Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Fahamu | Zingatia Haya Mambo Ufanikiwe Zaidi

Image result for success
Kwa kuwa maisha ni kama safari na malengo ndiyo dira, ukianza kuyafanyia kazi malengo yako utagundua unatakiwa kufanya nini ili safari yako ya maisha iwe rahisi. Lazima ufahamu mambo muhimu yatakayokusaidia kurahisisha safari yako kuelekea mafanikio.

Baada ya kuyatambua malengo yako, anza kutathmini kuhusu malengo yako na mahali pakuanzia, yakupasa kutambua kuwa safari yako ina milima na mabonde. Kuna ulazima wa kutafakari kwa kina mambo yanayoambatana na safari yako ya kuelekea kwenye kilele cha mafanikio.

Zingatia mambo yafuatayo:


-Taaluma yako: Haijalishi kama umesoma au la! Jiulize na tafakari mara nyingi juu ya uwezo na taaluma yako. Jielimishe juu ya mambo usiyoyafahamu yanayohusiana na kazi yako na hakikisha una taarifa zote muhimu kuhusu fani/kazi yako.

-Matumizi yako- Jiulize kuhusu uwezo wako kiuchumi. Jiulize kipato chako kwa siku na matumizi yako. Jitahidi kuyafanya matumizi yawe madogo kuliko kipato. Anza kuweka akiba kwa ajili ya matumizi ya siku za baadaye.

-Marafiki – Marafiki zako ni kina nani? Kuna usemi maarufu unaosema: Niambie kuhusu marafiki zako nami nitakwambia wewe ni nani. Marafiki na watu wanaotuzunguka wana ushawishi mkubwa wa kutufanya nasi tukawa kama wao. Kama una nia ya kweli ya kufika kwenye kilele cha mafanikio lazima uambatane na watu wenye mafanikio makubwa kukuzidi.

-Tabia/ Mwenendo- Namna tunavyoishi kwa kuendekeza tabia au mazoea fulani ndivyo tunavyojiweka mbali na mafanikio. Kama wewe ni mlevi uliyepitiliza kiwango au unaendekeza anasa, una kazi ya ziada kuyafikia mafanikio.

Baadhi ya tabia na mazoea yakijenga usugu akilini mwa mtu, humpunguzia uwezo wa kutafakari na kuzingatia malengo yake. Badala ya kuhifadhi pesa kwa ajili ya matumizi ya siku zijazo, hutaona tatizo kuzitumia kustarehe na marafiki zako kwa kunywa pombe na kufanya anasa nyingine. Badili tabia na mwenendo kwa dhati, hakika utafanikiwa.

-Afya yako- Vipi kuhusu afya ya mwili na akili? Ili ufanikiwe ni lazima uwe na afya njema. Kinga ya mwili wako lazima iwe imara na akili ifanye kazi kwa kiwango kinachotakiwa. Endapo afya yako haiko sawa (kimwili au kiakili), hakikisha unatafuta ufumbuzi mapema. Zingatia ulaji wa mlo kamili na kunywa maji mengi kila siku ili kuweka mifumo yote ya mwili wako katika hali ya ufanisi.

-Jamii inayokuzunguka: Unaishi vipi na jamii inayokuzunguka? Unajiona mjuaji wa kila kitu au unajishusha thamani? Unawasikiliza wengine au wewe ndiyo kinara wa kila kitu? Unapokea ushauri wa wengine na kuufanyia kazi? Ni busara kujiuliza maswali haya ili uishi vizuri na jamii inayokuzunguka.

Badala ya kujiona unajua kila kitu, jipe nafasi ya kuwasikiliza wengine, utajifunza mengi. Usifurahie kuona mwenzako anapatwa na matatizo, toa msaada kwa wengine kila inapobidi na hiyo itakuongezea nafasi ya kutimiza malengo yako.

-Ufanisi wako- Wengi wetu tuna uwezo wa kufanya mambo makubwa kwa kiwango kinachotakiwa lakini tunakwamishwa na ufanisi mdogo tunaouonesha. Kama malengo yako ni kuanzisha biashara kubwa ya kuuza duka, lazima uoneshe ufanisi mkubwa hata pale unapokuwa na mtaji mdogo. Usifikirie kuwa ukishapata mtaji mkubwa ndiyo utaweza kutunza mahesabu vizuri na kuzuia hasara. Onesha ufanisi tangu hatua ya awali.

-Jifanyie tathmini- Katika kila unalolifanya, hakikisha kuwa unajifanyia tathmini wewe mwenyewe. Usisubiri mtu wa pembeni akwambie kuwa unafanya makosa kwenye jambo hili au lile. Hakikisha kuwa kila siku kabla ya kulala unatathmini shughuli zote ulizozifanya kwa siku husika.

Ukizingatia kwa makini haya niliyoyaeleza, hakika milango yako kuelekea mafanikio ya kweli itafunguka.

Post a Comment

0 Comments