Askari wa Marekani wakiwa nje ya uliokuwa ubalozi wa nchi hiyo Tanzania baada ya shambulio la kigaidi mwaka 1998.
Dar es Salaam. Wakati mashambulizi ya kigaidi yakiendelea kutikisa maeneo mbalimbali duniani ikiwamo nchi jirani ya Kenya huku kukiwa na angalizo kuwa huenda na Tanzania ikashambuliwa, jarida moja la kimataifa limetaja mambo 10 ya kufanya baada ya shambulio.
Mambo hayo ambayo ni hatua za kumsaidia mtu aliyenusurika katika shambulio husika ili kunusuru maisha yake, yametajwa wakati zikiwapo taarifa za tisho la shambulizi katika miji ya Dar es Salaam na Mwanza.
Jarida hilo lilifanya mahojiano na wataalamu wa sayansi ambao walitoa mapendekezo ambayo mtu anaweza kufuata wakati au baada ya mlipuko na kuwa asilimia 50 ya watu wanaokutwa katika mashambulizi ya kigaidi hujeruhiwa na wengine kupoteza maisha kwa sababu hawafahamu jinsi ya kujihami.
Tanzania iliwahi kukumbwa na shambulio la ugaidi mwaka 1998 wakati Ubalozi za Marekani, jijini Dar es Salaam ulipolipuliwa na kusababisha vifo vya watu kumi na moja. Shambulio hilo lilitokea sambamba na lile la ubalozi wa nchi hiyo, Nairobi, Kenya lililosababisha vifo ya watu 213.
Uvumi zaidi umeendelea kuenea baada ya shambulio la kigaidi lililotokea wiki iliyopita katika Chuo Kikuu cha Garissa, Kenya na kuua wanafunzi 148.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alisema pamoja na kusikia taarifa hizo, mpaka sasa Serikali haijaweza kuthibitisha ripoti hizo zinazoenea, lakini inachukua tahadhari juu ya suala hilo.
Polisi, Serikali wajiandaa Akizungumzia tahadhari mbalimbali za mashambulizi ya kigaidi au Watanzania kushiriki katika ugaidi, Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman alisema hali hiyo ina taswira kuwa Taifa si salama kwa asilimia 100.
“Kuna usemi usemao mwenzako akinyolewa wewe tia maji, Tanzania si kisiwa, kuna changamoto kubwa kwa sababu tumepakana na wenzetu Kenya ambao wameathiriwa na ugaidi, ndiyo maana hatuwezi kusema tupo salama kwa asilimia 100,” alisema.
Alisema kutokana na hali ilivyo sasa, Watanzania hawana budi kutilia mkazo umoja kama njia ya kutokomeza uhalifu na kuacha kushabikia masuala ya ugaidi.
Kuhusu vijana kujiunga na makundi ya ugaidi, Diwani alisema wazazi hawana budi kuwafuatilia watoto huko shuleni ili wajue kinachoendelea.
“Tanzania ni lazima irudi kule ambako ilikuwa. Kila mmoja ni mlinzi wa mwingine, sasa hivi watoto wanaachwa hadi wanapumbazika na kujiunga na makundi ya ugaidi. Hii si kazi ya vyombo vya dola peke yake ni ya kila mmoja,” alisema.
Diwani aliwataka Watanzania kutoa taarifa za watu wenye nyendo zisizoeleweka ili ikiwezekana wanausalama wachukue hatua badala ya kukaa kimya na kuliacha hilo suala kwa wanausalama pekee.
Kitisho Machi 30 mwaka huu, tovuti ya al-Jazeera ilitoa taarifa za kukamatwa kwa mkanda wa video ulioonyesha mwakilishi wa kundi la kigaidi la Dola ya Kiislamu ya Iraq na Levant (ISIL) akimtaka kiongozi wa kundi la al-Shabaab kuliimarisha kwa kufanya mashambulizi ya kigaidi katika miji ya Mwanza na Dar es Salaam.
Siku chache baadaye, Mtanzania, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika, Sudan, Ummul Khayr Sadir Abdullah, alikamatwa huko Kenya akihisiwa kuwa alikuwa katika harakati za kuingia Somalia kujiunga na kundi la al-Shabaab.
Kadhalika, Mtanzania mwingine, Rashid Charles Mberesero amehusishwa na mauaji ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Garissa, Kenya.
Katika hotuba yake ya Februari, Rais Jakaya Kikwete alisema matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi yana chembechembe za ugaidi na ujambazi.
Akizungumzia hofu ya ugaidi nchini, Waziri Chikawe alisema Jeshi la Polisi lipo tayari kupambana na ugaidi ingawa ni kazi ngumu.
“Tunajua kuwa hii ni kazi ngumu kwa sababu tunapambana na adui tusiyemjua lakini tupo tayari na tumeshajua hali ilivyo,” alisema.
Alisema polisi imeimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote nchini licha ya kuwa magaidi hawatabiriki na wanalenga maeneo ambayo hayana kawaida ya kulindwa kama hospitali, vituo vya mabasi na kwenye vyuo vikuu.
“Hatudharau taarifa zozote zile hata zile zinazosambaa katika mitandao ya kijamii, tunafanyia kazi kila kitu na tunawaomba wananchi watupe ushirikiano,” alisema.
Kwa upande wake, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam limesema linaelekeza macho katika vitisho vya uvamizi wa kigaidi vinavyoendelea kutotolewa.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Suleiman Kova alisema: “Hatulali. Tunafanya kazi usiku na mchana. Tunafika kila pahala kwa namna tofauti katika kuhakikisha kuwa hakuna njama au uhalifu unatokea Dar.
“Vikosi vya upelelezi, intelijensia, wanamaji, anga pamoja doria za mbwa, farasi na pikipiki vyote vipo kazini,” alisema.
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na ulinzi thabiti katika kivuko cha Kigamboni kwani abiria hulazimika kupimwa kwa mashine maalumu (metal detectors) ili kuona kama wamebeba silaha za aina yoyote.
Wananchi kadhaa wanaoishi maeneo ya Kigamboni wameipongeza Polisi kwa hatua hiyo lakini wakashauri kuwa isiwe nguvu ya soda katika kipindi hiki
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena