Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imevitaka vituo vya redio na televisheni nchini kuepuka kurusha habari za uchochezi hasa katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu.
Rai hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Ally Simba,
alipokuwa akikabidhi leseni, cheti na kanuni na taratibu za utangazaji
kwa AFM Radio.
Dk. Simba alisema vyombo vya habari vinatakiwa kuepuka kurusha na kuandika habari zitakazochochea vurugu na uvunjifu wa amani.
Alisema jamii ina imani kubwa na vyombo vya habari na waandishi wa
habari, hivyo hawana budi kutumia weledi katika utoaji wa taarifa katika
kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu.
Alisema radio 106 na televisheni 28, zimesajiliwa nchini na kwamba
katika kuelekea uchaguzi mkuu, tayari vituo vitano vya televisheni
vimekuwa na makosa yaliyosababisha kupewa adhabu na onyo.
“Kwa wale ambao hukutwa na makosa, tunawaita TCRA na kuwaeleza
makosa yao, kisha tunawapa adhabu, lakini kosa linapojirudia tunawatoza
faini na mwisho kituo kinafungiwa... hivyo tunavisisitiza vituo kutoa
taarifa kwa usawa,” alisema.
Akikabidhi leseni kwa Radio AFM, Simba alisema kituo hicho ni cha
tisa kwa Mkoa wa Dodoma kukabidhiwa leseni ya utangazaji baada ya
kukidhi vigezo.
Alisema wamekuwa wakihimiza uwekezaji kwenye tasnia hiyo nchini ili
kuongeza ushindani ambao huleta ubora na ubunifu kwenye urushaji wa
matangazo.
Pia alikitaka kituo hicho kuzingatia masharti waliyopewa kwenye utekelezaji wa majukumu yao ya utangazaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa AFM Radio, Egbert Mhada, alisema
wapo tayari kuihudumia jamii ya wana-Dodoma kwa kufuata kanuni na
taratibu za utangazaji.
“Tumejipanga vizuri na tumefanya tafiti mbalimbali za kile jamii wanachohitaji,” alisema Mhada.
CHANZO:
NIPASHE
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena