Katika hotuba yake ya kumsindikiza Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, katika Safari yake ya Matumaini kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Kaluta, Kingunge ameyataja mambo makuu mawili ambayo dhahiri yanainyima sifa CCM kuendelea kutawala nchi hii.
Mambo mawili hayo ni kuendelea kukithiri kwa matatizo mengi katika nchi hii kwa miaka yote zaidi 50 ya Uhuru chini ya utawala wa CCM pamoja na chama hicho kumaliza orodha ya makada wake walioandaliwa kuongoza Taifa hili.
Akielezea au kufafanua kuhusu kukithiri kwa matatizo mengi katika nchi hii, Kingunge ameweka wazi kwamba marais wote waliopita chini ya utawala wa CCM wameshindwa kuyamaliza matatizo hayo, likiwemo tatizo la umasikini unaolikabili Taifa hili pamoja na wananchi wake, hivyo mtu pekee anayeona anaweza kumaliza matatizo hayo ni Lowassa.
Kuhusu kumalizika kwa makada walioakuwa wameandaliwa na CCM kwa ajili ya uongozi wa Taifa hili, Kingunge ameweka wazi kwamba chama hicho, katika mkakati wake wa kupata viongozi bora, kiliwapeleka makada wake hao kwenda kupata mafunzo ya kijeshi katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili waweze kuwa makada walioiva kisiasa, kiakili na kiukakamavu.
Kwa mujibu wa Kingunge, kada ya mwisho iliyobakia katika orodha hiyo ya makada wa CCM waliokuwa wameandaliwa kiuongozi kwa kupelekwa kupata mafunzo hayo ya JWTZ, ni ya kina Lowassa, Rais Jakaya Kikwete, Abdulrahman Kinana, Yussuf Makamba na wengine ambao hakuwataja katika mkutano huo uliokuwa umefurika watu wengi waliofika katika uwanja huo wa Sheikh Amri Abeid kushuhudia tukio hilo la Lowassa kutangaza nia ya kuwania urais wa Oktoba, mwaka huu, kupitia chama chake cha CCM.
Kutokana na hali hiyo, Kingunge anasema ameamua kumuunga mkono Lowassa katika orodha yote ya watia nia ya urais ndani ya CCM kwa kuwa ndiye pekee aliyebakia miongoni mwa watia nia wote hao wa chama hicho, ambaye alipata mafunzo ya JWTZ yaliyokuwa na lengo la kuwajenga kiuongozi na kinidhamu.
Mpaka hapo, mimi binafsi, kama nitakuwa nimemwelewa vizuri Ngombale, na ninadhani nimemwelewa vizuri, kwa kauli yake hiyo, ya kwamba Lowassa pekee ndiye amebakia, ni wazi kuwa katika hazina ya viongozi bora wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambayo aliwahi kuisemea kwamba katika mfumo huu wa sasa wa vyama vingi Rais wa Tanzania anaweza akatoka chama chochote cha siasa, lakini Rais Bora wa Tanzania lazima atatoka CCM, imehitimishwa na Rais Kikwete.
Kwa hiyo, kwa kuwa Rais Kikwete anahitimisha hazina ile ya Mwalimu, ya makada wa CCM waliojengewa uwezo wa kuongoza Taifa hili kwa kupatiwa mafunzo ya JWTZ na chama chao, Kingunge sasa anawataka Watanzania wamalizie ‘makapi’ yaliyobakia katika hazina hiyo, kwa kumchagua Edward Lowassa kuwa Rais wa Tanzania.
Kwa maoni yangu, kama Kingunge anakiri hadharani kwamba nchi hii, kwa miaka zaidi ya 50 ya Uhuru wake bado inakabiliwa na matatizo mengi. Kama anakiri hadharani kwamba Lowassa ndiye pekee aliyebaki katika hazina ya viongozi bora waliotajwa na Mwalimu, ama CCM inapaswa kupisha na kuondoka yenyewe kwa hiyari yake sababu haina tena kiongozi bora au Ukawa na wapenda mabadiliko wanapaswa kukiondoa kwa nguvu ya kura chama hiki.
Hakuna namna yoyote ambavyo Kingunge anaweza kuushawishi umma wa Watanzania ukubaliane na kauli yake hiyo ya kwamba Lowassa ndiye mwenye uwezo wa kuyamaliza matatizo ya umasikini, rushwa, ufisadi, uduni wa huduma karibu zote za kijamii na kadhalika, yaliyoshindikana kuondolewa na Mwalimu, Mzee Ali Hasan Mwinyi, Mzee Benjamin Mkapa na sasa Rais Kikwete, akiwa ndani ya CCM hiyo hiyo.
Miaka 54 ya utawala wao, imethibitisha kwamba CCM imeiongezea nchi hii na Watanzania kwa ujumla wao matatizo mengi zaidi, kiasi cha Kingunge kukiri hivyo hadharani. Bila shaka, mpaka sasa, tangu Lowassa atangaze nia yake hiyo ya Safari ya Matumaini akiwa amezungukwa na kundi la watu waliokwisha chafuka kama yeye, CCM itakuwa imepata mrejesho wa Watanzania wanaopinga mafisadi kupanga katika Ikulu yao na kuigeuza pango la walanguzi la mapapa na manyangumi, tena wakiwemo makada wake wazito kina Dk. John Malecela na Dk. Harrison Mwakyembe.
Kwa hali hiyo, dawa ya matatizo yote hayo yanayoikabili nchi hii, si kuungaunga kwa kuwapeleka ‘makapi’ kina Lowassa Ikulu. Kama CC itathubutu kumteua Lowassa kuwa mgombea wake wa urais, hiyo itakuwa ni fursa nzuri ya kuwaweka kando ili kizazi kipya nje ya kile cha Mwalimu kiweze kuwaongoza Watanzania kwa kutumia mfumo wao mwingine mpya kabisa wa kisera na kimikakati, na kazi hiyo lazima ianze sasa, hakuna kuchelewa.
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena