Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Magari Zaidi Ya 400 Kupigwa Mnada Na Tra


Magari zaidi ya 400 jijini Dar es Salaam ambayo wamiliki wake wameshindwa kuyalipa, yako hatarini kupigwa mnada na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Magari hayo, hayajalipiwa kodi na tozo mbalimbali ikiwemo leseni ya matumizi ya barabara (Road Licence)

Pamoja na magari hayo pia shehena ya mali mbalimbali zinazoshikiliwa kutokana na wamiliki wake kukwepa kodi, nazo huenda zikadaiwa.

Katika mali hizo, zimo nyumba tatu za nfanyabiashara maarufu, Said Lugumi baada ya kushindwa kulipa kodi ya TZS. bilioni 14 katika kipindi cha wili mbili alichopewa na TRA kuelekea ukingoni.

Kwa mujibu wa taarifa za uhakika zilizotufikia, magari ambayo yatapigwa mnada ni yale ambayo yalikamatwa na TRA kupitia wakala wake wa ukusanyaji kodi kampuni ya usalali ya Yono Auction Mart.

Magari hayo ni mabasi, malori na mengine madogo ambayo wamiliki wake ni kampuni za watu binafsi.

Habari hizo zinaeleza kuwa, magari hayo yamehifadhiwa katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, likiwemo eneo la kuhifadhia magari lilomilikiwa na Wakala wa Ufundi Umeme (TAMESA), lililopo Gerezani na Bahari Beach.

Kati ya nyumba tatu za Lugumi mbili ziko Dene Beach na moja mtaa wa Mazengo, Upanga, jijini Dar es Salaam.

Inadaiwa asilimia kubwa ya wamiliki wa magari hayo ni wale waliokuwa waliyamiliki kwa kutumia fedha za dili hivyo wameshindwa kuyagomboa baada ya serikali kuziba mianya ya matumizi ya fedha.

Baadhi ya wamiliki wameshuhudiwa wakihaha katika maeneo yalipohifadhiwa magari hayo, baada ya kusikia yako kwenye hati hati ya kuuzwa kwa bei chee na TRA kupitia Yono.

Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Yono, Scholastica Kevela, alisema kampuni yake inasubiri maelekezo ya TRA ili kukamilisha zoezi la kuuza mali hizo.

“Mali ambazo tunatarajia kuziuza ni magari zaidi ya 300 hadi 400 ambayo hayajagombolewa kwa muda mrefu na wamiliki. Magari hayo, yalikamatwa kutokana na wamiliki wake kukwepa kodi ya tozo ya leseni ya barabara,” alisema Scolastica.

Alisema mwezi uliopita pekee TRA kupitia Yono ilifanikiwa kukamata magari 15,000 kutokana na makosa mbalimbali, baadhi ya wamiliki waliyagomboa.

“Haya yaliyobaki tunasubiri maelekezo ya TRA ili tuweze kuyauza kwa mnada kwa sababu taratibu zinaeleza bayana kwamba mdaiwa akishindwa kulipa baada ya siku 14, mali yake iliyokamatwa itauzwa kwa mnada.” alisema mkurugenzi huyo.

Alisema “Rais Dk. John Magufuli anasisitiza kodi ndiyo mhimili wa kuendesha nchi. Hivyo, wakwepa kodi hawa tunawahesabia kama wahalifu wengine. Wale wenye uwezo wa kuja kuyakomboa, wafanye hivyo haraka, kwa sababu, mahali ambapo mkwepa kodi yupo na sisi tupo,”

Alisema maeneo ya kuhifadhia magari yaliyokamatwa na TRA kupitia Yono yako mengi, huku kampuni hiyo ikiingia gharama ya kulipa ushuru wa hifadhi.

“Hatuwezi kuendelea kuingia hasara na pia serikali inahitaji kodi ilipwe ili fedha za maendeleo zipatikane. Muda tuliowapa wengi umekwisha,” alionya mkurugenzi huyo.

Mbali na magari hayo, alisema kupitia TRA, Yono inashikilia shehena kubwa ya mali za wafanyabiashara ambao wanakwepa kutumia mashine za EFD.

“Mali nyingi ni za thamani kubwa. Hizi zimehifadhiwa. Tutauza kwa maelekezo ya TRA” alisema.

Kuhusu hatima ya mali za Lugumi, mkurugenzi Kevela alisema wanasubiri maelekezo ya TRA kabla ya hatua nyingine.

“Mbali na Lugumi, mfanyabiashara mwingine ni G. Dewji ambaye anadaiwa na serikali TZS bilioni 1.8 na kampuni ya Mutluhan Construction Industries inayodaiwa TZS. bilioni 45,” alifafanua.

Post a Comment

0 Comments