Tulipoishia >>>>> "Mimi kwanza nilikuwa na wasiwasi nikijua tumepambana na vijana wa CND, lakini hii imehakikisha kuwa kuna kundi la kijasusi mjini hapa na leo tumelitonesha kidogo, sasa tusubiri tuone nini kitafanyika", Robert alieleza. Willy alikagua mifuko yote ya Kasongo, kitu cha kutatanisha alichokipata kilikuwa kikaratasi kidogo kigumu kilichoandikwa, "Muone Kabeya Charles", Willy alikiangalia sana kikaratasi hiki kisha akampa Robert ambaye naye alikiangalia sana.
"Kitatue, lakini majina hayo yaweke kichwani, huenda yakawa na maana sana", alishauri Willy.
"Lazima ni ya maana sana, lakini tukiweke kwanza," alijibu Robert.
Waliondoka sehemu hii na kurudi mjini huku wakiwa na mawazo mengi sana juu ya tukio hili la kushangaza. Kwani huenda walikuwa kwa bahati mbaya wameligusa kundi linalohusika na mauaji ya wapigania uhuru, hivi ndivyo waifikiri wakati wakirudi . Endelea Hapa Chini >>>> WASIWASI
I
Ozu ambaye alikuwa amefikia Hoteli Regina, alimaliza kuoga. Aliangalia saa yake akakuta inakaribia saa kumi na moja za jioni akaona ajitayarishe kusudi awahi ahadi yake na Kofi huko Restaurant Namouna ambako waliagana wakutane mnamo saa kumi na moja na nusu, ili wapate kuelezana mambo yalivyokuwa. Alivaa vizuri akapanga vitu vyake vizuri, kisha akafungua mlango, akachukua kijikaratasi akakibana na mlango, akaufunga akaondoka kwenda zake. Funguo za chumba chake hakuzirudisha mapokezi isipokuwa aliondoka nazo moja kwa moja.
Restaurant Namouna iko ghorofa ya nne ndani ya jengo maarufu liitwalo Galleries Presidentielles. Na kutoka Hoteli Regina mpaka jumba hili ni karibu sana, kiasi cha mwendo wa dakika tano kwa miguu. Hivi Ozu aliondoka kwa miguu akaelekea kwenye mkahawa huu. Alipofika alimkuta Kofi tayari ameiwasili huku akiwa anakunywa kahawa na Sangweji.
"Katibu", Kofi alimkaribisha.
"Asante", alijibu Ozu huku anakaa. Kofi alimwagizia Ozu kahawa vile vile.
"Ehe, umekata shauri kwenda hoteli gani?" Ozu alimwuliza Kofi.
"Nimefikia Hoteli Intercontinental".
"Mimi niko Hoteli Regina", walielezana.
"Mimi safari yangu kutoka uwanja wa ndege ilikuwa safi kabisa. Maana nilipotoka hapo nje nilichukua taksi na hatukupata tatizo lolote mpaka tulipofika Intercontinental. Baada ya kuchukua chumba nimejitayarisha na kuja hapa, sijui wewe mwenzangu ilikuwaje", aliuliza Kofi.
Ozu alimeza mate, akamwangalia Kofi kwa macho makali kisha akamwambia. "Mimi rafiki yangu mambo hayakuwa mazuri kama yako. Wakati natelemka tu ndani ya ndege, ndipo hapo mambo yalianza. Kulikuwa na watu wanatusubiri. Inavyoonekana wewe hawakuweza kukutambua, hivi umepita bila taabu. Lakini mimi walinitambua na ndiyo sababu walinifuata. Ajabu ni kwamba kulikuwa na makundi mawili. Na walinifuata katika magari mawili tofauti. Nilipotaka kuhakikisha kama kweli nafuatwa nilimwamru taksi dereva achepukie kwenye barabara ya Poids Lourds, na kweli nilikuwa nafuatwa na makundi yote mawili. Sasa sikiliza kitu cha kushangaza. Nilipoona kuwa siwezi kuwakabiri watu hawa peke yangu nilimweleza dereva aongeze mwendo. Magari haya ya nyuma nayo yaliongeza mwendo. Tulipovuka Fiat tu, pale kwenye msitu, niliona lile gari la nyuma aina ya Benz linakuja kasi. Mimi nikajua sasa nitafungiwa kazi, kwa hiyo nikamwamru dereva azidishe mwendo kwa kadri ya uwezo wake. lakini Kofi, ajabu ni kwamba niliona kitendo cha ajabu. Lile gari la nyuma lilipolipita lile la mbele tu likafunga breki, ikabidi itokee ajali maana lile ambalo lilipitwa ilibidi lijigonge kwenye lile la nyuma na hapo hapo watu waliokuwa ndani ya magari haya waliruka nje na kuanza kushambuliana. Mimi kuona hivi nilizidi kumwamrisha dereva akaze mwendo na kuja moja kwa moja mpaka Hoteli Regina. Yaliyotokea hapo nyuma siyaelewi". Ozu alinyamaza kiasi cha kupitisha mate kisha akaendelea.
"Kitu kinachonishangaza sana ni kwamba watu hawa ni akina nani? Na kwanini wameshambuliana? Wamejuaje kuwa sisi tunafika? Nafikiri tukishajibu maswali haya basi tutakuwa tumeshapata jawabu la tukio hili", alimalizia Ozu.
"Ahaa, afadhali wewe maana umeona vituko. Mimi nafikiri makundi mawili ni makundi tofauti katika misingi ya shughuli zao. Tuliarifiwa kuwa tukifika hapa tumwarifu Robert ambaye atamwarifu Willy kuwa tumefika. Inawezekana Willy na Robert walishaletewa habari kuwa tutafika, hivi walifika kutupokea na wakati wanafanya hivi ndipo waligundua kuwa kuna kundi jingine lililokuwa linatusubiri. Kati ya wale watu uliowaona jukwaani lazima Willy na Robert au mmojawapo walikuwemo, lakini kwa sababu hatuwajui kwa sura ndiyo sababu hukuweza kuwatambua. Mimi nahisi kuwa Willy na Robert ndio walikuwa ndani ya Benz na walifanya mashambulizi ya kukunusuru wewe. Lakini tusichoshe vichwa vyetu maana itabidi tuonane na Robert jioni hii", alishauri Kofi.
"Mawazo yako ni sawa kabisa. Hata mimi nilikuwa nashauri katika misingi hiyo hiyo. Swali moja limebaki bila kujibiwa. Hili kundi jingine limejuaje kuwa sisi tunawasili hapa mjini na hali kuingia kwetu ni siri ya hali ya juu ", aliuliza Ozu.
"Kama Willy na Robert wamenusurika katika mashambulizi haya wataweza kutujibu swali hili," Ozu aliangalia saa yake akaona ni kiasi cha saa kumi na mbili unusu.
"Sijui tumpigie simu Robert au tumfuate nyumbani kwake?", Ozu aliuliza.
"Nafikiri tumpigie simu kama yupo, na kama yupo tumfuate", Ozu alitoa kijikaratasi ambacho kilikuwa kimeandikwa simu na sehemu ambayo Robert alikuwa akikaa kama walivyopewa na ofisi ya 'KK' ya Lusaka. Walikuwa wameelezwa kuwa Robert alikuwa akikaa sehemu iitwayo Macampagne mtaa wa Marais nyumba nambari ya kiwanja 2994. Ozu alikwenda kaunta akaomba kama anaweza kupiga simu. Kijana aliyekuwa kaunta alimruhusu apige kwa Robert, "Hallo," Ozu aliuliza simu ilipoinuliwa kule kwingine.
"Hallo, nani mwenzangu", sauti nzito ilijibu.
"Hapo ni nyumbani kwa Robert Sikawa?" Ozu aliuliza.
"Ndiyo", sauti ilijibu.
"Mwenyewe yupo?".
"Ndiye anazungumza".
"K.K", Ozu alisema.
"Kikosi cha Kisasi," Robert alijibu. Hii ndiyo namna walivyokuwa wanajitambulisha.
"Habari yako Robert? Ozu hapa".
"Nzuri, salama lakini".
"Salama kabisa, sisi tuko hapa Restaurant Namouna, pamoja na Kofi, tuonane wapi?"
"Nafkiri ingekuwa vizuri kama tungeonana hapa maana Willy naye yuko hapa kwa wakati huu. Mimi nakaa..."
"Usiwe na wasiwasi tunapajua mtusubiri tunakuja sasa hivi", Ozu alimkata kauli.
"Oke, tunawasubiri, fanyeni haraka maana Willy ana miadi yake,"
"Sasa hivi," alijibu Ozu na kukata simu. Wakati Ozu na Kofi wanaelekea nyumbani kwa Robert, katika ofisi za gereji G.A.D. kulikuwa na kikao cha dharura cha 'WP', viongozi wote wanne wa 'WP' walikuwepo katika kikao hiki. Pierre alikaa huku anavuta mtemba wake katika hali ya majonzi kabisa. Wenzake walikaa kimya wakisubiri atasema nini. Maana alikuwa amepata habari za kifo cha Mulumba lakini mpaka dakika hii walikuwa hawajapata habari zozote za Kasongo. Jinsi mambo yote yalivyotokea, walikuwa wamehisi na hiki ndicho kitu kilikuwa kinawapa wasiwasi mkubwa sana.
"Jamani hapa ndio tumefikia muda wenyewe. Huu ndiyo utakuwa muda wetu mgumu tangu ianzishwe 'WP', maana kwa mara ya kwanza 'WP' imeingiliwa kiasi cha vijana wao mmoja kuuawa na mwingine kutekwa nyara. Jambo hili naamini wote tulilitegemea na ndiyo sababu tumeunda kundi kubwa lenye nguvu la kuweza kuvunja nguvu zozote za upinzani. Hivi tupo hapa sasa hivi kulishughulikia suala hili kikamilifu. Toeni wasiwasi," alisema Pierre katika hali ya kuwatia wenzake moyo, maana alijua mambo yameharibika.
"Sisi, Patron hatuna wasiwasi, tuko tayari kabisa kupambana na hawa watu kikamilifu," alijibu Jean huku wengine wakitingisha vichwa kuonyesha kuwa wanamuunga mkono.
"Nafikiri sasa tuanze mipango ya kushughulika na jambo hili. Kitu cha kwanza ninachotaka kujua, Mulumba na Kasongo walikuwa watu wenye ujuzi kiasi gani?" aliuliza Pierre.
"Mulumba na Kasongo ni kati ya vijana wetu ambao walikuwa na ujuzi wa juu katika kumfuata mtu na wasiweze kutambuliwa. Ndiyo walikuwa wamefanya kazi hii kwenye matukio yote tuliyofanya sehemu mbali mbali katika Afrika na wakawa wameimudu vizuri sana. Kwa mfano, waliweza kumfuata Nelson Chikwanda yule tuliyemuua Lagos Nigeria kwa muda wa wiki moja bila kugunduliwa na wakaweza kutueleza nyendo zake zote kiasi ya kuwa ilikuwa rahisi kwa Masamba kumpiga risasi na wote wakaondoka bila kugunduliwa. Vile vile kwa upande wa kutumia silaha walikuwa na ujuzi wa hali ya juu sana. Wote wawili waliweza kutumia silaha kila aina, ukiongezea kuwa Mulumba alikuwa na ujuzi wa hali ya juu katika karate. Kwa ujumla Patroni, vijana hawa walijua kazi yao vizuri sana na ndiyo sababu waliwekwa mahali pa maana kama uwanja wa ndege," alieleza Jean.
"Hii ina maana kuwa watu hawa wawili walioingia si wa kuchezea", alizingatia Muteba.
"Ndiyo si wa kuchezea. Kutokana na habari kamili nilizozipata toka 'Boss' kwa kupitia wakala jioni hii kabla sijapata habari za mambo haya yaliyotokea, ni kwamba huyu mmoja aitwaye Petit Osei ni mpelelezi maarufu sana. CIA imekuwa inamwangalia kwa muda mrefu sana na inamtambua vizuri sana, na ndiyo sababu walipomnasa kwenye kanda zao za kipelelezi akija hapa baada ya tukio hili kubwa sana kutokea ilibidi kupasha mashirika mbali mbali wanayoshirikiana nayo, habari za safari ya mtu huyu. huyu wa pili hajulikani kabisa, ila alionekana akitembea na Osei mjini Lagos na CIA ikajuwa lazima walikuwa na safari moja. Na kweli wamesafiri pamoja na wote wana pass za Nigeria ambazo bila shaka ni za bandia. Vile vile wanatumia majina ya bandia, Osei anajiita Petit Ozu na mwenzie Mike Kofi. Kusema kweli CIA na Boss imeshaturahisishia kazi lililopo ni kuwasaka tujuwe wamefikia hoteli gani na kisha tuwafyagilie mbali, ndipo watambue 'WP' maana yake nini," alieleza Pierre kwa sauti ya uchungu.
"Kama ni watu wa ujuzi kiasi cha kwamba CIA inawatambua na wako kwenye orodha yao basi ni wajuzi kweli. Kwa hiyo mambo waliyowafanyia Mulumba na Kasongo ni kipimo chao. Hii ina maana kuwa lazima tokea sasa jambo hili liwe chini ya uangalizi wetu moja kwa moja maana sasa tunashughulika na watu wenye ujuzi kama sisi," alishauri Papa.
"Maelezo yako sawa kabisa, inatulazimu kufanya hivyo. Bila shaka itakuwa rahisi kwetu kuwapata upesi na kuwafutulia mbali maana sisi tunao watu na vifaa vya kutosha. Hii ni faida tunavyowazidi wao," Pierre alisema.
"Hili ndilo jambo ambalo linanikera. Kitu ninachoogopa wasije wakamlazimisha Kasongo akalopoka maneno ambayo yanaweza kuwafanya wakavumbua siri yetu hii ambayo tumeweza kuificha kiasi cha kwamba Serikali ya hapa haijatugundua. Hivi inatubidi usiku huu tutumie kila tulichonacho kutambua Kasongo yuko wapi," Pierre alinena. "Kuropoka Kasongo hawezi kuropoka, maana wamepewa amri ya kawaida ya 'WP' kuwa, mtu akishikwa na ukahisi kuwa unateswa kiasi ambacho huwezi kuvumilia unameza kidonge cha sumu na kujiua. Kama sisi wote tunavyojua, kama Kasongo amelazimishwa kusema lazima ameishajiua, maana afadhali ajiue kuliko kurudi 'WP' huku akiwa ametoa maelezo juu ya 'WP'. Anajuwa vizuri kuliko kufanya hivyo, maana haya maelezo niliwapa tangu nilipowachukua chini yangu. Kwa hiyo mimi nina imani asilimia mia moja kuwa Kasongo ameisha kufa hivyo hakuna haja ya kupoteza muda kumtafuta. Jambo la maana sasa la kufanya ni kuwatafuta hawa watu wawili tuweze kujua wapi walipo ili tukawafutilie mbali kabla hawajaleta madhara," alijigamba Jean.
"Kama una uhakika huo vizuri. Sasa lililopo ni kutaka kujwa hawa watu wamefikia hoteli gani," Pierre alisema.
"Hilo lisikupe taabu, Kabeya anazo njia za kuweza kutupatia hoteli pamoja na vyumba wanavyolala. Hebu nikawaone ofisi ya pili maana nilimwambia yeye na Charles wasitoke ofisini mpaka hapo nitakapowaeleza," alijibu Jean huku akiondoka kwenda kuwaona Kabeya na Charles. Wakati Jean ametoka mazungumzo kati ya hawa wengine yaliendelea.
"Jean atakapokuwa ametupatia hoteli walizomo, Muteba na kundi lako mtamshughulikia Kofi, wakati wewe Papa utamshughulikia Ozu. Nataka kufikia kesho saa kama hizi tuwe na mpango kamili wa kuwaua hawa watu au wawe wameishauawa tayari," alitoa amri Pierre.
"Hamna taabu Patroni, kazi rahisi sana, tukishaweza kuwaweka machoni kazi yao imekwisha," Papa aliwahakikishia.
Jean alirudi akiwa na uso wa furaha furaha, na kuwaeleza, "Vijana wangu wanafanya kazi nzuri sana. Kila mtu ambaye ni mgeni anayeingia hapa mjini na kuchukua chumba ndani ya hoteli yoyote kubwa na zile za hali ya katikati, majina yao yanapelekwa moja kwa moja kwa Kabeya. Kwa hiyo wageni wote walioingia Kinshasa anayo, Hata majina ya Kofi na Ozu ameisha yapokea lakini alikuwa bado hajaweza kujuwa ni kwa ajili gani wameingia hapa mjini. Kwa kifupi Petit Ozu yuko Hoteli Regina chumba nambari 108 na Mike Kofi yuko Hoteli Intercontinental chumba nambari 401,"
"Lo, kazi nzuri Jean, kazi nzuri kabisa, namna hii bila shaka kazi yetu itakwenda sawa. Sasa kazi imebaki kwenu yaani kwako Papa na Muteba, Jean atawasaidia katika kuwapa habari na katika kuwawinda hawa watu wawili. Tusipumzike mpaka tutakapokuwa tumeweza kunasa nyendo zao na kuwa tayari wakati wowote kuwashambulia," alisisitiza Piere.
"Usiwe na wasiwasi Patron, sisi sasa tunakwenda kushughulikia jambo hili kikamilifu. Vijana wote wako katika tahadhali, na usiku huu huu tutakujulisha mambo yalivyo," alieleza Muteba huku wote wakisimama tayari kuondoka kwenda kuanza kazi hii muhimu.
"Sawa, mimi nitakuwa nyumbani nikisubiri kutoka kwenu wakati wote," Pierre alisema huku anaingia ndani ya gari lake na wenzake nao wakiwa tayari kwenda kwenye uwanja wa mapambano. Wakati kikao cha dharura cha 'WP' huko kwenye ofisi za gereji ya G.A.D. kikiendelea. Kikao kingine cha 'KK' kilikuwa nacho kinaendelea nyumbani kwa Robert Sikawa huko Macampagne. Kofi na Ozu baada ya kumpigia Robert simu walitelemka chini na kuchukua teksi iliyowapeleka moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Robert. Waliwakuta wenzao wakiwasubiri kwa hamu na kweli walipoonana walikumbatiana kwa furaha kubwa. Kusema kweli kama ungewaona vijana hawa ungeamini kuwa ni watoto wa mzee mmoja maana walifanana. Kweli ni ajabu sana Ozu na Kofi walimfurahia sana Willy kumuona maana sifa zake nyingi walikuwa wamezisikia. Kwa mawazo yao walifikiri ni mtu wa kutisha sana, lakini kwa mshangao wao walimkuta ni kijana wa rika yao na sura ya kupendeza ajabu kiasi kuwa mtu kwa mtu yeyote angempenda. Kweli alikuwa rijali. Willy na Robert nao waliwafurahia wenziwe na katika muda wa dakika chache vijana hawa walitaniana na kuchekeshana kana kwamba walishafahamiana miaka kumi iliyopita. Baada ya mazungumzo haya ya kukaribishana, waliingia katika mazungumzo ya kikazi, Willy alieleza kwa kirefu sana mambo yote kuhusu nia na utekelezaji wa kazi waliyopewa. Baada ya maelezo haya aliwaeleza maendeleo waliyokuwa wameyafanya katika shughuli, na kuwafikisha mpaka kwenye tukio la akina Ozu, Mulumba na Kasongo. "Kwa kifupi ndivyo hivyo mambo yalivyokuwa mpaka sasa hivi. Swali linabaki pale pale hawa watu ni akina nani, na wanawakilisha kundi gani?".Alimalizia Willy. "Vizuri sana umetuweka katika hali nzuri ya kujua mambo yalivyo. Kweli suala linabaki ni hilo hilo," Ozu alisema. "Hiki kijikaratasi huenda kina maana. Kabeya ni nani na Charles ni nani? Ndilo suala jingine", Willy alijaribu kutafuta mawazo. "Unajua katika Zaire siku hizi majina ya kizungu hayatumiwi, basi hii inaonyesha kuwa aliyeandika kikaratasi hiki ambaye ni Charles si Mzaire", Robert alieleza. Willy alikitoa kile kikaratasi ndani ya mfuko wake wa shati na kuanza kukiangalia tena. "Ahaa angalieni mwandiko huu ni wa Kizungu si wa Kiafrika, unajua miandiko ya Kizungu na Kiafrika inatofautiana! Wote walicheka kutokana na jinsi Willy alivyokuwa akieleza. "Ni kweli, huu ni mwandiko wa Kizungu", walikubaliana wote. "Hii ina maana hawa watu walikuwa na uhusiano na mzungu. Kwa hiyo itabidi tujaribu kumtafuta Kabeya na huyu Charles, naamini tukiwapata watatueleza zaidi", alizungumza Willy kimatani. "Tutawapataja na huku kuna Kabeya chungu mzima Kinshasa na akina Charles chungu nzima vile vile", alisema Robert. "Ndiyo sababu sisi tunaitwa wapelelezi," Willy alimkumbusha, "Sasa itabidi tupeleleze hata ikiwa ni lazima kuwakusanya watu wote wa majina haya itatubidi tufanye hivyo. Maana maelezo yoyote tuliyonayo sasa ya kuweza kutusaidia ni hayo tu na lazima tuyatumie", alimalizia Willy. "Majina haya yanaweza kuwa ya bandia na yakawa hayana maana yoyote", Ozu alisema. "Si kitu, sisi tutajaribu tu, kitu ambacho najua ni kweli kwamba watu hawa wapo hata kama majina haya ni majina ya bandia watu hawa wapo na wana uhusiano mkubwa na watu wale tuliopambana nao mchana. Mimi nina miadi yangu saa moja ambayo sasa imeshafika tayari kwa hiyo itabidi niondoke. Kitu muhimu cha kufanya sasa, inabidi sisi wote sasa tuwe macho hasa wewe Ozu maana wewe tayari wamekwisha kutambua na ni imani yangu kuwa wako mbioni kukusaka. Hivyo wewe ndiwe utakuwa chambo na wewe ndiwe utaweza kutufanya tuwajue watu hawa. Hivi lazima tuwe katika tahadhari kubwa maana kitu chochote kinaweza kutokea wakati wowote. Huu ni wakati wa wasiwasi sana hivi itabidi tuwe na moyo wa utulivu kabisa. Kesho asubuhi nitajaribu kuwaona watu wa STK, ili nipate kujua ni nani aliyekuwa amekodi lile gari walilokuwemo wale majambazi. Mmefikia hoteli gani?" Alimazia Willy kwa kuuliza. "Mimi niko hoteli Regina chumba nambari 108 na Kofi amefikia Hoteli Intercontinental," alijibu Ozu. "Chumba nambari 401," aliongezea Kofi. "Vizuri, kama nilivyokwisha sema kaeni macho. Kama kitatokea kitu chochote habari ziletwe hapa kwa Robert. Mimi nimefikia Hoteli Memling, chumba nambari 240, ikiwa nitahitajika. Ninayo imani kubwa saba baada ya kuwaona, Kuwa Mungu akipenda tutashinda vita hivi. Robert peleka habari Lusaka kueleza kuwa wote tumekwishawasili mjini hapa na shughuli zimeanza. Vile vile gari nililokodi tulifanyia ajali, liweke ndani mpaka kwanza tuone uchunguzi wa tukio hili utafikia wapi, mimi nitaendelea na gari hili ulilokodi wewe. Asanteni mimi naondoka," Willy alimalizia kunena huku akisimama tayari kwa kuondoka. "Vipi una miadi na mtoto nini?", Ozu alitania "Kitu kama hicho", alijibu Willy huku akimwemwesa. "Una bahati basi mara hii tayari. Haya starehe njema," Ozu alimwombea. "Asante." Waliagana Willy akaondoka kuwahi miadi yake na Mwadi ambayo alikuwa tayari amechelewa. Aliingia ndani ya gari alilokuwa amekodi Robert, baada ya kufanya ajali na lile gari jingine, na akaondoka kwenda zake. Robert na wageni wake walibaki na wote kwa pamoja wakakata shauri kutengeneza chakula cha jioni hapo nyumbani kwa Robert wao wenyewe. Kwani Robert hakuwa hata na mfanyakazi hivi ndivyo alivyokuwa akiishi. Mtu aliyekuwa akifika hapa nyumbani kwake mara kwa mara na kumsaidia kusafisha nyumba na mara nyingine kumsaidia kupika alikuwa rafiki yake msichana aitwaye Ebebe, ambaye walipendana sana. Ilikuwa yapata saa mbili kamili Willy alipoingia mtaa wa Kimbondo katika sehemu ya Bandalungwa. Aliendesha pole pole huku akiangalia namba za nyumba kila mara, na kusimama ili kuona vizuri. Mwishowe aliona nyumba nambari 79. Aliposimamisha gari tu mbele ya nyumba hii. Mlango ulifunguliwa na Mwadi akatokeza kuja kumpekea. "Karibu Willy, nilikuwa na wasiwasi mkubwa kuwa huenda umeponda miadi yetu". "Lo, hiyo isingewezekana Mwadi, nilikuwa bado nakuja ila tu nilicheleweshwa na watu fulani waliofika tuweze kuzungumza mambo ya biashara. Unajua tena mambo ya biashara!" Willy alieleza huku wanaingia ndani. "Karibu keti," Mwadi alimkaribisha Willy. Willy aliketi kwenye kochi. Nyumba ya Mwadi ilikuwa ndogo yenye sebule na chumba kimoja cha kulala, ikiwa pamoja na jiko, bafu na choo. Sebule ilikuwa na vyombo vizuri vya gharama ya juu ambavyo vilifanya chumba kuonekana maridadi kabisa, hasa ukiongezea kwamba hiki chumba ni cha msichana na wewe mwenyewe unajua jinsi wasichana wanaojipenda wanavyofanya. "Hapa ndipo ninapoishi". "Mahali pazuri sana Mwadi". "Asante," alijibu Mwadi, "Utakunywa nini bia au Whiski?" "Nipe bia", alijibu Willy. "Skol au Primus?". "Nipe Primus". Mwadi alifungua barafu na kutoa bia mbili za Primus, kisha akazifungua na alichukua bilauri na kumimina. "Karibu", alisema huku akimkabidhi Willy kinywaji. Willy aliinua bilauri yake na Mwadi akainua ya kwake, kisha Willy akasema. "Triniens." "A la sante ya Willy," alijibu Mwadi wakagonganisha bilauri zao wakaanza kunywa. Muziki taratibu ulitokea kwenye santuri, Willy aliamka akaenda kuchagua sahani za santuri ambazo zilikuwa nyingi sana, hii ilionyesha kuwa Mwadi alikuwa mpenzi wa muziki maana nikitaka kusema ukweli alikuwa na maktaba nzima ya muziki. Sahani zilipangwa kwenye kabati kubwa, na kila fungu la sahani lilikuwa na karatasi ambayo iliandikwa majina ya kila wimbo. Willy alitafuta kati ya rekodi alizozipenda, akapata rekodi moja ya Orchestra Shamashama iitwayo 'SHAMASHAMA' akaiweka kwenye santuri na kuicheza. Wakati Willy anashughulika na muziki Mwadi alishughulika jikoni kutayarisha chakula. Willy alipokuwa ameweka sahani na santuri za kutosha kwenye santuri alimfuata Mwadi jikoni huku amebeba bia yake. "Nimekuja unionyeshe jinsi ya kupika maboke", Willy alisema. "Bahati mbaya nimeishapika 'maboke' yameiva, ingekuwa vizuri kama ungewahi kabla sijapika. Hata hivyo kama bado upo tutapika wote siku moja". "Haya, kati ya siku hizi za karibuni tutakuja tupike maboke wote", walikubaliana. Mazungumzo matamu kati yao yaliendelea mpaka wakati wa chakula, Willy alikula 'maboke' chukula ambacho alikuta kitamu sana na kilikuwa kimepikwa vizuri sana. Kusema kweli alikula sana. "Kweli Mwadi mpenzi, kwa muda mrefu sijala chakula kitamu namna hii, chakula hiki sintakisahau maishani. Asante sana," alisema Willy alipomaliza kula. "Bila ya asante Willy", alijibu Mwadi kwa moyo wa furaha. Ilipofika saa tatu na nusu, walikata shauri waende kwenye dansi. "Unaonaje tukienda kwenye muziki," alishauri Mwadi. "Hata mimi nilikuwa na mawazo hayo hayo," Alijibu Willy. "Chagua mahala pa kwenda maana wewe ndiye mwenyeji hapa". "Wewe unapendelea bendi gani?." Aliuliza Mwadi. "Nimekuachia uchague wewe, bendi unayopenda ndiyo hiyo hiyo itakuwa chaguo langu", Willy alijibu. "Mimi napendelea Orchestra Veve ya Verckys." "Vizuri twende huko huko. Leo wanapiga wapi?" "Wapo Parafifi Bar", alijubu Mwadi. "Haya kajitayarishe twende". Mwadi aliingia chumbani na kuanza kujitayarisha. Willy alibaki sebuleni akisikiliza muziki huku akiendelea kunywa bia. Mwadi alipomaliza kuvaa alijitokeza sebuleni. Alikuwa amevalia vitenge toka juu mpaka chini katika staili ya Kizaire. Kusema kweli alionekana wakupendeza sana. Willy alithibitisha ya kwamba alikuwa amepata msichana mzuri wa kutosha. "Ama kweli nina bibi", Willy alisema Mwadi alipojitokeza. "Mimi ndiye nimepata bwana wa sheria yake basi," alijibu Mwadi kimatani. Baada ya kutaniana hivi waliamua kuondoka. Kwa sababu Willy alikuwa amepita hotelini kwake jioni ile na kubadili nguo hakukuwa na sababu kwake kubadili tena, maana alionekana nadhifu wa kutosha. Hivi waliondoka moja kwa moja kuelekea Parafifi Bar. 'Parafifi Bar' ni bar mojawapo maarufu sana mjini Kinshasa ambapo vijana wengi hupenda kwenda na kustareheshwa na muziki wa bendi mbali mbali ambazo huwa zinafika hapa kuwaburudisha. Bar yenye iko kwenye kona ya mtaa wa Assossa na mtaa wa Victoire. Willy na Mwadi walipofika kwenye bar hii ilikuwa kiasi cha saa nne na nusu na tayari magari yalikuwa yamejaa sana kuonyesha kuwa watu wengi walikuwa wamewahi. Walihangaishwa kidogo na mahali pa kuegesha gari maana sehemu yote ya karibu na bar ilikuwa imejaa, kwa bahati mtu alikuwa akitoka, wakapata mahali pa kuegesha. Walifunga gari lao na kuelekea kwenye mlango wa kuingilia ambapo walikata tiketi za kuingilia kwa wote wawili. Willy alilipa Zaire tatu. Watu kama walivyokuwa wamehisi, walikuwa wamejaa tayari. Muziki ulikuwa unaendelea na watu kadhaa walikuwa uwanjani wakilisakata rumba. Walitafuta mahala pa kukaa na kwa sababu Mwadi alikuwa anafahamika sana pale walifanyiwa msaada na kupata mahala pa kukaa. "Tumepata nafasi nzuri, maana ni karibu na watu wanapochezea. Hii itatupa nafasi ya kuona mitindo ya dansi ya hapa mjini Kinshasa," alieleza Mwadi. "Na hasa, maana huu ndio mji wenyewe kwa muziki. Tena inafurahisha sana kuwaona hawa wapiga muziki macho kwa macho maana sisi tumezoea kuwasikia mwenye redio na santuri tu," alijibu Willy kisha waliagiza vinywaji. "Mimi niagizie Whisky ndiyo itaniletea nishai upesi. Maana mimi bila nishai nakuwa mzito katika kucheza dansi," Mwadi alieleza. "Hamna taabu, hata mimi Whisky ndiyo itanifaa kwa wakati huu," Willy alijibu. Hivi waliagiza whisky na walipoiletewa wakanywa huku wakiendelea na mazungumzo ya hapa na pale. Ilipofika saa sita ndipo muziki ulipopamba moto. Watu walikuwa wengi sana sasa, na wengi wao wakiwa wawili wawili walikuwa uwanjani wakilisakata rumba, kila mmoja akijaribu kuonyesha ujuzi wake. Akiwa Willy waliendelea kuzungumza huku Willy macho yake yakiwa uwanjani ambapo alifurahishwa sana na mitindo ya dansi iliyokuwa ikitokitolewa na wachezaji. Vijana wa Orchestra Veve nao ilipofika wakati huu, wakaanza kupiga zile nyimbo tamu tamu. Ulipoanza kupigwa ule wimbo uitwao 'Natamboli motu' Mwadi alisimama na kumwambia Willy, "Tukacheze wimbo safi sana huu. Unajua maana yake?" alimuuliza Willy huku wakiingia uwanjani. "Hapana," alijibu Willy. "Unasema kichwa changu hakifanyi kazi, na mimi Willy kichwa changu, nacho hakifanyi kazi sasa hivi kwa ajili yako," alisema Mwadi huku wanaanza kucheza. Willy alizubaa tu kwa maneno ya huyu msichana ambaye alionekana alikuwa amejawa na mapenzi makali juu yake, hivi hakujibu neno. Mwadi naye kama wasichana wengi Kinshasa alikuwa anajua namna ya kulisakata rumba sawasawa, kiasi kwamba wakati mwingine Willy alikuwa akijisahau na kusimama huku akifurahia jinsi Mwadi alivyokuwa akikatika maungo hasa kiuno. Wasichana wote waliokuwa uwanjani utafikiri walikuwa wakishindana, maana kila mmoja alicheza na kujinyonga kwa mtindo wake. Baada ya wimbo huo vijana wa Veve walipiga wimbo mwingine uitwao 'Zonga Andowe' yaani kwa kiswahili 'Rudi Andowe'. Bila kwenda kupumzika Mwadi na Willy waliendelea na kucheza nyimbo hizi tamu. Hivi ndivyo walivyostarehe usiku huu ambao wote wawili walijuana katika ulimwengu wao wa kipekee. Wakati walipokuwa wamerudi mezani pao wanaburudika na vinywaji hali ya kimapenzi ilikuwa imepamda sana rohoni mwao , "Mwadi sikujua ungeweza kuwa msichana wa kusisimua hivi. Sasa hivi najiona kama niko juu ya dunia", alidiriki kusema Willy. "Mimi je? Mimi ndiye siwezi hata kueleza, maana naona hata haya kukueleza jinsi moyo wangu ulivyokufa juu yako, ee Willy wangu mtoto wa Kizambia", alisema Mwadi kwa sauti ambayo ungefikiri anataka kulia. Wakiendelea na mazungumzo yao ya kimapenzi mara Willy aliona watu wanaangalia sehemu uliko mlango wa kuingilia. Maana 'Parafifi Bar' ina mlango mmoja tu na huku ikiwa imezungukwa na sehemu zote na nyumba na nyumba ya ghorofa. Willy alipogeuza kichwa chake kuona watu wanaangalia nini, moyo wake uliruka mapigo. Maana aliona msichana mzuri ajabu akielekea sehemu waliyokuwa wamekaa na huku macho yote ya wanaume kwa wanawake waliokuwepa hapo, yakimwangalia na kuthibitisha kuwa kweli huyu alikuwa ni mrembo hasa. Msichana huyu alikuwa mrefu wa kutosha, na rangi yake, rangi ya shaba. Alikuwa na nywele nyingi nyeusi sana na nzito na jinsi alivyokuwa amezichana zilitoa sura ya ki- Afro. Uso wake ulikuwa na umbo la moyo. Alikuwa na macho makubwa yaliyozungukwa na nyusi nyeusi nzito na kope nzito. Pua yake ilikuwa ndogo na ya kuchongoka kiasi cha kupendeza. Midomo yake ilikuwa ile ambayo kila mtu alitamani kuibusu, maana ilijaa ujana. Mashavu yake yalijaa kiasi cha kufanya sura ya uso mzima wa msichana huyu kuonekana ya kupendeza sana. Kifua chake kilijaa matiti ambayo yalikuwa yamejaa kabisa kiasi cha kwamba hata ungeyaminya ungesikia ugumu wake. Na bila shaka yalikuwa na joto la kutosha. Tumbo lake lilinyooka jembemba utafikiri hali chakula. Miguu yake ilikuwa mirefu kiasi kinachohitajina na ilikuwa imeshiba kiasi kwamba ukiangalia hutapenda kutoa macho yale kwa jinsi ilivyoumbika vizuri, nyuma alikuwa amejengeka kwa namna ya peke yake, kiasi kwamba siwezi kukuelezea mpaka umuone wewe mwenyewe mrembo huyu. Kwani matako yake pamoja na sehemu za mgongo kuteremka chini, alikuwa ameumbwa kwa mahesabu ya peke yake. Alikuwa na shingo la urefu uliotakiwa kupendeza umbo lake zima. Alikuwa amevaa 'maxy ya kijani kibichi ambayo ilizidisha rangi yake ya shaba kung'aa. Msichana huyu ndiye alikuwa na haki ya kiitwa kisura. Willy aliendelea kumwangalia msichana huyu akisogea. Alikuwa akitembea taratibu kwa hatua zilizokuwa zinatupwa kwa mahesabu. Msichana huyu aliangalia huku na kule lakini kwa chati sana kiasi kwamba mpaka uwe mtu mjuzi kama Willy ndipo ungeweza kutambua. Hii ilimtambulisha Willy kuwa msichana huyu alikuwa akijua kuwa yeye ni mrembo sana hivi kila jambo alilolifanya alilifanya kwa sheria yake. Miondoko yake ilikuwa vile vile ya peke yake, ili kukamilisha urembo wa msichana huyu ambaye nimeshindwa maneno ya kuelezea urembo wake, afadhali siku moja ukipata nafasi fika Kinshasa umtafute mrembo huyu ili ujue uzuri ni nini. Alipozidi kusogea mahali walipo Willy alihisi kuwa huenda alikuwa anamtafuta mtu. Mwadi alimgusa Willy kwenye mkono na kumshitua kutoa mawazo huko yalikokuwa. "Msichana mzuri sana au siyo Willy?" Aliongea Mwadi huku akumwangalia Willy machoni. Willy hakutambua kwa nini Mwadi aliuliza swali hili, lakini ili aweze kueleza ukweli wake alijibu. "Ndiyo ni msichana mzuri sana". "Ni rafiki yangu." Mwadi alijibu kwa mkato. Willy alishangaa kusikia msichana huyu tena ni rafiki wa MWadi. "Kweli maajabu hayataisha ulimwenguni," alijisemea rohoni. Kabla mshangao wake haujaisha msichana huyu akawa amefika kwenye meza yao. Alikuwa akitabasamu, tabasamu lililofanya nywele za Willy kusimama na jasho kumtoka mwili mzima. "Eee Mwadi, mbote," yule msichana alisamu katika Kilingala. "Mbote," alijibu Mwadi huku naye akitabasamu. "Sango nini?" "Malamu," alijibu Mwadi kisha akamkaribisha, "Approchez". "Merci," alijibu yule msichana. Kisha yule msichana akamgeukia Willy macho yao yakaonana. Macho ya huyu msichana yalikuwa malegevu lakini yenye nguvu fulani ambazo zilimwingia hata Willy. "Mbote", Willy alisalimiwa. Willy alitabasamu, na baada ya kusita kidogo alijibu "Mbote," Mara moja yule msichana alihisi kuwa huyu kijana aliyekuwa na Mwadi si mwenyeji wa Kinshasa na wala Zaire. Moyoni mwake msichana huyu alivutiwa sana na kijana huyu aliyekuwa na Mwadi akakata shauri kuvuta kiti, akakaa. "Nafikiri inabidi niwafahamishe," Mwadi alisema. "Litakuwa jambo la maana", alijibu Willy. Mwadi alimwangalia yule msichana akamwambia, "Huyu ni Willy Chitalu ni raia wa Zambia. Yeye ni mfanyabiashara na yuko hapa katika mapumziko ya kikazi kwa muda mfupi." Kisha alimgeukia Willy na kumfahamisha, "Huyu msichana ni rafiki yangu anaitwa Tete. Yeye anafanya kazi na kampuni iitwayo Agence Sozidome." Baada ya kufahamishwa walishikana mikono na kusalimiana. "Habari za siku nyingi," Mikono ya msichana huyu ilikuwa laini sana, kiasi cha kuufanya mwili mzima wa Willy usisimke. "Mimi nilipomuona tu huyu rafiki yako nilijua si kinois," Tete alimweleza Mwadi. "Unajua kinois ni nani?" Mwadi alimuuliza Willy huku akicheka. "Kinois ni mtu yeyote ambaye maskani yake ni hapa hapa mjini Kinshasa bila kujali anatoka wapi", Mwadi alieleza. "Kwa hiyo hata mimi nikihamia hapa nitaitwa kinois." "Bila wasiwasi", alijibu Mwadi. Willy alimwagizia Tete kinywaji, huku wakiendelea na mazungumzo ambayo yalinoga zaidi kwa kuongezeka kwa Tete. "Kampuni unayofanya kazi inashughulika na mambo ya wakala au siyo?" Aliuliza Willy maana neno Agence ina maana wakala. "Ndiyo kampuni yetu ni wakala ya makampuni mengi sana ya nje ambayo yanapenda kufanya biashara na Zaire," alijibu Tete. "Ahaa, kumbe tuko kwenye kazi sawa maana hata mimi kampuni yangu inashughulika na shughuli za Wakala, inaitwa 'Zambia Overseas Agency'. Hata safari yangu hii kama Mwadi alivyokueleza ni ya mapumziko na kikazi. Huenda itakuwa vizuri nikifika ofisini kwenu ambako naweza kuonana na wakubwa wako wa kazi ambao wanaweza kunieleza vizuri juu ya makampuni ambayo naweza kufanya nayo biashara", Tete alifurahi sana kuona kuwa ameweza kukutana na mfanya biashara ambaye angeweza kuletea kampuni yake biashara. Maana ofisini kwao walikuwa wameelezwa kuwa kila walipo wao ni wawakilishi wa makampuni yao. "Itakuwa vizuri. Kampuni yetu ni kampuni kubwa na inajulikana sana. Hata imeweza kuwa Wakala wa makampuni ya Afrika Kusini katika Zaire. Kwa mfano miezi miwili iliyopita tuliweka saini mkataba kwa niaba ya Serikali ya Zaire, mkataba ambao ulikuwa kati ya Serikali na kampuni moja ya Afrika Kusini iitwayo Grindrod Cots Stevedoring ya mjini East London wa kusafirisha tani 125,000 za shaba ziendazo Japan kwa kupitia kwao. Hii itakuonyesha jinsi kampuni yetu ilivyo maarufu. Mimi naamini kuweza kuwa na uelewano mzuri zaidi kati yetu na makampuni ya Zambia kuliko nchi nyingine yoyote", Tete alisisitiza. Kwa kusikia maneno haya moyo wa Willy ulipiga haraka haraka maana maelezo haya yalikubaliana sana na maelezo aliyopewa na Robert juu ya uhusiano wa Zaire na Afrika Kusini kibiashara. Vile vile alikumbuka wasiwasi wa Robert kuwa makampuni yanayoshughulikia maslahi ya wafanyabiashara wa Afrika Kusini, yanaweza kutumiwa kijasusi na nchi hiyo ambayo iko mstari wa mbele katika kupinga maendeleo ya nchi huru za Kiafrika na zile ambazo bado zinapigania uhuru. Bila kuonyesha dukuduku lake Willy alisema, "Ni jambo la bahati sana kuonana mimi na wewe, na inabidi nimshukuru Mwadi kunifahamisha kwako. Hii kampuni yenu ni ya Kizaire au ni ya watu kutoka nje?" Aliuliza Willy. "Hii kampuni inaongozwa na Wabelgiji. Lakini wamekuwa hapa kwa muda mrefu sana, na wameweza kufanya biashara na nchi karibu zote za Afrika. "Vizuri basi, nitafika ofisini kwenu kesho. Ofisini zenu ziko wapi?" Tete alifungua kimfuko chake kidogo akatoa kadi ya biashara akampa Willy, "Hiyo itakupa maelezo yote." Tete alisema. Willy aliangalia kadi hiyo akajibu, "Asante sana." "Mimi nitaondoka Mwadi, maana nilikuwa napita tu. Muteba alikuwa amenipigia simu tuonane 'Vis-a-vis bar ambako O.K Jazz wanapiga leo, lakini nimemsubiri sana hakuja. Nilitoka nikaenda nyumbani kwake hayuko vile vile nilifikiri yuko hapa lakini pia hayupo. Nikimuona atanikoma." Tete alimweleza Mwadi. "Lazima atakuwa amepata matatizo. Ninavyomjua Muteba alivyokufa juu yako, hawezi kuwa hakufika hivi hivi tu," Mwadi alijibu huku akitabasamu. "Wacha maneno yako," alijibu Tete huku akisimama. Willy na Mwadi nao walisimama na kumuaga mrembo huyu. "Haya tutaonana kesho," Willy alisema. "Vizuri, mimi nitakuwepo. Maana ukifika tu mapokezi utanikuta mimi pale," alijibu Tete. Aliondoka taratibu, huku mamia ya watu waliokuwepo hapa wakifurahia miondoko ya mrembo huyu wa aina ya peke yake. Willy alijiona mtu mwenye bahati sana kufahamiana na mrembo huyu kwani hata watu walibaki wakiwaangalia Tete alipokuwa ameondoka. Willy na Mwadi waliendelea kunywa na kucheza kwa muda mfupi, na kwa vile Mwadi alianza kulewa aliomba waondoke. Walipotaka kuondoka vijana wa Veve wakiongozwa na mwanamuziki mashuhuri Verckys walipiga wimbo mmoja uitwao 'Toweli Nini' yaani 'Mnagombea nini.' "Muziki mtamu sana huo, tukacheze ndiyo uwe wa mwisho", alishauri Mwadi. Baada ya wimbo huu waliondoka na kelekea Bandalugwa nyumbani kwa Mwadi, na ilikuwa saa tisa walipofika nyumbani. Wakiwa wana nishai ya kutosha, waliingia ndani na tayari kwa kupumzika. "Willy mimi ninakupenda sana," alisema Mwadi huku akijitoa kabisa kwa Willy. "Na mimi vile vile," alisema Willy akimvuta na kuanza kumbusu, busu motomoto. Hali hii ya kimapenzi iliwajaa, wakaanza kufanya mapenzi ambayo yaliwafanya wote kutosheka kabisa. Wakiwa wanapumzika, Mwadi akiwa anambabata Willy kifuani alisema. "Willy mimi mapenzi yangu kwako yalianza toka siku ile uliyoingia tu pale hotelini. Nilipokuona tu mwili wangu wote ulisiimkwa sana nikajua nimepata mwanaume ambaye mwili wangu umempenda, na niliamini kuwa wewe tu ungeweza kunitosheleza kimapenzi. "Kweli," alijibu Willy huku akisikia usingizi. "Kweli kabisa, hata kuna mtu mmoja huwa ananilipa mimi kwa kumpatia majina ya wageni wanaoingia hapo hotelini, hata jana aliniomba majina ya watu walioingia hapo hotelini kwetu, lakini bila sababu moyo wangu haukupenda nimpe jina lako, sijui kwa nini nilifanya hivi, huenda ni kwa sababu nilikuwa nimekupenda sana kuanzia wakati huo". Kusikia maneno haya Willy aliyekuwa anasinziasinzia, mara moja usingizi wote ulimtoka na akili yake ikawa katika hali ya tahadhari. "Mtu gani huyo", aliuliza Willy kana kwamba hana haja ya kujua. "Mtu mmoja anaitwa Kabeya," Kwa kutaja jina hili Willy alistuka. "Majina hayo huwa anayahitaji kwa nini?" Willy aliuliza. "Sijui mimi huwa anayahitaji kwa ajili gani. Huwa nikisha mpa ananilipa basi yanakwisha. Sasa jana aliniambia nimpe majina ya watu walioingia jana na niendelee kumpa majina hayo mpaka atakaponiambia yeye mwenyewe, akasema atanilipa mara tatu ya kawaida. "Huyu mtu anafanya kazi wapi?" "Aliwahi kuniambia siku moja kuwa anafanya kazi gereji moja iitwayo G.A.D. iliyoko barabara ya T.S.F. sehemu za Gombe." "Na unasema jina langu hukumpa?". "Ndiyo, kwani nilifanya vibaya?". "Hapana, ulifanya vizuri sana", Willy alifikiria habari hizi alizokuwa amezipata, akaonaa mtu mwenye bahati sana, na kufikiria kuwa Mungu ndiye alikuwa amepanga yeye apendane na msichana huyu ili aweze kupata habari hizi alizozipata. Kwani huyu Kabeya ndiye kile kikaratasi alichokikuta mfukoni mwa yule mtu aliyejiua kilikuwa kikimtaja. Hivyo alijua sasa amepata mahali pa kuanzia kesho yake. Alipanga kesho yake aende kwenye gereji hii ya G.A.D. ajue nini kiko pale. Mawazo haya yakiwa yanapita kichwani mwake alimvuta Mwadi na kumkumbatia. ITAENDELEA
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena