Header Ads Widget

Responsive Advertisement

KUTANA NA NISHER ALIYEZUNGUMZA NA GPL -JEMBE LILILOIBULIWA NA WEUSI

https://sundayshomari.files.wordpress.com/2014/11/nisher.jpg
Nisher ni kati ya watengenezaji bora wa video Bongo ambao wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuleta mabadiliko katika sekta hiyo. Jamaa huyu makazi yake yapo Arusha na kazi zake zote anafanyia huko. Kama ukiangalia video ya Jikubali iliyoimbwa na Ben Pol kisha Mama Yeyoo ya G.Nako ama video ya Nje ya Box au Chuna Buzi ya Shilole utatambua uwezo wake wa kuzipika video kiufundi.
Juzikati Nisher alitinga ndani ya Global Publishers na kufanyiwa mahojiano katika Kipindi cha Mtu Kati kinachorushwa kupitia Mtandao wa Global TV Online na katika makala haya anafunguka zaidi:
Unazungumziaje wasanii kurekodi video nje ya nchi? Ni sawa kwani ni biashara na ni fedha ya mtu na huwezi kumkataza mtu anapotaka kuwekeza.
Lakini kwa sanaa ya nchi yetu inatakiwa uangalie unatangaza vipi nchi yako. Muunganiko ni muhimu lakini usifanye muunganiko utakaokufanya ukawasahau madairekta wa nchi yako.
Ni kweli tatizo ni mandhari ndiyo maana wanakimbia Bongo? Hapana! Ujue mandhari hapa Bongo zipo tena nyingi kwangu mie wanavyokimbilia huko naona ni changamoto tena nzuri kwani inatufanya tuone wapi tunakosea.
Ila tatizo la Wabongo wakishafanya video huko nje watakuja na kujisifu kuwa wamefanya kwa mkwanja mrefu lakini mtu huyo huyo akija kwako analia-lia anataka umtengenezee hata kwa bure.
Kwa nini gharama zako ni kubwa kurekodi? Ni kweli gharama zangu ni kubwa na zimelenga kwa wale wenye kipato kikubwa kutokana na uzuri ninaoufanya. Nimekuwa na uzoefu kwa kufanya kazi na wasanii wakubwa kwanza naona inanipa wakati mzuri wa kujifunza mengi kupitia wao, namuamini na Mungu pia.
Upoje uhusiano wako na Weusi? Weusi ni kama familia yangu, Joh Makini ni baba, G.Nako ni kaka na Niki wa Pili ni ndugu wa karibu. Najivunia kuwa nao kwa sababu ni wa kwanza kunitangaza na watu wakajua kuwa kuna mtu anaitwa Nisher.
Watu gani wamesaidia mafanikio yako? Namshukuru Mungu kwani ndiye anayenisaidia kufanya ubunifu pia wazazi wangu na ndugu na marafiki mbalimbali.
Kwa nini ni ngumu staa kumkubali staa mwenzake?Wanakubaliana ila sema kwenye nyanja za kazi hutakiwi kumpigia mwenzako magoti kwa sababu ni kazi. Ni sawa na mabondia kabla hawajaanza mpambano wanakumbatia lakini baada ya hapo wanaachana.
Ni kweli unatoka na Lulu? Hapana! Lulu ni rafiki yangu tu wa kawaida tena urafiki wetu ni wa ndani ya Mtandao wa Instagram.
Yeye yupo na maisha yake na mimi ya kwangu na mara zote tumekuwa tukitaniana sana wala sijawahi kutoka naye kimapenzi.
Kitu gani kinasababisha maprodyuza kupotea ghafla? Kikubwa ni kulewa sifa ama kujisahau kwani ni kitu rahisi sana,hata mie nilipokuwa naanza nilikuwa nikipata simu nyingi huku wengi wakinipongeza na kuniambia nisilewe sifa.
Kwa hisani ya GPL TV.

Post a Comment

0 Comments