Header Ads Widget

Responsive Advertisement

JE WAJUA? MWALIMU NYERERE ALIPOMGOMEA MUHAMMAD ALI



•Hii ilikuwa ni Jumamosi tarehe 02-Feb-1980 katika uwanja wa ndege wa Dar-es-Salaam (ambao hivi sasa ni Terminal 1) siku bondia Muhammad Ali alipowasili Tanzania.
•Katika kilele cha vita baridi (cold war), Muhammad Ali alitumwa na rais wa Marekani Jimmy Carter kuja kuishawishi Tanzania isusie mashindano ya Olympic Games ambayo mwaka huo wa 1980 yalikuwa yanafanyika Urusi (USSR) Moscow kutokana na kitendo cha serikali ya ki-soviet kuivamia kijeshi nchi ya Afghanistan mwaka 1979.
•Muhammad Ali, ambaye kabla ya kujiunga na dini ya Black Muslim mwaka 1964 alikuwa anaitwa Cassius Clay, alitumwa kuzishawishi nchi 5 za kiafrika ambazo ni Tanzania, Kenya, Nigeria, Liberia na Senegal.
•Utamu wa ziara ya Muhammad Ali uliishia uwanja wa ndege ambapo alipokelewa na watu nyomi wakiongozwa na aliyekuwa waziri wa utamaduni Chediel Mgonja. Labda pia na Kilimanjaro Hotel (hivi sasa Hyatt Regen 
alipokaa kwenye ziara hiyo ya siku 3.
•Pamoja na umaarufu wake wa kimichezo na ushawishi mkubwa wa ubalozi wa Marekani, juhudi zake za kukutana na Mwalimu Nyerere zilishindikana kabisa. Inasemekana Mwalimu Nyerere alikasirika na hakutaka kukutana na Muhammad Ali kwa vile aliona Muhammad hakuwa na ngazi ya kidiplomasia ya kuweza kukutana naye.
•Baada ya hapo, “The Greatest” alienda nchi nyingine 4 ambapo Nigeria pia hakupokewa na rais Alhaj Shehu Shagari. Alipokelewa na marais kwenye nchi 3 za Kenya (Daniel arap Moi), Senegal (Leopold Sedar Senghor) na Liberia (William R. Tolbert, Jr). Nchini Senegal alielezwa kwamba nchi ina sera ya kutochanganya mambo ya michezo na siasa. Alifanikiwa kwenye nchi 2 tu za Kenya na Liberia. Ila baadaye Liberia ilibadili msimamo (kabla ya mashindano) baada ya kupinduliwa na kuuwawa kwa rais William R. Tolbert, Jr (Apr-1980). Uongozi wa kijeshi ulioingia madarakani (chini ya Samuel Doe) ukaipeleka timu Moscow lakini baadaye wakaiondoa baada ya sherehe za ufunguzi. Ziara ya Muhammad Ali haikuwa na mafanikio sana kwa vile kama angefanikiwa kuishawishi Tanzania, nchi nyingine nyingi za Afrika zingeweza kubadili msimamo.
•Timu ya Tanzania ilienda Moscow, Urusi kushiriki mashindano na kurudi na medali 2 kutoka kwa wanariadha Filbert Bayi na Suleiman Nyambui (Silver Medals). Hii ndio michuano pekee ya Olympic ambayo Tanzania iliwahi kupata medali. Bila shaka kama nchi nyingine zisingegoma, isingekuwa rahisi Tanzania kupata medali hata moja.
•Lakini kisa kikuu cha mwalimu Nyerere kuwakomalia wamarekani kinatokana na tukio la mwaka 1976 kwenye Olympic Games zilizofanyika Montreal, Canada. Nchi za kiafrika mwaka huo, zikiongozwa na Tanzania, zilisusia mashindano hayo kutokana na kitendo cha timu ya New Zealand kushiriki mashindano hayo. Nchi za Afrika zikiongozwa na Tanzania ziliomba IOC (International Olympic Committee) isiiruhusu New Zealand kushiriki mashindano hayo kutokana na timu yake ya Rugby mwanzoni mwa mwaka 1976 kuzuru Afrika Kusini na kucheza na timu ya Afrika ya Kusini kitendo ambacho kilionekana ni kinyume na maazimio ya kuitenga Afrika ya Kusini kijamii na kiuchumi kutokana na sera za ubaguzi wa rangi (apartheid). Kutokana na ombi hilo kukataliwa ,nchi nyingi za Afrika zilisusia mashindano hayo ya mwaka huo. Nchi nyingine kama Marekani ziliendelea kushiriki bila kuziunga mkono nchi hizo za Afrika bila kujua ambacho kitatokea baadaye miaka mi-4.

Post a Comment

0 Comments