Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya
Juu (HESLB), imesema ilichelewa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu
nchini kutokana na sababu mbalimbali, zikiwamo kuchelewa kwa fedha
kutoka serikalini, marejesho madogo ya mikopo na uchache wa fedha
zilizokusanywa.
Akizungumza na NIPASHE, Mkurugenzi
Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa,
alisema HESLB ilishindwa
kupeleka fedha kwa wakati kutokana na vyanzo
vilivyotegemewa kutoa fedha kuchelewesha huku akisisitiza kuwa fedha
iliyokwisha kusanywa haikuweza kutosheleza idadi ya wanafunzi wenye
mahitaji.
“Siyo kama inavyoelezwa na vyombo vya
habari, mikopo katika mihula yote ya kwanza ilitolewa kwa wakati, katika
kipindi hiki cha muhula wa mwisho wa masomo mikopo imechelewa kwa
sababu ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya mikopo kuchelewa na urudishaji
wa mikopo usioridhisha, alisema Mwaisobwa.
Aidha, alisema mikopo haikuchelewa
kupelekwa katika vyuo vyote vyenye wanafunzi wenye mahitaji na kuongeza
kuwa hata vyuo vilivyofanya migomo, baadhi ya vitivo vilikuwa vimepatiwa
mikopo.
Alisisitiza kuwa HESLB imeshapeleka fedha
za mikopo kwenye vyuo vyote na kuwa vyuo ambavyo wanafunzi
hawajapokea, vina utaratibu wake wa kuwapatia fedha hizo.
Hivi karibuni, wanafunzi wa Vyuo Vikuu
nchini vikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha
Dodoma (Udom), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph, Chuo Kikuu cha Iringa na
Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu cha Dar es Salaam (DUCE) waligomea
masomo kuishinikiza serikali kupitia HESLB kuwapatia fedha za kujikimu.
Chanzo: NIPASHE
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena