Taarifa mpya ya Shirika la Afya Duniani (WHO), inaeleza kwamba kuna aina mpya vimelea vya ugonjwa wa kisonono vinavyoendelea kusambaa kwa kasi duniani, ambavyo vinahimili dawa zilizokuwa zinatumika kutibu ugonjwa bila kudhulika.
Kwa mujibu wa WHO, vimelea hivyo vipya havisikii dawa, hivyo baadhi ya dawa zilizokuwa zikitumika huko nyuma, zimekuwa hazina tena athari kwa vijidudu vipya hivyo.
Tayari nchi nyingi duniani zimeripotiwa kukumbwa na usungu wa kisonono hata pale mgonjwa anapopatiwa tiba sahihi ya Antibiotiki (Viuasumu) za jamii ya Sefalosporini na kadhalika, zikiwemo Hongkong, Australia, Ufaransa, Japan, Norway, Sweden na Uingereza.
Aina hii mpya ya vimelea vya kisonono vinadaiwa kuonyesha usugu dhidi ya dawa zote za Antibiotiki zinazotumiwa kuviangamiza, zikiwemo dawa hizo za jamii ya Sefalosporini, ambazo WHO inazitaja kama dawa za mwisho katika kutibu ugonjwa wa kisonono.
Dk. Manjula Lusti-Narasimhan, kutoka Kitengo cha Afya ya Uzazi na Utafiti cha WHO, amekaririwa na Rorya Finest Blog akisema: “Kwa mara ya kwanza, vimelea sugu vya ugonjwa wa kisonono dhidi ya Antibiotiki (Viuavijasumu) jamii ya Sefalosporini viliripotiwa katika nchi ya Japan, ikifuatiwa na Uingereza, Hongkong na Norway."
Daktari huyo hakukomea hapo, bali anasema katika miaka michache ijayo, aina hii mpya ya vimelea vya ugonjwa wa kisonono, huenda ikawa sugu kwa dawa zote ambazo zinapatikana kwa sasa ulimwenguni. Dk. Manjula anasema: “Ugonjwa sugu wa kisonono si tatizo la Bara la Ulaya au Afrika pekee, bali ni tatizo la dunia nzima. Lazima tahadhari zichukuliwe mapema. Upo uwezekano wa vimelea hivi sugu vya kisonono kusambaa kwa haraka duniani kote bila kugundulika. Hii inatokana na nchi nyingi kutokuwa na ufuatiliaji na utunzaji kumbukumbu mzuri wa wagonjwa wake.”
Baadhi ya Wanasayansi wa magonjwa hayo ya zinaaa wanaamini kwamba matumizi holela ya dawa aina ya Antibiotiki pamoja na uwezo wa vimelea vya ugonjwa huo kubadilika na kuzoea mazingira mapya, ndicho chanzo kikuu cha ugonjwa huo kwa sasa kuwa sugu.
Kwa mujibu wa wanasansi hao, ugonjwa wa kisonono ambacho si sugu kilicho kwenye shingo ya kizazi (Cervix), Urethra na Puru, hutibiwa kwa Antibiotiki (Kiuavijasumu) jamii ya Sefalosporini, ambapo mgonjwa hupewa dozi moja ya dawa hizo pamoja na dawa aina ya Macrolide kama vile Azithromycin, na za jamii ya Penicillin kama vile Doxycyclin kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa Chlamydia.
Mara nyingi kwa wagonjwa walio na umri wa chini ya miaka 18 na wanawake wajawazito, hutibiwa kwa kuchomwa sindano. Mgonjwa lazima afuate masharti na ushauri wa daktari kabla hajatumia dawa hizo, kwa kuwa dawa nyingi huwa na madhara kwa wajawazito kwa mfano Doxycyclin.
“Kawaida ushauri nasaha hutolewa kwa washirika wote wawili wa ngono. Na ni vizuri wote wawili watibiwe hata kama mmoja wao hatakuwa na dalili za ugonjwa huu wa kisonono,” wanasema Watafiti na Wanasayansi kuhusu tiba sahihi ya ugonjwa huo.
Namna ya kujikinga na ugonjwa huo mpya wa kisonono
Utafiti wa wanasayansi waliobobea katika magonjwa ya binadamu, wanasema kwamba mtu anaweza kujikinga na ugonjwa wa kisonono kwa kuwa mwaminifu katika ndoa na kujiepusha vitendo vya zinaa na uasherati. Aidha, mtu anaweza kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo kwa kuchukua tahadhari na kuzungumzia juu ya ugonjwa huo kwa mshirika wake wa ngono pindi mmoja wapo anapojibaini kuwa na hali yenye dalili zote za ugonjwa ili wote kwa pamoja waweze kutibiwa na kupata ushauri wa daktari mapema.
Njia nyingine ya kujikinga ni kuepuka kufanya ngono na mtu aliyeambukizwa gono au kujenga tabia ya kutumia mipira ya kiume (Kondomu) wakati wa kujamiiana. Kwa upande wa wanawake wajawazito ni muhimu kuhudhuria kliniki mapema ili waweze kuchunguzwa na kupatiwa tiba muafaka iwapo watagundulika kuwa na ugonjwa huo wa zinaa au ugonjwa mwingine wowote.
Kwa mujibu wa WHO, wanawake wajawazito wanatakiwa wajifungulie katika Vituo vya Kutolea Huduma za Afya ili kama watoto wanaozaliwa watabainika kuathirika kwa ugonjwa huo wa kisonono waweze kupata matibabu ya mapema mara tu baada ya kuzaliwa hivyo kuwaepusha na uwezekano wa kupata upofu.
Kutokana na kasi ya kusambaa kwa ugonjwa huo mpya wa kisonono, kila nchi duniani, kupitia Serikali zao na madaktari wao, zinapaswa kuongeza umakini katika ufuatiliaji wa aina hii mpya ya ugonjwa wa kisonono kwa sababu ugonjwa huo una madhara makubwa kwa afya ya binadamu kama vile kusababisha ugumba kwa wanawake, utasa kwa wanaume, upofu, moyo, uvimbe, ubongo na homa ya mapafu.
Takwimu zilizopo kutoka WHO, zinaonyesha kwamba kisonono ni ugonjwa hatari kwa usalama wa binadamu, hivyo muda si mrefu ugonjwa huo unaweza kutangazwa kama moja ya majanga makubwa ya dunia, kama hatua madhubuti na haraka hazitachukuliwa kwa kila nchi. Kutokana na hali hiyo, WHO imezitaka nchi zote duniani kuongeza ufuatiliaji wa wagonjwa wake, pamoja na kudhibiti matumizi holela ya dawa za Antibiotiki hadi pale taarifa kamili za ugonjwa huo zitakapojulikana.
Chanz0: Fikra Pevu.com
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena