MAHAKAMA Wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu, leo imemhukumu kulipa faini ya Sh. 2,000 tu au kwenda jela miezi sita, kada mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, Ahamed Ismail, kwa kosa la matumizi mabaya ya silaha yake.
Ismail alikumbana na hukumu hiyo leo Mei, 6, 2015 baada ya kusomewa mashtaka mawili. Shitaka la kwanza lilidai kuwa Aprili 22, mwaka huu, saa 10 jioni, alikwenda kwenye mkutano wa hadhara wa CCM katika Mtaa wa Isanga, huku akiwa na silaha aina ya bastola iliyokuwa ikionekana wazi.
Kosa la pili, ilidaiwa kwamba siku na tarehe hiyo hiyo, kiasi cha saa moja jioni, Ismail akiwa kwenye msafara wa Mbunge wa Jimbo la Bariadi Magharibi, Andrew John Chenge, alitoa silaha ya moto hadharani kisha kufyatua risasi tatu karibu na Ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Bariadi.
Pamoja na maelezo mengine kadhaa, baada ya kusomewa tuhuma hizo, mshitakiwa alikiri makosa yote hayo mawili, na alipotakiwa na Mahakama kujitetea kabla hajatiwa hatiani kwa makosa hayo, akasema: “Hili ni kosa langu la kwanza na sikujua kama ni kosa.”
Baada ya utetezi huo, Mahakama ilimtia hatiani Ismail kwa kumhukumu kwenda jela miezi sita au kulipa faini ya Sh.1,000 kwa kila kosa ambapo jumla yake ni Sh. 2,000. Mshtakiwa alilipa faini hiyo mahakamani. - See more at: http://mwanaharakatimzalendo.blogspot.com/2015/05/aliyefyatua-risasi-akiwa-na-chenge.html#sthash.DBGYQPJ3.dpuf
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena