Kutokana na dhana ya mahusian
o kuwa pana kama nilivyotoa mifano michache hapo juu,na uhitaji wake kuwa mkubwa,natamani leo tuzungumzie kwa kifupi mahusiano muhimu ya mtu na mtu na umuhimu na athari zake pia.
Karibu tena msomaji wa makala zetu kwenye mtandao wetu. Leo nimechagua kukushirikisha mada inayoitwa “UMUHIMU WA MAHUSIANO” na nikushukuru tu kwa muda wako uliotenga uendelea kufuatilia mada hizi. Nathamini sana mchango wako huo.
Mahusiano mazuri yana mchango mkubwa katika maisha ya watu na kadhalika mahusiano mabaya ndicho chanzo cha migogoro mingi kati ya mtu na mtu. Mahusiano ni kitu kizuri sana kikitumiwa na pia kina madhara makubwa hasi kama kikitumiwa vibaya katika mahusiano ya mtu na mtu.
Ukikosea katika kipengere hiki cha mahusiano basi uwe na uhakika unaweza kusababisha gharika kubwa katika maisha yako ambayo yanaweza kugusa hata maisha ya watu wengine wanaokuzunguka.Na ukifanya vizuri basi madhara yake pia yatagusa mpaka watu wanaokuzunguka.
Watu wenye furaha katika maishani ni wale ambao kwa sehemu fulani,wamefanikiwa katika kipengere hiki cha mahusiano kwa kujua ama bila hata kujua;wana maarifa ya namna ya kuhusiana na watu wengine katika maisha yao kila siku na maisha yao yanavutia watu wengine.
KWA NINI MTU MMOJA AFANIKIWE NA MWINGINE ASHINDWE KATIKA MAHUSIANO?
Anthony Robbin amefafanua sana katika kitabu chake cha “Unlimited Power”.Ili uweze kuhusiana vizuri na watu inabidi kuwa na taarifa ambazo zinakuhusu wewe binafsi na hata watu wengine hapo utafaulu katika swala zima la mahusiano.
Kwanza ni muhimu kuwa na taarifa kuwa mahusiano siyo kitu cha kuchagua ni kitu cha lazima kwa hiyo ili tuishi kama binadamu tunahitaji kuhusiana vizuri na watu kwa sababu mahusiano ni swala linalohusu mtu na mtu au watu na watu.Mahusiano haliwezi kuwa swala la mtu mmoja tu! Ingekuwa hivyo dunia ingekuwa haina mvuto kabisa.
Kama mahusiano ni swala la mtu na mtu basi mwenyezi Mungu alivyoumba hao watu hawawezi kufanana tabia,hulka na hata vitu wanavyotamani katika maisha yao.Tunatofautia sura na hata namna tunavyowaza pia. KIla mtu jinsi alivyoumbwa anao umuhimu wa pekee katika maisha,hatupaswi kumpuuza mtu hata mmoja.
Wapo watu wanaokuunga mkono katika kila jambo unalofanya,wapo watu wanaokupinga katika kila jambo,wapo wanaokupenda mpaka wewe unajua kuwa wanakupenda,wapo wanaokuchukia tu mpaka wewe unajua wanakuchukia,wapo marafiki zako na wapo wale ambao wanakupa changamoto katika kila unalofanya. Nataka nikukumbushe wote hao kama walivyoumbwa na Mungu ni watu muhimu sana.
TUFANYE NINI ILI TUWEZE KUFANIKIWA KATIKA SWALA LA MAHUSIANO?
- KUJITAMBUA WEWE KAMA WEWE
Kama unatamani kufanikiwa katika swala zima la mahusiano maishani unapaswa kuwa na uhakika wewe ni nani,unatoka wapi,upo hapa kufanya nini na unakwenda wapi. Hatua ya kujifanyia tathmini inapaswa kuzingatiwa kwa sababu huwezi kutegemea kutambua watu wengine ikiwa wewe mwenyewe huna uwezo wa kujitambua.
Hii itakusaidia hata kuweka viwango vyako vya mahusiano,ni mambo gani ambayo unapaswa kujielekeza kwayo katika swala zima la mahusiano,kina nani unapswa kushirikiana nao na kina nani unapaswa kuwapenda lakini usiwape nafasi ya kutosha kushirikiana nao kwa sababu hawakusaidii kufika kule unakotaka kufika.
- TAMBUA UNAKOTAKA KUFIKA
Hatua ya kuwa na taarifa juu ya kule unakotaka kufika itakusaidia sana kukuwezesha kuchagua nini cha kufanya na nini cha kuacha kutegemeana na picha ya kule unakotamani kufika.Kama utaona kwa kuchukua uamuzi fulani itakuchelewesha kufika kule unakotaka kufika ni uamuzi mzuri kuacha kufanya uamuzi. Ni muhimu sana kutambua kusudi la kuwepo kwako hapa duniani na hilo kusudi basi litakujengea nidhamu ya nini cha kufanya na nini usifanye bila kusukumwa na mtu yeyote. Kwa kifupi utaishi wewe kama wewe.
- TAMBUA KIGEZO CHAKO
Kwa mujibu wa Tony Robbin kila mtu unayemjua na yule usiyemjua katika eneo lolote la maisha ana kitu kinaitwa “Blue Print” kwa kiswahili haikai vizuri sana lakini unaweza kuita “kigezo au mategemeo” na katika eneo la mahusiano watu wote jinsi tulivyo tunacho kigezo tulichojiwekea.
Katika eneo la mahusiano pia kila mtu ana kigezo kwenye eneo hilo.Blue print ina orodha ya taarifa ambazo mtu anapaswa kuwa nazo ili kuwa mtu mzuri kwenye mahusiano au kitu chochote.
Mtu mmoja akifanya kitu kinachokubaliana na kigezo ulichoweka utakuta mambo yanakaa vizuri na hapa mahusiano yanaimarika,lakini vikitofautiana inaweza kutokea ajali na mahusiano yoyote kukaa vibaya.
Hivi vigezo huhitaji kufanyiwa maboresho mara kwa mara kutegemeana na wakati.Kigezo kilichofaa kutumiaka miaka ya 1970 yawezekana kisifae kabisa kwa mazingira ya sasa hivyo kinahitaji kufanyiwa maboresho.
Changamoto kubwa katika mahusiano ni kwamba watu wengi tuna matarajio chanya makubwa lakini hatujali kufanyia maboresho vigezo vyetu ili vilingane na mahitaji ya wakati.Hatutaki kubadilika kabisa hatuko tayari.
Hebu nimalizie kwa kutoa mfano huu mfupi ili iweze kueleweka vizuri.Chukua picha kichwani mwako ya watu wawili wanandoa. Watu hao nao wana uhusiano unaoitwa ndoa.Mke ana kigezo chake katika eneo hilo,na mume ana kigezo chake katika eneo hilo la mahusiano yanayoitwa ndoa.
Ili iwe ni ndoa ya furaha na kutolea mfano kigezo cha mume kina vitu kama mke lazima awe ni msikilizaji,akiitwa na mumewe anaitika na kukimbia,akirudi kutoka kazini lazima apokelewe na mkewe,yeye ni kichwa cha familia ni mtu wa kutoa amri na mke anatekeleza.Na mume ndiye anayemiliki sehemu kubwa ya uchumi wa familia.
Kigezo cha mke katika eneo hilo ndoa kina orodha ya vitu kama haja ya kusikilizwa na mume wake,kuongozana wakienda kusali au wakitoka out,kutokumkemea mbele ya watu anapokosea,kuwezeshwa kiuchumi ili naye awe na mchango katika bajeti ya familia,kumletea zawadi mara kwa mara na kumnunulia nguo kila siku sikuu n.k.
Hao ni wana ndoa wawili ambao wanakaa pamoja na kila mmoja ana orodha ya vitu anavyotaka mwenzake awe navyo.Unaona blue print za wanandoa hawa zinavyotofautiana? Huyu anafikiri hivi,mwenzake anafikiri tofauti.Hapo yasipokuwepo maarifa ya kujisadia au kusaidiwa ili kuboresha kutatokea ajali kila siku katika mahusiano ya hawa wana ndoa kwa sababu wanagongana mara kwa mara katika maeneo mengi.Ule mvuto wa mke na mume uliokuwepo mwanzo unatoweka pole pole na mwisho wa siku watajikuta wanaishi kama watu tu.
- IMARISHA MAWASILIANO
Watu wengi hawana taarifa juu ya vigezo vya mahusiano vya wenzao ambao wana mategemeo makubwa kutenda mambo ambayo yangeimarisha uhusiano wao. Hawajui wenzao wanavyowaza,wala vipaumbele walivyoweka katika eneo zima la mahusiano.
Itawezekanaje utegemee mtu atende unavyotaka bila wewe kujua kilicho kwenye orodha ya vigezo vyake vya mahusiano wala yeye bila kujua wewe kwenye mahusiano mategemeo yako ni nini?
Mawasiliano ndio hatua pekee inayoweza kukusaidia kuboresha mahusiano na watu unaotamani mhusiane vizuri. Bila mawasiliano inawezekana kabisa mahusiano kuharibika hata kwa mtu ambaye mlikuwa mnaheshimiana sana.Kufunga mlango wa mawasiliano ni sumu ambayo inaweza kuchafua mahusiano.
Ukiona mahali kuna mahusiano na maelewano ya kutosha hiyo ni dalili ya wazi kwamba mahali hapo kuna mawasiliano ya kutosha.Kila upande una mdomo na sikio la kusikiliza na kusikilizwa pale inapobidi.
- BADILIKA WEWE
Mara nyingi kwa kuwa unajitambua wewe ni nani,ulitoka wapi na pia unayo picha ya kule unakotaka kwenda,basi mwenye jukumu la kusaidia katika swala zima la mahusiano ni wewe unayejitambua.
Mtu hajui yeye ni nani,anatoka wapi,yupo hapa kufanya nini wala anakoelekea hajui! Unategemea awe kama unavyotegemea? Kama inawezekana kubadilika wewe badilika kwa sababu hiyo iko ndani ya uwezo wako,na kamwe usijaribu kulzaimisha kumbadilisha mtu,utajikwaa kila siku.
Hebu kafanye tena utafiti kwa watu wawili jirani,rafiki au ndugu yako mnaeelewana chunguza blue print yako na yake na yule msiyeelewana chunguza pia.Ukifanya kwa uangalifu utapata matokeo ya kukuvutia sana hata wewe mwenyewe.Na ukiijua siri hii utafanikiwa sana katika eneo la mahusiano na hutagongana na mtu hata siku moja.
Maisha ni fursa nasi binadamu tunayo nafasi ya kufurahia maisha kwa kuhusiana vizuri na watu wanaotuzunguka,ndugu zetu,rafiki,jirani na watu wote wanaotutakia mema na mabaya,wanaotuombea na wasiotuombea,wanaotupenda na wasiotupenda,kwa sababu wao ni muhimu sana kwa uwepo wao kwani maisha ni watu.Mahusiano ni sanaa!!!!
Kusoma zaidi bonyeza linki hapa chni.
Naamini utakuwa umepata kitu katika mada hii fupi.Kama utakuwa na uhitaji wa kutaka ushauri wa namna ya kuboresha au kuingia ndani zaidi katika mada hii,basi usisite kuwasiliana nami kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno,whatsap au kupiga kupitia simu hapo chini.
Ni mimi rafiki na kocha
Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale
Simu +255784503076
Email:maishanifursa2017@gmail.com
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena