Tulipoishia >>>>>Taarifa hii ilianza kuvuja ndani kwa ndani… simu zikaanza kumiminika. Inasemekana mpaka rais wa nchi ya Brazil kipindi kile Fernando Cordoso alipiga simu kutaka ufafanuzi kwa nini Ronaldo hatocheza mchezo huo wa fainali. Ndipo hapo ambapo Mario Zagolla akiwa anabubujikwa na machozi akawatobolea siri kwamba, kwa mud wa masaa sabini na mbili yaliyopita Ronaldo de Lima amekuwa anadondoka kifafa na kupoteza fahamu hivyo hawezi kumchezesha kwa kuwa anahofia kuhatarisha maisha ya mchezaji wake. Tuendelee Hapa Chini Ilikuwa ni habari ya kushtusha na kushangaza mno kwa sababu Ronaldo tangu azaliwe hajawahi kupatwa na kifafa maisha yake yote, iweje masaa sabini na mbili kabla ya mechi kubwa kama hiyo aanze kuanguka kifafa?? Kombe lile la dunia la mwaka 1998 lilikuwa na umuhimu wa aina yake… lilikuwa ni kombe la dunia la kwanza chini ya uongozi wa Sepp Blatter baada ya kushika wadhifa wa Rais wa FIFA. Lakini hili pia lilikuwa ni kombe la dunia la kwanza kabisa kwa kanuni mpya ya "goli la dhahabu" kuanza kutumika. Lakini pia lilikuwa ni kombe la dunia la kwanza ambalo lilishuhudia mwanzo wa refarii wa nne kutumia ubao wa elektroniki. Lakini pia mechi ya fainali kwenye ratiba ilikuwa imepangwa kufanyika siku mbili kabla ya siku ya Uhuru/Taifa wa Ufaransa maarufu kama Bastille Day.
Kwa hiyo fainali hii ya kombe hili la dunia ilikuwa na msisimko wake wa kipekee. Na kitendo cha Brazil mabingwa watetezi kufika fainali na kukutana na wenyeji timu ya Ufaransa ilifanya fainali hiyo kuwa ya historia.
Nilieleza namna ambavyo jina la Ronaldo liliachwa nje ya kikosi cha Brazil ambacho kilitarajiwa kuikabili Ufaransa, kitendo ambacho kilifanya mpaka rais wa nchi kuhitaji maelezo kwanini nyota huyo ameachwa nje ya kikosi. Na nilieleza maelezo ambayo kocha Mario Zagolla aliyatoa kwamba Ronaldo alikuwa anaanguka kifafa ghafla tu na hikuwa sahihi kumchezesha kwa kuhofia afya yake lakini pia hakudhani kama ataweza kucheza kwa ufanisi.
Turejee nyuma kidogo… masaa machache kabla
Masaa 72 kabla ya siku ya fainali kuna tukio lilimpata Ronaldo, kuanguka kifafa lakini tukio hili lilifichwa kwa ustadi kabisa pasipo wachezaji wenzake kujua zaidi ya daktari wa timu tu Dr. Lidio Toledo. Lakini wanasema hakuna marefu yasiyo na ncha, na hakuna siri inayoweza kudumu milele. Siku ile ya fainali 12 July 1998, mida ya mchana wachezaji wakiwa kwenye hoteli ya Chateau de Grande nje kidogo ya mji wa Paris walipata chakula cha machana na kisha kurejea kwenye vyumba vyao.
Wachezaji wote walikuwa wanakaa chumba kimoja wawili wawili na Ronaldo alikuwa anakaa chumba kimoja na Roberto Carlos. Kwa muda wa siku mbili au tatu hivi mfulululizo, Roberto Carlos alikuwa akimshuhudia mara kadhaa Ronaldo akijiinamia peke yake chumbani na kisha kuanza kulia. Ubaya ni kwamba alikuwa hataki kuongelea suala ambalo lilikuwa linamfanya kulia kila siku. Hali hii pia ilitokea siku hiyo ya fainali baada ya kumaliza kula chakula cha mchana na kurejea vyumbani mwao kujiandaa kuelekea uwanjani. Ronaldo alijiinamia tena kwa dakika kadhaa na kuanza kulia na kama ilivyo ada Roberto Carlos hakumuuliza nini hasa kilichokuwa kinamliza kwakuwa alifahamu fika kabisa Robaldo hataki kuulizwa swali hilo. Lakini tofauti na siku zote siku ya leo kilio cha Ronaldo kilikatizwa na kudondoka kitandani na kuanza kupaparika kama vile kuku aliyekatwa shingo. Alikuwa anapaparika huku povu likimtoka mdomoni.
Roberto Carlos alishikwa na taharuki asijue afanye nini, kitu pekee ambacho alikifanya ni kupiga yowe kubwa la kelele kuomba msaada.
Chumba cha Ronaldo na Roberto Carlos kilikuwa mkabala na chumba ambacho walikuwa wanalala Edmundo na Cesar Sampaio. Kwa hiyo alipopiga uyowe wa kuomba msaada Edmundo na Cesar ndio walikiwa wakwanza kuingia chumbani kwao walikokuwemo.
Walipoingia chumbani walimkuta Roberto Carlos anatetemeka kwa taharuki huku jasho likimtoka macho amekodoa kitandani. Nao walipotupa macho kitandani walimuona Ronaldo akiwa anapaparika povu likimtoka mdomoni. Ulimwengu wa soka unapaswa kumshukuru mno Cesar Sampaio, kwani pasipo yeye leo hii tusingekuwa na Ronaldo de Lima akiwa hai. Ronaldo alikuwa anapaparika, povu likimtoka mdomoni na akionyesha dalili kwamba alikuwa anaumeza ulimi. Ni Cesar Sampaio ambaye alirukia kitandania haraka haraka na kuingiza vidole vyake haraka haraka mdomoni kwa Ronaldo na kuzuia asimeze ulimi.
Wachezaji wenzake haraka wakatoa taarifa kwa uongozi wa timu na mara moja kocha Mario Zagolla na Daktari wa timu Dr. Lidio Toledo waliwasili. Wakati wanawasili Ronaldo alikiwa tayari amepoteza fahamu na hajitambui.
Roberto Carlos alianza kuwaeleza kocha na daktari juu ya sintofahamu aliyokuwa anamuona nayo Ronaldo kwa muda wa siku tatu nzima ambapo alikuwa akijiinamia peke yake na kuangua kilio. Kisha akawaeleza namna ambavyo siku hiyo husika ilikiwa tofauti baada ya kilio chake kukatizwa kwa kudondoka kitandani na kuanza kupaparika huku povu likimtoka mdomoni.
Walisubiri kwa dakika kadhaa mpaka pale ambapo fahamu zilimrejea Ronaldo na kuamka. Alipoamka ajabu ni kwamba Ronaldo alishikwa na bumbuwazi kuona watu wengi vile kwenye chumba chao. Aliamka akionekana dhahiri kabisa kwamba alikuwa hajui ni nini hasa kilikuwa kimetokea. Ili kuogopa kumpa taharuki zaidi mwanzoni walijitahidi kumficha wasimwambie kipe ambacho kilikuwa kimetokea… lakini Ronaldo aliweza kuzisoma nyuso za huzuni za wachezaji wenzake na akaendelea kuwalazimisha kwamba wamueleze ukweli ni nini hasa kimetokea. Ndipo hapo ambapo Dr. Lidio Toledo alimueleza ukweli juu ya kifafa ambacho kilikuwa kimempta ghafla.
Ronaldo alianza kulia tena na kuwataka wote watoke chumbani kwake anahitaji kuwa peke yake apumzike. Bila kukaidi kocha, daktari na wachezaji wenzake wote wakatoka nje ya chumba na kumuacha Ronaldo peke yake.
Kocha Mario Zagolla na Dr. Lidio Toledo walishindwa kuzuia machozi yao walipokuwa wanatoka nje ya chumba… kitendo hiki cha daktari nguli kama Lidio kububujikwa na machozi kiliashiria kwamba alihisi kabisa kuwa kuna uwezekano Ronaldo alikuwa na tatizo kubwa zaidi. Uongozi wa timu wakamuuliza Dr. Lidio anapendekeza nini kifanyike? Lidio aliwajibu kwamba iitwe ambulance haraka na Ronaldo achukuliwe na kupelekwa kwenye hospitali ya karibu na kufanyiwa vipimo kuangalia kama kuna tatizo kwenye mfumo wake wa neva.
Wakati uongozi wa timu wakiongea na Dr. Lidio ili kujua hatua za haraka za kuchukuliwa, wachezaji wa Brazil wakiongozwa na nahodha wao Dunga walimzunguka kocha wao Mario Zagolla kutaka kujua nini kinafuata na kwanini alikuwa analia. Zagolla akawaeleza bayana kwamba machozi yanamtoka kwa kuwa inamlazimu kuukacha mkakati wake wa kiufundi wa mchezo wa leo na waingie uwanjani na mkakati mwingine wa kiufundi. Walipomuhoji zaidi kutaka kujua zaidi ni nini hasa alikuwa anamaanisha, Zagolla akawaeleza kwamba anamuondoa Ronaldo katika kikosi ambacho kitamenyana na Ufaransa siku ya leo.
Ilikuwa ni mshituko mkubwa… habari mbaya zaidi ambayo hawakutamani kuisikia. Licha ya Ronaldo kuwa ndiye lulu wa timu yao, lakini katika mkakati wa kiufundi ambao walikuwa wameuweka juu ya mechi hiyo ya fainali Ronaldo ndiye ambaye alikuwa amepewa jukumu la kumkaba Zinedine Zidane akiwa pembeni ya uwanja. Zidane alikuwa ndiye mchezaji hatari zaidi ambaye walikuwa wanamuhofia na alikuwa na uwezo mkubwa sana katika kucheza mipira ya pembeni. (Goli zote mbili ambazo Zidane alifunga kwenye mechi hiyo hapo baadae ilikuwa ni mipira iliyotoka pembeni ya uwanja). Kwa hiyo habari hii kwamba Ronaldo hatokuwemo kwenye kikosi cha timu hiyo ilikuwa ni habari mbaya zaidi ambayo hawakutaka kuiamini wakitamani iwe ni ndoto tu wanaota.
Lakini swali kubwa ambalo lilikuwa linawatatiza lilikuwa ni nini hasa kimemkuta Ronaldo?? Inawezekana vipi awe mzima siku zote lakini siku ya leo, siku ambayo ulimwengu mzima ulikuwa unamsubiri kumuona, siku ambayo taifa lale lilikuwa linamuhitaji kuliko siku yoyote ile, siku ambayo ilikuwa ni muhimu zaidi hata kwake binafsi kuliko siku yoyote, ghafla tu apatwe na tatizo ambalo hajawahi kuwa nalo?? Lilikuwa ni swali kubwa ambalo halikuwa na jawabu la dhahiri…
Simu zikaanza kupigwa… mpaka rais wa Brazil alipiga simu kutaka kujua ni nini hasa kimetokea. Hakukua na mwenye jibu. Kila mtu alikuwa na dhahania tu… majibu ya labda, labda, labda…. Labda ilikuwa ni dawa ya maumivu ya goti ambayo alipewa na dokta Lidio wiki moja iliyopita labda ilileta matokeo hayo mtambuka. Lakini hii haikuwa sahihi kwa sababu dawa hiyo haina 'side effects' za namna hiyo na hata vipimo vya hospitali baadae vilidhihirisha hilo.
Labda Ronaldo alikuwa na tatizo hilo muda mrefu na amekuwa akilificha. Lakini hii haiingii akilini… kwa sababu Ronaldo kabla ya kujiunga na timu ya Taifa, alifanyiwa 'vetting' ya kutosha kama ilivyo ada kwa wachezaji wote wanaojiunga na timu ya taifa ya Brazil maisha yao kuchunguzwa nje ndani. Ronaldo alichezea timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 15, akachezea tena timu ya Taifa chini ya miaka 17… hivyo wanamjua vyema na hakuwahi kuwa na hili tatizo.
Wengine walisema labda alipata "mparaganyiko wa mfumo wa neva" (nervous breakdown) kutokana na taifa lake kumtegemea mno, na ulimwengu wote kumtegemea mno na wakitaka kuona makubwa kutoka kwake. Kwamba presha hiyo ilikuwa imezidia na kusababisha tatizo hilo. Lakini hii pia haikuwa inaingia akilini, kwa sababu Ronaldo ni mchezani wa kaliba ambayo amezoea presha. Hili halikuwa kombe lake la dunia la kwanza. Alijiunga na timu ya taifa akiwa ni kijana wa miaka 17 tu na alishiriki fainali za mwaka 1994 ambapo Brazil walichukua ubingwa. Lakini pia ndio alikuwa ametoka kumaliza msimu wa Serie A huko Italia huku timu yale ya Inter Milan wakichukua ubingwa na yeye akiwa mfungaji bora wa ligi. Amecheza michezo yote mikubwa ya Ligi ya mabingwa wa Ulaya. Presha ilikuwa kama kitafunwa kwenye chai, presha haiwezi kumteteresha mchezaji wa kaliba ya Ronaldo.
Kulikuwa na jambo… jambo kubwa hasa. Jambo ambalo mpaka leo hii limetia doa ulimwengu wa soka na kufichua namna ambavyo ushushu na ujasusi umetawala ulimwengu huo. Dili ya Nike na Ronaldo ilikuwa na thamani ya Euro milioni 10. Na papo hapo pia Nike walikuwa wanaidhamini pia timu y taifa ya brazil, udhamini ambao ulikuwa unagharimu karibia kiasi cha Euro milioni 105.
Papo hapo pia kama ambavyo nilieleza hapo nyuma kwamba Zinedine Zidane naye alikuwa ana mkataba mkubwa na kampuni ya adidas, kwahiyo mechi hii ya fainali pamoja na kwamba lilikuwa ni pambano la kukata na shoka kati ya miamba hii miwili lakini pia pambano hili lilikuwa ni la kibiashara kati ya kampuni ya Nike na kampuni ya Adidas.
Wakati ambao wachezaji wengine wakiwa wanajiandaa kuelekea uwanjani ni mida huo pia ambapo Ronaldo alikuwa amepelekwa hospitali kama ambavyo nilieleza.
Wakati bado mkanganyiko ukiwa ni mkubwa kutokana na taharuki ambayo ilikuwa imetokea kutokana na kocha Mario Zagolla kuliondoa jina la Ronaldo katika kikosi cha siku hiyo, ni muda huo huo ambapo wawakilishi wa Kampuni ya Nike waliwasili katika hotel ya Chateau de Grande ambayo kikosi cha Brazil kilikiwa kimefikia.
Ieleweke kwamba mpaka muda huo yalikuwa yamebakia kama masaa matatu tu kabla ya mtanange wa fainali kuanza katika uwanja wa Stade de France ulioko Saint-Denis.
Jambo moja ambalo tunapaswa kufahamu ni kwamba mkataba wa Nike na Brazil ulikuwa ni kama kitanzi shingoni mwa Brazil, Nike walikuwa na malaka makubwa sana juu ya hatma na kila ambacho kilikuwa kinaendelea kwenye timu hiyo ya taifa. Kuna wakati ulifika mpaka wachezaji walitaka kugoma na kuondoka kambini jijini Paris kutokana na mashinikizo ambayo wawakilishi wa kampuni ya Nike walikuwa wanayatoa. Muda wote wawakilishi hao wa Nike walikuwa hapo hotelini kana kwamba nao walikuwa ni sehemu ya benchi la ufundi la Brazil.
Kutokana udhamini huo ambao Brazil walikuwa wanautoa kwa timi ya taifa ya Brazil ilikuwa inawapa nguvu hata ya kushinikiza masuala ya kiufundi. Kwa mfano katika mechi za kirafiki za kujipima nguvu kabla ya kombe la dunia kuanza walikuwa wanashinikiza kuwa kikosi kizima kichezeshwe kikiwa na nyota wote wa timu hiyo. Kwa hiyo siku hii walipofika hoteli ya Chateau de Grande suala kuu ambalo lilikuwa limewapeleka ni kuhakikisha kuwa Ronaldo anacheza mechi hiyo ya fainali. Lakini kama ambavyo nimeeleza kuwa Ronaldo alikuwa katika hali mbaya sana kiafya kutokana na sababu zisizojulikana hivyo kumchezesha uwanjani kungeweza kuigharimu timu pamoja na maisha yake yeye mwenyewe… lakini waliokuwa wanajua namna ambavyo Nike wanashinikiza nyota wa Brazil kuchezeshwa walikuwa na presha wakitafakari ni nini kitatokea endapo Nike wakija na shinikizo la kiwendawazimu wakitaka Ronaldo achezeshwe.
Kikao cha dharura kikaitishwa hotelini kati ya wawakilishi wa Nike na benchi la ufundi la timu ya taifa ya Brazil. Kilikuwa ni kikao cha siri ambacho hatuna details haswa za nini kiliongelewa lakini kuna ushahidi wa kutosha kwamba kikao hicho wawakilishi wa Nike walikuwa wanashinikiza Ronaldo achezeshwe kwa madai kwamba tatizo lake la kuanguka kifafa ni mchezo mchafu ambao umechezwa na kampuni ya Adidas wakitaka Ronaldo asichezeshwe kwenye mechi ya fainali na Zinedine Zidane aweze kung'ara pekee kwenye mchezo huo ambao ndio tukio lenye kutazamwa zaidi dunia i kuliko tukio lolote lile.
Kikao kilikuwa cha karibia masaa mawili huku kikiwa na siri kubwa.
Katika kikosi kipya ambacho kilitangazwa kwa waandishi wa habari jina la Ronaldo halikuwemo na katika nafasi yake aliwekwa mchezaji Edmundo.
Wachezaji wote wa Brazil walikwea kwenye basi na kuelekea uwanjani pasipo Ronaldo. Kuna jambo la ajabu pia lilitokea… katika lile basi ambalo wachezaji wa Brazil walipanda kwenda uwanjani moja ya wachezaji wa kutegemewa mkongwe Leonardo Araujo ambaye alikuwepo kwenye kikosi kilichotangazwa hakuwepo kwenye basi na basi liliruhusiwa kuondoka kwenda uwanjani.
Leonardo Araujo ambaye miaka ya hivi karibuni aliwahi kuifundisha timu ya AC Millan na kwa sasa akiwa Director of Football katika klabu ya PSG ya ufaransa anatajwa kama mchezaji aliyekuwa anaheshimika sana na Ronaldo. Leonardo alikuwemo pia kwenye kikosi cha Brazil ambacho kilibeba kombe la dunia mwaka 1994.
Baada ya wachezaji wote kuondoka hotelini, Ronaldo alirejeshwa kutoka hospitali. Baada ya kurejea hotelini Ronaldo na Leonardo Araujo walionekana akiwa kwenye bustani ya hoteli wakitembea huku wakiafanya maongezi.
Walikuwa wanaongea nini?
Wanasema siri ya watu wawili… siri ya watu wawili ni ngumu kuijua labda mmoja wao aivujishe. Inakuwaje sasa isipovuja?? Tunapaswa kutazama mazingira na matokeo ya usiri wao na twaweza kung'amua siri ilihusu nini.
Kama ambavyo nimeeleza kwamba Leonardo alikuwa ni mtu mwenye kuheshimiwa mno na Ronaldo. Kuna kila dalili kwamba Nike walijaribu kumshinikiza Ronaldo acheze maechi hiyo lakini alikataa… ndipo hapa ambapo waliamua kumtumia Leonardo kumshawishi.
Inaaminika kwamba Nike walitoa "ultimutum" kwa Ronaldo kwamba kama hatocheza mechi hiyo basi mkataba wake na Nike utasitishwa.
Ndipo hapa ambapo dakika nusu saa tu kabla ya mechi ya fainali kuanza Ronaldo aliwasili kwenye chumba cha kubadilishia nguo uwanjani na kumvuta kocha Mario Zagolla pembeni. Mkononi alikuwa ameshika karatasi na kumueleza kocha… "…estou bem. En quero jogar.!" (Niko sawa sawa. Nataka kucheza)
Karatasi ile ilikuwa ni maelezo kutoka kwa daktari yakieleza kwamba Ronaldo hana tatizo lolote lile. Ilikuwa ni ajabu… iweje mtu aliyekuwa anadondoka kifafa dakika chache zilizopita ati daktari amthibitishe kwamba yuko fiti kwa kucheza mechi?? Inawezekanaje?? Hakuna shaka kabisa kwamba mchezo huu ulifanywa na Nike… kupika taarifa ya daktari. Kocha Mario Zagolla hakuwa na namna nyingine zaidi ya kuruhusu Ronaldo kucheza mechi hiyo. Unaweza kujiuliza kwa nini kocha aruhusu mchezaji kucheza ilhali akijua fika kwamba afya yake haiko fiti. Zagolla mwenyewe hata leo hii anaeleza kwamba akipewa nafasi nyingine ya kufanya maamuzi eidha kumchezesha Ronaldo siku ile au la, anasema atafanya uamuzi ule ule wa kumchezesha japo anajua kuwa afya yake haikuwa sawa. Sababu kuu anayoeleza ni kwamba siku ile ulimwengu mzima ulikuwa unasubiri kumuona Ronaldo, Ronaldo alikuwa ni tegemeo la timu na nchi. Baada ya kuona afya yake haiko sawa alifanya uamuzi sahihi wa kumuondoa kwenye kikosi… lakini kabla ya mechi analetewa "maelezo ya daktari" kuthibitisha ati yuko fiti. Kama angemuacha kwenye mechi ile bila kumchezesha alafu wangefungwa, ulimwengu mzima usingelimuelewa Zagolla na angeonekana amehujumu timu kwa kutomchezesha Ronaldo wakati "daktari amethibitisha" yuko fiti.
Kwahiyo Zagolla akajivua lawama… akamrejesha Ronaldo kikosini. Taarifa ikatolewa tena kwa vyombo vya habari kwamba kikosi kimebadilishwa tena, Ronaldo atacheza mechi hiyo.
Ulimwengu ukashangilia kwamba hatimaye watamuona shujaa wao usiku huo. Lakini wajuzi wa mambo taa zikawaka vichwani… walihisi kuna suala kubwa na baya linaendelea nyuma ya pazia.
Wote tunafahamu nini kilitokea usiku ule… Brazil walionyesha kiwango kibovu ambacho hakikuwahi kushuhudiwa na kuambulia kipigo cha mbwa koko cha bao tatu kwa sufuri. Zinedine Zidane akitupia bao mbili zote katika kipindi cha kwanza na magoli yote akiyafunga kwa kichwa kwa mipira kutoka pembeni ya uwanja. Mahala ambako Ronaldo alipewa jukumu la kumkaba Zidane. Katika dakika za nyongeza Emannuel Petit akitupia dakika goli la tatu baada ya kupata pasi mwanana kutoka kwa Patrick Vieira. Ronaldo ambaye ulimwengu ulimuona siku ile hakuwa Ronaldo ambaye walimfahamu. Ilikuwa inasikitisha kumuona anazunguka tu uwanjani kama mtoto mdogo. Akikosa magoli ya wazi kabisa… mfano kwenye kipindi cha kwanza alipokea pasi ndefu kutoka kwa dunga na alibakia yeye na kipa tu Fabien Barthez lakini akashindwa kufunga. Au katoka kipindi cha pili ambako pia alipata nafasi ya wazi ndani ya boksi na alitakiwa "kupasia neti" tu lakini matokeo yake alipiga fyongo kwenda mikononi kwa Barthez. Ilikuwa ni ajabu hata Leonardo ambaye ndiye "mchezeshaji" wa timu alishindwa kufurukuta. Hata 'genius' Rivaldo alikuwa kama vile hayupo uwanjani.
Mbaya zaidi ni kwamba Brazil ilishindwa kuifunga ufaransa ambao uwanjani walikuwa wachezaji kumi tu baada ya Marcel Desailly kupewa kadi nyekundu dakika ya 65.
Ulikuwa ni usiku wa maumivu na maumivu makubwa zaidi yalikuwa ni namna ambavyo shujaa wetu Ronaldo alicheza kwa kiwango kibovu.
Kwa upande wa Ufaransa ilikuwa ni shangwe na vifijo… walikuwa wameandika historia kwa kubeba ubingwa wa kombe la dunia kwa mara ya kwanza kabisa. Utamu zaidi ulikuwa ni kwamba wamebeba ubingwa huo siku mbili kabla ya Bestille Day, sikukuu ya Taifa la Ufaransa. Ulikuwa ni msisimko wa kipekee, ilikuwa ni 'romance' ya aina yake. *Najaribu kuwaza kwa sauti…* Kuna baadhi ya watu waliandika kipindi kile kwamba chama cha soka cha Brazil kilihongwa Euro Milioni 40 kutoka kwa Sepp Blatter (FIFA) ili timu yao ya taifa ikubali kipigo kutoka kwa ufaransa. Pia walipewa ahadi kwamba wakikubali kufanya hivyo basi FIFA itawaachia njia nyeupe waweze kushinda kombe la dunia litakalofuata la mwaka 2002 na pia watapewa wenyeji wa kombe la dunia miaka michache ijayo.
Kipindi kile watu walipuuzia shutuma zile… lakini inafikirisha mno tukikumbuka namna ambavyo katika michuano ya kombe la dunia mwaka 2002 namna ambavyo miamba ya soka Brazil walipangwa na vibonde watupu katika kundi lao la Group C ambapo walipangwa na China, Uturuki na Costa Rica. Brazil wakapenya kiulauni mno na mwishinu walitwaa ubingwa wa kombe la dunia 2002.
Bila kusahau pia mwaka 2014 Brazil walikuwa wenyeji wa kombe la dunia.
Picha hii ya Ronaldo inafikirisha sana... hapa ilikuwa ni baada ya mechi kuisha na wakiwa wakichrazwa goli tatu bila na wakiwa wametoka kupokea medali za mshindi wa pili.. lakini Ronaldo alipata "courage" ya kuning'iniza viatu vya Nike shingoni... labda alikuwa anajaribu kutuma ujumbe kwa ulimwengu ni nani tunapaswa kumlaumu au labda alikuwa ameendelea kupewa shinikizo la kuendelea 'kufanya tangazo' Je, zile shutuma zilikuwa na ukweli.? Inafikirisha zaidi namna miaka michache iliyopita Sepp Blatter alikumbwa na kashfa za ufisadi uliopelekea kujiuzuru wadhifa wa Urais wa FIFA.
Yatosha tu kusema kwamba mchezo wa mpira wa miguu ambao kwa karne karibia mbili sasa ulikuwa ukionekana "innocent" na msafi, mchezo wenye kuunganisha watu, mchezo wenye kutia faraja, mchezo wenye burudani ya kipekee… lakini mechi ile ya fainali ya mwaka 1998 ilitia doa sugu ambalo limeuganda mchezo huu hata leo hii.
Dhahiri kabisa kwamba kila uchwao ndivyo pia uhuni, ujasusi na skandali zinavyogubika mchezo huu.
Kuelekea kombe la dunia nitaendelea kuandika matukio mengi zaidi yaliyo nyuma ya mpira wa miguu.
Je uko tayari kwa kufahamu ujasusi unaofanywa na George Mendez au kama wamuitavyo kwenye ulimwengu wa soka "super agent" na kampuni yake ya GestiFute??? Stay here…
Habibu B. Anga "The Bold" - 0718 096 811 To Infinity and Beyond
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena