monstor) na kuhimiza ni lazima ang’oke madarakani, huku Mobutu akijaribu kung’ang’ania kusalia ofisini huku ikiwa ni dhahiri hakuwa tena na uwezo wa kutoa amri kwa jeshi na likamtii kutokana na malamamiko ya muda mrefu ya askari kutokulipwa na hali duni ya kimaisha.
Wakati himaya ya Zaire ikiwa mbioni kuanguka ,maswali mengi kuhusu utajiri wa Mobutu—na namna alivyoupata, yalizidi kuvuta hisia, kwa kuwa kwa kipindi kirefu cha utawala wake alinufaika na mamia ya mamilioni ya dola yaliyotolewa na marekani kama msaada kwa nchi hiyo, ambapo marais wa Marekani enzi hizo walimuona kama ni kiongozi muhimu na rafiki aliyeweza kukabili wimbi la itikadi ya kikomunist katika eneo la maziwa makuu lisilo stahimilivu kisiasa.
Mobutu alinyakua madaraka kwa mtutu wa bunduki akisaidiwa na shirika la kijasusi la Marekani CIA mwaka 1965, baada ya kifo cha kiongozi wa kitaifa mzalendo Patrice Lumumba katika kipindi dhoruba na mashaka miongoni mwa wakongomani kwenye nchi iliyoonekana kama ni kitivo cha mapambano ya Vita Baridi (Cold War) barani Afrika.
Wapinzani walibeba utajiri wa Mobutu kama turufu, na baadhi ya Wazairwaa waliompinga walisema wangalithubutu kujaribu kufuatilia walichoamini kuwa ni utajiri wa wizi aliofuja nchini humo.
Kwa upande wake, Mobutu alikataa katakata kujibu madai ya wapinzani kwamba alikuwa ‘muuaji’ na ‘mwizi’
“ Sinta sema chochote, Historia itanihukumu…,” Mobutu alinukuliwa na shirika la habari maarufu duniani la Reuters akiwaambia wafuasi wake huku akivalia miwani nene ya macho na kofia yake ya Chui ikiwa ni alama ya utawala wake dhalimu.
Kiwango halisi cha utajiri wa Mobutu hakikujulikana. Hata hivyo,makisio ya awali, yaliyobainishwa na Wakongoma walio uhamishoni na waandishi wa habari hata na wabunge wa Marekani, alikuwa na utajiri wa dola bilion 5, huku maofisa wa serikali wa marekani wakipunguza kiwango hicho kwa makumi ya mamilioni ya dola.
“Ameanzisha genge la wizi na kumaliza wizi wote, ameweka mizania itakayolinganisha wezi wa kimataifa wa siku za usoni” Alisema mbunge Stephen J Solarz, mjumbe wa kamati ya mambo ya nje wa Bunge la Marekani, ambaye alikisia utajiri wa Mobutu kuvuka mabilioni.
“ Mobutu Alifanya Marcos aonekane kama ni mcheza kamari aliyeweza kupuna dau dogo”
Hata hivyo baadhi ya wanadiplomasia na wafuatiliaji wa siasa za Zaire walisema kiwango cha pesa Mobutu anachodaiwa kuiba limezidishwa mno “ Ni upuuzi” alisema ofisa mmoja wa ubalozi wizara ya mambo ya nje ya Marekani—wao walikadiria utajiri wa Mobutu kuwa kati ya dola 50 milioni au 125 tu.
“Alikuwa mfujaji tu, hakuwa akitunza pesa” alisikika afisa mmoja wa kidiplomasia akisema.
Utajiri binafsi wa Mobutu unaweza kuwa umepunguzwa, alisemwa mwana diplomasia huyo na wenzake, kwa kuwa alikuwa na tabia ya kutumia fedha nyingi kuwanunua maadui zake kwa lengo la kuwamaliza. Wanadiplomasia walisema Mobutu alikuwa anaweza kununua majumba ya kifahari na kuwapa wapinzani wake wa kisiasa kwa lengo la kuwanyamazisha, mara nyingine aliwagharamia safari za anasa barani ulaya na kuna siku alinunua magari 140 mapya na kuyatoa kama zawadi kwa wafanyakazi wa chuo kikuu waliokuwa wakilalamika mishahara midogo.
“ Mabilioni yamekamuliwa, ingawa yote yanarejea kulainisha mashine,” Alisema ofisa mmoja wa CIA huko Zaire aliyewekeza vitega uchumi nchini humo.
Katika mahojiano yake na shirika la habari la Africa News, Mobutu alisema Akaunti zake zilizopo nje ya nchi zilikuwa na dola million 50. “ Hii si pesa nyingi, ukizingatia nimekuwa Rais wa nchi hii kubwa kwa miaka 22” Alisema Mobutu huku akitoa macho makali nje ya miwani yake nene.
Mtafiti na mwanasayansi wa siasa kutoka chuo kikuu cha Wisconsin, aliyefanya tafiti mbalimbali zinazohusu utajiri aliouficha Mobutu alisema “Sina shaka baadhi ya pesa zake zilirudi kwenye mzunguko wa uchumi. Hata hivyo kusema kwamba alikuwa na dola 50 million tu ni ujuha”
Jijini Washington, Mfuasi wa Mobutu na mshirika wa biashara Mamadi Diane, aliyejipambanua kama ni rafiki wa Rais wa Zaire wa miaka 9 alisema kwenye mahojiano ya simu kwamba madai kuwa Mobutu ni billionaire yametiwa chumvi.
“ Watu wanatoa shutuma nyingi bila ya ushahidi,” alisema. “ Hakuna mtu hata mmoja aliyeonyesha ushahidi wa utajiri mbali na nyumba alizokuwa akimiliki. Hata sisi hapa Marekani tulidhani Shah wa Iran alikuwa na mabilioni, hata hivyo hakuna aliyeyaona…hatujayaona mabilioni ya Marcos wala Manuel Antonio
"Mobutu, unaweza sema alikuwa na maisha ya anasa,” Alisema Diane “Maisha ya anasa mno. Alikuwa na mtindo wa maisha wa aina yake. Aliishi kama mtemi wa Africa.
Kilicho bayana kuhusu Mobutu ni kuwa alikuwa mmiliki mkubwa ya mali zisizohamishika. Kwa mujibu wa wanadiplomasia wa marekani, Mobutu alimiliki Kasri la karne ya 16 mjini Lalencia, Nyumba ya anasa mtaa wa Foch Paris, na hekalu la vyumba 32 Lausanne, Uswisi, alikuwa na majuba Italia, Ureno na miji kadhaa ya Africa ikiwemo Abidjan, Ivory Coast na Dakar, Senegal
Mobutu pia alijenga himaya kubwa kwenye mji aliozaliwa kaskazini mashariki mwa Zaire mji wa Gbadolite—himaya hiyo ilijulikana kama “Versailles in the Jungle”
Mobutu alikuwa mtu wa matanuzi sana hasa akiwa safarini Ulaya. Hakuona shida kukodi ndege kubwa ya Concorde kutoka Ufaransa kwa safari zake, huku akiambatana na watu zaidi ya 100. Mmoja wa wasaidizi wake alisemekana kutembea na begi la kuburuza lililosheheni dola za kimarekani kwa ajili ya kulipia bili mbalimbali za hoteli.
Mobutu alikosolewa mwaka 1982 kwa kutumia ndege ya serikali ya Zaire kusafirisha wasaidizi wake 100 kwenda kutanua Disney world huko Florida marekani. Gharama inasadikiwa kuwa dola milioni mbili.
Haijulikani kama safari hizo zilizoambatana na bata la kufa mtu kama zililipiwa kutoka mfuko binafsi wa Mobutu, au Serikali ya Zaire.
Staili ya Maisha ya Mobutu inafanana na baadhi ya viongozi wa Africa waliojulikana wakati huo kama “ The Big Men”( Watu wazito) waliotawala kwa mkono wa chuma na ukandamizaji wa wananchi huku wakifanya kufuru ya bata kwa majina yao.
Balaa na laana iliyoikumba Zaire, wanasema wadadisi wa mambo, ni ile ya taifa tajiri lenye rasilimali kukuki hata hivyo linaloshindwa kujitosheleza kwa chochote si chakula wala mafuta. Yote hayo yalisababishwa na Mobutu aliyejulikana kwa lugha ya lingala kama Kuku Bgendu wa zabanga, yaani Jogoo aneyeweza kupanda majike yote! Mtumee!!! Mobutu ana dhambi!!!! Khaa!!
Kwa mujibu wa maofisa wa intelligensia wa Marekani mtawanyiko wa limbikizo la mali za Mobutu ilikuwa pamoja na kuhujumu migodi ya shaba, Kobati na almasi. Makampuni ya Gecamines ya almasi na MIBA( Miniere de Bakwanga) yanaelezewa kuwa vyanzo vikuu vya fedha za Mobutu alizozipata misili ya mfugaji anayekamua ng’ombe wake maziwa.
Benki ya Dunia na Mamlaka ya maendeleo ya kimataifa zilisema mwaka 1988 zaidi ya dola milioni 400 zitokanazo na mapato ya madini ya Zaire zilitoweka na kamwe hazikupatikana.
Nguza Karl-I-Bond, aiyewahi kuwa waziri mkuu chini ya Mobutu, na baadae kuwa mpinzani alitoa kiapo mbele ya kamati ya Bunge la Marekani mwaka 1981 kwamba mapema mwaka huo zaidi ya tani 20,000 za shaba zenye thamani ya dola milioni 35 ziliuzwa kinyemela, na pesa zote kwenda kwenye akaunti binafsi za Mobutu.
Waziri mkuu huyo wa zamani aliliambia Bunge la marekani alijua ndege za kukodi zilizokuwa zikibeba madini ya kobati na almasi ili yauzwe Ulaya, huku pesa hizo zikiwekwa kwenye akaunti binafsi ya Mobutu! Shubamit!!
Mikataba minono ya makampuni ilipewa kwa wanafamilia wa Mobutu na makuhadi wake. Mmoja wa watu walionufaika ni marehemu binamu wa Mobutu, Litho Maboti—aliyejulikana wakati huo nchini Zaire kama “ Mjomba Lito” aliyeweza kunufaika na amri ya kutaifisha ya mwaka 1973, kujenga himaya kubwa ya kibiashara na kilimo. Kwa mujibu wa chanzo kimoja, alivyokufa mwaka 1980 Litho alikuwa na pesa zipatazo Dola bilioni moja kwenye akaunti ya Benki Uswisi
Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa Young, kwenye kitabu chake cha mwaka 1985, kilichojulikana kwa jina la “MWANZO NA MWISHO WA TAIFA LA ZAIRE” aliorodhesha mashamba 14 chini ya usimamizi wa Celza ikiajiri wafanyakazi 25,000—na kuifanya mwaka 1977 kuwa kampuni kubwa ya uajiri nchini Zaire
Kwa mujibu wa Young, Mobutu pia alikuwa mwenyehisa mkubwa kwenye benki ya Kinshasa, (Banque du Kinshasa) ambapo makampuni yote ya taifa yanaweka fedha zao, pamoja na kupata, riba isiyo ya moja kwa moja kutoka katika makampuni ya kimataifa yanayofanya kazi Zaire kama vile ITT, Bell, Fiat, gulf, Pan Am Renault, Peugeot, Volkswagen na Unilever
Mbinu moja aliyoitumia Mobutu kuanzisha kampuni bubu ilia pate faida ilihusisha kampuni ya Risnelia iliyoandikishwa huko Panama, iliyoratibu pambano la masumbwi mwaka 1974 kati ya bondia maarufu duniani Mohammad Ali na George Foreman lililojulikana kwa kimombo kama ‘Rumble in the Jungle’
Kwa mujibu wa msomi wa Zaire Stephen R. Weissman, kama alivyoandika kweye Makala ya jarida la Nation mwaka 1974, Kampuni ya Resnelia ilikuwa ni mali ya Mobutu, aliyosimamia mapato ya pambano hilo.
Kwa mujibu wa Weissman, aliyemuhoji mwenyekiti wa Risnelia, Serikali ya Zaire ililipia promosheni ya pambano hilo kwa kutumia fedha za umma, huku Mobutu kupitia ofisi ya Rais, alitarajiwa kupata 42.5% ya mapato ya pambano hilo.
Katika wimbo wake maarufu wa propaganda uliojulikana kwa kifaransa kama Candidat na biso Mobutu, Mwanamuziki Franco alimpamba Mobutu ambaye kwa hakika alikuwa ni mgombea pekee katika kura ya ‘Ndiyo’ au Hapana. Licha ya kuwa mgombea pekee kwenye uchaguzi huo Mobutu hakufanya ajizi kufanya kampeni nchi nzima akipeleka ujumbe wake kote nchini Zaire. Kwa kweli wimbo huu ulikuwa ni nguzo imara ya propaganda. Baada ya matokeo kutangazwa Mobutu alipata asilimia 99.99%
Zifuatazo ni baadhi ya beti kwenye wimbo huo
Wake kwa waume wa Zaire
Nendeni mitaani,tawanyikeni kanda zote
Piga kelele kama radi, Kwa mgombea marshall
Mobutu Sese Seko
Tuwe wakweli, tuwe wawazi
Tunakataa unafiki, tunakataa kukosa fadhila
Nani atakayeisimamia nchi yetu, kama si Mobutu nani mwingine?
Mobutu sese seko
Kutoka Januari hadi Machi, Mwamko wa watu umerindima
Machi hadi mei, Wake kwa waume jeshini wamewezeshwa
Kutoka Mei hadi Novemba, Kila mtu ataichunguza dhamiri yake
Fikiria tulikotoka ,Shangilia, Shangilia jina la Mobutu
Haitakugharimu chochote kushangilia Ita jina la mobutu
Makala hii imeandikwa kwa msaada wa gazeti la Washington Post na vitabu mbalimbali vinavyoelezea historia ya Kongo.
Asalaam kudo
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena