Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Charles Mlingwa, akizungumza na waandishi wa habari Mkoani Mara hii leo kuhusiana na mkoa huo kuwa mwenyeji wa siku ya mazingira.
****************
MKOA wa mara umechaguliwa kuwa mwenyeji wa Siku ya mazingira duniani ambapo kitaifa itaadhimishwa kitaifa mkoa wa Mara katika Wilaya ya Butiama kuanzia Juni 1-6 mwaka huu.
Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Januari Makamba anataraji kufungua maadhimisho hayo na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan anataraji kuwa mgeni rasmi katika kilele chake.
Maadhimisho hayo yatafanyika katika uwanja wa Mwenge Mjini Butiama ambapo kutakuwapo na kongamano na tafrija mbalimbali kuhusiana na maswala ya mazingira.
Mkuu wa mkoa wa Mara, Dk Charles Mlingwa alisema kuwa katika siku hiyo ya mazingira inategemewa kupandwa miche ya asili 1,500 ya miti katika misitu mbalimbali eneo la Butiama kama ilivyo kawaida ya maadhimisho hayo.
Aidha Dk Mlingwa amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi ili kujumuika pamoja kwenye maadhimisho hayo muhimu ambayo yatafanyika mkoani Mara kwa mara ya kwanza.
Mbali na hapo Mlingwa alisema kuwa wananchi watapata faida katika maadhimisho hayo kama kuijengea jamii uwezo juu ya uelewa wa masuala ya mazingira na changamoto za kijamii zinazojitokeza katika utunzaji wa mazingira na kuwezesha wadau kushiriki katika fursa zinazohusiana na upandaji wa miti.
Pia watapata fursa ya kujadili mwendelezo wa utekelezaji wa shughuli zilizoratibiwa katika mkoa na wizara kuhusu namna bora ya uhifadhi wa mazingira na kuenzi kazi zote za Baba wa Taifa Mwal. Julius Nyereree katika hifadhi ya mazingira.
Mlingwa alisema kuwa wataelimishwa kupanda miti ili kukidhi mahitaji ya dunia ya kupambana na ongezeko la hewa ya ukaa.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Hifadhi mazingira muhimili wa Tanzania ya viwanda” ikiwa na maana ya ulinzi na uhifadhi wa mazingira nchini kuleta maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena