Header Ads Widget

Responsive Advertisement

NEWS | BAJETI YA WIZARA YA AFYA YADAIWA KUPUNGUA KILA MWAKA




 

Dar es Salaam. Taasisi ya Sikika imebainisha kuwa fedha kwa ajili ya kununulia dawa zinazotengwa  katika bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii hupunguzwa kila mwaka katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Akizungumzia mapitio ya bajeti ya mwaka 2015/16 itakayowasilishwa bungeni leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Sikika, Irenei Kiria alisema Sh37 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa muhimu na vifaa tiba katika hospitali zote za umma.

Kiria alisema kiasi hicho ni kidogo kikilinganishwa na Sh70.5 bilioni zilizotengwa mwaka 2014/15. Alisema miaka mitano iliyopita fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa muhimu zimepunguzwa na wakati mwingine fedha hizo hutolewa kwa kuchelewa.

“Tunaitaka Serikali kuongeza bajeti ya dawa muhimu na vifaa tiba, pia fedha hizo zitolewe kwa wakati ili kuokoa maisha ya Watanzania wanaokufa kwa kukosa dawa na huduma muhimu za afya,” alisema Kiria.

Mkurugenzi huyo alifafanua kwamba mwaka 2011/12, bajeti ya dawa ilikuwa Sh123.4 bilioni, mwaka uliofuata bajeti ilishuka mpaka kufikia Sh80.5 bilioni na Sh64 bilioni mwaka uliofuata. Kiria alisema mwaka jana Sh70.5 bilioni zilitengwa lakini ni Sh23.5 bilioni tu zilizotolewa.

Aliongeza kuwa licha ya bajeti ya wizara ya afya kupunguzwa, mwaka hadi mwaka, mahitaji ya dawa yamekuwa yakiongezeka pia kutokana na ongezeko la watu na kupanda kwa gharama za maisha.

Alisema mwaka 2011/12, mahitaji yalikuwa Sh188 bilioni, huku fedha zilizotolewa zilikuwa Sh98 bilioni. Mwaka 2012/13, mahitaji yalikuwa Sh198 bilioni, fedha zilizotolewa zilikuwa Sh80.5 bilioni.

Mwaka 2013/14, mahitaji yaliongezeka mpaka kufikia Sh549 bilioni na fedha zilizotolewa zilikuwa Sh50 bilioni. Mwaka 2014/15 mahitaji yalifikia Sh577 bilioni, huku Sh23.5 pekee zikitolewa.

“kuchelewa kutolewa kwa fedha kunaathiri mfumo mzima wa ununuzi na usambazaji wa dawa. Kuchelewa huku ndiko kunakosababisha kuongezeka kwa tatizo la uhaba wa dawa nchini ambao tayari umesababishwa na bajeti ndogo inayotengwa,” alisema Kiria.

Naye Mkuu wa Idara ya Dawa na Huduma wa Sikika, Alice Monyo alisema sekta binafsi imekuwa na mchango mkubwa katika ununuzi wa dawa lakini wanaitaka Serikali iwajibike katika suala hilo kwa sababu ndiyo jukumu lake la msingi.

“Bohari Kuu ya Dawa bado ina hali mbaya kwa sababu haina mtaji wa kutosha wa kununua dawa. Wanapewa fedha kidogo sana ambazo haziwezi kuwahudumia Watanzania 45 milioni wanaohitaji huduma ya afya,” alisema Monyo.

Alisema Serikali ilishasema kuwa itatumia fedha zitakazopatikana kwenye Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na Mfuko wa Bima ya Taifa ya Afya (NHIF) ili kuziba pengo la uhaba wa dawa.

Post a Comment

0 Comments