"…haina maana kusema kuwa unajiamini alafu unaogopa ufanya vitu hatarishi…"
- The Bold, 2017
Nilieleza katika sehemu ya pili ya mfululizo wa makala hii kwamba, siku zote soko la dunia la fedha huwa linainfluence exchange rate ya sarafu husika. Kwa hiyo serikali ambayo imeamua kuweka fixed exchange rate mara nyingi wanajikuta wanaingia kwenye mtego wa kushiriki kwa kiwango kikubwa kuliko kawaida katika soko ili kuhakikisha kwamba kiwango walichokiweka kinabakia pale pale.
Lakini kuna msemo wanasema kwamba ukweli una tabia ya kutopendwa kupuuzwa. Lakini pia hata ukijenga ukuta imara kiasi gani, hauwezi kuyazuia mafuriko milele, iko siku na saa ambayo hautatarajia ukuta huo utadondoshwa na nguvu ya mafuriko.
Kilichowapata Uingereza kwa kiasi fulani kilikuwa kinafanana kabisa na hiki.
Mpaka kufikia mwishoni mwa robo ya kwanza ya mwaka 1992, hali ya ndani kwa ndani serikali kulikiwa na kiasi kikubwa cha taharuki juu ya uhalisia wa thamani ya Paundi. Japokuwa viongozi wa serikali katika vikao vyao na waandishi wa habari na Bungeni walikuwa wanajitahidi kuonyesha nyuso za furaha lakini uhalisia ni kwamba taharuki ilikuwa ni kubwa mno chini kwa chini hasa hasa kwa Exchequer (Hazina ya Uingereza). Kulikuwa hakuna ubishi kwamba thamani ya Paundi ambayo ilipewa baada ya kujiunga na mpango wa ERM haikuwa sahihi. Paundi ilipewa thamani kubwa sana tofauti na uhalisia.
Licha ya taharuki kubwa ambayo ilikuwa inafukuta ndani kwa ndani, maswali yalipokuwa yakiulizwa na vyombo vya habari… serikali ilikuwa inajiapiza kuwa watahakikisha thamani ya Paundi inabaki juu na hivyo wanaoinunua kwenye soko la kimataifa wasiwe na shaka yoyote.
Uchumi ukaendelea kuonekama unashamiri na soko la fedha likaendelea 'kutrade' Paundi ya Uingereza katika kiwango cha kuridhisha kabisa.
Lakini uhalisia fukuto la chini kwa chini lilikuwa ni kubwa kweli kweli.
Kwanza kabisa Puaundi ilikuwa inatrade katika 'lower end', kwa kiwango cha mwisho kabisa ambacho kilikuwa kimeruhusiwa chini ya mpango wa ERM (2.78 DM). Maana yake ni kwamba presha ya kushuka chini kwa thamani ilikuwa ni kubwa kiasi kwamba ilikuwa inailazimu serikali kuweka kiwango hicho cha mwisho kabisa ili kukidhi masharti ya mpango wa ERM.
Lakini Pili, nchi ya Uingereza ilikuwa na 'current account deficit' kubwa kupita kawaida. Maana yake ni kwamba licha ya dalili za kutengemaa kwa uchumi lakini walikuwa wananunua na kuagiza zaidi bidhaa kutoka nje kuzidi vile ambavyo walikuwa wanauza.
Hizi zote zilikuwa ni dalili za wazi kwamba kuna tatizo kubwa linalofukuta chini kwa chini katika uchumi wa Uingereza na serikali walikuwa wanatumia mabavu ya mpango wa ERM kuendelea kuweka juu thamani ya Paundi.
Huko nje serikali ilikuwa inaendelea kujitutumua kuwa thamani ya Paundi itabaki pale ilipo. Watu wa masoko ya fedha waliendelea kuamini kauli hii ya serikali na biashara zikaendelea kama kawaida. Kujitutumua huku kwa serikali ya Uingereza kuliwawezesha kuvuka robo ya kwanza na robo ya pili ya mwaka na hatimaye kuingia robo ya tatu.
George Soros kutokana na kubobea kwenye uchambuzi na kufuatilia masoko ya hisa na masoko ya fedha kwa miaka kadhaa, naamini alilikuwa mtu wa kwanza kabisa nje ya serikali ya Uingereza kung'amua hili mapema, kwamba kulikuwa na hatari ya anguko kubwa la kiuchumi kutokea.
George Soros miaka ya tisini
Mara tu baada ya George Soros kuhisi 'harufu' ya tukio kubwa la kiuchumi kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kwenda kutokea akaanza 'kukunja misuli' yake vyema ya kiutendaji.
Nilieleza kwamba hedge funds mara nyingi (na kwa uhalisia ni mara zote) wanajihusisha na biashara za fedha zenye hatari kubwa ya hasara au faida. Na mara nyingi hizi 'scheme' ambazo huwa wanazifanya huwa zinalenga uwezekano wa kutokea matukio fulani makubwa ambayo yataathiri nguvu ya sarafu au uchumi wa nchi husika au hisa za kampuni fulani wanayoilenga.
Kwa hiyo hii 'harufu' ambayo George Soros aliinusa ilikuwa ni fursa adhimu kwake na kampuni yake ya Quatumn Fund kutokana na asili ya biashara zao sekta ya hedge funds.
Kwa hiyo mwanzoni kabisa mwa mwezi August 1992, Gorge Soros akaanza kutengeneza 'position' yenye thamani ya dola bilioni 1.5 ( Karibia Trilioni 4 za Kitanzania). Wengi waliopita pale darasani TMT kwa Bw. Ontario (au mahala kwingine) naamini wanaweza kuelewa nikisema 'kutengeneza Position', lakini kwa faida ya wote, Position ni kile kitendo cha trader kuweka 'commitment' ya kuuza au kununua kiasi fulani cha financial instrumet (hisa, sarafu, dhamani za serikali au hati fungani) kwa gharama mahususi. Kwa hiyo taratibu hapo mwanzoni mwa mwezi August 1992, Soros akaanza kutengeneza hiyo position ya dola bilioni 1.5 ambapo position hiyo ilikuwa ni 'short sell'.
Kiti pekee ambacho alikuwa anakisubiri ni kupata 'good entry point' aweze kuingia miguu yote miwili katika position hiyo. Na hiyo entry point ambayo alikuwa anaisubiria ilikuwa ni kiashiria cha kuanza kuanguka rasmi kwa Paundi kwenye soko la dunia.
Serikali ya Uingereza iliendelea kutunisha misuli. Thamani ya Paundi ikaendelea kuwekwa juu kuzidi uhalisia. Wafanyabiashara wengi kwenye soko la fedha la dunia waliendelea kuwa na imani juu ya Paundi lakini George Soros bado aliendelea kuwa na ndoto kwamba lazima Paundi idondoke.
Joto na fukuto la ndani kwa ndani likapanda kweli kweli. Mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi wa nane joto hili likaanza kuvuka nje ya mipaka ya Uingereza. Watu wa ndani wa mabenki kuu mengine, hasa hasa benki ya 'Buba' (Bundesbank - Benki Kuu ya Ujerumani) ambayo ndiyo ilikuwa na ushawishi mkubwa zaidi kwenye soko la fedha ulaya wakaanza minong'ono ya kwamba Paundi ilikuwa imewekwa thamani ya juu mno kuzidi uhalisia. Hii ilikuwa inazorotesha biashara kati ya Uingereza na nchi nyingine, na pia kufanya uchumi wa Uingereza udorore na mtokeo yake kuwagharimu nchi nyingine zote za Ulaya.
Kwa mfano, siku ya August 25 moja ya wajumbe wa bodi ya Bundesbank, Bw. Reimut Jochumsen alitoa hutuba ambayo ilieleza uwezekano wa kufanya marekebisho baadhi ya sarafu. Baadae pia wiki hiyi kuna afisa wa Bundesbank ambaye hakutajwa jina na vyombo vya habari ambaye alitoa maneno ya kuonyesha kutoridhishwa na thamani ya Paundi ilivyowekwa.
Yote haya yalizidi kuweka presha kwenye thamani ya Paundi kwenye soko. Na imani ya Soros kwamba Paundi inaelekea kuporomoka ilizidi kuimarika.
Mwezi wa August hatimaye ukapita kwa salama huku serikali ya Uingereza ikiendelea kutunisha msuli na thamani ya Paundi ilibaki pale pale.
Lakini gharika lilikuja katikati ya mwezi Septemba… presha ilikuwa kubwa zaidi. Uchumi wa Uingereza ulizidi kuzorota, current account deficit ilikuwa kubwa zaidi na watu wa ndani wa mabenki makuu mengine ya Ulaya uvumilivu wao ukaanza kukoma.
Rais wa Benki kuu ya Ujerumani, Bundesbank, Profesa Helmut Schlesinger alifanya mahojiano na Wall Street Journal. Katika mahojiano hayo waliongea masuala mengi yahusuyo hali ya kiuchumi ya Ulaya na masuala mengine mengi ya kibenki.
Katika mahojiano hayo ambayo yalichapwa kwenye ukurasa mzima wa jarida la WallStree Journal kulikuwa na kitu kidogo sana, aya moja tu ambayo kwa haraka haraka ilionekana ni ya kawaida lakini ndiyo hasa George Soros alipoiona ilimpatia 'good entry point' na hatimaye ilipelekea anguko la benki kuu ya Uingereza.
Jarida hili baada ya kutua mezani kwa Soros, alipoisoma mahojiano hayo na Rais wa Benki Kuu ya Ujerumani… katika ukurasa mzima wa hayo mahojiani kuna paraghaph moja tu ambapo alipoisoma moyo ulimlipuka.
Nanukuu kama ambavyo iliandikwa na Wall Street Journal;
"…the president of the Bundesbank, Professor Helmut Schlesinger, does not rule out the possibility that, even after the realignment and the cut in German Interest Rates, one or two currencies could come under pressure before the referendum in France. He conceded in an interview that the problem are of course not solved completely by the measures taken…"
Aya hii moja tu kwenye interview yote iliyopamba ukurasa mzima wa jarida, ndiyo ambayo ilizua kizaa chote. Ni aya hii ambayo Soros aliitumia kuthibitisha imani yake ambayo alikuwa nayo kwa miezi kadhaa kwamba Paundi ya Uingereza ilikiwa inaelekea kudondoka kwa kishindo.
Nimeanza sehemu hii ya nne kwa maneno haya kwa makusudi kabisa, kwamba "…haina maana kusema kuwa unajiamini alafu unaogopa ufanya vitu hatarishi…"
George Soros japokuwa alikuwa anafanya kitu cha hatari sana, lakini imani yake kuhusu tukio la kuanguka kwa Paundi ilikuwa ni kubwa na sasa ilithibitika zaidi. Hivyo alikata shauri, "…haina maana kusema kuwa unajiamini alafu unaogopa ufanya vitu hatarishi…"
Akaongeza mtaji kwa kuazima mabilioni ya dola na kuongeza position yake kutoka dola bilioni 1.5 mpaka dola bilioni 10 (zaidi ya trilioni 22 za kitanzania).
(Baadae Soros aliongeza tena hii position… nitaeleza)
Sasa kabla sijaenda mbali zaidi naomba kama nilivyoahidi kwenye sehemu iliyopita nieleze namna ambavyo "short-sell" inavyokuwa na kwa nini unapata faida thamani ya hiyo sarafu (au hisa) inaposhuka.
Tuanze kwa mfano rahisi…
Tutumie mfano ule ule wa hisa za kampuni ya Airtel.
Tuseme kwamba hedge fund fulani wamefanya uchambuzi na kuhisi kwamba hisa za kampuni ya Airtel zimefika kilele cha juu kabisa ya thamani yake na kuna tukio litatokea na litasababisha anguko kubwa la hisa hizo. Tuseme kwamba kwa sasa kila hisa moja ya Airtel ina thamani ya Tshs. 5,000/- na unahisi kwa hakika kabisa kuwa kuna anguko litatokea na thamani ya hisa hizi kushuka. Kwa hiyo unachokifanya unashort sell.
Inakuwaje?
Unaenda kwa broker, au mtu au kampuni ambayo wanamiliki kiwango fulani kikubwa cha hisa za Airtel na kuazima kiasi fulani cha hisa hizo. Kwa mfano tuseme TMT ya Ontario wanamiliki kiwango kikubwa cha hisa za Airtel, kwa hiyo unaenda na kuazima kwao labda tuseme hisa milioni moja. Naomba nieleweke hapa, haununui hisa hizo, unaziazima kama hisa. TMT watakupa masharti labda uzirudishe hisa hizo ndani ya miezi mitatu labda mathalani, na ukizirudisha utarudisha na riba ya 10% ya thamani ya hisa hizo.
Profesa Helmut Schlesinger (kulia mwenye miwani) aliyekuwa Rais wa 'Buba' (Bundesbank - Benki Kuu ya Ujerumani)
Kwa hiyo baada ya miezi mitatu, utawarudisia TMT hisa milioni moja (ikumbukwe sio fedha shilingi milioni moja bali ni hisa milioni moja) pia utawapa na fedha za riba 10% ya thamani ya hisa walizokupa. Maana yake utawapa fedha shilingi milioni 500 na hisa zao milioni moja.
Katika ile miezi mitatu wewe unanufaikaje?
Nilieleza kwamba unafanya short sell pale pekee ukihisi kuna uwezekano mkubwa wa anguko la hisa au sarafu fulani.
Kwa hiyo baada ya kuchukua hisa hizo milioni moja kutoka TMT (ambazo thamani yake ni shilingi bilioni tano na nasisitiza tena hauzinunui bali unaziazima kama hisa na unazirudisha kama hisa) unaanza kuziuza sokoni. Kwa hiyo kwa kuwa hisa hizo zina thamani ya 5,000/- kila hisa, maana yake ukiuza hisa hizo milioni moja utapata jumla ya shilingi bilioni tano.
Kama uko sahihi na lile tukio ambalo umelihisi na likatokea kweli na hisa za Airtel zikaporomoka kweli, mfano ndani ya miezi hiyo mitatu kutoka ile 5,000/- mpaka kufikia 1,000/- kwa hisa moja. Unachofanya baada ya miezi mitatu hiyo unaenda kwenye soko la hisa na kuzinunua tena hisa milioni moja kwa thamani ya 1,000/- ya thamani ya sasa kwa kila hisa.
Maana yake ni kwamba miezi mitatu iliyopita uliazima hisa milioni moja ukaziuza kwa thamani ya shilingi 5,000/- na kupata shilingi bilioni 5. Kwa hiyo leo hii ukizinunua tena kwenye soko la hisa (baada ya tukio kutokea na thamani kuporomoka) maana yake utazinunua kwa jumla ya bilioni 1 tu. Kwa hiyo unakuwa umetengeneza faida ya bilioni 4. Ukitoa ile 10% riba ya TMT (milioni 500) unabakiwa na faida ya shilingi 3.5 Bilioni za kitanzania.
Hiyo ndivyo short sell inavyofanyika.
Je short sell ya sarafu inakuwaje?
Tuseme kwa mfano unataka kushort sell 'Tshs' na leo hii dola moja ya marekani ina thamani ya shilingi 2,000 ya Tanzania. Kwa hiyo unaenda kwenye bank, au kampuni au mtu binafsi na kuazima kiasi kikubwa cha shilingi. Labda tuseme shilingi bilioni 5. Lengo lako ni kushort sell 'Tsh' kwa kuwa umeona kuna tukio fulani litatokea na kusababisha thamani ya shilingi kuporomoka.
Kwa hiyo tuseme ukaingia mkataba na Mzee Kimei na CRDB yake na wakakupa hizo shilingi bilioni 5. Lakini wakataka urudishe na riba ya 5% (shilingi milioni 250).
Ikumbukwe kwamba wewe unafahamu kwa mujibu wa chambuzi zako kwamba thamani ya shilingi inaelekea kuporomoka. Kwa hiyo 'unachenji' zile shilingi bilioni 5 za kitanzania kuwa dola 2.5 Milioni.
Baada ya mwezi mmoja tukio ulilolihisi likatokea na thamani ya shilingi kuporomoka kutoka shilingi 2,000 kwa dola moja na kuwa 3,500 kwa dola moja. Kwa hiyo hapa unabadili tena hizi dola milioni 2.5 kuwa shilingi na utapata jumla ya shilingi bilioni 8.75.
Utarudisha shilingi bilioni 5 ya Mzee Kimea na CRBD yake pamoja na riba yao ya 5%, na mfukoni utabakiwa na shilingi bilioni 3.5.!
My friends… hiyo ndiyo short sell na hivyo ndivyo ambavyo watu wanatajirika katila global financial markets.
Usiku wa kuamkia tarehe 16 Septemba 1992 wakati ambao ulimwengu mzima umelala George Soros kupitia Quatumn Fund alikuwa anaazima na kuuza Paundi ya Uingereza kuzidi katika kiwango kikubwa na cha kutisha. Alikuwa anaazima kutoka kwa kila benki na mashirika makubwa ambayo yalikuwa tayari kumpatia. Naamini mpaka sasa wote tunaelewa kwa upana maana ya short sell na hivyo tunaelewa kwa nini Soros alikuwa anaazima na kuiuza Paundi.
Katika ulimwengu wa masoko ya fedha duniani, wafanyabiashara wa fedha wana tabia kama mbwa mwitu. 'Hawalali' muda wote wakiwinda fursa za kuuza au kununua sarafu fulani. Kwa hiyo kitendo hiki cha George Soros kuuza kwa kasi Paundi na kwa kiwango kikubwa mawimbi yake yaliwafikia pia Hedge Funfmds nyingine na wafanyabiashara wengine wa soko la fedha. Japokuwa kama nilivyoeleza huko awali kwamba katika kipindi hiki Soros bado hakuwa Bilionea maarufu kama tumjuavyo sasa lakini wafanyabiashara wengi wa soko la fedha walikiwa wanamfahamu yeye na kampuni yake na walifahamu na kuheshimu umahiri wake hasa hasa kwenye uchambuzi wa masoko ya Ulaya.
Hivyo basi baada ya kusikia kuwa George Soros alikuwa akiazima Paundi kwa kiwango kikubwa na kuziuza, karibia soko lote la fedha duniani likaanza kuuza Paundi ya Uingereza.
Mpaka kufikia muda ambao London Market inafunguliwa mida ya asubuhi, maafisa wa serikali waliianza siku kwa kushuhudia mabilioni ya Paundi yakiwa yameuzwa tayari. Kama ambavyo nilieleza kuwa sarafu fulani ikiwa inauzwa sana thamani yake kwenye soko inashuka. Ikinunuliwa sana, thamani yake inapanda. Kwa hiyo kitendo cha Paundi kuwa inauzwa sana kilisababisha kuwe na presha ya kuitaka thamani yake ishuke. Kilichokuwa kinasaidia pekee ni ile hali ya serikali kuzingatia sharti kwamba Paundi isiuzwe chini ya 2.78 DM.
Lakini kitendo cha serikali kung'ang'ana kwamba thamani ya Paundi ibaki pale pale kilikuwa kinaumiza zaidi sarafu yao. Hakuna mfanyabiashara wa fedha ambaye alikuwa tayari kuinunua kwa thamani hiyo huku akijua fika kwamba kuna mabilioni kwa mabilioni ya Paundi yanauzwa na hii ikiashiria kwamba thamani ya Paundi inaelekea kuporomoka kwa kasi ya radi.
Kwa hiyo kulikuwa na njia mbili za kuhakikisha kwamba thamani ya Paundi inabaki juu. Njia ya kwanza ilikuwa ni kuhakikisha inaanza tena kununuliwa kwa kiwango kikubwa. Na njia ya Pili ilikuwa ni kuanza kucheza na Interest Rates. Njia zote mbili hizi zilikuwa na changamoto zake. Njia ya kwanza ya kuhakikisha inaanza tena kununuliwa ilikuwa haiwezekani kwa maana ya kwamba wafanyabiashara wakubwa wote walikuwa wanafuata kile ambacho Soros alikuwa anakifanya. Walikuwa wanauza kila Paundi waliyonayo na ile ambayo waliweza kuazima. Njia ya Pili ya kuongeza Interest Rates ilikuwa ni hatari zaidi kwa kuwa nchi ilikuwa imetoka kwenye mdororo wa kiuchumi, kwa hiyo walihitaji kuhakikisha kuna spending kubwa kwa wananchi ili uchumi uendelee kuchangamka.
Ndio hapa inaturejesha tena kwenye kikao cha Waziri Mkuu John Mayor na wasaidizi wake nyumbani kwake Whitehall siku hiyo hiyo ya Septemba 16, 1992.
Nyumbani kwa Waziri Mkuu
Hali ya kikao ilikuwa tete kweli kweli. Wanasema siku ya kufa nyami miti yote inateleza. Ndicho ambacho kilikuwa kinawakuta serikali ya Uingereza. Kila suluhisho ambalo walikuwa wanalijadili na kulipendekeza lilikuwa haliwezekani kiutekelezaji. Ndipo hapa wakafikia uamuzi ambao walikuja kuujutia baadae.
Kwa kuwa hakukuwa na mfanyabiashara mkubwa au shirika lolote la fedha au mabenki ambao walikuwa tayari kununua Paundi ya Uingereza (kila mtu alikuwa anauza) serikali ya Uingereza ikafikia uamuzi kwamba wao wenyewe kama serikali waanze kuinunua Paundi. Kitu ambacho nataka ukumbuke ni kwamba, unaponunua sarafu fulani maana yake ni kwamba unatoa/unauza sarafu nyingine. Yaani kwa mfano ukisema unataka kununua sarafu ya kitanzania yenye thamani ya bilioni moja. Maana yake unatakiwa utumia mfano dola kama laki nne na nusu hivi kuinunua bilioni moja ya kitanzania. Ndio hapa tinasema unakuwa umenunua shilingi na umeuza dola.
Kwa hiyo kitendo cha serikali ya Uingereza kufikia uamuzi wa kutaka kuanza kuinunua Paundi maana yake ni kwamba walikuwa wanatumia akiba yao ya fedha za kigeni (Foreign Reserve) kuinusuru Paundi. Kama ikitokea George Soros akashinda vita hii maana yale ni kwamba watapata hasara mara mbili, sarafu yao kushuka thamani na watakuwa wamepoteza kiwango kikubwa cha akiba ya fedha za kigeni.
Mida ya saa 8:40 AM serikali ya walijibu mapigo ya Soros kwa kununua Paundi Bilioni moja!
Ajabu ni kwamba hakukuwa na muitikio wowote ule chanya katika soko. Bado watu waliendelea kuuza Paundi kwa kasi ya radi.
Ndipo hapa ambapo serikali ya Uingereza ikaanza mchezo mchafu wa propaganda. Waziri wa Fedha wa Uingereza Bw. Norman Lamont akafanya kikao na waandishi wa habari na kueleza kwamba kuna mfanyabiashara (George Soros) ambaye alikuwa amedhamiria kuubomoa uchumi wa Uingereza. Waziri Lamont akajiapiza kwamba watatumia misuli yao yote kupambana na 'dhalimu' huyo ili kutetea uchumi wa Uingereza na akaweka hadharani mpango wa Serikali kutumia dola bilioni 15 kuitetea Paundi.
Kwa wale ambao wanafanya biashara ya Forex nadhani wanajua ni kwa kiasi gani ambavyo 'News' zinaathiri soko la fedha. Leo hii Trump hata akitweet tu tayari kwenye soko utaona athari zake. Ukisikia Mario Draghi, Rais wa Benki ya Ulaya anaongea na kama unahold 'pair' fulani yenye Euro ndani yake basi presha inakupanda. Ukisikia mwanamama Janet Yellen, Mwenyekiti wa Federal Reserve ya Marekani ana mkutano na waandishi wa habari alafu wewe unaifanyia biashara pair yenye USD ndani yake unaweza kuzimia. Ni kwa sababu hicho kitakachoongelewa eidha kitakupa faida ambayo itakufanya utabasamu mpaka koromeo lidondoke au habari hiyo itakupa kilio cha uchungu kufanana na msiba. Binafsi naweza kusema katiba biashara ya fedha (forex) News ndio factor kubwa zaidi inayoamua uelekeo wa thamani ya sarafu. Na factor ya pili ni kubwa ni 'market markers' (hawa tutawaongelea huko mbele saikolojia yao na namna wanavyocheza na masoko ya fedha).
Kwa hiyo mkutano huu na vyombo vya habari ulilenga mambo mawili. Moja ni kutaka kuingiza hali ya uzalendo kwa mabenki ya Uingereza kuitetea Paundi ili kupambana na 'dhalimu' wa kimarekani ambaye anataka kuuzamisha uchumi wa Uingereza, na pili ni kujaribu kuiokoa Paundi kwa factor ya 'positive news' (nadhiri ya kutumia dola bilioni 15 kuitetea Paundi) maana yake thamani ya Paundi iende juu.
George Soros na Girlfriend wake Adrianna Ferreyr mcheza sinema kutoka Brazil
George Soros anajulikana kwa namna ambavyo yuko 'notorious' kwenye kutake risk za kibiashara. Baada ya kusikia kuwa serikali ya Uingereza wanatumia dola bilioni 15 ya akiba yao ya fedha ya kigeni kuitetea Paundi, naye akaongeza position yake kutoka dola bilioni 10 mpaka dola bilioni 15.
Kwa hiyo kile kikao cha Waziri Lamont na waandishi wa habari pamoja na nadhiri ya kutumia dola bilioni 15 kuitetea dola haikuwa na matokeo yoyote chanya kwenye soko. Paundi iliendelea kuuzwa kwa kasi na kwa kiwango kikubwa katika soko la fedha la dunia.
Serikali ya Uingereza hawakuishia hapo tu. Japo walitangaza kutumia dola bilioni 15 kuitetea Paundi lakini walijikuta wanatumia fedha za kigeni zenye thamani ya Puandi bilioni 27 kuinunua Paundi.
Lakini misuli ya Soros ilionekana ngangari zaidi yao. Ulimwengu ulikuwa na imani zaidi na Soros kuzidi serikali ya Uingereza. Soros aliendelea kuhold position yake dhidi ya Puandi na ulimwengu mzima wa soko la fedha ulikuwa nyuma yake kwa kuendelea kuiuza Puandi kwa mabilioni na mabilioni.
Serikali ya Uingereza ilishikwa na kiwewe zaidi.
Kila mti ulikuwa unateleza.
Mbele yao walikiwa na silaha moja ya mwisho… Interest Rates.
Saa 9:00 AM Waziri wa fedha wa Uingereza wa kipindi hicho, Norman Lamont akampigia simu Waziri Mkuu John Mayor akiwa na pendekezo la mwisho la kuinusuru Puandi. Kwamba waongeze Interest Rates. Naamini tunakumbuka nilivyofafanua namna gani ukiongeza interest rates thamani ya sarafu yako inapanda kwa kuwa wafanyabiashara na mabenki watainunua ili waiuze kwa faida hiyo ya juu. Lakini kwa mazingira ambayo Uingereza walikuwa wanapitia ilikuwa ni wendawazimu kuongeza Interest Rates. Nilieleza kwamba nchi ikiwa kwenye mdororo wa kiuchumi unapaswa kushusha interest rates ili kuchochea spending na mzunguko wa fedha. Na ikumbukwe kwamba ukiongeza interest rates watakaonufaika moja kwa moja ni wafanyabiashara ya fedha na mabenki na sio mwananchi wa kawaida. Lakini pia kama wangelifanya hivi kulikuwa na tishio la kuurejesha uchumi wa Uingereza kwenye mdororo ambao wametoka mwaka mmoja tu uliopita.
Kwa hiyo pendekexo hili la Waziri Lamont ilikuwa ni wendawazimu katika viwango vyote. Lakini uwendawazimu huu ndio ilikuwa silaha yao pekee ambayo ilikuwa imebakia.
Mara hii ya kwanza saa tatu asubuhi Waziri Mkuu John Mayor alikataa katakata kuongeza Interest Rates.
Kwenye soko la dunia Paundi ilikuwa inauzwa kwa kasi zaidi.
Saa 10:00 AM Waziri wa Fedha Norman Lamont alipiga tena simu kwa Waziri Mkuu akimuomba akubali ombi lake la kuongeza Interest Rates. Waziri Mkuu John Mayor akakataa kwa mara nyingine.
Paundi ikaendelea kuuzwa zaidi kwenye soko la Dunia.
Saa 11:00 AM Lamont akapiga tena simu kwa Waziri Mkuu. Safari hii akimtaka Waziri Mkuu amwambie wafanye nini? Waziri Mkuu hakuwa na jawabu… wala hakuna mtu yeyote kwenye serikali ya Uingereza ambaye alikuwa na jawabu. Silaha pekee ambayo walibakiwa nayo ilikuwa ni Interest Rates. Hivyo basi saa 11:30 AM Waziri Mkuu John Mayor alikubali ombi la Waziri wa Fedha kuongeza Interest Rates.
Kwa hiyo majira ya saa sita kasoro mchana, serikali ya Uingereza ilitangaza kuongeza Interest Rates kwa basis points 200… yaani kutoka 10% mpaka 12%.
Ilikuwa ni 'dili' nono ambayo ingewatoa mate wafanyabiashara wote wa fedha duniani. Lakini watu katika ulimwengu wa fedha walikuwa wanamuangalia Soros atafanya nini. "Don't bite!" Ndilo jibu pekee ambalo Soros aliwajibu wafanyabiashara wenzake na mabenki ambao mate yaliaanza kuwatoka kutokana na kuongezwa kwa interest rates. Aliwaonya kwamba 'meli' inaelekea kuzama. Wasijitumbukize wakazama nayo.
Waziri Norman Lamont akiwa na mentee wake, David Cameroon kipindi akiwa kijana
Bundi aliendelea kulia mlangoni kwa serikali ya Uingereza… ulimwengu uliendelea kuuza Paundi kwa kasi. Licha ya kuongeza interest rates bado watu walikuwa na imani na kile ambacho Soros alikuwa anakiona akilini mwake. Anguko la Paundi la Kihistoria.
Ndipo hapa ambapo serikali ya Uingereza ikafanya jambo lingine la uwendawazimu zaidi. Majira ya saa 04:00 PM Waziri Lamont alielekea nyumbani kwa Waziri Mkuu John Mayor maeneo ya Whitehall kuungana na wengine walioko huko kufanya mjadala nini zaidi kifanyike kuinusuru Paundi. Baada ya majadiliano ya masaa kadhaa wakatoka na moja ya uamuzi wa ajabu zaidi kiuchumi kuwahi kufanyika.
Serikali ya Uingereza ikatangaza tena kuongeza Interesf Rates kutoka ile 12% waliyoongeza awali mpaka 15%..!!!
Ilikuwa ni ajabu kweli kweli hasa ukizingatia hali tete ya kiuchumi ambayo Uingereza walikuwa nayo kipindi hicho. Naomba ieleweke kwamba mfano sasa hivi, serikali nyingi ulimwenguni huwa wanatangaza viwango vipya vya interest rates maro moja kwa mwezi. Kwa hiyo kitendo cha serikali ya Uingereza kutangaza interest rates na kuzipandisha mara mbili ndani ya siku moja kilikuwa ni kitu cha ajabu kuzidi maelezo ninayoweza kuyatoa.
Mabenki na wafanyabiashara wengi mate yalianza kuwatoka. Lakini macho yao yalikuwa kwa Soros. Atafanya nini? Soros alikuwa na jibu moja tu… kwamba serikali ya Uingereza ilikuwa 'desperate'! Wanachokifanya si jambo la kawaida kiuchumi, na hii inaonyesha ni kiasi gani ambavyo walikuwa desperate na hawana mbinu yoyote waliyobakiwa nayo kuinusuru Paundi. Hii maana yake ni kwamba walikuwa wanaelekea kusalimu amri na kupiga magoti. Walikuwa wanapaparika kama kuku anayekata roho. Hawakuwa na ujanja. Walikuwa wamewashika 'sehemu nyeti' na muda si mwingi watasalimu amri.
Kwa hiyo Soros akawahamasisha wenzake… "sell it!! Sell it as much as you can get!! Sell the GBP! Sell it against any other currency… Sell it against the US Dollar, Sell it against AUD, sell CAD, sell it against chinese Yen, sell it against Korean Won… just sell it as much as you can and by the time we go to sleep today we will have a fortune.."
Paundi iliuzwa kama njugu kwenye soko la fedha la dunia. Kwa mabilioni na mabilioni zaidi. Na kwa kasi ambayo haijawahi kutokea.
Serikali ya Uingereza hawakuwa na ujanja tena. Hawakuwa na silaha nyingine yoyote ile. Mafuriko ambayo walikuwa wameyazuia kwa mikono kwa siku nzima yalikuwa yamewazidi nguvu. Ulikuwa ni muda wa kupiga magoti, kuelekea kibla na kuchinjwa.
Muda wowote ulimwengu ulikuwa unatarajia serikali ya Uingereza kutangaza kushusha thamani ya Paundi na kujitoa kwenye mpango wa ERM.
Wanasema kwamba kama unaweza kuona 'aura' ya binadamu unaweza kujua kabla kifo akija mpata. Kwamba ukiangalia mfano picha ya mwisho ya marehemu Tupac, machoni mwake unaweza kukiona kifo kabisa. Unaweza kuona woga ambao anao. Unaweza kuona hofu ndani ya nafsi yake. Unaweza kuona kabisa kifo kikiwa kinamnyemelea.
Ndivyo ambavyo aura ya Waziri Norman Lamont ilivyokuwa alipoingia kwenye ukumbi wa mkutano na waandishi wa habari mida ya saa 07:30 PM. Chumba chote kilikuwa kimya. Kelele cha kamera tu ambazo zilikuwa zinafotoa picha ndizo ambazo zilikuwa zinasikika. Waziri Lamont aliingia akiwa ameongozana na wasaidizi wake kadhaa pamoja na watu wa benki kuu na hazina. Wananchi wa Uingereza ambao walikuwa wanafuatilia mubashara mkutano huu wa Waziri na waandishi wa habari hofu ilikuwa imewajaa mioyoni mwao. Ni mwaka mmoja tu wametoka kwenye mdororo wa kiuchumi na leo hii kitakachotamkwa na Waziri kinaweza kuirudisha Uingereza kwenye mdororo kama ule au zaidi.
Lakini kwa upande wa Soros hii ulikuwa ni wakati ambao amekuwa anausubiri kwa zaidi ya miezi miwili tangu aanze kujenga position yake ya mabilioni dhidi ya Paundi. Na wakati huo ndio ulikuwa umewadia. Yeye pamoja na vijana wake walikuwa wamejikusanya mbele ya runinga ofisini kwao New York wakifuatilia mubashara kabisa mkutano huu wa Waziri Lamont na wanahabari.
Wakati wa kujua mbivu na mbichi ulikuwa umewadia.
SEHEMU YA SITA
Waziri wa fedha Norman Lamont alikwenda moja kwa moja mpaka mahala pa kuzungumza ambako alikuwa ameandaliwa.
Muda mchache uliopita alikuwa amemaliza kikao na Waziri Mkuu John Major, Waziri wa mambo ya nje Douglas Hurd, Rais wa Bodi ya Biashara nchini Uingereza Bw. Michael Heseltine na Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Kenneth Clarke. Alikuwa amefika hapa kutangaza uamuzi ambao ulikuwa umefikiwa na kikao hicho cha dharura.
Baada ya waandishi wa habari kutulia, Waziri Lamont kwanza alianza kueleza namna ambavyo kuna hali ya dharura ya kiuchumi ambayo imeikumba Uingereza. Kwamba uchumi umeanza kwenda kombo tofauti na ambavyo walikuwa wanatarajia. Pia alieleza namna ambavyo sarafu yao ilikuwa kwenye msongo mkubwa wa kushindwa kuwezesha biashara kufanyika na kuchochea uwekezaji kutokana na kuonekana thamani yake iko juu zaidi tofauti na uhalisia.
Hivyo basi kutokana na Uingereza kuwa ndani ya mpango wa ERM ambao unatoa sharti la kuweka thamani ya Paundi kati ya 2.78 DM na 3.31 DM, kwa hiyo kwa masikitiko makubwa Waziri Lamont alitangaza kwamba Uingereza inajitoa kwenye mpango wa ERM na kufloat sarafu yake (kuacha thamani ya sarafu iamuliwe na soko la fedha). Waziri Lamont alieleza pia kuwa interest rates inashushwa mpaka 12% (kesho yake ilishushwa tena kurudi 10%).
Kimya cha woga kilitawala kwenye chumba cha mkutano wa habari, lakini huko jijini New York kwenye ofisi za Quatumn Fund pamoja na ofisi nyingine zote za hedge funds na wafanyabiashara wa fedha kulitawaliwa na vifijo na nderemo.
George Soros na wote walioamini katika kile ambacho alikuwa anakiona kwa muda wa miezi miwili iliyopita walikuwa wameshinda ushindi wa kishindo.
Dakika chache tu baada ya Waziri Lamont kutangaza kuwa Uingereza wanajitoa kwenye mpango wa ERM na kufloat sarafu yao, thamani ya Paundi ilishuka kwa 25% dhidi ya dola.
Nilieleza kwamba position ya Soros dhidi ya Paundi ilikuwa na thamani ya $ 15 Bilioni. Siku hiyo mara tu baada ya Waziri Lamont kutoa tangazo la kufloat Paundi, thamani ya position ya Soros ilipanda mpaka $ 19 Bilioni na wiki mbili baadae ikaongezeka mpaka $ 22 Bilioni. Au kwa maneno machache, George Soros na Quatumn Fund walitengeneza faida ya Dolla Bilioni saba.!! Nilieleza kuwa Hedge Fund managers wanapata 20% ya kila trade ambayo inaleta faida kwenye kampuni. Kwa hiyo katika trade George Soros alipata kiasi cha dollar billion 1.4 za kimarekani.
Asili ya biashara ya fedha ni kwamba kama wewe ukipata faida maana yake kwamba kuna mtu anapata hasara. Na katika trade hii George Soros alipata faida hiyo ya kutisha huku Benki kuu ya Uingereza ikiingia kwenye hasara ya karibia Dollar Billion 10 za kimarekani. Pamoja na hasara hii pia Uingereza walikuwa wamepoteza mabilioni ya akiba ya fedha za kigeni siku hiyo walipokuwa wakijitahidi kuokoa thamani ya Paundi.
Mwanzoni kabisa mwa makala hii nilieleza kwamba kabla ya mwaka 1992 kipindi Margareth Thatcher alipokuwa Waziri Mkuu, alipinga vikali Uingereza kuingia kwenye mpango wa ERM na serikali kujihusisha kwenye kuweka exchange rate ya Paundi. Alitala thamani ya Paundi iamukiwe na soko. Lakini John Major na wafuasi wake walipambana vikali kutaka Uingereza kuingia kwenye mpango wa ERM. Shukrani za Dhati zimwendee mwandishi Mahiri...The Bold. Compiled by R.T.Edson | Rorya Finest Media | Jukwaa la Maarifa | RoryaPixels
0 Comments
Unapenda kuhabarika? Jiunge nasi Katika Twitter na Facebook ili tuhabarishane.
Kumbuka Kuacha maoni yako hapa pindi usomapo habari zetu. Karibu Tena