Nilizaliwa
tarehe 28 Januari 1974 mjini Singida, kwa Bi. Josephine Joseph na Bwana
Yusuf Makamba. Mwaka 1978, nilipelekwa kuishi kijijini kwa bibi mzaa
mama Kyaka, Kagera wakati mama ameenda kuendelea na masomo ya uuguzi.
Kijijini kwetu ilikuwa umbali mfupi kutoka Mutukula, mpakani mwa
Tanzania na Uganda. Idi Amini alipovamia Tanzania mwaka huo, kitongoji
chetu kinachoitwa Kituntu, sio Kituntu ya Karagwe unayoijua wewe Padre,
karibu na Kyaka nacho kilipigwa mabomu. Mimi na bibi yangu tulikimbia
makazi yetu na kuhamia kwenye kambi ya wakimbizi eneo linaloitwa Mwisa.
Baba yangu wakati huo alikuwa mstari wa mbele kwenye vita dhidi ya Idi
Amin. Tulikaa kambini kwa muda baadaye tukafanyiwa utaratibu wa kuondoka
kwenda Biharamulo na mama akaja kutuchukua. Sina kumbukumbu kubwa sana
ya kipindi hiki kwa kuwa nilikuwa bado mdogo ila nakumbuka mvua nyingi,
milio ya ndege na mabomu.
Nimesoma shule nne
za msingi katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu kutokana na wazazi
kuhamishwa mara kwa mara katika utumishi wa umma. Lakini pia kuanzia
darasa la tatu hadi la tano nilirudishwa tena kijijini, Kituntu Kyaka,
kukaa na bibi. Maisha ya kijijini siwezi kuyasahau. Enzi hizo, miaka ya
mwanzoni mwa 1980, maisha ya kijijini yalikuwa magumu sana, bidhaa
muhimu kama sukari, sabuni, dawa za mswaki, chumvi, na nyinginezo,
zilikuwa adimu. Kutoka kitongojini Kituntu hadi shuleni ilikuwa mwendo
mrefu na baada ya shule nilikuwa na kazi ya kwenda kuchunga mbuzi wa
bibi, na baada ya kuchunga mbuzi kila jioni saa moja ilikuwa ni kazi ya
kuchota maji mtoni, na baada ya hapo ilikuwa ni kumsaidia bibi kuuza
pombe ya lubisi usiku na Jumamosi ilikuwa ni kwenda shamba kupalilia
migomba na mikahawa. Maisha yale yalinifundisha mambo mengi. Baada ya
miaka mitatu, nilirudi kukaa na wazazi na kumalizia darasa la saba Shule
ya Msingi Masiwani, Tanga Mjini.
Nilianza Sekondari katika shule
ya Sekondari Handeni, Tanga. Nakumbuka wakati naanza pale shule ile
ilikuwa bado inajengwa, sisi tulikuwa Form 1 wa pili na ilikuwa haina
tofauti kabisa na shule ambazo sasa zinaitwa shule za Kata. Kwa kuwa hii
ilikuwa shule ya kutwa, mzazi wangu alipohamishwa kikazi kutoka
Handeni, nikahamia Shule ya Sekondari Galanos Tanga, ambayo ilikuwa
shule ya Serikali ya boarding.
Nilikuwa mwanafunzi mzuri pale
Galanos, na, nikiwa kidato cha tatu, nikachaguliwa kuwa Makamu wa
Kiranja Mkuu. Nilikuwa nafanya vizuri darasani, nikachagua mchepuo wa
sayansi nikiwa na combination ya Chemistry (Kemia), Biology (Baiolojia)
na Agriculture (Kilimo) (CBA). Nilipata daraja la kwanza kwenye mtihani
wa kanda wa mock wa kidato cha nne, nikiwa na uhakika wa kuendelea na
A-Level katika Shule ya Sekondari Kibaha, shule pekee iliyokuwa
inafundisha mchepuo wa CBA hapa nchini. Hata hivyo, nilifanyiwa hujuma
kubwa kutokana na siasa zinazomhusu Mzee wangu na kufutiwa matokeo ya
mtihani wa kidato cha nne.
Sikufa moyo, nilirudia mtihani kama
mtahiniwa binafsi na kufaulu na kuweza kusoma A-Level katika Shule ya
Sekondari Forest Hill Morogoro na nikapata Daraja la Pili kwenye mtihani
wa Kidato cha Sita. Kabla ya kwenda Chuo Kikuu, niliamua kwenda kufanya
kazi kwenye makambi ya wakimbizi kutoka Burundi yaliyokuwa wilaya ya
Kasulu, Mkoani Kigoma. Niliipenda sana kazi ile ya kuhudumia wakimbizi
na kuifanya kwa bidii kubwa. Nilipewa madaraka zaidi hadi kufikia nafasi
ya Meneja wa Kambi Msaidizi wa Kambi ya Mtabila 2 iliyokuwa na
wakimbizi zaidi la laki moja. Nilibahatika kuwa na wajibu na dhamana
kubwa ya kuongoza kambi kubwa na wafanyakazi wengi nikiwa na umri mdogo
tu wa miaka 21. Nilikuwa na wafanyakazi wengi, tena wengine watu wazima,
waliokuwa wanaripoti kwangu. Nilikuwa na wajibu wa kuhakikisha kwamba
wakimbizi laki moja wanapata viwanja vya kuishi, wanapata vifaa muhimu
kama mahema, na wanapata chakula. Kazi ile ilibadilisha kabisa mtazamo
wangu juu ya maisha. Baada ya kushuhudia adha wanayopata wanadamu
wenzetu kutokana na vita hadi kukimbia makazi yao na nchi yao na kuja
kukaa maporini kwenye nchi yetu, na baada ya kutafakari kuhusu
udhalilishwaji na mateso yanayotokana na ukimbizi, niliamua kuachana na
azma ya kusoma sayansi na uchumi na nikaamua kwamba maisha yangu
nitayatoa katika kuchukua masomo kuhusu amani, na namna ya kutafuta
amani ili nitoe mchango kwenye kuepusha vita na kupatikana kwa amani
duniani. Hivyo, nilianza kutafuta vyuo duniani vinavyofundisha masuala
ya amani. Nilipata chuo kimoja cha Wakatoliki Marekani, kinachoitwa St.
John University. Lakini kilikuwa Chuo aghali kidogo, kwa hiyo nikaanza
kusoma masomo ya awali kwenye Chuo kingine kidogo katika jiji la Boston
kinachoitwa Quincy College na baadae nikajiunga na St. John University
na kupata shahada ya kwanza ya sayansi ya masomo ya amani (Bachelor of
Science in Peace Studies). Gharama za masomo zilikuwa kubwa na
nilihangaika kufanya kazi mbalimbali, ikiwemo kazi za ulinzi na
kuhudumia watu wenye magonjwa ya akili ili kulipia ada ya shule.
Baada
ya kumaliza shahada ya kwanza, nilishinda tuzo ya kujiunga na taasisi
ya Rais Mstaafu wa Marekani, Jimmy Carter, inayoitwa Carter Presidential
Center iliyopo Atlanta hukohuko Marekani. Ilikuwa changamoto kubwa na
fursa nzuri kwa sababu vijana wote waliojiunga pale walikuwa ni vijana
mahiri sana na wenye uwezo mkubwa. Taasisi ile ilinipeleka nchini Sierra
Leone kusimamia uchaguzi mkuu na kutekeleza mradi wa kufufua taasisi za
haki zilizoporomoka baada ya vita. Nako pia nilijifunza mengi kuhusu
ujenzi wa taifa.
Baada ya hapo nikaamua kuchukua shahada ya pili
(Masters degree) kwenye Chuo Kikuu cha George Mason kilichoko Jimbo la
Virginia, Marekani. Nilipata wakati mgumu kulipa ada, kiasi cha
kukaribia kufukuzwa shule. Niliomba msaada kwa watu mbalimbali akiwemo
Rais wa wakati ule Mhe. Benjamin William Mkapa. Bahati nzuri, alikubali
kusaidia kwa sharti kwamba nije kutumia utaalamu wangu Serikalini
nitakapomaliza masomo. Na ndivyo nilivyofanya. Baada ya masomo hayo,
nikajiunga na Wizara ya Mambo ya Nje.
Mwaka 2005 nilifunga ndoa
na mchumba wangu wa miaka minne, Ramona Urasa, na nimekuwa na familia
yenye furaha sasa mwaka wa kumi. Pale Wizarani, nilipata fursa ya
kufanya kazi na Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo, Mhe. Jakaya Mrisho
Kikwete. Nahisi alipenda kazi zangu na mara alipoamua kuwania nafasi ya
Urais akanitaka nichukue likizo isiyo na malipo Serikalini ili niwe
msaidizi wake kwenye kampeni zile. Siwezi kusahau maishani mwangu ile
fursa kubwa kwani niliweza kuijua kwa kina nchi yangu na watu wake. Na
kwa kuwa kampeni zinahusu ahadi za utatuzi wa kero za watu, nilipata
fursa ya kujua kero za Watanzania kwenye kila wilaya ya nchi yetu.
Baada
ya Rais Kikwete kushinda aliniteua kuwa Msaidizi wake Ikulu, nikiwa na
jukumu la kumsaidia kuandika hotuba zake, pamoja na mambo mengine mengi
ya uendeshaji wa shughuli zake za kila siku. Kazi ile ilikuwa ngumu kwa
sababu inakulazimisha kujifunza na kujua karibu kila kitu ndani ya
Serikali na duniani kwa ujumla, na kufanya utafiti karibu kila siku kwa
sababu Rais anazungumza kila siku kuhusu mambo mbalimbali na kwa makundi
mbalimbali. Pia kazi ile inakupa fursa ya kuhudhuria vikao vya Baraza
la Mawaziri kama msikilizaji ambapo pia unajifunza mambo mengi ya
uendeshaji wa Serikali, ikiwemo maamuzi muhimu ya kisera na kiutendaji
yanavyofanywa. Ni nafasi ya heshima sana na sitamsahau Rais Kikwete kwa
kunipa fursa ile.
Baba yangu alikuwa mwanasiasa karibu maisha
yake yote lakini sikupata kuwaza kuingia kwenye siasa katika maisha
yangu hadi nilipofanya kazi na Rais Kikwete. Baada ya kufanya kazi ile
Ikulu kwa miaka mitano, nami nikahamasika na kuamua kushiriki katika
uongozi wa umma. Niliamua kwenda kwetu Bumbuli kugombea nafasi ya Ubunge
mwaka 2010, nikafanikiwa. Baada ya kuingia Bungeni nikapata nafasi ya
kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini. Kazi ile
tuliifanya vizuri sana na wenzangu kwenye Kamati hasa katika kipindi
kile kigumu cha mgao wa umeme na matatizo ya mafuta nchini.
Baada
ya kitambo kidogo, nikateuliwa kwenye Sekretarieti ya Chama nikiwa kama
Katibu wa NEC wa Siasa na Mambo ya Nje, na nikawa Mjumbe wa Kamati Kuu
na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Nilishika nafasi hizi katika kipindi
kigumu sana kisiasa kwa Chama chetu na nilijifunza mambo mengi na kutoa
mchango wangu kwenye kukijenga na kukiimarisha. Baada ya kitambo
kingine, nikateuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia.
Kuhusu kubebwa na jina la mzazi, kama nilivyosema
hapo awali, pamoja na kwamba mzazi wangu alikuwa kwenye siasa kwa muda
mrefu, binafsi, ingawa nilipenda na nilishiriki kuwa kiongozi tangu
shuleni, sikuwa na mawazo ya kuingia katika siasa. Nilipokuwa Sekondari
nilipenda kuwa mwanasayansi wa kilimo.
Baada ya kuzunguka nchi
nzima kwenye kampeni ya 2005 na baada ya kufanya kazi ya kumsaidia Rais
Ikulu ndipo nilipobaini kwamba siasa, ukiiendesha vizuri na kwa manufaa
ya watu, inayo nafasi ya kubadilisha maisha ya watu. Nilipofanya uamuzi
wa kugombea Ubunge, sikutaka ushauri wa baba yangu kwa sababu nilikuwa
na uhakika kwamba angenikatalia. Niliamua mwenyewe na nikaanza harakati
na ndipo nikamwambia. Kwa hiyo, unaweza kuwa na mzazi mwanasiasa na bado
ukaweza kuwa na uhuru wa kujiamulia mwenyewe unataka kufanya nini.
Ni
kweli kwamba jina maarufu la mzazi aliye kwenye siasa linasaidia kwa
maana tayari kuna watu ambao wanamheshimu na ambao wapo tayari
kukusaidia. Lakini pia jina hilohilo linaweza kukuharibia kwa sababu pia
unaweza kurithi maadui zake, ambao wanakuona wewe ni sehemu ya yeye
hata kama una mawazo na mtizamo huru. Kwa hiyo, siasa yangu nimejitahidi
kuifanya kama mimi binafsi. Mimi na baba yangu tuna staili tofauti za
siasa na mimi nina namna yangu ya kufanya mambo ambayo inatofautiana na
yake. Lakini pia kuna mambo mengi mazuri ambayo nimejifunza kutoka kwake
ikiwemo haja ya kuwa na msimamo usioyumba katika unayoyaamini na haja
ya kutokumuogopa mtu yoyote
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena