MAKUNDI ya vijana jana
yalionekana kumiminika mithili ya kumbikumbi warukapo wakati wa masika
wakimsindikiza mgombea urais Edward Lowassa anayewakilisha Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Lowassa ambaye alifika
makao makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu za
kugombea, alifanya hivyo chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA), ulioanzishwa wakati wa Bunge Maalum la Katiba.
Makundi ya vijana
yalionekana katika nyuso zilizojaa furaha na bashasha wakithibitisha
imani yao kwa Lowassa ambaye alihamia Chadema baada ya kukatwa jina lake
katika kile alichokieleza mwenyewe “mpango wa kunihujumu.”
Vijana walijitokeza na
masanduku ya mfano wa jeneza, wakiimba nyimbo za kumtaka Dk. John
Magufuli anayegombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ahame chama
hicho na kuingia kambi ya Ukawa.
Vijana wanaonekana
kuguswa na nguvu iliyoimarika katika kundi la UKAWA wakiamini nguvu hiyo
itakidhi kiu yao ya mabadiliko ya uongozi nchini.
Lowassa alihama CCM
mapema mwezi huu na kujiunga Chadema, chama alichosema kimepata
mafanikio makubwa katika kujenga mtandao nchi nzima.
Tangu alipohama CCM,
Lowassa amekuwa akirudia maneno yaliyosemwa na Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Nyerere kwamba“Watanzania wanataka mabadiliko na wakiyakosa ndani
ya CCM watayatafuta nje ya CCM,” akimaanisha kuwa ameingia Chadema na
kubeba dhamana ya UKAWA ili kusaidiana na viongozi wao kutafuta
mabadiliko waliyoshindwa kuyaleta CCM.
Hali imekuwa tofauti na
ilivyotarajiwa kuwa kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha
Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, kuwa kungesababisha mpasuko CUF
na UKAWA, badala yake maelfu ya wanachama wanaendelea kumuunga mkono
Lowassa kuwa Rais.
“Nimepata faraja sana
kujiunga na Ukawa japo kumekuwa na misukosuko. Ni lazima tuwe wamoja,
mtunze kadi zenu za kupigia kura. Mwaka huu lazima tushinde, tena kwa
kura asilimia 90 ili wakiiba asilimia 10 tusisikitike,” alisema Lowassa
alipozuru Ofisi Kuu za CUF juzi ambako pia alihutubia Baraza Kuu la
Uongozi la Taifa lililofanya kikao cha dharura kutafuta kuziba nafasi ya
mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa chama hicho.
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena