Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Shule za msingi 6 zabainika kuwapa majibu wanafunzi darasa la saba

Baada ya baraza la mtihani Tanzania (NECTA),kutangaza matokeo ya mtihani wa taifa wa darasa la saba uliofanyika Septemba 8 hadi 9, mwaka huu, baadhi ya shule zimebainika kuwa zilifanya udanganyifu kwa kuiba mitihani, kuandaa majibu na kuwapa watahiniwa.
dk-charles-e-msonde
Akizungumza na waandishi wa habari,Katibu mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde amesema kuwa takribani shule 6 zimefanya udanganyifu huo.
“Pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na waendeshaji wa mitihani hiyo, kulijitokeza matukio machache ya udanganyifu yaliyofanywa na baadhi ya wasimamizi wa mitihani, wamiliki wa shule na walimu wakuu,” amesema Msonde.
Katika shule zilizofanya udanganyifu alitaja kuwa ni pamoja na Tumaini iliyopo Sengerema mkoani Mwanza ambapo mmiliki wake Jafari Mahunde anatuhumiwa kuiba mtihani, kuandaa majibu ambayo watahiniwa waliyaandika kwenye sare za shule na kuyatumia ndani ya chumba cha mtihani.
Shule nyingine ni ya Little Flower, iliyopo Serengeti, Mara, ambapo mwalimu mkuu wa shule hiyo Cecilia Nyamoronga anadaiwa kuiba mtihani na kuandaa majibu na kumpa msimamizi mkuu pamoja na wasimamizi ili wawapatie watahiniwa.
Shule nyingine alizozitaja ni Mihamakumi iliyopo Sikonge,Tabora, Qash iliyopo Babati mkoani Manyara, St. Getrude Madaba mkoani Ruvuma, na Kondi Kasandalala iliyopo Sikonge, Tabora.
Aidha Msonde alisema baraza hilo limeshatoa taarifa za waliohusika na kushiriki udanganyifu wa matokeo kwa mamlaka zao za utumishi ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma.
Jumla ya shule 16,350 zilishiriki katika mtihano huo, ambapo watahiniwa 795,739 walisajiliwa kufanya mtihani huo.
BY: EMMY MWAIPOPO

Post a Comment

0 Comments