Header Ads Widget

Responsive Advertisement

FAHAMU | Ajali ya M.V Bukoba Iliua watu na MTU - Chris Cyrilo

Image result for Abu 'Ubaidah al-Banshiri.AJALI YA MV BUKOBA ILIUA WATU NA MTU.

Mungu awarehemu wote waliopoteza maisha katika ajali ya meli ya MV BUKOBA, tarehe kama ya leo, miaka 22 iliyopita.
Umbali wa maili kama 30, sawa na kilometa 56, meli hiyo ilizama mita 25 chini ya maji ya ziwa Victoria. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1979, meli ya MV Bukoba ilikuwa chini ya umiliki wa Shirika la Reli; TRC, pamoja na meli zingine za MV Serengeti ya ziwa Victoria na MV Mwongozo ya ziwa Tanganyika na zingine huko ziwa Nyasa. Shirika la Reli lilichukua jukumu la kuendesha huduma za meli baada ya jumuia ya Afrika mashariki kuvunjika mwaka 1977.
Tarehe 21 mei 1996, meli ilitoka Bukoba ikiwa na abiria wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 1000. Abiria 443 walikuwa katika daraja la kwanza na la pili huku daraja la tatu likiwa na abiria wengi kuliko uwezo wake. Meli hiyo ilikuwa uwezo wa kubeba tani 850, lakini mara kwa mara katika safari zake ilibeba mizigo mingi yenye uzito mkubwa zaidi.
Kapteni Joseph Muguthi, aliyekuwa kapteni wa chombo hicho, mkenya aliyehudumu katika jeshi la maji la Kenya na mwandishi wa gazeti la Nairobi Daily News, alilaumu mamlaka kwa kupuuza mambo muhimu katika huduma za usafiri wa majini. Upungufu wa vifaa vya uokozi, waendesha meli wasiokuwa na ujuzi, kutokuwa na ratiba maalum ya kufanya marekebisho na kutokuwepo kwa utaratibu mzuri wa ukaguzi, zilitajwa kuwa sababu zilizopelekea ajali ya MV Bukoba. Jambo moja la kushangaza ni kwamba, ilibidi waokoaji watoke Afrika ya kusini, na kweli walifika, kuokoa mabaki ya meli. Taarifa za kiserikali zinadai watu 864 walipoteza maisha, vyanzo vingine vinadai watu zaidi ya 1000 walipoteza maisha.
Baadhi ya maofisa wa TRC walifunguliwa mashitaka baada ya tukio hilo. Na mwaka 1997, kitengo cha usafirishaji wa majini kilijitenga kutoka TRC na kujitegemea.

Wanaume, Wanawake na watoto walipoteza maisha. Mnara wa kumbukumbu ulijengwa kuwaenzi marehemu hao, na Rais Benjamin Mkapa alitangaza siku tatu za maombolezo.
Mungu awarehemu.

Hata hivyo, miongoni mwa ndugu waliopoteza maisha, alikuwako pia mmoja wa watu hatari duniani wakati huo. Jina lake hasa la kuzaliwa ni Ali Al Amin 'Ali al-Rashid, Lakini katika shughuli zake alijulikana kama Abu 'Ubayda al-Banshiri. Jina hilo alijipa akiwa nchini Pakistan miaka ya 1980 hadi 1989 akiwa katika mapambano dhidi ya vikosi vya umoja wa nchi za muungano wa ki-isovieti, akishirikiana na Ahmed Shah Massoud aliyekuja kuwa kiongozi wa Takriban wakati mauti yakimfika Al- Rashidi.

Haifahamiki hasa alizaliwa tarehe gani, lakini ni mwezi wa tano mwaka 1950 huko mjini Cairo nchini Misri. Al Rashidi, pengine alijua siku moja atakufa kwa bomu au kwa risasi, au kwa mateso ya CIA huko Guantanamo Bay, lakini alikufa kwa maji wakati akiwa mtu mwenye nguvu katika Al Qaeda, nafasi ya pili tu baada ya Osama Bin Laden wakati huo.

Al Rashid alianza kuwa mtumishi katika jeshi la polisi la Misri. Lakini serikali ya Misri iliwafukuza askari wengi waliokuwa waislamu wenye misimamo mikali, Al Rashid akiwa mmoja wao.

Historia yake inaanzia mwaka 1981 wakati wa mauaji ya Rais Anwar Al Saddat wa Misri. Moja ya wahusika wa mauaji hayo ni Abd-Hamid ‘Abd al-Salam, aliyekuja kuwa shemeji wa al-Rashidi, baada ya wote kuoa ndugu wa familia moja, huko Kenya. Ni mwaka 1983 ambapo Al Rashid alifunga ndoa na Hafsah Sa'd Rwashan.

Al Rashid na mkewe walihamia Jedda Saudi Arabia katika nyumba iliyomilikiwa na Osama Bin Laden, na baadye walihamia Medina katika nyumba ya Mohammed Matawi. Hapo waliishi kwa siku kumi tu, na kisha kutimkia Pakistan. Mke wa Al Rashid, Hafsah alikuja kueleza kuwa safari hizo ziligharamiwa na mtu asiyemjua. Katika mji wa Peshawar huko Pakistan, Al Rashid alijiunga katika kambi la mafunzo la Sada, akijitambulisha kama Abu Ubayda. Ndipo alipokutana na Ayman Al Zawahiri, aliyemtambulisha kwa Osama Bin Laden.
Osama alimkubali sana Al Rashidi. Walikuwa marafiki na walianzisha makundi mengi ya jihadi huko Pakistan. Mafanikio yao makubwa yaliyowapa umaarufu ni katika kile kilichoitwa "Battle of Jaji".
Katika mapambano hayo makali ya mjini Jaji, kikosi cha akina Osama na Al Rashid kiliwashinda kikosi maridadi cha jeshi la sovieti kilichoundwa na makomandoo wa Spetsnaz, wenye ujuzi mkubwa sawa na Navy Seal ya US, au Sayeret Matkal ya Israel.
Lakini baada ya mapambano hayo, baadhi ya vikosi vya jihad vilishindwa kutoa ushirikiano kwa Osama na wenzake.
Mkutano wa siku nne wa Tarehe 17-20 Agosti 1988, Al-Rashidi akiwa na Osama bin Laden, Wael Julaidan na
Mamdouh Mahmud Salim walijadili na kuanzisha Al Qaeda. Ingawa jina hilo lilikuwapo awali, lakini kundi rasmi lilianzishwa katika mkutano huo.

Kwa maneno yake Osama bin Laden, mnamo October 21, 2001, anakumbusha, kwamba "jina la Al Qaeda ni la zamani sana. Lakini kaka Al Rashid alianzisha mafunzo ya vijana wa kupambana dhidi ya manyanyaso ya wasovieti, ndipo jina Al Qaeda, "The base" lilipokolea"

Kundi la Al Qaeda lilijikita zaidi nchini Afghanistan na kuanzisha Makambi mengi ya mafunzo. Mwaka 1990, Al Qaeda walifikiria kutanua mapambano nje ya Afghanistan, wazo lilopelekea kuanzisha shughuli zake nchini Sudan. Lakini kwanza ilibidi wapitie Yemen, na mwaka 1992 walifika Sudan. Al Rashid aliratibu shughuli za Al Qaeda huko Yemen na katika Pembe ya Afrika, Sudan, Somalia, Kenya, Tanzania na Uganda.
Mwaka 1993, mkutano wa Al Rashid na Osama bin Laden uliamua kuanza kushambulia vituo vya kijeshi vya Marekani vilivyopo nchini Somalia na kwingineko Afrika. Baadae wazo hilo lilikua na kujumuisha balozi za Marekani.
Ili kuficha shughuli zao, Al Rashid na wenzake Muhammed Atef, and
Mohammed Sadiq Odeh walianzisha biashara ya uvuvi mjini Mombassa, Kenya mwaka 1994.
Pia, Al Rahid na Wadih Al Hage walianzisha makampuni ya kuuza Vito vya thamani, Dhahabu na Tanzanite kutoka Mererani, Arusha, kwa ajili ya kupata fedha za kuendesha shuguli zao.
Taarifa za shirika la kijasusi la ndani la Marekani, FBI, zinadai kwamba Al Rashid alimiliki ardhi mjini Mwanza, alikuwa na kampuni iliyoitwa Taheer Ltd aliyoianzisha mwaka 1993, ambayo kwa mujibu wa "global witness ", kampuni hiyo ilijihusisha na biashara ya Magendo ya Alimasi, kutoka Mwadui na/au Congo, pamoja na shughuli za kutakatisha fedha.
Rafiki yake Al Rashid, Wahid Al Hage alimiliki kampuni ya Tanzanite King, iliyojihusisha na biashara ya madini ya Tanzanite pamoja na Almasi zilizopatikana kimagendo kutoka kampuni ya Taheer Ltd.
Ili kuficha zaidi shuguli zao za kigaidi, Al Rashid na Al Hage walianzisha mashirika yasiyo ya kiserikali kwa ajili ya kusaidia watu masikini katika pembe ya Afrika, mfano, "Mercy International Relief Agency" na
"Help Africa People".

Haitegemewi mtu wa aina ya Al Rashid asheherekee siku ya kuzaliwa, labda pengine ilikuwa ndio siku yake ya kufa. Mei 21, 1996 alimaliza kazi wakati akiandaa kazi ya kulipua ofisi za ubalozi wa Marekani mjini Dar es Salaam, Tanzania na Nairobi, Kenya. Hakuishi kuona ndoto hiyo ikitimia. Lakini alikwishandaa mtandao.
Vyanzo vingine vinadai, Al Rashid alisafiri ndani ya MV Bukoba kuelekea Mwanza akiwa katika kutafuta mali ghafi za kutengeneza bomu-chafu, hakufika.

Baada ya kifo Chake, Kundi la Al Qaeda liliwatuma Fazul Mohammed Abdullah na Wadih Al Hage ili kuhakikisha kuwa kweli Al Rashid amekufa na kwamba kifo hiko kilitokana na ajali na sio mauaji ya kupangwa.

Credits;
Abu Ubaidah al-Banshiri, GlobalSecurity.org
Al-Qaeda gains first members, GlobalSecurity.org
Status of Embassy Bombings Investigation, FBI Executive Summary. Nov. 18, 1998.
Lake Victoria tragedy, Tanzania in May 21". Arai's Zanzibar, Tanzania Page. Arai Shin-Ichi. images (3).jpeg 

Post a Comment

0 Comments