Header Ads Widget

Responsive Advertisement

MICHEZO | YANGA WATUPWA NJE MICHUANO YA CLUB BINGWA AFRICA

MABINGWA wa Tanzania, Dar Young Africans wamefungwa goli 1-0 na Etoile du Sahel katika mechi ya marudiano ya hatua ya 16 bora iliyomalizika usiku huu mjini Sousse, Tunisia.
Kwa matokeo hayo Etoile wanasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa magoli 2-1 kutokana na sare ya 1-1 waliyopata kwenye mechi ya kwanza iliyopigwa majuma mawili yaliyopita uwnaja wa Taifa, Dar es salaam.
Mechi ilianza vizuri kwa timu zote kutengeneza nafasi, lakini Etoile walionekana kuwa hai zaidi na kupeleka presha langoni kwa Yanga.
Etoile du Sahel walitengeneza nafasi nzuri dakika ya 7’, lakini Soussi alishindwa kumalizia kwa kichwa mpira wa faulo wa Tej.
Dakika mbili Baadaye, Yondani alifanya kazi nzuri ya kuokoa mpira uliompita Dida baada ya kupigwa na Soussi.
Dakika ya 18’ Naguez alipiga krosi ambayo Mouhbi alipiga shuti ambalo lilikwenda nje ya lango.
Baada ya safari hiyo ya mashambulizi ya Etoile, El Jemmal alifunga goli la kuongoza kwa kichwa akimalizia krosi ya Bangoura.
Dakika mbili baadaye Yanga walifanya shambulizi zuri ambapo Amissi Tambwe aligonga kichwa kumalizia krosi ya Juma Abdul, lakini mpira huo ukagonga mwamba.
Yanga wakaendelea kufanya kazi nzuri na katika dakika ya 33, Sherman alipoteza nafasi nzuri akipiga shuti lililopaa langoni akimalizia pasi ya Mrisho Ngassa.
Etoile walipata pigo dakika ya 42 kufuatia Kom kuoneshwa kadi nyekundu kutokana na kumfanyia faulo Msuva na hii ilikuwa baada ya kadi ya pili ya njano, ya kwanza aliipata kwa kumchezea vibaya Mrisho Ngassa.
Hadi mapumziko, Etoile walikuwa wanaongoza kwa goli 1-0 na kwa ujumla mpira ulikuwa sawa, Yanga walicheza vizuri, lakini makosa ya kujisahau yaliwagharimu.
Safu ya kiungo Yanga walicheza vizuri, lakini safu ya ushambuliaji bado hawakuelewana sana na wangejitambua na kucheza kwa malengo wangeshinda goli.
Mapema kipindi cha pili dakika ya 48, Etoile walimtoa Soussi na nafasi yake ikachukuliwa na Brigui Alaya.
Dakika ya 62’ Mrisho Ngassa aliingiza krosi nzuri kutoka winga ya kulia, lakini Sherman alishindwa kuitumia vizuri.
Dakika ya 65’ Yanga walifanya mabadiliko kwa kumtoa Sherman na nafasi yake kuchukuliwa na Hussein Javu.
Dakika ya 72’ Kelvin Yondani alioneshwa kadi ya njano baada ya kumchezea vibaya mshambuliaji wa Etoile.
Dakika ya 82’ Yanga walifanya mabadiliko kwa kumtoa Salum Telela, nafasi yake ikachukuliwa na Andrey Coutinho.
Kwa ujumla Yanga walicheza vizuri kipindi cha pili, wakipigiana pasi, wakitengeneza mashambulizi, lakini washambuliaji walioongozwa na Tambwe Hussein Javu aliyeingia kuchukua nafasi ya Sherman hawakuwa makini.
Ngassa alijitahidi kupiga krosi kutoka winga ya kulia, lakini hazikuweza kuzaa matunda.
Takwimu zilionesha kuwa Yanga wamemiliki mpira kwa asilimia 51 kwa 49 za Etoile katika kipindi cha pili, kilichokosekana na mipango tu.
Msimu ujao Yanga watacheza ligi ya mabingwa barani Afrika kwasababu ndio mabingwa wa Tanzania msimu huu.
Kikosi cha Etoile: Ben Aymen, Nguez Hamdi, Abdelrazek Ghazi, Boughattas Zied, El Jemmal Ammar, Frank Kom, Ben Amine, Bonguora Khaly, Tej Marouen, Mouihbi Youssef, Soussi Zied.
Kikosi cha Yanga: Deogratius Munish ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Kelvin Yondan, Juma Said, Salum Telela, Mrisho Ngassa, Amissi Tambwe, Kpah Sherman, Simon Msuva.

Post a Comment

0 Comments