Header Ads Widget

Responsive Advertisement

UJASUSI | Fahamu Kwa Nini Mapinduzi Ya Kijeshi Yalifeli Uturuki Mwaka Huu!

Image result for turkey revolution 2017 attempt
Julai 15 mwaka huu, serikali ya Uturuki ilinusurika kupinduliwa katika jaribio la mapinduzi liliyodumu kwa chini ya masaa 12. Tayari watu zaidi ya 60,000 aidha wamekamatwa, wamesimamishwa au wamefukuzwa kazi kwa tuhuma za kuhusiana na jaribio hilo lililofeli.

Jaribio la mapinduzi lilitokeje?

Awali daraja kuu katika mkondo wa Bosphorous liliwekewa vizuizi na kundi la wanajeshi wakitumia vifaru, na wakati huohuo ndege za kivita zilikuwa zikiruka katika anga la mji mkuu wa nchi hiyo, Ankara, huku milio ya bunduki ikisikika sehemu mbalimbali.

Baadaye, Waziri Mkuu Binali Yildrim, alitangaza kwamba kulikuwa na jaribio linaloendelea la kuipindua serikali.

Muda mfupi baadaye, kikundi cha wanajeshi kilitangaza kupitia radio ya taifa kuwa jeshi limechukua madaraka kutoka kwa Rais Recep Tayyip Erdogan ili kulinda demokrasia.

Kisha likafuatia tangazo la hali ya hatari (curfew), sheria za kijeshi (marshall law) na maandalizi ya katiba mpya.

Rais Erdogan ambaye alikuwa likizoni alifanikiwa kuwasihi wananchi waingie mtaani kupinga mapinduzi hayo. Alitoa wito huo kwa kutumia app ya Facetime ya iPhone na kuonyeshwa live kama inavyoonekana pichani chini.




Katika usiku huo, vituo vya televisheni vilivamiwa na wanajeshi, milipuko kadhaa ilisikika sehemu mbalimbali za Ankara na Istanbul, abaadhi ya waandamaji walishambuliwa na wanajeshi na kuuawa au kujeruhiwa, jengo la bunge na ikulu zilishambuliwa, helikopta ya jeshi ilitunguliwa, na mnadhimu wa jeshi kuchukuliwa mateka.


Jaribio la mapinduzi liliishaje?

Ili jaribio hilo la mapinduzi lifanikiwe, wahusika walihitaji sapoti ya sehemu kubwa zaidi ya jeshi badala ya kikundi kidogo tu, na sapoti ya wananchi mtaani. Yote mawili hayakutokea. Kana kwamba hiyo haikutosha, vyama vya upinzani navyo vilijitokeza kulaani jaribio hilo.

Kufikia Jumamosi asubuhi -  chini ya masaa 12 baada ya tangazo la mapinduzi - baadhi ya wanajeshi walioshiriki katika jaribio hilo walianza kujisalimisha.

Soldiers involved in the coup surrender on the bridge over the Bosphorus in Istanbul (16 July)



Kadhalika, polisi walifanikiwa kurejesha sehemu mbalimbali muhimu mikononi mwa dola kutoka kwa waasi. Kufikia Jumamosi mchana, mitaa ilikuwa imesheheni wananchi wakilaani jaribio hilo la mapinduzi na kuunga mkono serikali ya Erdogan.


Kwanini jaribio hili la mapinduzi lilifeli?

Kwanza, jaribio hilo halikuwa na sapoti ya kutosha ndani ya jeshi la nchi hiyo. Kilichoonekana ni kikundi kidogo tu cha wanajeshi kilichojumisha wanajeshi wapya, pasipo uwepo wa viongozi waandamizi wa jeshi la nchi hiyo.

Pili, jaribio hilo halikuwa na spaoti ya wananchi. Mara baada ya Rais Erdogan kuwataka wananchi waingie mtaani kupambana na jaribio hilo, ikageuka kuwa mapambano kati ya wanajeshi na wananchi, kitu ambacho kwa vyovyote kingeathiri 'uhalali' wa mapinduzi hayo.

Tatu, wahusika wa jaribio hilo la mapinduzi kushindwa kudhibiti njia zote za mawasiliano kati ya viongozi wakuu wa serikali na wananchi, kwa mfano vituo vya televisheni na redio. Mwelekeo wa jaribio hilo la mapinduzi ulibadilika kwa kiasi kikubwa baada ya Rais Erdogan kuonekana kwenye kituo kimoja cha televisheni akiwataka wananchi waingie mtaani.

Nne, Uturuki ni taifa lenye asilimia kubwa ya watu wenye kipato cha kati na cha juu. Ni vigumu sana kwa taifa lenye wananchi wa aina hii kuunga mkono mapinduzi. Ni rahisi kwa mapinduzi kuungwa mkono katika nchi masikini ambapo mara nyingi 'chuki' dhidi ya serikali huwa kubwa.

Jaribio hilo la mapinduzi lilionekana kufeli bayana baada ya Rais Erdogan kurejea Instanbul na kuhutubia katika uwanja wa ndege wa Ataturk.

Arriving at Ataturk airport in Istanbul, President Erdogan was greeted by hundreds of supporters


Hali ikoje sasa?

Idadi halisi ya waliokamatwa, kusimamishwa kazi au kutimuliwa kazi na hatua nyingine zilizochukuliwa ni kama ifuatavyo

  • Watumishi 300 wa Wizara ya madini wametimuliwa.
  • Watumishi 184 wa Wizara ya Forodha wametimuliwa.
  • Waandamizi wanane wa Bunge wameondolewa.
  • Waturuki wote wanapaswa kuwa na nyaraka za ziada wanapofanya safari nje ya nchi.
  • Watumishi 86 wa taasisi ya udhibiti na usimamizi wa mabenki wametimuliwa.
  • Watumishi 51 wa Soko la Hisa wametimuliwa.
  • Majaji 140 wa Mahakama Kuu wametumiwa hati za kukamatwa.
  • Watumishi 15,200 wa Wizara ya Elimu wametimuliwa.
  • Vyombo vya habari 24 vimefutiwa hati za usajili.
  • Watu 429 wa taasisi ya umma ya masuala ya dini (Diyanet) wameondolewa.
  • Walimu binafsi 21,000 wamefutiwa leseni zao.
  • Watumishi 393 w Wizara ya Familia na Sera za Jamii wametimuliwa.
  • Watumishi 257 katika ofisi ya Waziri Mkuu wametimuliwa.
  • Wakuu (deans) 1577 wa vyuo vikuu wametakiwa kujiuzulu.
  • Magavana 33 wametimuliwa.
  •  Watumishi 9,000 wa Wizara ya Mambo ya Ndani wametimuliwa.
  • Maafisa Usalama wa Taifa 180 wamesimamishwa kazi
  • Majaji 2,745wametimuliwa.
  • Watumishi wa umma milioni tatu wamezuwia kwenda likizo.
  • Mjadala kuhusu kurejeshwa kwa hukumu ya kifo umeanza, na Rais Erdogan ametanabaisha kuwa pindi bunge likiridhia kurejeshwa kwa hukumu hiyo basi wote waliohusika na jaribio hilo la mapinduzi watahukumiwa kifo.
  • Maafisa 1,500 wa Wizara ya Fedha wametimuliwa.
  • Majenerali na maadmirali 85 ni miongoni mwa maelfu ya wanajeshi waliokwishakamatwa. Pia zaidi ya polisi 8,000 wamekamatwa, wametimuliwa au wamesismamishwa kazi.
Mashushushu wa Uturuki walikuwa wapi wakati mapinduzi hayo ynaandaliwa na hadi yakakaribia kufanikiwa?

Makala hii inahusu hasa swali hilo hapo juu, kwa moja ya kazi kuu za Idara ya Usalama ya taifa lolote lile ni kutambua, kuzuwia na kudhibiti matishio ya usalama wa taifa, ikiwa ni pamoja na mapinduzi. Sasa wakati serikali ya Uturuki ikionekana kuchukua hatua kali dhidi ya watumishi mbalimbali wa umma ikiwa ni pamoja na kuwakamata, kuwasimamisha kazi na kuwatimua, ni idadi ndogo tu ya maafisa usalama wa taifa waliochukuliwa hatua (angalia juu nilipoandika kwa maandishi mekundu).

Lakini swali kubwa zaidi ni kwamba je Idara ya Usalama wa Taifa ya nchi hiyo, MIT, haikufahamu kuhusu mipango ya kufanyika kwa mapinduzi hayo, na kwanini?

Turudi nyuma kidogo. Oktoba mwaka jana, mhadhiri wa chuo kikuu cha Haifa , Israel, Norman Bailey, alieleza kwa uhakika kuwa jeshi la Uturuki linaweza kuchukua madaraka ya nchi hiyo iwapo litaona nchi inaelekea kusikofaa.

Kadhalika, Machi mwaka huu, wachunguzi wa masuala ya usalama wa Russia walionya kuwa jeshi la Uturuki lilikuwa likijiimarisha kisiasa, na hivyo kujenga msingi wa mapinduzi.

Baadaye mwezi huohuo, Michael Rubin wa taasisi ya American Enterprise, aliuliza "je Uturuki itakumbwa na mapinduzi?" na akajibu kwamba "isiwe jambo la kushangaza iwapo jeshi la Uturuki litajaribu kumng'oa (Rais) Erdogan na kuwatupa jela watu wake wa karibu."

Machi 30, jarida linaloheshimika la Foreign Affairs lilichapisha makala ya Gonul Tol, Mkurugenzi mwanzilishi wa Taasisi ya Mashariki ya Kati, kituo cha stadi za Uturuki, alieleza kuwa nchi hiyo ilikuwa ikikabiliwa na mapinduzi.

Kadhalika, mwanzoni mwa mwezi huu, Joseph Fitsanakis wa tovuti ya IntelNews alizungumzia kuhusu hali tete iliyokuwa ikiikabili Uturuki na kutanabaisha kuwa hakuna nchi katika eneo hilo ambayo ilikuwa 'haijatulia' kama Uturuki.

Pia, wachambuzi wa taarifa za kiusalama wa Marekani walikuwa wakihofia kitambo kuhusu hali ya usalama nchini Uturuki. Swali lilibaki kuwa lini kungetoa jaribio la mapinduzi na lingeongozwa na nani.

Sasa, kama wataalamu hao mbalimbali wa masuala ya usalama waliokuwa wakitegemea 'vyanzo vya wazi vya taarifa za kishushushu' (open sources) waliweza kutoa tahadhari kuhusu uwezekano wa jaribio hilo la mapinduzi, inatarajiwa kuwa mashushushu wa Uturuki pia walikuwa na tahadhari hiyo.

Kwa kuangalia 'sintofahamu' iliyoikumba serikali ya Rais Erdogan wakati wa jaribio hilo la mapinduzi, yayumkinika kuhisi kuwa idara ya ushushushu ya nchi hiyo nayo ilikuwa katika 'sintofahamu' pia. 

Na kuthibitisha kuwa taasisi hiyo haikuwa imejipanga vizuri, asuhuhi ya Julai 16 makao makuu yake yalishambuliwa na helikopta za jeshi pasipo upinzani wowote. 

Wakati serikali ikikabiliwa na jaribio la mapinduzi, mkuu wa idara ya ushushushu ya nchi hiyo, Hakan Fidan, alikuwa mafichoni.




Kuna sababu kuu tatu zinazoweza kueleza kwanini idara ya ushushushu ya nchi hiy, MIT, ilionekana kutokuwa na taarifa kuhusu jaribio hilo la mapinduzi na kushindwa kwake kulizuwia.

Kwanza, uwezo wa utendaji kazi wa taasisi hiyo ni duni, na kwa kiasi kikubwa umekuwa ukikuzwa na vyombo habari kuliko hali halisi. Taasisi hiyo inaelezwa kuwa yenyeurasimu mkubwa, yenye kutumia mbinu za kale, in uhaba mkubwa katika mtandao wake wa upatikanaji taarifa za kiusalama, sambamba na mapungufu katika uwezo wake kwenye uchambuzi wa taarifa za kiusalama.


Pili, kuchanganya siasa na taaluma ya ushushushu. Awali, taasisi hiyo ilikuwa ikijitegemea na kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia taaluma na utaalam wa ushushushu. Hata hivyo, tangu Erdogan aingie madarakani mwaka 2003, taasisi hiyo imekuwa kama chobo cha kisiasa cha AKP, chama tawala chenye mrengo wa kulia kidogo kidini kinachoongozwa na Erdogan.

Tatu, kwa takriban muongo mzima sasa, MIT imekuwa 'bize' zaidi na changamoto za matishio ya usalama kwa Uturuki kutoka nje, yaani tishio la kikundi cha kigaidi cha ISIS, harakati za uhuru za Wakurdi na wapiganaji wao wa PKK, kuibuka kwa taifa lisilo rasmi la Rajava huko Syria, na  hali tete ya usalama huko Iraki na Syria kwa ujumla. Changamoto hizo zimepeleka taasisi hiyo kuwekeza nguvu nyingi katika kukabiliana na matishio kutoka nje badala ya matishio ya kiusalama ya ndani ya nchi.


Kwa upande mwingine, kumekuwa na hisia kwamba huenda Erdogan alishirikiana na MIT kuruhusu wapinzani wa chama tawala na serikali ndani ya jeshi la nchi hiyo kufanya jaribio hilo la mapinduzi , lengo likiwa ni kuwa mapinduzi hayo yakishindikana (na lengo ni yashindikane) basi Erdogan awe na kila sababu na haki ya kuendesha taifa hilo kwa mkono wa chuma. Ikumbukwe kuwa kwa muda mrefu Erdogan amekuwa akifanya jitihada za kutaka taasisi ya urais wa nchi hiyo iwe ya kiutendaji kuliko sasa ambapo kinadharia mkuu wa serikali ni Waziri Mkuu.

Post a Comment

0 Comments