Elimu ya fedha imekuwa ni bidhaa adimu mno kwa miaka mingi katika jamii yetu ya kitanzania. Sio uongo kuwa mtanzania wa kawaida tu hayuko vizuri katika matumizi yake binafsi ya fedha.
Uzoefu unadhihirisha kuwa asilimia kubwa mno ya watanzania wenye umri zaidi ya miaka 40 hawakuwahi kujifunza wala kuhudhuria mafunzo yoyote yanayohusu fedha (personal finance) wakati wa utoto ama ujana wao. Hali hii imepelekea mfadhaiko mkubwa wa kifedha (financial distress) katika jamii yote; sio kwa vijana tu mpaka wazee. Tunashuhudia baba wa familia akienda kulala na kuamka akiwa na wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya kiuchumi ya familia yake. Hii hali ya wasiwasi ambayo kwa kimombo inaitwa Financial nervous inaleta madhara makubwa kwa kuchochea tabia zingine ambazo zinajengwa na kuwa matatizo ya kijamii (social problems).
Katika kitabu maarufu cha “Rich Dad, Poor Dad” kilichoandikwa miaka ishirini iliyopita (1997) na Robert Kiyosaki, tajiri-mwekezaji lakini pia mwandishi nguli katika masuala ya kifedha (Personal finance) anaamini kuwa kuna haja kubwa ya kubadili mitazamo na mifumo ya familia kuhusu elimu ya fedha juu ya watoto wetu. Ni vyema mno kupeleka watoto shule, na hii ni muhimu sana, lakini ni kwa kiwango kipi elimu ya shuleni inawaanda watoto kwaajili ya maisha halisi?
Kwa kile ambacho Kiyosaki amekielezea katika kitabu chake kama mawazo ya zamani kuhusu fedha (Old rule of money), pale ambapo wazazi huwasisitiza mno watoto wao kuwa wasome kwa bidii, wapate matokeo mazuri na wakimaliza shule watapata kazi nzuri zenye mshahara mnono. Kwa muda mrefu vijana waliolelewa kwenye hali hii wameshindwa kabisa kuhusisha ufaulu wao wa darasani na mafanikio yao baada ya kumaliza shule.
Haijalishi uliamua kusoma kitu gani ukiwa chuoni; aidha uliamua kuwa mhasibu ama mhandisi, ukitaka kuwa tajiri ni lazima uwe na elimu ya fedha. Pamoja na ukweli kwamba bado tuna uhitaji mkubwa wa elimu ya darasani, lakini kama utapata mshahara mkubwa bila kuwa na elimu itakayokusaidia kufanya mshahara wako uwe na maana katika maisha yako na familia yako haitakuwa sawa.
Watoto na vijana wanahitaji majibu mapya juu ya maisha yao kutoka kwa wazazi wao, kuendelea kuamini katika “high grades” ni jinamizi litakaloendelea kutunyima furaha kizazi mpaka cha kumi baada ya hiki. Matokeo mazuri ya darasani ni kama minyororo iliyotufunga lakini imepakwa rangi ya dhahabu inayovutia na tunaendelea kuihusudu kwa mvuto wake lakini inatunyima fursa za kufikia mafanikio yetu ya msingi, jambo baya zaidi ni ukweli kwamba hatujang’amua madhara yake pamoja na kwamba bado yanaendelea kutokea.
Bado nasisitiza; wazazi wapeleke watoto wao shuleni lakini elimu itakayoongoza maisha yao kiuchumi ifundishwe nyumbani kwasababu Formal education is not designed to help a student to solve personal financial difficulties.
Utafiti wa kisayansi unaonyesha kuwa kile ambacho unawapa watoto wako katika umri mdogo ndicho kitakuwa maisha yao ya baadaye. Watu matajiri huwafundisha watoto wao kuhusu fedha wakati wa chakula cha jioni kila siku. Watu wa uchumi wa kati hawana muda wa kukaa na watoto wao kwasababu muda wote wanafanya kazi na badala yake wanawaletea watoto wao zawadi kama ishara ya kuziba pengo la kutokuwepo kwao, wanaamini ni mapema mno kumuelekeza mtoto chochote kuhusu fedha lakini pia ni kumfundisha tabia isiyofaa na isiyostahili kwasababu atapenda sana pesa.
Hii ndio sababu matajiri wataendelea kuwa matajiri na maskini wataishi maisha yao yote wakiwa maskini, kwa sababu ya tofauti ya elimu wanayowapa watoto wao nyumbani. Ninaye rafiki yangu ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Rutgers (Rutgers University) nchini Marekani, aliwahi kunieleza kuhusu tamaduni iliyopo kwa baadhi ya wamarekani juu ya watoto wao eneo analoishi.
Wazazi wametambulisha kwa watoto wao kitu kinaitwa “Monthly allowance”, pesa hizi mtoto anapewa kwa mwezi,kwa mfano; $100 kwa mtoto mwenye umri wa miaka 12 na $50 kwa mtoto mwenye umri wa miaka 9 ( inaweza kuzidi ama kupungua) ambapo akishapewa haruhusiwi kuomba chochote kinachohusu matumizi yake kwa muda wa mwezi mmoja, na anatakiwa kuweka akiba, kuwekeza na kununua mahitaji yake ya kila siku kutokana na hiyo pesa anayopewa kwa mwezi.
Rafiki yangu huyo alienda mbali zaidi na kunipa niongee na kijana wake mwenye umri wa miaka 12, I was surprised and motivated -the boy was nothing but a master in stocks. Alikuwa na uwezo mkubwa wa kuelezea masoko ya hisa ambayo aliniambia yeye pia ni mwekezaji tangu akiwa na umri wa miaka tisa, lakini baba yake alianza kuwekeza kwaajili yake tangu akiwa na umri wa mwaka mmoja. Hii ni aina ya elimu tunahitaji kuwapa watoto wetu kabla hatujawapeleka swimming na fun city.
Wakishakula hizi nondo za muhimu sana kwenye maisha yao ya baadaye you can go relax somewhere while talking the same language. Sio mapema hata kidogo kuanza kumfundisha mtoto elimu ya fedha bali utakuwa umechelewa sana kama utasubiri mpaka awe na umri mkubwa. Kuweka akiba na kuwekeza ni tabia inayotengenezwa kwa muda mrefu sio ya siku moja ama mwezi mmoja na inafaa zaidi kufundishwa katika umri mdogo. Haiwezekani January iendelee kuwa ngumu kwa babu mpaka mjukuu aendelee kuiongelea hivyohivyo. We need to give our kids new answers of life.
Ukiangalia maisha ya mtanzania aliyepata tu elimu ya kawaida (Average-educated), anayefanya kazi kwa bidii, kuna njia moja inayofanana kwa wote. Mtoto anazaliwa na kwenda shule. Wazazi wanajawa na furaha kwa sababu mtoto wao anasonga mbele, anapata maksi zinazomuwezesha kuendelea na anachaguliwa kujiunga chuo kikuu. Mtoto anahitimu chuo kikuu ama anaendelea tena na digrii ya pili halafu baadaye anafanya kama vile amekuwa programmed: anatafuta kazi iliyo salama zaidi (secured job or career) anaajiriwa aidha na serikali ama kampuni binafsi.
Kwa kifupi kijana anaanza kutengeneza pesa kutokana na elimu yake, anapata uwezo wa kukopa kutokana na kazi yake. Anachukua mkopo ananunua gari (anazidi kuongeza matumizi bila kujua), anapanga nyumba nzuri yenye gharama na anakopa pesa ya kununua fenicha. Makato yanaongezeka kwenye mshahara wake; makato ya lazima (statutory deductions) kama kodi, pension funds, vyama vya wafanya kazi, na sasa mkopo wa gari, kodi ya nyumba na mkopo wa elimu ya juu. Ukiangalia hali yake ya kiuchumi utagundua upande wa madeni ni mkubwa kuliko upande wa mali zinazoingiza pesa. Kijana amelelewa na kufundishwa kwa vitendo kutengeneza madeni zaidi kuliko mali.
Nina hisia chanya kabisa kuwa matumizi binafsi ya fedha ni 80% tabia na 20% tu elimu ya kichwani. Nguvu kubwa kwa wazazi iwekezwe kwa kuwajengea watoto tabia ya matumizi sahihi ya fedha katika umri mdogo. Kama nilivyosema hapo awali; haijalishi una taaluma gani, kama ukitaka kuwa tajiri unahitaji kujifunza elimu binafsi ya fedha. Ni muhimu kuanza kuathiri hii tabia kwa watoto, huna muda? Matajiri huwafundisha watoto wao kuhusu fedha wakati wa chakula cha usiku. Hakikisha kila siku unapata muda wa kula na watoto wako usiku.
Imeandikwa na:
JAPHET J. S. LUTAMBI
(Financial Education advocate)
JAPHET J. S. LUTAMBI
(Financial Education advocate)
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena